Sunday, June 3, 2012

Kafulila alitega Bunge

Best Blogger Tips
 SIKU moja baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kumshikilia Mbunge wa Jimbo la Bahi, Omary Badwel (CCM), kwa tuhuma za rushwa, Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, amelipa Bunge masharti magumu na kulitaka liyatekeleze katika mkutano ujao wa bajeti unaoanza Juni 12.

Kafulila amelitaka Bunge, kumvua wadhifa wa ubunge, Badwel mara moja, na pili kuivunja Kamati ya Hesabu za Serikali (LAAC) chini ya Uenyekiti wa Augustine Mrema.

Aliwaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuwa, ametaka Bunge lifanye maamuzi hayo mapema, kwa sababu, hayo ni matokeo ya kitendo chake cha kupuuzia tuhuma nzito alizowatuhumu baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo, akiwemo mbunge huyo wa Bahi kwa madai ya kupokea rushwa kutoka kwa baadhi ya watendaji.

“Ilikuwa ni Bunge la Juni 13 mwaka jana wakati nikichangia hoja ya mpango wa maendeleo wa miaka mitano, nilitoa taarifa inayowahusu wabunge watatu akiwemo Mbunge huyu Badwel wa kamati hiyo kutuhumiwa kwa rushwa.

“Lakini sikupewa ushirikiano toka kwa wadau wote, likiwemo Bunge lenyewe na Tamisemi. Sasa hatimaye imedhihirika kuwa kile nilichokisema, wakakidharau kimekuwa kweli, na ninatamka rasmi kuwa sina imani tena na kamati hii kwa kuwa imepoteza uhalali wa kuendelea kuwa kamati ya kusimamia na kudhibiti hesabu za serikali,” alisema Kafulila.

Kwa kuzingatia hoja hiyo, alisema sasa ni wajibu wa Spika kutafakari upya kuhusu hadhi ya kamati na kuipanga upya kwa maslahi ya umma, heshima na hadhi ya Bunge.

Kwa mujibu wa Kafulila, akiwa kama Mjumbe wa Kamati ya Maadili ya Bunge na kwa kuwa Bunge lina mamlaka ya kumvua ubunge mbunge yeyote kwa azimio la Bunge, anaiomba kamati kuiwasilisha hoja hiyo katika mkutano ujao wa Bunge ili stahiki zichukuliwe kulinda heshima ya chombo hicho.

Alitahadhalisha kuwa ikiwa Spika hataona umuhimu wa kuyatendea kazi mambo hayo mawili, ajue itakuwa aibu kubwa kwa Bunge.

Alionya kuwa ikiwa hakutachukuliwa hatua kali kwa wabunge wanaopata tuhuma, huenda siku za usoni Bunge zima likajikuta lina watuhumiwa na hivyo kupoteza imani kwa wananchi ambao wanalitegemea katika kutoa maamuzi makubwa na kuisimamia serikali kufanya kazi zake kwa kufuata uadilifu.

Alitoa mfano wa Bunge la Uingereza lililowawajibisha wabunge wake zaidi ya mara 59 na Bunge la India likafanya hivyo hivyo mwaka 1979, hivyo haoni kwa nini Bunge la Tanzania lisuesue kuchukua hatua kama hizo.

Alipoulizwa ni kwa nini hatua zichukuliwe kwa mbunge huyo wakati tayari kuna wabunge wengi wanaotuhumiwa kwa tuhuma mbalimbali, Kafulilia alisema huu ni mwanzo wa kuanza ukurasa mpya, na kuacha tabia ya kusema mbona fulani alifanya.

Mbunge Badwel alikamatwa juzi na TAKUKURU katika hoteli ya Peacock majira ya saa 9:00 akipokea rushwa ya sh milioni 1 kutoka kwa maafisa wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkurunga mkoani Pwani.
Chanzo: Tanzania Daima

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits