TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) inamshikilia Mbunge
wa Jimbo la Bahi (CCM), Omary Badwel kwa tuhuma za kupokea rushwa ya Sh1
milioni kutoka kwa kiongozi wa Serikali.
Habari zilizopatikana
na kuthibitishwa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa taasisi hiyo, Alex Mfungo
zinaeleza kuwa Badwel alikamatwa na maofisa wa Takukuru jana saa 9:00
alasiri katika Hoteli ya Peacock jijini Dar es Salaam.
Badwel
ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa
(LAAC) anadaiwa kukamatwa wakati anapokea rushwa kutoka kwa maafisa wa
Halmashauri ya Wilaya ya Mkurunga mkoani Pwani jana.
Mfungo
aliliambia Mwananchi Jumapili kuwa wanaendelea kumshikilia huku wakati
wanafanya uchunguzi hadi kesho ambapo watamfikisha mahakamani.
“Siwezi
kumataja aliyekuwa akitoa rushwa kwa sababu bado tunaendelea na
upelelezi, ila mpaka sasa yuko mahabusu na tutamfikisha mahakamani
Jumatatu(kesho),” alisema Mfungo.
Alisema kuwa mbali na kumfikisha mahakamani, pia watatoa taarifa zaidi za tukio hilo kesho.
Naye
Katibu wa Bunge, Thomas Kashilillah alilithibitishia gazeti hili jana
kukamatwa mbunge huyo na kwamba wanasubiri taarifa zaidi kutoka Takukuru
kuhusiana na suala hilo.
“Nimepata taarifa ya kukamatwa kwa
Badwel, lakini sina taarifa za ndani nasubiri wenzetu wa Takukuru watupe
ufafanuzi zaidi,” alisema Kashillilah.
Wakati mbunge huyo
akikamatwa jana, Mwenyekiti wa Kamati ya LAAC, Augustine Mrema alikuwa
Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere akielekea Uingereza.
Bedwel
ni mmoja kati ya wabunge wawili waliotajwa na Mbunge wa Kigoma Kusini,
David Kafulila (NCCR Mageuzi) katika Bunge la Bajeti mwaka jana kwamba
waliomba rushwa katika halmashauri ambayo hakuitaja.
Akichangia
Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano, Kafulila aliwataja bungeni Mbunge
wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi na Mbunge wa Bahi, Omary Badwel wote
wa CCM akidai kwamba aliwakuta wakiomba rushwa kwa viongozi wa
halmashauri.
Wakati akitaja majina hayo, Kafulila nusra aingie
katika mgogoro na aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge, George Simbachawene
ambaye alikuwa akimwamuru kukaa chini kutokana na muda wake wa kuchangia
kumalizika. Hivi sasa Simbachawene ni Naibu Waziri wa Nishati na
Madini.
Wakati Simbachawene akimwamuru akae chin, Kafulila
alikuwa akiendelea kuzungumza bila kujali kengele ya pili iliyopigwa
kuashiria kwamba muda wake ulikuwa umekwisha.
"Mheshimiwa
Mwenyekiti kwa wakati wa sasa ni vigumu kusimamia matumizi kwani mfumo
wetu wa uongozi unaruhusu ufisadi, wapo viongozi, mawaziri, wabunge
wanaomba rushwa...." alisema Kafulila na kuamsha zogo ambalo
liliambatana na sauti zisizo rasmi katika ukumbi wa Bunge zikiuliza
".....wapo humu humu?" Kafulila alijibu "Ndiyo..."
Sauti moja
ilisema wataje, hapo ndipo aliposema "....Wapo kina Zambi, Badwel,
niliwakamata na nilichukua hatua, hatuwezi kuendelea namna hii," kisha
akaketi.
Baada ya dakika chache tangu alipoketi, Kafulila
alionekana akiteta jambo na Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali na
Augustine Mrema wa Vunjo na baadaye Mkosamali aliomba mwongozo wa
Mwenyekiti wa Bunge, akitaka waliotuhumiwa watajwe ili wafahamike
vizuri.
Zambi na Badwel ni wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa pamoja na Kafulila chini ya Mwenyekiti wao, Mrema.
Mwenyekiti
wa Bunge, Simbachawene akijibu hoja hiyo alisema atatoa mwongozo wake
baadaye, katika muda ambao ataona unafaa. Hata hivyo, hadi sasa hakuna
mwongozo ambao umetolewa na bunge kuhusiana na kauli ya Kafulila.
Naibu Spika
Kauli
ya Naibu Spika, Job Ndugai alisema taarifa ya tuhuma za rushwa kwa
wabunge ziliwahi kutolewa katika kikao cha Kamati ya Uongozi na Mrema,
ijapokuwa majina ya watuhumiwa na mlalamikaji hayakutajwa.
Kafulila
aliwahi kukaririwa akieleza kuwa tayari taarifa za tuhuma hizo za
rushwa zilikuwa zimefikishwa kwa Spika kwa maandishi pamoja na Mrema kwa
ajili ya hatua zaidi.
Kadhalika, Mbunge huyo alisema taarifa
hizo zilikuwa zimekwishawafikia viongozi wa juu wa Ofisi ya Waziri Mkuu,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na kwamba aliwahi kukutana na
Spika kuhusu suala hilo ijapokuwa hakukuwa na hatua zozote ambazo
zilichukuliwa.
Wakati hayo yakiendelea Habari zilizopatikana jana
kutoka kwa watu walio karibu na Kafulila zimeeleza kuwa huenda leo
mbunge huyo akafanya mkutano na waandishi wa habari na kuanika uozo
uliopo katika kamati hiyo.
Chanzo: Mwananchi
Saturday, June 2, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment