Rai ya Jenerali Ulimwengu
JUMAMOSI iliyopita chama-tawala, CCM, kilionyesha kuwa kumbe bado
kinaweza kukusanya maelfu kwa maelfu ya wanachama na mashabiki wake na
kikawaweka kwa muda wakisikiliza hotuba baada ya hotuba za serikali
wakieleza walichokifanikisha na wanachotaraji kukifanikisha katika
kipindi kifupi kijacho.
Mkutano huo wa Jangwani ulihudhuriwa na watu wengi mno, na wengi
walionekana wakiwa wamevaa sare za chama hicho, ambazo nazo zilionekana
kama mpya. Kwamba chama hicho kliweza kuwakusanya watu wengi kiasi
hicho ni jambo muhimu kwa sababu kwa muda mrefu kilikuwa kikionekana
kama vile kimepigwa sindano ya ganzi na kimeduwaa.
Najua kwamba watazamaji na wachambuzi wengi wamekuwa wakisema
kwamba umati huo ulikuwa mkubwa kiasi hicho kwa sababu tu wakuu wa
chama mkoani Dar es Salaam walitumia fedha nyingi sana kukodi magari ya
kuwasomba wanachama hao, na kwamba baadhi yao walilipwa ili wahudhurie
kikao hicho cha maonyesho.
Hata kama hilo ni kweli, ni kweli pia kwamba watu walikwenda
Jangwani kwa hiari yao, kwa sababu hatujapata taarifa za ye yote
aliyetekwa nyara na kubebwa kupelekwa Jangwani.
Jambo jingine la kuliangalia kama ushindi wa chama-tawala ni kile
kitendo cha mawaziri wa Serikali kuonyesha kuwajali wananchi kiasi cha
kujihisi kwamba wanawajibika kutoa taarifa za utendaji wa idara zao
moja kwa moja kwa wananchi, jambo ambalo huko tulikotoka halikuzoeleka.
Sasa inaelekea mawaziri wataanza utaraibu wa “kuripoti” moja kwa moja
kwa wananchi, ambao sasa wanatambua kwamba ndio matajiri wao.
Jambo la tatu ambalo limajitokeza ni kwamba chama-tawala sasa
kimeamua kujibu mapigo ya chama kikuu cha upinzani kwa kuchukua kauli
za wapinzani hao na kuzikosoa huku kikionyesha kwamba ndicho kilicho na
uhalali wa kuendelea kuitawala nchi yetu.
Ingawawaje mapema wakuu wa chama-tawala walitaka watu waamini kwamba
lengo la mkutano huo wa Jangwani halikuwa “kujibu mapigo” ya CHADEMA ,
lakini mwenye masikio haambiwi sikia. Mkutano ule ulikuwa wa kujibu
mapigo kuanzia mwanzo hadi mwisho na wala haukuwa na lengo jingine lo
lote.
Jambo la nne nililolichukua kutoka mkutano ule ni kwamba chama-tawala
kimeanza kampeni kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu ujao. Tumezoea kuwasikia
wakuu wa chama hicho wakiwakosoa wapinzani kwa kufanya kampeni
zisizokuwa na mwisho, wakisema kwamba uchaguzi umekwisha na kwa hiyo
hakuna haja ya kufanya kampeni. Inawezekana kwamba msimamo wa
kutokufanya kampeni hadi mwaka 2015 umeonekana kuwa na gharama kubwa
kwa chama hicho na ndiyo maana kikaamua kufanya kama wafanyavyo wakuu
wa CHADEMA.
Sasa, angalau tunajua kwamba vyama vikuu vya kisiasa nchini, CCM na
CHADEMA, vimeingia katika kampeni ya kudumu, na kwamba kampeni hizi
zitatusaidia kujua zaidi kuhusu sera na mipango ya vyama hivi. Ni
upuuzi kutaka chama cha siasa kisifanye kampeni eti kwa sababu uchaguzi
umemalizika, kisubiri hadi uchaguzi ujao. Ni sawa na kujiambia timu ya
mpira isifanye mazoezi na isisajili wachezaji wapya kwa sababu ligi
haijaanza.
Nasema kwamba kilichojitokeza Jumamosi iliyopita ni ishara kwamba
chama-tawala hakiko tayari kuendelea kubamizwa na wapinzani
wanaokikosoa kila siku kwa lengo la kukifanya kionekani kama hakifai
kutawala, lengo la kimkakati likiwa ni kukiondoa madarakani. Sasa
chama-tawala kitajibu mapigo, na hiyo ndiyo raha ya siasa, mapigo na
majibu ya mapigo, hoja na majibu dhidi ya hoja.
Nitakachokitarajia sasa ni kwamba katika kujibu mapigo, chama-tawala
hakitajitengenezea matatizo mengine zaidi ya yale kilicho nayo, kwamba
hakitajitia kitanzini chenyewe bila kujua. Ni rahisi kwa kundi la watu
waliohamanika kujisemea maneno bila kuyapima na baadaye kujuta kwa nini
waliyasema maneno hayo.
Kwa mfano, katika mkutano ule katika viwanja vya Jangwani, sura
iliyojitokeza ilikuwa ni Serikali zaidi kuliko chama-tawala. Ni kweli
mawaziri waliokuwa Jangwani ni wanachama wa chama-tawala, na wala hilo
haliwezi kuwa na shaka. Pia alikuwapo Katibu wa Itikadi na Uenezi
pamoja na mlezi wa Mkoa wa Dar es Salaam. Lakini Mwenyekiti alikuwa
wapi, Katibu Mkuu alikuwa wapi na Makamu Mwenyekiti alikuwa wapi?
Ujumbe mzito wa Halmashauri Kuu ulikuwa wapi kudhihirisha dhamira ya
kweli ya chama hicho ya kufanya kazi ya kujibu mapigo ya wapinzani kwa
njia ya kudumu?
Ninachoshuku ni kwamba hii ilikuwa ni hatua ya zima-moto, maandalizi
ya dharura ya kujaribu kupunguza kasi ya upinzani kwa kupitia huko huko
walikopitia na kufanya yale yale waliyofanya wapinzani.
Ni ishara kwamba mambo yamebadilika sana. Kuna wakati katika miongo
miwili iliyopita ambapo tulishuhudia vyama vya upinzani vikijaribu
kuiga kila kilichofanywa na chama-tawala; sasa ni kinyume chake kwa
sababu ni chama-tawala kinachoanza kuiga yanayofanywa na wapinzani.
Ni rahisi kuwaambia mawaziri waende Jangwani waeleze ni nini Serikali
yao imefanya na ni nini inakusudia kufanya, kuliko kuwapelekea wakuu
wa siasa ndani ya chama kwenda kuelezea siasa ambazo hata wao hajui
zimekaa vipi na zinaelekea wapi. Hii ndiyo maana ya kuwapeleka mawaziri
badala ya viongozi wa chama kama viongozi wa chama.
Isitoshe, ahadi ni deni, na tayari chama-tawala kimekwisha kujivisha
madeni mpaka kinatakiwa kiogope kutoa ahadi nyingine. Kumekuwa na tabia
ya kutoa ahadi za uongo “mchana kweupe’ ili watu wavutike na
wakichague chama hicho, bila kuangalia athari zake katika siku zijazo.
Mwaka 2010 tulisikia ahadi nyingine nyingi mno, ambazo kama zingekuwa
zinatekelezwa leo hii zingeweza kuwa zimefikia nusu ya utekelezaji.
Utekelezaji u wapi?
Miaka minane iliyopita, kwa mfano, tulisikia ahadi za kutengeneza
ajira kwa mamilioni; mwaka 2010 hatukusikia sana hadithi za ajira,
ingawaje wapo waliojaribu kusema kwamba ajira zimetengenezwa ingawa si
wengi walioamini hadithi hizo.
Ni muhimu kwa wanasiasa kutambua kwamba hali ya nchi na wananchi wake
imebadilika sana. Leo hii tunao watu wengi, na hasa vijana, ambao
wanafutailia kwa makini na kwa karibu mno kila kitu kinachosemwa na
kufanywa na watawala wao, na wanaweka kumbukumbu. Si watu wa kusikiliza
na kisha kusahau walichokisikia.
Kwa bahati mbaya tumejenga utamaduni unaotaka kutufanya tuamini
kwamba siasa ni uongo, na kwamba ili ufanikiwe katika siasa huna budi
kuwa mwongo, na hilo ndilo tunalolishuhudia leo hii. Wanasiasa wetu si
wanasiasa wa kweli bali ni waongo ambao hata katika uongo wao
hawaonyeshi umahiri wo wote.
Haiyumkiniki kuwaambia wananchi kwamba Serikali yao inashughulikia
mfumuko wa bei na hali ngumu ya maisha wakati kila mtu anaona kwamba
hali inazidi kuwa mbaya zaidi kila uchao.
Hata kama unachowaambia ni kwamba Serikali imenduka kutoka
usingizini na sasa imejenga mikakati na mbinu kulishughulikia suala
hilo, na ukawataka wananchi wavute subira, si watavuta subira tu, kwani
watafanya nini? Baada ya nusu mwaka, mwaka mmoja, au miaka mitatu
ijayo utawaambia nini tena?
Katika kampeni hii iliyoanza Jumamosi iliyopita ni dhahiri
tutajifunza mengi. Kwa mfano sasa najua kwamba iko mipango ya kuanzisha
usafiri wa reli jijini Dar es Salaam. Utaanza lini, na utahusu maeneo
gani tutakuja kujua baadaye. Lakini tunakumbuka kwamba zaidi ya miaka
kumi iliyopita tuliambiwa kuhusu mabasi yaendayo kasi jijini Dar es
Salaaam; leo ndiyo tunaona barabara zinajengwa kwa kusuasua. Hiyo reli
ni ya mwaka ujao au ya miaka 15 ijayo? Na wala wazo hili la reli si
jipya!
Ingewasaidia wakuu wetu kama wangekuwa na utaratibu wa kuketi
pamoja, katika vikao vya chama, na kujadili masuala yote makuu ya
kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni kabla ya kutoka kwenda
Jangwani kutoa ahadi nyingine.
Wapinzani hawana la kuthibitisha kwa sababu hawajakamata madaraka.
Chama-tawala ndicho kilichobeba mzigo wa kuthibitisha kimefanya nini
katika kipindi chote cha utawala wake kabla hakijasema kinadhamiria
kufanya nini na kutoa ahadi nyingine zitakazokuja kuwa kitanzi kwake.
Ushauri wangu: Punguzeni ahadi; tekelezeni zile mlizokwisha kuahidi.
Chanzo: Raia Mwema
Wednesday, June 13, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment