WIMBI la viongozi na makada wa CCM kuhamia vyama vya upinzani
linaendelea kukitikisa chama hicho, baada ya viongozi wa chama hicho
mikoa ya Iringa na Singida kujiunga Chadema.Chadema kimewateka makada
hao kilipofanya mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Kihesa Sokoni,
juzi mjini Iringa kwa lengo la kuendeleza mkakati wake wa Movement For
Change-M4C (Vuguvugu la Mabadiliko) na kufafanua bajeti ya Serikali ya
mwaka 2012/13.
Wimbi la makada wa CCM kuhamia Chadema lilipamba
moto Aprili mwaka huu baada ya Ole Millya kuondoka akifutiwa na viongozi
kadhaa wa chama hicho, akiwamo Katibu wa Uhamasishaji wa UVCCM Wilaya
ya Longido, wenyeviti watano wa vitongoji na wanachama 2,402 wa CCM
wilayani Ngorongoro.
Viongozi wa CCM waliojiunga Chadema jana, ni
Katibu Mwenezi wa chama hicho Wilaya ya Iringa Vijijini, Yohana Mwena na
Mjumbe wa Baraza la Utekelezaji la Umoja wa Vijana (UVCCM) wilayani
humo.
Wengine ni Katibu wa UV-CCM Mkoa wa Singida anayesoma
katika Chuo Kikuu cha Ruaha (Ruco) kilichopo Iringa, Kasifia Sumpta,
mwanazuoni wa chuo hicho, Dk Matabazi Lugazia, na kada wa siku nyingi wa
chama hicho, Zuberi Mwachura ambaye alirejesha kadi sita za CCM kutoka
katika familia yake.
Licha ya Chadema kupewa kibali cha kufanyia
mkutano huo kwenye uwanja mdogo uliozungukwa na barabara zenye magari
mengi, umati wa watu ulifurika, huku wengine wakilazimika kukaa juu ya
nyumba na miti.
Katika mkutano huo ambao ulihutubiwa na Naibu
Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe, Mwenyekiti wa zamani wa UVCCM,
Mkoa wa Arusha, James ole Millya na Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema),
Mchungaji Peter Msigwa, wanachama wengine zaidi ya 200 wa CCM
walirudisha kadi na kujiunga na Chadema.
Mbali na shughuli ya
kupokea wanachama hao kwa mtindo wa ‘kuvua gamba na kuvaa gwanda’,
viongozi wa Chadema waliichambua bajeti ya Serikali inayoanza kujadiliwa
bungeni leo, wakifafanua ni kwa jinsi gani haitamnufaisha mwananchi wa
kawaida.
Waliovua gamba
Wakizungumza wakati
wakirudisha kadi hizo, makada na viongozi hao walisema kuwa, wameamua
kufanya hivyo baada ya kuchoshwa na sera za CCM, ambazo walidai kuwa
hazitekelezeki.
Akizungumzia kuhama kwake CCM, Mwena alisema amechoka
kuona rasilimali za taifa haziwanufaishi wananchi, badala yake
zinawanufaisha matajiri, huku kukiwa na tofauti kubwa ya kipato.
“Mwenzenu
nimevumilia nimeshindwa, leo nimeamua kuondoka CCM, nimechoka kuona
sera ambazo hazitekelezeki, huku wananchi maskini wakiendelea kuwa
maskini wa kutupwa wakati kuna rasilimali nyingi za taifa zinazoliwa na
matajiri,” alisema Mwena.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na
maelfu ya wakazi Mji wa Iringa na vitongoji vyake, baadhi ya waliopewa
nafasi kueleza kero zao walisema, hawaikubali bajeti iliyosomwa hivi
karibuni kwa kuwa haijalenga kuwasaidia wananchi maskini.
“Bajeti
iliyosomwa inataja kupandisha kodi ya pombe na sigara, ikimaanisha kuwa
uchumi wetu unategemea vilevi hivyo, hivi Watanzania tukigoma kunywa
pombe ina maana Serikali itashindwa kujiendesha, bajeti iliyosomwa
tunaikataa na tunawaagiza mkawaeleze, kuwa hiyo imelenga kuwaneemesha
wao na siyo sisi maskini,” alisema Yohana Mkule, mkazi wa manispaa hiyo.
Kutokana
na wananchi wengi, kuigomea bajeti hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema,
Zitto Kabwe aliwaunga mkono, huku akiahidi kuwa Kambi ya Upinzani
haitakubali bajeti hiyo ipitishwe.
“Uwendawazimu ni kufanya jambo
lilelile, kwa njia zilezile huku ukitegemea matokeo tofauti. Serikali
inatumia njia zilezile ikidhani mfumko wa bei unaweza kupungua, huu ni
uwendawazimu, nawatoa hofu kwa sababu hatutakubali bajeti hii
ipitishwe,” alisema Kabwe.
Alisema vitu vinavyofanya maisha ya
Watanzania kuwa magumu ni mfumko wa bei, hasa katika vyakula ambao ni
asilimia 25, na nishati ambayo ni asilimia 27, huku Serikali ikishindwa
kudhibiti hali hiyo kwa kuandaa bajeti inayolenga kukomoa wananchi.
Hata
hivyo, aliwataka wakazi wa Iringa kuendelea kuwa wavumilivu wakati
mbunge wao atakapokuwa akifanya kazi za kuleta mabadiliko katika maeneo
mengine, ili kukiandaa chama hicho kushika dola mwaka 2015.
Mwenyekiti
wa zamani wa UVCCM Mkoa wa Arusha, James Millya aliwataka wakazi wa
Manispaa ya Iringa kutoendelea kuivumilia CCM ambayo imeshindwa kutambua
kitu gani wananchi wake wanataka.
“Mimi niliondoka baada ya
kuona hoja zangu hazifanyiwi kazi ndani ya CCM, nimeingia Chadema
nikitarajia mabadiliko makubwa kwa nchi yangu, msikubali kuumia, lazima
tulete mabadiliko,” alisema.
Millya alisema nchi nyingi ikiwamo
Kenya zimeving’oa vyama tawala, isipokuwa Tanzania ambayo katika
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 lengo hilo litatimia.
Mbunge wa
Iringa Mjini, Msigwa alisema viongozi wa Chadema wameamua kugawana siku
za mwisho wa wiki kufanya kazi za chama hicho kutokana na mkutano wa
Bunge unaoendelea katika siku za kawaida.
Chanzo: Mwananchi
Monday, June 18, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment