MKUU wa Shule Msaidizi katika Sekondari ya Ndedo wilayani Kiteto
mkoani Manyara, amejeruhiwa vibaya baada ya kupigwa marungu na kuchapwa
mwilini mwake na vijana wa jamii ya kifugaji wa Kimasai maarufu Morani.
Akizungumza juzi na waandishi wa habari nyumbani kwake baada ya
kutoka hospitali ya Wilaya ya Kiteto, Mwalimu huyo, Hassan Didii alidai
alipigwa na vijana hao wiki iliyopita baada ya kutoa adhabu ya kumchapa
viboko mwanafunzi mmoja wa kidato cha pili wa shule hiyo.
Alidai kuwa morani hao walimchapa viboko na kumpiga rungu usoni,
mgongoni na mikononi na kumuachia maumivu mwilini mwake baada ya
mwanafunzi huyo kwenda kushtaki nyumbani kwao kuwa alichapwa.
Mwalimu Didii alidai hadi hivi sasa hali yake si nzuri kwani
anajisikia maumivu mwilini mwake kutokana na majeraha aliyoyapata baada
ya kupigwa na kundi la vijana hao wa jamii ya Kimasai.
Pia alilalamikia kitendo cha vijana hao kutochukuliwa hatua yoyote
japokuwa alishatoa taarifa kwenye Kituo cha Polisi cha Mjini Kibaya.
Mganga wa zamu wa Hospitali ya Wilaya ya Kiteto ambaye hakutaka
kutajwa jina lake gazetini kwa kuwa si msemaji, alithibitisha kumpokea
Mwalimu Didii akiwa na majeraha ya kupigwa na walimpatia matibabu na
kuongeza kuwa hivi sasa hali yake inaendelea vizuri.
Askari Polisi anayeshikilia jalada la kesi hiyo ambaye pia hakutaka
kutajwa jina lake gazetini, alithibitisha kwamba Mwalimu Didii alishatoa
taarifa kwenye kituo hicho na hivi sasa wanajipanga kwenda eneo la
Ndedo kwa kuwa kuna umbali mrefu kutoka Kibaya hadi eneo hilo.
Adhabu hiyo inafanana na aliyowahi kuitoa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba,
Albert Mnali ambaye Februari mwaka 2009, aliacha maswali miongoni mwa
walimu baada ya kufanya ziara ya kushitukiza katika shule tatu za msingi
za kata ya Katerero na kuamuru walimu 16 kucharazwa viboko kwa kile
alichodai ni utoro na uchelewaji wao.
Mnali baada ya kuagiza adhabu hiyo, alikiri kuisimamia ifanyike kwa
kuwa walimu hao ni wazembe waliochangia wilaya yake kuibuka na matokeo
mabaya katika mtihani wa darasa la saba mwaka jana.
“Nilimwita askari wangu nikamwambia Mwalimu Mkuu atoke, tukafunga
mlango nikawaambia walimu kama watoto wanaochelewa mnawapa adhabu na
mimi nawapa adhabu,” alisema Mnali kuthibitisha kucharazwa viboko vinne
kila mmoja.
Alipoulizwa kama adhabu hiyo haikuwa udhalilishaji wa walimu, alikana
na kusema haikutolewa mbele ya wanafunzi na kwamba yeye si mtu wa
kwanza kutoa adhabu ya aina hiyo aliyoiita kuwa ndogo.
Mbali na kutoa ufafanuzi huo, alisema tayari amemwandikia Mkurugenzi
juu ya adhabu hiyo akiambatanisha na majina ya walimu walioadhibiwa na
kusema inabidi wachukuliwe hatua zaidi kwa vitendo vyao vya uzembe na
utoro shuleni. Baada ya tukio hilo, Rais Jakaya Kikwete alimfukuza kazi
Mnali kwa kitendo hicho.
Source: Habarileo
Monday, June 18, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment