Wednesday, June 27, 2012

Lowassa, Zitto wamtega JK

Best Blogger Tips
 NAIBU Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Zitto Kabwe, ameitaka serikali ya Rais Jakaya Kikwete kuwachunguza na kuwachukulia hatua zikiwemo kuwataja, kuwashtaki na kuwafilisi mafisadi wanaodaiwa kupora fedha za miradi ya gesi, madini na petroli na kuzihifadhi kwenye akaunti nchini Uswisi.

Aliyasema hayo bungeni jana wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na kuongeza kuwa kuna wizi wa fedha za serikali zaidi ya sh bilioni 300 ambazo baadhi ya watumishi wa serikali wamepewa kama hongo na wawekezaji wa sekta hiyo.

Wakati Zitto akisema hayo, Waziri Mkuu wa zamani ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ulinzi, Mambo ya Nje na Usalama, Edward Lowassa, ameitaka serikali kutolea maelezo madai ya kufichwa kwa shilingi bilioni 300 katika benki mbali mbali nchini Uswisi ambazo zinadaiwa kuwekwa na wanasiasa na watu wa kada mbalimbali nchini.

Akizungumza Bungeni jana Zitto aliitaka Ofisi ya Waziri Mkuu, vyombo vya usalama na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) kuchunguza na kuchukua hatua mara moja.

Zitto aliitaka serikali kuiga mfano wa India ambayo ilipata mkasa kama huo na kuwataja watuhumiwa, kuwachunguza na kuzirudisha serikalini pesa zilizoonekana kuwa zilipatikana kinyume cha sheria.

Alitaka serikali ihakikishe kuwa watuhumiwa hao wanatajwa, wanachukuliwa hatua na pesa zinarudishwa nchini huku akionya kuwa inashangaza hata kabla ya miradi kuanza watu wameanza ufisadi na kupora mali za umma.

Gazeti la The Guardian la Jumamosi iliyopita lilichapisha taarifa za ufisadi huo uliofanywa na Watanzania sita waliopokea hongo kutoka makampuni yanayotafiti gesi, madini na petroli na kuweka pesa zao Uswisi.

Kwa upande wake Lowassa alitoa kauli hiyo jana wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari waliotaka kujua msimamo wa kamati ya ulinzi na usalama juu ya kuwepo kwa fedha hizo katika mabenki hayo ya Uswisi huku Watanzania wakiendelea kutaabika kwa mfumko mkubwa wa bei.

Akizungumzia kuhusu hilo, Lowassa ambaye hakutaka kuzungumzia kwa kirefu alisema hata wao kama kamati wamesoma taarifa hizo kwenye magazeti na kwamba wenye majibu mazuri kuhusiana na suala hilo ni serikali.

Hoja ya Zitto
Aidha Zitto katika hoja yake hiyo pia akizungumzia mjadala wa mafuta na gesi alishauri suala hilo lisiwe la Muungano kila upande uachiwe jukumu la kutafuta na kuchimba nishati hizo.
“Kila upande wa Muungano ushughulikie gesi na mafuta yake hakuna sababu ya kuchelewesha suala hili,” alisema.

Akiunga mkono hatua hiyo mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Kessy, aliitaka serikali kutoa maelezo ya hatua zilizochukuliwa dhidi ya Watanzania walioingia mikataba ya rada.

Alisema Waingereza waliwashtaki watuhumiwa wake na kurudisha fedha ya rada kwa Tanzania na kuhoji serikali nayo imefanya nini kwa watuhumiwa walioingia mikataba mibovu ya rada humu nchini?
Alitaka waliofilisi mashirika ya umma kama Shirika la Ndege –ATC, Reli na Bandari wakamatwe, washtakiwe, kufilisiwa na kunyongwa hata kama walifanya hivyo miaka 20 iliyopita.

Aliliambia Bunge kuwa hata kama walioua mashirika wamekufa pingu zipelekwe kwenye makaburi yao na kusisitiza kuwa dawa ya walioua mashiriki ya umma ni kuuawa.

Alipendekeza wauliwe kwani wamewaua Watanzania kwa kuwaibia stahili zao kama dawa zilizokuwa ziwatibu na kusababisha vifo vyao.

Aliongeza kuwa sheria za Tanzania ni mbaya kwani zinawalinda wezi na kuwatetea mafisadi na kuiponda serikali kuwa ina masikio lakini haisikii ina pua lakini hainusi.
Aliishangaa miradi ya usafiri jijini Dar es Salaam iliyotangazwa na Waziri wa Ujenzi Dk. John Magufuli ya kujenga vituo saba vya usafiri wa boti kutoka Bagamoyo hadi Feri na kusema huo ni ubadhirifu wa fedha za umma.

Aliitaka serikali kuwashughulikia watuhumiwa wanaodaiwa kuhifadhi fedha za rushwa ya gesi na petroli kwenye benki za Uswisi na yenyewe kukaa kimya.
Aliongeza kuwa Takukuru imeshindwa kazi na inashangaza kuona kuwa inawaambia wananchi wawaletee majina ya wala rushwa wakati wanawajua na watu wanaiba fedha za umma na kujenga maghorofa na kumiliki mali za wizi.

Alisema maofisa wa Takukuru wanawachuuza wananchi wanaowapa majina ya wala rushwa kwa kutoa taarifa kwa watuhumiwa waliotajwa kisha kuwaomba rushwa.
Alikataa kuunga mkono bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa maelezo kuwa inaifanya mikoa mingine kuwa peponi na mingine kuwa motoni.

Nacho Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kupitia taarifa yake kilirudia kutoa wito kwa Rais Kikwete kutumia mamlaka yake ya kikatiba kuagiza kukamatwa kwa watuhumiwa wote wa ufisadi wa rada ambao iliwataja kwa nyakati mbalimbali ikiwemo katika orodha ya mafisadi (list of shame) Septemba 15 2007 katika Uwanja wa Mwembeyanga.

Katika taarifa iliyotolewa kwenye vyombo vya habari na kusainiwa na Mkurugenzi wa Mambo ya Habari wa CHADEMA, John Mnyika, alisema kutokana na sheria za usiri za Uswisi, wanaitaka serikali inayoongozwa na CCM kuwasiliana na serikali ya nchi hiyo ili kuanza mchakato wa kuwezesha mahakama za nchi hiyo kutoa ruhusa kutolewa kwa taarifa zote kuhusu wenye akaunti hizo na makampuni yaliyoweka kiasi hicho cha fedha ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa kwa mujibu wa Sheria za Tanzania na Sheria za Kimataifa.

“CHADEMA inatambua kwamba kuachwa kwa mafisadi bila kuchukuliwa hatua kamili za kisheria na mali zao kufilisiwa kunafanya taifa kuendelea na ufisadi ikiwemo ule wa Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), Richmond na sasa tuhuma mpya za ufisadi kwamba kuna vigogo wenye kiasi cha bilioni 303 kwenye akaunti Uswisi ambazo zinadaiwa kuwekwa na makampuni ya madini, mafuta na gesi asili,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha chama hicho kimekumbusha kuwa katika orodha yake ya mafisadi iliwataja pia kwa majina viongozi wa serikali ambao waliingia mikataba ya kifisadi ya madini na rasilimali nyingine za taifa kutolewa kwa taarifa hizo za benki za nje kutathibitisha ukweli na pia kubainisha watuhumiwa wengine zaidi.

Pamoja na hilo imeitaka serikali inayoongozwa na CCM kuzingatia mpango kati yake na serikali ya Uingereza kupanga matumizi ya fedha kiasi cha shilingi bilioni 72.3 za rada zilizorejeshwa baada ya kubainika zilizochotwa kifisadi na kampuni ya BAE Systems ya Uingereza.

Wakati huohuo, CHADEMA imeshangazwa na uamuzi wa serikali inayoongozwa na CCM kubadilisha mpango wa kujenga nyumba za walimu kinyume na mpango huo wakati huu ambapo serikali iko katika mgogoro na walimu kutokana na kutowatimizia madai yao ya msingi ikiwemo nyongeza ya mishahara, kulipa madeni na kupunguza kodi kwenye mishahara.

Chama hicho kimeitaka serikali kukumbuka kwamba mpango huo ulikuwa moja ya ushahidi muhimu uliotolewa mahakamani kumshawishi jaji kutoa uamuzi wa kuridhia makubaliano kati ya SFO na BAE kwamba fedha hizo zingetumika kununua vitabu 4.4 milioni kwa ajili ya wanafunzi, vitabu 192,000 Kwa ajili ya walimu kufundishia, madawati 200,000, kujenga nyumba 1,196 za walimu wa shule za msingi vijijini, kujenga vyoo 200,000 kwenye shule za msingi.

Kadhalika imeonyesha kuguswa na taarifa kwamba zabuni ya kuchapa vitabu hivyo imetolewa kwa kampuni ya Kiingereza ya Oxford University Press hali ambayo itafanya sehemu kubwa ya fedha hizo kurejea hukohuko Uingereza.
Chanzo: Tanzania Daima

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits