Sunday, June 10, 2012

Afrika Mvunja Nchi Ni Mwanasiasa, Kiongozi Wa Kidini

Best Blogger Tips
Makala ya Maggid Mjengwa

SWALI ambalo mara nyingi nakutana nalo ni hili; ’Huogopi’?  Swali hili linatokana na mambo niandikayo.

Ukweli, kuna Watanzania wengi sana wanaishi kwa hofu.
Ndiyo, hofu zimetawala mioyo ya Watanzania wengi. Ni muhimu na busara kukawapo na mazingira ya wanajamii kutoa  fikra zao kwa uhuru, hata kwenye masuala yenye kuhusu imani.

Hatuwezi kuzuia kero na migongano ya kijamii kwa kuikimbia mijadala. Kufanya hiyo ni kuahirisha matatizo, na zaidi kuyalundika. Na siku yakifumuka, athari yake huwa ni kubwa na mbaya zaidi.

Mimi nadhani, kuwa  Watanzania wengi hatuna maarifa ya dini. Shule zetu hazina masomo ya dini kwa ujumla wake. Kuna wanaosoma elimu kuhusu maarifa ya Uislamu ( Islamic  Knowledge) . Kuna wanaosoma kuhusu maarifa ya Biblia, hivyo Ukristo (Bible knowledge).

Lakini, shuleni hakufundishwi maarifa kuhusu dini kwa ujumla wake, ( Religious Knowledge) Hili ni tatizo, kwamba  Wakristo wanapata mafundisho juu ya Ukristo, Waislamu vivyo hivyo. Wahusika wanakosa ufahamu juu ya dini za wengine. Ingelikuwa vyema, kama tangu shule za msingi,  watoto wakajifunza juu ya dini mbalimbali za dunia hii.

Na kuna Watanzania wengi ambao hawajui kuwa kuna tofauti ya Uarabu na Uislamu; kwamba si kila Mwarabu ni Mwislamu. Watanzania wengi bado hawajui kuwa kuna dini nyingine za dunia zaidi ya Uislamu na Ukristo hata kama Uislamu na Ukristo ndizo dini kubwa na maarufu hapa duniani.

Na lililo kubwa kabisa; dini zote za dunia zinahimiza uwepo wa amani na upendo miongoni mwa wanadamu. Katika kuishi kwangu sijapata kusikia dini ambayo misingi yake imejengwa katika kuwafanya waumini wake wawachukie na kuwabagua wanadamu wenzao wasio wa imani yao.

Duniani hakuna dini inayohimiza waumini wake kuwatendea maovu wanadamu wenzao wasio wa imani yao. Kuna  wanadamu wenye hulka mbaya, ikiwamo kutenda maovu.

Na hao wamo miongoni mwa Wakristo, Waislamu, Wahindu, Wapagani na wengineo. Na kamwe, maovu yakifanywa na wachache si haki kuhukumu wote katika kundi analotoka mtenda maovu.

Na kwa Afrika, mvunja nchi si mwananchi, bali ni mwanasiasa na hata kiongozi wa kidini. Ni kwa kutanguliza mbele maslahi  binafsi na ya kundi dogo  badala ya yale ya  kitaifa.

Watanzania tukubali sasa, kuwa nchi yetu imepatwa na bahati mbaya ya baadhi ya Watanzania wenzetu kuanza kupandikiza mbegu za chuki miongoni mwetu. Hili ni jambo la hatari sana.

Taratibu tumeanza kuizoea misamiati ya sisi na wao. Mathalan, sisi Wakristo na wao Waislamu. Sisi Wachaga na wao Wazaramo.
Tunasahau, kuwa katika nchi yetu hii hakuna Sisi na Wao. Kuna SISI tu.Tutakapokumbwa na maafa ya kitaifa watakaoathirika ni SISI, hakutakuwa na WAO.

Wahenga walisema ”kamba hukatikia pabovu”. Kamwe huwezi kuwavuruga Watanzania na kuwafanya wachinjane kwa sababu za kudai kuna upendeleo wa ukabila au wa kisiasa.
Mahala ambapo unaweza kuwagawa Watanzania na hata kufanikiwa wachinjane ni kwenye masuala ya imani. 



Tusikubali dini iwe ndiyo penye ubovu kwenye kamba inayotuunganisha Watanzania.
Hekima ituongoze katika kutambua, kuwa nchi yetu ina makabila zaidi ya mia na ishirini. Ina waumini wa dini za kimapokeo; Uislamu na Ukristo, ina waumini wa dini za jadi, kuna Wahindu na wengineo. Na kisiasa, nchi yetu ina  vyama vingi vya siasa .
 
Hivyo basi, haiwezekani kwa kabila moja tu kuweza kuongoza nchi hii. Haiwezekani kwa Watanzania wa dini moja tu kuongoza nchi hii. Haiwezekani kwa chama kimoja tu cha siasa kikashika hatamu zote za uongozi na kufanikiwa bila kushirikiana na vyama vingine.
 
Ndiyo, kilichotusumbua huko nyuma ni kuendekeza ubaguzi wa kisiasa. Ndicho kinachotusumbua sasa. Na kwa vile kuna ombwe ( vacuum) la uwepo wa siasa za upinzani zinazokubaliwa na walio madarakani. Kwamba jamii yetu, na hususan wanaokuwa madarakani,  bado hawajakubali kwa moyo wote uwepo wa siasa za upinzani. Kukubali kuwa  tofauti za kifikra na kimitazamo ya kisiasa na kiuchumi ni jambo la siha kwa taifa.
 
Na kama ombwe hili litaendelea kuwapo,   nahofu kuwa huko tuendako siasa za ’Chai- Maharage’ zitachukua nafasi zaidi kuziba ombwe hili la siasa za upinzani.
 
Tunaona leo jinsi wanasiasa wetu wanavyoshindwa kutenganisha dini na siasa katika kazi zao. Tunawaona wakishiriki mikusanyiko ya kidini na kutoa matamko ya kisiasa na hata kupigana vijembe. Ni hatari sana. Nahitimisha.
Mungu Ibariki Tanzania.

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits