MWANAFUNZI wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Nyakamwaga
wilayani Geita, Fikiri Mtasimwa, amenusurika kifo baada ya kujeruhiwa
kwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake na kukatwa kiganja cha mkono
wake wa kushoto na Baba Neema baada ya kumtuhumu kutembea na mke wake.
Akizungumza mjini hapa jana katika wodi aliyolazwa katika Hospitali ya
Wilaya ya Geita, mwanafunzi huyo ambaye ni mkazi wa Kijiji cha
Gengetano, Kata ya Nyakamwaga, alisema alikutwa na mkasa huo Juni 17,
mwaka huu, usiku wakati akinywa uji kijijini hapo.
Alisema
mwanamume huyo alimvamia katika kijiwe hicho cha uji na kuanza
kumshambulia kwa mapanga sehemu za kichwani, mgongoni na begani, kabla
ya kumkata mapanga katika mkono wake wa kushoto na kupelekea kiganja cha
mkono wake huo kunyofoka, akimtuhumu kutembea na mkewe, Mama Neema na
kumuachia maumivu makali.
“Wakati nakunywa uji kwenye kijiwe
hicho mara alitokea huyo jamaa na kumuuliza muuzaji wa uji (Mektirida)
kama kuna huduma hiyo, alijibiwa vizuri kwamba uji upo na ndipo baadaye
nilimuona anachomoa panga kiunoni mwake na kuanza kunikata kwa kunilenga
shingoni.
“Nilikwepa lakini bahati mbaya lilitua kisogoni na
kunijeruhi na ndipo nilipoamua kukimbia, lakini sikufika mbali kwani
nilidondoka chini, akanifuata na kunikata panga jingine la pili
kichwani, sikukata tamaa nilinyanyuka tena na kukimbia huku damu
zikiendelea kuvuja, nikadondoka tena kwa mara nyingine akakata jingine
la tatu nikajikongoja na kunyanyuka nikakimbia huku nikikinga shingo
asinichinje.
“Lakini kwa kuwa jamaa alivyoonekana alikuwa na
lengo la kuniuwa hakukata tamaa alizidi kunikimbiza na baada ya kuanguka
chini kwa mara nyingine tena alinifuata nilipokuwa nimeangukia na
kuanza kukata mkono wangu wa kushoto.
“Alikata panga la kwanza,
la pili, la tatu na la nne lilipelekea kiganja kunyofoka na ndipo rafiki
yangu mmoja aitwaye Fikiri William, ninayesoma naye kidato cha tatu
alipofika kunisaidia na ndipo mwanamume huyo alipoogopa kukamatwa na
kuamua kukimbia kusikojulikana,” alisema Mtasimwa.
Alisema
kutokana na majeraha hayo alipoteza fahamu na alizinduka akiwa wodini na
hakumbuki ni akina nani waliompa msaada wa kumwahisha hospitalini.
Alisema
siku moja kabla ya tukio hilo alikutana na mwanamume huyo njiani na kwa
kuwa alikuwa akimheshimu kama kaka yake, alimsalimia lakini aligoma
kuitikia salamu yake zaidi ya kumpa vitisho.
“Nakumbuka siku moja
kabla ya tukio nilikutana naye nilipomsalimia alinijibu wewe kijana
unadharau sana wala sihitaji salamu yako, ila kaa ukijua maisha yako ni
mafupi sana na utakufa kifo kibaya,” alisema Mtasemwa.
Alisema
kutokana na majibu ya mtuhumiwa alipojaribu kuhoji kulikoni ajibiwe
hivyo, alidai hakupata ufafanuzi wowote na mwanamume huyo aliondoka
akimuacha na maswali mengi kichwani mwake yasiyokuwa na majibu na siku
ya tukio ndipo alijua maneno aliyomwambia siku moja kabla hayakuwa ni
utani.
Alisema kutokana na hali duni ya kipato cha wazazi wake
anajishughulisha pia na upigaji picha, kwa ajili ya kupata mahitaji
muhimu ya shule na familia yake na kati ya wateja wake wakubwa mke wa
mtuhumiwa naye alikuwa miongoni mwa watu hao na anadhani inaweza kuwa
sababu ya kuhisiwa kutokana na kumpiga picha mwanamke huyo.
“Unajua
sisi ni masikini wa kipato na ninaishi na mama baada ya kutengana na
baba na ninajishughulisha na kupiga picha mtaani baada ya muda wa masomo
na mke wa jamaa aliyenifanyiwa unyama huo alikuwa ni mteja wangu, naona
ndiyo sababu mwanaume huyo alihisi natembea naye japokuwa sina tabia
hiyo na nilikuwa namheshimu kama dada yangu,” alisema Mtasimwa.
Kaimu
Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk. Ndallo Ndallo, alithibitisha kuwapo
kwa majeruhi huyo katika hospitali hiyo, aliyelazwa wodi namba nane na
kuongeza kuwa hali yake ni mbaya kutokana na majeraha aliyoyapata sehemu
mbalimbali za mwili wake na juhudi za kuokoa maisha ya mwanafunzi huyo
zinaendelea.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Leonard Paulo,
alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo na juhudi za kumsaka mtuhumiwa huyo
zinaendelea baada ya kutoroka na kukimbilia kusikojulikana.
Alisema
mke wa mtuhumiwa pia alitoroka baada ya kupatiwa taarifa na majirani
zake kuwa mumewe huyo amepanga kumchinja baada ya kutoka kumjeruhi
kijana huyo.
Chanzo: Mtanzania
Thursday, June 21, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment