WAZIRI wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, amefanya ziara ya
kushitukiza katika Kituo cha Mabasi cha Msamvu, Manispaa ya Morogoro na
kufanya ukaguzi wa mabasi ya abiria yaendayo mikoani.
Katika ukaguzi huo, mabasi matatu aliyaamrisha yalipe faini ya Sh
250,000 kila moja, kutokana na makosa mbalimbali, likiwamo la kutokuwa
na dereva wa akiba.
Ziara hiyo aliifanya mapema wiki hii asubuhi,
kwa kushirikiana na maofisa wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi
Kavu na Majini (SUMATRA) na lengo lake ni kukagua mabasi yanayofanya
safari za mikoani na nje ya nchi na kuona kama yanakidhi vigezo katika
shughuli ya kusafirisha abiria.
Katika ziara hiyo, Dk. Mwakyembe,
alifika katika kituo hicho cha mabasi na kuegesha gari lake mbali
kidogo, kisha kuelekea katika mabasi huku akiwa kama abiria na kuingia
ndani ya mabasi hayo kisha kuanza kukagua leseni za madereva na
vitambulisho vya kampuni za mabasi wanavyotumia madereva.
Ukaguzi
mwingine alioufanya ni ratiba za safari pamoja na usalama wa mabasi na
baadaye aliamrisha madereva walioonekana kuwa na makosa kulipa faini.
Mabasi
yaliyolipishwa faini ni pamoja na Royal Coach linalofanya safari zake
kutoka Dar es Salaam kuelekea Bukoba, ambalo dereva wake hakuwa na
kitambulisho cha kampuni, basi la Super Najimunisa na Muro Investment
yanayofanya safari zake Dar es Salaam kuelekea Mwanza ambayo yalikuwa na
kosa la kutokuwa na dereva wa akiba.
Baada ya kubaini makosa
hayo, aliwataka madereva ambao walionekana kuwa na makosa kulipa faini
ya papo hapo, vinginevyo aliwataka SUMATRA kuwafikisha mahakamani, hata
hivyo, madereva hao walikubali kulipa faini hiyo baada ya kuwasiliana na
wamiliki wa mabasi wanayofanyia kazi.
Akizungumza na maofisa wa
SUMATRA na madereva, alisema makosa kama hayo yanaweza kusababisha ajali
za barabara na hivyo kupoteza maisha ya watu, vilema vya kudumu na
uharibifu wa mali na ataendelea kufanya ziara za namna hiyo mara kwa
mara kwa ajili ya kubaini makosa mengine.
Aidha, aliwataka
SUMATRA na kikosi cha usalama barabarani kusimamia sheria za usalama
barabarani na kutowaonea aibu madereva watakaoonekana kuwa na makosa,
kwa kuwa kufanya hivyo kutasaidia kupunguza ajali ambazo ni tishio hapa
nchini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Usalama Barabarani mkoani hapa,
Leonard Gyindo, alisema Kikosi cha Usalama Barabarani kimejipanga
kudhibiti ajali za barabarani kwa kufanya ukaguzi kabla ya gari
halijaondoka katika kituo hicho na kwa madereva wenye makosa wamekuwa
wakilipishwa faini ya papo hapo na wengine kufikishwa mahakamani.
Hata
hivyo, alimpongeza Dk. Mwakyembe kwa jitihada zake katika kusimamia
sheria, hasa za usalama barabarani na kuahidi kuwa kikosi hicho kitampa
ushirikiano na kutekeleza maagizo yote atakayotoa.
Chanzo: Mtanzania
Wednesday, June 27, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment