Mauwaji ya zaidi ya raia 100 katika mji wa Houla
nchini Syria wiki iliyopita huenda ukaelezewa kama uhalifu dhidi ya
binadamu, kwa mujibu wa Kamishna wa Haki za binadamu kwenye Umoja wa
Mataifa.
Bw.Pillay aliyasema haya wakati akihutubia Kikao cha dharura cha Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa.
Hapo awali, wanaharakati wa upinzani walisema kua kuna mauwaji mengine ya raia yaliyofanywa na wana mgambo wanaoungwa mkono na serikali.
Wafanyakazi 13 wa kiwanda kimoja waliamrishwa kutoka ndani ya basi walilokua wakisafiria na kuuawa na ''Shabiha'' Jina la wanamgambo hao wanaoiunga mkono serikali siku ya alhamisi huko al Buwaida al Sharkiya, karibu na mji ulio magharibi mwa nchi wa Qusair.
Video kadhaa zilizotumwa kupitia mtandao zilionyesha maiti zenye majeraha ya risasi zilizopigwa kichwani na kwenye tumbo, ikiashiria walipigwa risasi na mtu aliye karibu nao.
Madai hayo ya wanaharakati hayana uthibitisho huru, lakini wasimamizi wa Umoja wa Mataifa walioko huko Syria waliweza kuthibitisha madai kama haya mara mbili katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.
Baraza la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa, likiwa ndilo shirika la kiwango cha juu duniani, lilianza mkutano wa dharura kujadili ghasia za nchini Syria. Hii ni mara ya nne kwa Baraza hili kujadili Syria tangu vuguvugu la kumpinga Rais Bashar Al Assad lianze mnamo mwezi Machi mwaka 2011.
Chanzo: BBC
No comments:
Post a Comment