I. UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
kwa niaba ya Kambi ya Upinzani, ninatoa maoni ya Kambi ya Upinzani
kuhusu Bajeti ya Nchi ya mwaka wa fedha 2012/2013 kwa mujibu wa Kanuni
za Bunge Kifungu cha 99(7) toleo la Mwaka 2007.
Mheshimiwa Spika, Natoa
pongezi za dhati kabisa kwa Ndugu William Augustao Mgimwa, Mbunge wa
Jimbo la Kalenga mkoani Iringa kwa kuteuliwa na Rais kuwa Waziri wa
Fedha na Uchumi. Vile vile nawapongeza Ndugu Saada Mkuya na Ndugu Janeth
Mbene kwa kuteuliwa kwao kuwa Wabunge na baadaye kuwa Manaibu Mawaziri
katika Wizara hii nyeti sana. Ninawapa pole pia maana Wizara ya Fedha
sio Wizara lelemama. Kambi ya Upinzani itaendelea kuisimamia Wizara hii
kwa ukaribu sana kama ilivyofanya katika kipindi cha miaka miwili
iliyopita. Mtakapofanya vizuri tutawapongeza ili muongeze juhudi,
mtakapoharibu tutawawajibisha.
Mheshimiwa Spika, Ni
dhahiri kwamba Mwaka wa Fedha uliopita ulikuwa mwaka mgumu sana kwa
Watanzania. Ni mwaka ambao gharama za maisha zilipanda kwa kasi kubwa
sana na
juhudi za Serikali kuwakwamua wananchi na hasa wananchi wanyonge kutoka
kwenye lindi la ufukara ziligonga mwamba. Kambi ya Upinzani inawapa
pole Watanzania kwani hili ndilo walilochagua. Muhimu ni kuvumilia mpaka
uchaguzi ujao na kufanya mabadiliko ya Serikali ili kuweka Serikali
itakayoongozwa na CHADEMA na itakayoweza kukabili changamoto za sasa na
za baadaye.
Mheshimiwa Spika, naomba tufanye mapitio kidogo ya Bajeti inayomaliza muda wake.
- UTEKELEZAJI WA BAJETI ILIYOPITA
Mheshimiwa Spika,
kabla ya kutoa bajeti mbadala ya Kambi ya Upinzani ni vema kufanya
tathmini ya utekelezaji wa bajeti ya Serikali iliyopita ili kuona ni kwa
namna gani Serikali inathamini fedha za walipa kodi, na dhamira yake ya
kuleta maendeleo ya kiuchumi katika Taifa. Katika kufanya hivyo,
tutapitia baadhi ya maeneo ambayo Kambi ya Upinzani tunaona kuwa
hayakutekelezwa katika bajeti iliyopita.
Kupunguza Makali ya Maisha
Mheshimiwa Spika,
Katika Bajeti ya mwaka 2011/12 Serikali ilitangaza nia yake ya
kupunguza makali ya maisha. Hatua mbali mbali zilichukuliwa ikiwamo
kupunguza kodi na tozo kwenye mafuta ya Dizeli na Petroli, kuanza
kutekeleza mpango wa dharura wa umeme na kutoa fedha za kununua chakula
kwa Wakala wa Chakula. Serikali
ilitumia shilingi bilioni 296 na dola za Marekani milioni 183 kwenye
Umeme. Vilevile Serikali ilitumia shilingi bilioni 27 kununua Mahindi na
kusambaza kwenye masoko.
Mheshimiwa Spika, licha
ya hatua hizo zilizochukuliwa Mfumuko wa Bei uliongezeka maradufu
kutoka wastani wa asilimia 6.3 mwaka 2010/11 mpaka wastani wa asilimia
17.8 mwaka 2011/12. Serikali imefeli katika lengo lake la kupunguza
makali ya maisha kwa wananchi. Sio tu kwamba Serikali imeshindwa
kudhibiti upandaji holela wa gharama za maisha bali pia hatua za
Serikali zimeongeza kasi ya kupanda kwa makali ya maisha.
Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani Bungeni katika Hotuba yake mbadala ya mwaka 2011/12
iliitaka Serikali kushughulikia msingi wa mfumuko wa Bei hapa nchini
ambao ni uzalishaji mdogo wa mazao ya chakula. Tumeelezwa na Waziri
Kivuli wa Mipango na Uchumi kwamba Chakula peke yake ni asilimia 48 ya
kapu la bidhaa na huduma ambazo mwanachi anatumia. Mfumuko wa Bei ya
Chakula kinacholiwa nyumbani na kwenye migahawa ilikuwa asilimia 25
mwezi Aprili 2012 (BoT monthly Economic Review, May 2012). Vile vile
mfumuko wa bei wa nishati inayotumika nyumbani na mafuta ya Dizeli na
Petroli ulifikia asilimia 25 pia mwezi Mei mwaka 2012. Ni dhahiri kwamba
iwapo tutadhibiti mfumuko wa bei ya chakula tutaweza kushusha mfumuko
wa bei kurudi kwenye tarakimu moja.
Endelea kusoma hotuba hii......
Chanzo: Matukio - Michuzi
No comments:
Post a Comment