Wednesday, June 20, 2012

Mbunge CCM ajilipua

Best Blogger Tips
 KATIKA kile kinachoweza kutafsiriwa kama ujasiri wa kujitoa kafara, Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina (CCM), ameungana na wabunge wa kambi ya upinzani kuipinga bajeti ya serilaki ya mwaka 2012/2013 iliyowasilishwa bungeni Alhamisi ya wiki iliyopita.

Tofauti na wabunge wengine wa chama hicho tawala, wanaochangia mjadala wa bajeti hiyo kwa kutumia muda mwingi kuisifu bajeti hiyo na kuporomosha kejeli kwa ile ya wapinzani, Mpina kama alivyokuwa ametahadharisha hapo awali, jana hakuuma maneno.

Akichangia mjadala huo kwa kujiamini, aliwataka wabunge wenzake kumsaidia Rais Jakaya Kikwete, kuiondoa bajeti hiyo bungeni ili iweze kufanyiwa marekebisho katika maeneo mbalimbali ambayo hayako sawa.

Alisema kuwa hakubaliani na bajeti hiyo kwa sababu fedha zilizotengwa kwenye bajeti iliyopitishwa na Bunge mwaka jana hazikupelekwa zilikokusudiwa, na hivyo kusisitiza kwamba hatakuwa tayari kuiunga mkono, hadi hapo serikali itakapoleta maelezo kuhusiana na fedha hizo ili Bunge lijiridhishe kama hazikwenda kwenye maeneo waliyoyaidhinisha ijulikane zimekwenda wapi na kwa idhini ya nani.

“Matumizi yanayozungumzwa hapa, asilimia 87 hayahusiani na matumizi yalivyo katika fedha zinazopelekwa katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya miradi,” alisema.

Mbunge huyo ambaye alikuwa akishangiliwa na wabunge wa upinzani, huku wenzake wa CCM wakimwangalia kwa utulivu na wengine wakinong’ona, alidai sababu nyingine inayomfanya akatae bajeti hiyo, ni kitendo cha Bunge kuanza kujadili bajeti mpya wakati hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mwaka wa 209/2010 hazijajibiwa.

Alisema kwa kufanya hivyo serikali imevunja sheria ya nchi kifungu cha 40 ya kulitendea haki Bunge hilo kwani zilipaswa kujadiliwa kabla ya kuleta bajeti mpya ili Bunge hilo lijiridhishe.

Aidha, alisema serikali imevunja sheria ya ukaguzi ya mwaka 2008 kifungu cha 40 1-3 ya kulitendea haki Bunge hilo ili lijadili na kujiridhisha kama matumizi ya fedha za Watanzania zimefanya kazi iliyokusudiwa.
Mpina aliongeza kuwa, Bunge linatakiwa lijiridhishe na kuona kama kuna malalamiko ili liweze kuyajibu kabla ya kupeleka fedha nyingine.

“Si halali hata kidogo Bunge kuanza kujadili bajeti mpya wakati haya yote hayajatekelezwa, kwani kwa kufanya hivyo serikali imevunja sheria hiyo, na ilipaswa kupelekwa mahakamani kwani sheria ziko wazi kwa watu wanaovunja sheria,” alisema.

Akizungumzia matarajio ya Watanzania, Mpina alisema bajeti iliyowasilishwa si sahihi kwa kuwa imekiuka mpango wa maendeleo wa miaka mitano uliopitishwa na Bunge Juni 2011.

Mpina pia alisema bajeti hiyo imekinzana na azimio la Bunge na makubaliano ya kutenga sh trilioni 2.7 katika bajeti kila mwaka wa fedha ili zipelekwe katika miradi ya maendeleo, na asilimia 35 ya fedha za ndani zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zisitumike kwa matumizi mengine yoyote.

Alisema kwa kufanya hivyo, serikali imekiuka azimio la Bunge kwa sababu haikuzingatia hayo yote, ambapo badala ya kutenga sh trilioni 2.7 katika miradi ya maendeleo, imetenga sh trilioni 2.2 sawa na asilimia 30.

Mpina alisema wakati mapato yakiongezeka, matumizi yamepanda huku miradi ya maendeleo ikipunguziwa fedha kwani matumizi ya kawaida yamepangiwa sh trilioni 3.6.

Alisema wakati Watanzania wakisubiri ongezeko la utoaji wa huduma, serikali imekuwa ikienda kinyume na matarajio yao.

Alilitaka Bunge kumsaidia rais ikiwa amekosa watu wa kumsaidia na kuikataa bajeti ya sasa, kwa kuwa haina tija kwa wananchi.

Alisema kutokana na utekelezaji dhaifu wa mipango ya maendeleo, imewafanya Watanzania wengi kuondoa imani na serikali yao.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Mpina alisema ameamua kusimama katika ukweli na kuachana na ushabiki wa vyama, kwa manufaa ya Watanzania, akidai kuwa yuko tayari kuchukiwa na chama chake.

Spika awasuta wabunge
Katika hatua nyingine, Spika wa Bunge, Anne Makinda amewacharukia wabunge na kuwataka kujadili bajeti badala ya kuendeleza malumbano, kutoleana lugha za matusi na kuoneshana ufundi wa siasa bungeni.
Alisema kuwa hatua hiyo inawafanya wabunge kujiharibia wenyewe kwani wapiga kura wao wamekuwa wakiwaangalia muda wote na kumpigia simu, wakieleza kushangazwa na vitendo hivyo vya aibu wanavyovifanya.

Makinda alilazimika kutoa angalizo hilo kutokana na hatua ya wabunge kuendeleza malumbano ya vyama badala ya kujikita kwenye mjadala husika.

“Wabunge rudisheni heshima ya Bunge hili, kwani imepotea kabisa… acheni malumbano, jadilini mambo ya msingi ambayo yatasaidia kuboresha bajeti ili iweze kuwasaidia wananchi,” alisisitiza Spika Makinda.

Juzi, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, alimtoa nje ya ukumbi wa Bunge mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), kwa madai kuwa alikiuka kanuni za Bunge kwa kutoa lugha isiyo ya staha, uamuzi uliopingwa na wapinzani wakisema wabunge wa CCM wanatukana pasipo kuchukuliwa hatua.

Makinda aliwataka wabunge kuheshimu kanuni, sheria na taratibu za Bunge hilo na kuacha kutumia lugha chafu na za matusi ili kurejesha heshima kama ilivyokuwa zamani.

“Mnatakiwa kutambua kuwa kila mbunge anayesimama hapa, wananchi wake wanamwangalia, hivyo mna kila sababu ya kujikita katika kujadili bajeti na si vinginevyo,” alisema.
Chanzo: Tanzania Daima

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits