Wednesday, December 28, 2011

Korea Kaskazini yafanya maziko ya Kim Jong - Il

Best Blogger Tips
Korea Kaskazini inafanya maziko ya kitaifa ya kiongozi wake Kim Jong-il huku msafara mkubwa wa magari yaliyosindikiza jeneza la kiongozi huyo ukipitia mji mkuu Pyongyang.

Picha cha runinga zimeonyesha maelfu ya wanajeshi wakitoa heshima za mwisho kwa picha ya kiongozi huyo iliyopitia kwenye barabara za mji.

Mridhi wa uwongozi ambaye ni mwanawe wa kiume Kim Jong-Un amezindikisha jeneza la babake lililokuwa juu la gari maalum. Kim Jong-il alifariki dunia Decemba 17 baada ya kupatwa na mshtuko wa moyo akiwa na miaka 69.

Hakuna viongozi wa nje walioalikwa wala waandishi wa habari wa kimataifa. Wadadisi wanasema mazishi ya leo ni sambamba na ya mwasisi wa nchi hiyo Kim IL-Sung mwaka 1994 yalioandamana na gwaride kubwa ya kijeshi.

Kiongozi mtarajiwa Kim Jon-Un ameandamana na mjombake Chang Song-taek anayetarajiwa kuwa na ushawishi mkubwa katika uwongozi mpya pia mkuu wa jeshi Ri Yong-ho, alionekana kando ya jeneza la Kim Jong-Il.

Kabla ya kufariki kiongozi wa Korea Kaskazini alikuwa katika mchakato wa kumtayarisha mwanawe Kim Jong-Un kuchukua hatamu za uwongozi. Kifo chake cha ghafla cha Kim Jong Il kimepelekea hofu ya kuzuka mzozo wa uwongozi katika taifa hilo lenye msingi wa ujamaa.
Chanzo: BBC

Tuesday, December 27, 2011

Hali ya Hewa: Mafuriko makubwa yanakuja Dar

Best Blogger Tips
Eneo la Jangwani likiwa limezingirwa na maji
Yasema alhamisi hadi Jumamosi kuwa siku mbaya zaidi, pia kuyakumba maeneo mengine nchini. 

 MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imetoa tahadhari ya kuendelea kunyesha mvua kubwa zaidi katika siku 10 zijazo, huku ikizitaja Alhamisi hadi Jumamosi kuwa ni siku za mafuriko mengine makubwa zaidi katika jiji la Dar es Salaam.

Wakati TMA ikitoa tahadhari hiyo, Shirika la Reli Tanzania (TRL), limesitisha safari za treni ya abiria kwa muda usiojulikana kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma, kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali ya nchi.

Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Agnes Kijazi alisema jana katika taarifa yake kuwa kutokana na mvua hizo, ni vyema tahadhari zote zikachukuliwa mapema ili kuepuka maafa zaidi.

“Wale wananchi ambao wanaishi mabondeni na waliokumbwa na mafuriko, wahame kutokana na mvua zinazoanza kunyesha Desemba 27 (jana), hadi Desemba 31 mwaka huu, kwani zitaleta madhara makubwa kwa wanaoishi mabondeni na sehemu nyingine mbalimbali,” alisema Dk Kijazi.

Alisema kwamba ukanda wa mvua unatarajia kuimarika maeneo mengi nchini na mvua zinatarajiwa kuanza kwenye ukanda wa pwani, ikiwemo Mkoa wa Dar es Salaam na kuongezeka kuelekea mwaka mpya wa 2012.

Dk Kijazi alisema mifumo ya hali ya hewa inaonyesha kuimarika kwa hali ya joto katika Bahari ya Hindi na kuongezeka kwa msukumo wa hewa yenye unyevunyevu kutoka misitu ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC).

Alisema hali hiyo imesababisha makutano ya upepo katika eneo la Mashariki na Kusini Magharibi mwa nchi, kuanzia leo kuelekea mwaka mpya... “Hali hii inatarajia kusababisha kuanza kwa vipindi vya mvua kubwa katika maeneo mengi hapa nchini.”

Alisema maeneo ya mikoa ya ukanda wa Pwani (Dar es Salaam, Pwani, Mtwara, Lindi na Unguja), yanatarajiwa kuwa na vipindi vya mvua kubwa.

Dk Kijazi aliyataja maeneo mengine kuwa ni ya Nyanda za Juu Kusini Magharibi ambayo ni Mikoa ya Mbeya, Iringa na Rukwa na Kanda ya Kati katika Mikoa ya Dodoma na Singida.

“Kwa upande wa Magharibi mwa nchi, Mikoa ya Kigoma na Tabora na maeneo machache ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki katika Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara, yanatarajiwa kuwa na vipindi vya mvua kubwa,” alisema.

Alisema kutokana na viwango vikubwa vya mvua vilivyonyesha, ongezeko kidogo la mvua linatarajia kusababisha mafuriko na uharibifu wa miundombinu, hivyo ni muhimu tahadhari stahili ziendelee kuzingatiwa.

Msimbazi wagoma
Licha ya tahadhari hiyo ya TMA, baadhi ya wakazi waishio katika Bonde la Mto Msimbazi wamedai kuwa hawataondoka katika nyumba zao zilizokumbwa na mafuriko hadi watakapoona maji yamejaa katika mto huo.

Wakizungumza jana kwa nyakati tofauti wakazi hao walisema hawana pa kwenda licha ya kuisikia tahadhari hiyo ya TMA.

“Ningekuwa mpangaji sawa, sasa mimi nimejenga nitakwenda wapi na kwetu ni mikoani huko,” alisema Ramadhani Kimbuyu wakati akifanya ukarabati wa nyumba yake huku akisisitiza kuwa kipimo chao kitakuwa Mto Msimbazi.

Alisema kosa walilofanya awali ni kupuuza licha ya kuona mto huo umejaa jambo ambalo alidai hawatalirudia... “Tukiona yamejaa tu tunahamia juu relini, yakipungua tunarudi.”

Kauli ya RC
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki amesema Serikali itawachukulia hatua kali watakaokaidi amri ilivyotangazwa na Rais Jakaya Kikwete ya kutorejea katika maeneo hatarishi ya mabondeni.

“Tangu mwaka 1979 Serikali ilitoa amri ya watu kuondoka mabondeni lakini wamekuwa wakikaidi na kuendelea kuishi,  kitendo hicho kimechangiwa na uzembe kwa baadhi ya viongozi katika kutekeleza agizo hilo,” alisema.

Sadiki alisema baadhi ya watu wameanza kurejea kwenye mabonde yaliyoathirika na kuwaonya wasirudi na badala yake watafute maeneo mengine kuendesha makazi yao.

Alisema Serikali itawapatia waliojenga mabondeni viwanja na siyo wapangaji. Wakazi hao wametengewa viwanja katika eneo la Mabwe Pande lililoko mpakani na Bagamoyo, Pwani na kwamba mpaka sasa viwanja 700 vimeshapimwa.

“Baada ya kugawa viwanja hivi tutaanza zoezi la kuzibomoa nyumba walizokuwa wanaishi maeneo ya mabondeni ili kutoruhusu watu kurudi tena huko kwani bila kufanya hivyo, hatutafanikisha lengo hilo,” alisema Sadiki.

Treni zatishwa
Kutokana na mvua kubwa zinazonyesha maeneo mbalimbali nchini wa TRL, jana ulitangaza kusitishwa kwa safari za treni ya abiria kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma... “Safari hizo zimesitishwa hadi itakapotangwa vinginevyo baadaye,” alisema Meneja Uhusiano wa TRL, Midladjy Maez.

Alisema abiria wote waliokuwa wamepanga kusafiri jana na katika treni zijazo, wanatakiwa kufika na tiketi zao katika ofisi za Stesheni Masta wa kituo husika ili warejeshewe fedha zao.

Walia na huduma mbovu
Waathirika wa mafuriko waliopo katika Kituo cha Hananasifu, Kinondoni Dar es Salaam, wamelalamikia uongozi wa kituo hicho kutoa huduma za chakula na malazi usiku bila umeme.
Wakizungumza kambini hapo jana waathirika hao walisema, uongozi unatoa huduma hizo waathirika kuanzia saa 4:00 hadi saa 6:00 usiku kitendo ambacho kinafanya baadhi yao wapoteze vifaa vyao.Kambi ya Hananasif imeshapoteza magodoro 50, ambayo inaelezwa na wananchi hao kuwa waliohusika ni baadhi ya viongozi waliopewa dhamana ya kuhudumia eneo hilo.

“Hapa kituoni hatuna umeme, lakini utaona viongozi wanakaa  kimya mpaka ifike saa nne ndipo wanaanza kugawa magodoro, wengine wakishirikiana na vibaka usiku  kuhamisha baadhi ya magodoro kupeleka mahali kusikojulikana,” alisema Hamed Shaban.

Habari hii imeandikwa na Boniface Meena, Keneth Goliama na Aidan Mhando, Pamela Chilongola, Joseph Zablon, Ibrahim Yamola.
Chanzo: Mwananchi

Maji ni Dawa kubwa Lakini Hatujui!

Best Blogger Tips
Kheri ya Krismasi mpenzi msomaji, natumaini umekula, umekunywa na umefurahia maisha, sasa ni wakati wa kuutibu mwili wako kama baada ya kula na kunywa kwenye sikukuu hii vimekuletea ‘mgogoro’ tumboni.

Bila shaka kila mtu anafahamu umuhimu wa maji, lakini si watu wote wanafahamu kuwa maji ni dawa pia, licha ya kutumika kwa ajili ya kunywa ili kukata kiu.

Nchini Japan na nchi nyingine nyingi za Bara la Asia, ni jambo la kawaida kwa watu wake kunywa maji kwanza asubuhi kabla ya kula kitu chochote.
Tabia hii ina faida kubwa kwa afya ya binadamu na hata utafiti wa kisayansi uliofanywa, umethibitisha thamani ya maji katika kuponya, kuzuia au kudhibiti magonjwa kadhaa yanayosumbua watu wengi.

Chama Cha Madaktari wa Japan (Japanese Medical Society) kimethibitisha kuwa maji yana uwezo wa kutibu, kwa asilimia 100, magonjwa sugu na maarufu yafuatayo, iwapo mtu atafuata kanuni na taratibu za kunywa maji hayo kama tiba:
Kuumwa kichwa, maumivu ya mwili, mfumo wa moyo, moyo kwenda mbio, kifafa, uzito mkubwa, pumu, kifua kikuu, uti wa mgongo, ugonjwa wa figo, magonjwa ya mkojo, kutapika, vidonda vya tumbo, kuharisha, kisukari, saratani, ukosefu wa choo, matatizo ya macho, tumbo, hedhi, sikio, pua, nk.

JINSI YA KUTUMIA MAJI KAMA TIBA
Ili maji yatumike kama tiba, kunywa kiasi cha lita moja na robo (glasi nne kubwa) za maji safi na salama (yasiwe maji baridi) asubuhi na mapema kabla ya jua kuchomoza na kabla ya kupiga mswaki.

Baada ya kunywa kiasi hicho cha maji, usile wala kunywa kitu kingine hadi baada ya dakika 45 au saa moja. Baada ya muda huo, sasa unaweza kusafisha kinywa na kula mlo wako wa asubuhi kama kawaida.
Aidha, mara baada ya kula mlo wako wa asubuhi, usile wala kunywa kitu chochote hadi baada ya muda wa saa mbili kupita. Hivyo hivyo utafanya baada ya mlo wako wa mchana au jioni.
Kwa wale wagonjwa ambao hawawezi kunywa kiasi cha maji cha lita 1 na robo kwa wakati mmoja, wanaweza kuanza kwa kunywa na kiasi kidogo watakachoweza na kuongeza taratibu hadi kufikia kiwango hicho cha glasi nne kwa siku.
Utaratibu huu wa kunywa maji ulioelezwa hapo juu, una uwezo wa kutibu maradhi yaliyotajwa hapo awali na kwa wale ambao hawana maradhi yoyote, basi wataimarisha afya zao zaidi na kujipa kinga itakayowafanya waishi maisha yenye afya bora zaidi.

UNAWEZA KUPONA BAADA YA MUDA GANI?
Yafuatayo ni baadhi ya magonjwa na idadi ya siku zake za kupona zikiwa kwenye mabano kama ilivyothibitishwa na watafiti:
Shinikizo la damu (High Blood Pressure) (siku 30), vidonda vya tumbo (siku 10), kisukari (siku 30), saratani (siku 180) na kifua kikuu (siku 90).
Kwa mujibu wa watafiti, tiba hii haina madhara yoyote, hata hivyo katika siku za mwanzo utalazimika kukojoa mara kwa mara. Ni bora kila mtu akajiwekea mazoea ya kunywa maji kwa utaratibu huu kila siku katika maisha yake yote ili kujikinga na maradhi mbalimbali.
KUNYWA MAJI ILI UWE NA AFYA NJEMA NA UBAKI MCHANGAMFU SIKU ZOTE!
Chanzo: Global Publishers

Saturday, December 24, 2011

Nawatakia Sikukuu Njema

Best Blogger Tips

Friday, December 23, 2011

Hameni -JK

Best Blogger Tips
Mafuriko Jijini Dar-es-salaam
 RAIS Jakaya Kikwete amewahakikishia waathirika wa mafuriko ya mvua zinazoendelea kunyesha kwa siku tatu mfululizo sasa, kuwa Serikali itawapa msaada wa hali na mali, lakini
lazima wahame mabondeni.

Amesema Serikali ipo tayari kuwatafutia maeneo ya kujenga makazi ya kudumu na kwa dharura iliyopo kuwapa hifadhi ya mahema, vyakula, magodoro, vyoo, maji na huduma ya afya kama ilivyofanyika, lakini haina msamaha juu ya wao kuendelea kuishi mabondeni.

“Wenzetu wa hali ya hewa wanasema mvua hizi zinaendelea, Makamba (Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kabla ya Abbas Kandoro) aliwahamisha kwa helikopta, sasa Sadiki (Said Mecky-Mkuu wa Mkoa wa sasa) naye anawahamisha vivyo hivyo, hivi hali hii tutaiacha ijirudie mpaka lini?.....

“Ni vizuri mjiondoe kwenye maisha ya mashaka, nawahakikishia Serikali yenu ipo nanyi katika hali ngumu hii, lakini ni vizuri muondoke maeneo hayo ya hatari, suala kubwa ni mnahamaje?

Kamati ya Maafa ya Mkoa ihakikishe hilo linatekelezwa kwa ubora na mapema,” alisema Kikwete akizungumza na waathirika hao.

Alizungumza na waathirika walio katika Kambi ya Mchikichini, wilayani Ilala, wapatao 1,900 kwa niaba ya waathirika wengine wa kambi nyingine saba zilizowekwa katika shule za sekondari na msingi kwa hifadhi.

Kabla ya kuzungumza nao, Rais Kikwete alipata nafasi ya kuzunguka kwa helikopta kuona athari za mafuriko hayo katika jiji na pia kutembelea kambi hiyo.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, watu zaidi ya 20 wamepoteza maisha na 4,900 wameathirika kwa kukosa makazi.

Aidha, vifo zaidi havijaripotiwa kwa kuwa bado baadhi ya nyumba zimezingirwa na maji na matope.

Akihutubia hadhara hiyo, Rais alisisitiza watu kuheshimu mikondo ya maji kwa kuwa hakuna mwanadamu anayeweza kuzuia maji, upepo au moto na kutolea mfano kwa Marekani, Australia na nchi zenye teknolojia ya juu, lakini maji huwashinda.

Rais Kikwete aliwaagiza Mipango Miji wafanye kazi ipasavyo kwa kuwa wao ndio wamekuwa vinara wa kugawa maeneo kwa hati halali wakati wakijua wazi ni maeneo hatari kwa maisha ya watu, mabondeni na kwenye mikondo ya maji.

“Maji hayana tajiri wala masikini, nilikuwa napita kwa helikopta nikaona hata kwenye kampuni ile Jangwani (Kajima) ukuta umeenda, Mipango Miji fanyeni kazi vizuri kuepusha yanayoweza kuepukika, mikondo ya maji iachwe nafasi, baadhi ya hawa watu wana hati halali, mmewapa ninyi,” alisema Rais.

Aidha, aliwahakikishia waathirika hao kufuatiliwa kwa karibu suala lao na kuwaahidi kuwa viongozi wakiwemo mameya, wabunge, madiwani na watendaji wahakikishe usiku na mchana watawahudumia mpate makazi maeneo yafaayo.

Awali, akihutubia, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sadiki alisema walioathirika ni 4,900 na vifo vilivyoripotiwa mpaka jana asubuhi ni 20 ambapo miili 18 imetambuliwa na miwili bado ipo Hospitali ya Taifa Muhimbili, aliwataka watu wakatambue miili hiyo.

Katika hotuba yake, Sadiki alisema uongozi wa mkoa kwa kushirikiana na viongozi wa kisiasa wamefikia hitimisho la kuwataka wakazi hao wa mabondeni kuridhia kuhama baada ya kutenga eneo katika Wilaya ya Kinondoni la ekari 2,000 linalotoa viwanja 2,800 ili wakazi hao waanze kujenga makazi mapya.

“Lakini tuna taarifa huko nyuma kwamba kuna waliopewa maeneo Wazo Hill, Yombo Dovya, hawakuhamia huko, wakauza na hata hizi huku wakauza, muda si mrefu shule zitafunguliwa hivyo tutahakikisha mnapata hifadhi ya dharura huko ili tuwapishe wanafunzi huku,” alisema Sadiki.

Kwa mujibu wake, kuna kambi zaidi ya saba jijini Dar es Salaam na vitu mbalimbali vimetolewa na wasamaria wema, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi yakiwemo mahema, vyakula, nguo, dawa na mikeka. Mbunge wa Ubungo, John Mnyika ametoa vitu vyenye thamani ya Sh milioni moja kwa kambi tano.

Gazeti hili lilitembelea katika baadhi ya kambi hizo kwa lengo kujionea hali ilivyo ambapo katika kituo cha Rutihinda, hadi saa 5.45 asubuhi, waathirika 52 waliokuwa wameandikishwa walilalamika kutokuwepo kwa huduma yoyote ikiwemo ya chakula, na magodoro tangu wafike kambini hapo juzi asubuhi.

Akizungumzia suala hilo, msimamizi wa kambi hiyo ambaye pia ni Mtendaji wa Kata ya Kigogo, Kassim Mbezi, alisema iliwalazimu baadhi ya waathirika kuondoka na kujitafutia hifadhi na chakula.

Walikuwa zaidi ya 100 kambini hapo na kubaki hao 52. “Hadi hivi sasa watu waliopo hapa ni 52, awali waliokuwepo wengi lakini wanapokuja na kukuta hali ya kambi ilivyo wanaamua
kuondoka na kurudi katika maeneo waliyotoka na wengine kwenda kujitafutia chakula kwa kuwa wana watoto,” alisema Mbezi.

Alipotafutwa Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuf Mwenda kwa lengo la kuzungumzia tatizo la kambi hiyo, alisema idadi kamili ya waathirika ndiyo kikwazo cha kufikishwa mapema kwa misaada hiyo na hadi kufikia muda huo, tayari walishaipata idadi yao hivyo utaratibu wa kuwafikishia misaada ulikuwa ukiendelea.

Kambi ya Azania iliyopo Manispaa ya Ilala iliyo na waathirika 426, hali ilikuwa ikiendelea vizuri na waathirika wote kupata mahitaji yao muhimu ikiwemo ya vyakula vilivyotolewa na taasisi mbalimbali na wasamaria.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa ya Kata ya Kariakoo, Mathias Muyenjwa, alisema ukiacha kituo hicho vituo vingine vilivyopo katika Kata ya Kariakoo na idadi ya waathirika katika mabano ni Mtambani A (343), Mtambani B (1,340) pamoja na Kariakoo Kaskazini yenye waathirika 302.

Kuhusu hali ya kambi hiyo, Muyenjwa alisema huduma mbalimbali zinaendelea kutolewa kwa waathirika ikiwemo ya afya huku akiitaja misaada iliyotolewa na kuwa ni michele, mikate, maji ya kunywa, juisi, mafuta ya kula, sabuni, mablangeti, mashuka pamoja na nguo za kawaida.

Baadhi ya waliotajwa kufa kutokana na mvua hizo ni Tulihama (65) mkazi wa Ubungo Msewe, Maganga Said (8) mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kanjenje Tabora, Gathi Mseti (30) na mwanawe Thomas Rashid (8) wakazi wa Kipunguni, Vian Maxmilian (13) mkazi wa Mburahati, Magreth Makwaya (6), mkazi wa Luhanga, Ibrahim Lusuma(60), mkazi wa Ubungo Msewe.
Chanzo: HabariLeo

Monday, December 12, 2011

Raia wa Afrika Kusini 'auliwa' China

Best Blogger Tips
China imempa adhabu ya kifo mwanamke mmoja raia wa Afrika kusini kwa kufanya biashara haramu ya kusafirisha dawa za kulevya, ikikataa ombi la Rais Jacob Zuma la kumwachia. 

Janice Bronwyn Linden, mwenye umri wa miaka, 38, aliuliwa zaidi ya miaka mitatu baada ya kukamatwa.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu tayari yamekuwa yakilaani China mara kwa mara kwa kutekeleza sheria ya hukumu ya kifo, yakisema mfumo wake wa sheria hauna haki.

Serikali ya Afrika Kusini imesema hatua hiyo haitoathiri mahusiano ya karibu ya kidiplomasia na China.

Serikali ya China iliwaruhusu dada zake wawili Bi Linden kukaa naye kwa saa nzima kabla ya kutekeleza hukumu hiyo kwa sindano ya sumu, gazeti binafsi la Afrika Kusini e. News, likimnukuu mwandishi kutoka China.

'Haijashughulikiwa vya kutosha'

Bi Linden alikamatwa Novemba 2008 baada ya kukutwa na kilogramu tatu za methamphetamine alipowasili uwanja wa ndege mjini Guangzhou kusini mwa nchi hiyo.

Aliendelea kutetea nafsi yake, akisema dawa hizo za kulevya zilitumbukizwa kwenye sanduku lake bila yeye kujua.

Hata hivyo, mahakama kuu ya Guangdong na ya rufaa huko Beijing zilikataa rufaa yake.

Msemaji wa idara ya uhusiano wa kimataifa, Clayson Monyela, aliiambia BBC kuwa Bw Zuma aliingilia kati kutaka hukumu hiyo ibadilishwe na apewe kifungo cha maisha.

Bw Monyela alisema, "Tumefanya kila namna kumnusuru hata katika nyanja zote za juu."

Alisema, serikali ya China itakabidhi majivu yake kwa familia yake, kufuatia kuchomwa maiti yake, kulingana na makubaliano yaliyofanywa baina ya mataifa hayo mawili.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa upinzani wa chama cha Democratic Alliance (DA) wa Afrika Kusini, Stevens Mokgalapa, amesema serikali haikufanya vya kutosha kuokoa maisha ya Bi Linden , gazeti binafsi la Afrika kusini Times Lives limeripoti.


Saturday, December 10, 2011

Vitambulisho vya Taifa bure

Best Blogger Tips
KILA Mtanzania atakuwa na kitambulisho cha Taifa kufikia mwaka 2015 ambacho kitatolewa bure na Serikali, na tayari watumishi wa umma wameanza kujaza fomu za utambuzi na usajili na ifikapo Aprili mwakani, watakuwa na vitambulisho hivyo, imefahamika.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), baada ya wafanyakazi wa Serikali, watafuatiwa wanafunzi, wafanyabiashara na hatimaye umma kwa ujumla utafikiwa na kazi hiyo muhimu kwa Taifa.

Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Dickson Maimu akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali
vya habari Dar es Salaam jana kuhusu maendeleo ya mradi wa vitambulisho vya Taifa, alisema
ingawa vitatolewa bure, kwa ye yote atakayepoteza atalazimika kuvilipia.

Mradi mzima unatarajiwa kugharimu kiasi cha Sh bilioni 350.

Maimu alisema ni lengo la Serikali kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa na kitambulisho cha
Taifa ifikapo mwaka 2015 na hilo litasaidia kuboresha Daftari la Kudumu la Wapigakura, na hivyo kuipunguzia mzigo mkubwa Serikali katika kuboresha daftari hilo kila wakati wa uchaguzi unapowadia.

“Kwa kuwa zoezi la utambuzi na usajili litafanyika kwenye maeneo yenu nawaomba mtoe
ushirikiano wa kutosha kwa wananchi wote na niwakumbushe kuwa huduma hii ni bure
kwa mujibu wa maagizo ya Baraza la Mawaziri, na hivyo Serikali haitarajii mtendaji yeyote kuomba au kupokea chochote au kuweka tozo.

“Tunawasihi wananchi na wageni, wasikubali kudanganywa au kulipa fedha zozote kwani
kitambulisho ni bure na huduma zote zinazoambatana na zoezi hili ni bure. NIDA haitasita
kuchukua hatua za kisheria kwa ye yote atakayebainika kukiuka uratatibu huu.”

Alisema wameanza na wafanyakazi wa Serikali kwa sababu vitambulisho kwao si tatizo kwa maana ya mfumo walionao una urahisi katika kuwashughulikia, lakini zaidi, itasaidia katika kudhibiti watumishi hewa.

“Hawa kwao kitambulisho kwao kidogo si tatizo, kwani wana mifumo mizuri na hawa tunataka kuwatumia kama majaribio kwa mradi huo. Lakini zaidi, itasaidia katika kudhibiti tatizo la watumishi hewa serikalini,” alisema Maimu na kuongeza kuwa watafuata wanafunzi kwa sababu ya kusaidia katika suala la mikopo ya elimu ya juu na kwa wafanyabiashara ili kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi na kusaidia kuongeza mapato.

“Kutokana na ratiba yetu ya utekelezaji, tutaanza kutoa vitambulisho kwa awamu ya kwanza
mwezi Aprili 26, 2012 wakati wa maadhimisho ya sherehe za Muungano kwa watumishi wa
Serikali ambao tayari usajili umeanza,” alieleza Maimu na kuongeza kuwa katika utekelezaji wa mradi huo, Mamlaka itatoa vitambulisho katika makundi matatu; Watanzania, wageni wakazi na wakimbizi.

“Tutatoa vitambulisho hata kwa mwizi, kwa sababu moja ya faida kuu za mradi huu ni kudhibiti
suala la usalama wetu kwa kila pointi. Ndiyo maana dhana kuu ya mfumo huu inatakiwa ijibu maswali makuu manne; nani ni nani; yuko wapi; anamiliki nini na anafanya nini”alieleza mkurugenzi huyo.

Aliongeza kuwa vitambulisho hivyo katika eneo la usalama, vitasaidia kuimarisha usalama
wa raia na mali zao na kupunguza vitendo vya uhalifu na hasa unaofanywa na raia kutoka
nchi jirani na wafungwa waliomaliza adhabu zao au kuachiwa huru kwa msamaha wa Rais.

“Ni wazi kuwa udhibiti wao umekuwa mgumu kutokana na kushindwa kuwatambua. Pia itasaidia kuweka kumbukumbu za matukio ya uhalifu katika daftari,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa NIDA.

Alisema baada ya usajili kukamilika, jukumu kubwa litakalofuatia ni uhakiki wa taarifa za makazi, umri na uraia wa mwombaji aliyesajiliwa ili kupata uhakika wa taarifa zake kwa lengo la kumpatia kitambulisho kinachowiana na kundi lake.

Katika udahili, mwombaji atatakiwa kuthibitisha kama amekuwa akiishi Tanzania kwa kipindi kisichopungua miezi sita; uthibitisho wa umri wa miaka 18 na uthibitisho wa uraia wake.

Aidha, viambatanisho muhimu vitahitajika ambavyo ni cheti cha kuzaliwa; cheti cha ubatizo/falaki; kitambulisho cha Mpigakura; pasipoti ya Tanzania na cheti cha kuhitimu elimu ya msingi.

“Jukumu hili ni la muhimu sana na linatakiwa kufanywa kwa umakini mkubwa bila kuharakishwa kwani uharaka kidogo tu unaweza kabisa kuharibu zoezi zima,” alifafanua
mkurugenzi huyo.

Alisema ili kufanikisha kazi hiyo, wanashirikiana kwa karibu sana na Serikali za Mitaa kwa
lengo la kutambua makazi halali ya mwombaji; Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa lengo la kutambua umri wa mwombaji na Idara ya Uhamiaji kutambua na kubaini uraia wa
mwombaji.

Aidha, alisema katika mkutano ujao wa Bunge, wanatarajiwa utapelekwa muswada wa
mabadiliko ya sheria ambayo itakuwa ni lazima kwa kila mtu anayeishi nchini, kuwa na kitambulisho hicho cha kudumu ambacho kadi yake itakuwa ni ya miaka 10.

NIDA imeingia mkataba na mkandarasi wa vitambulisho hivyo, Kampuni ya IRIS Corporation
Berhad ya Malaysia tangu Aprili 21, mwaka huu.

Mshauri mwelekezi wa mradi huo ni Kampuni ya Gotham International Ltd (GIL), na tayari Mamlaka hiyo imepata viwanja katika wilaya zote nchini kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya ofisi za usajili wilayani wakati kituo kikuu cha kuhifadhi takwimu zote za nchi kitakuwa Kibaha, Pwani.

Maimu alisema kulikuwa na uchelewaji wa kutoa fedha kwa mkandarasi kuanza kazi, lakini
tayari Oktoba mwaka huu amekabidhiwa fedha hizo baada ya kuidhinishwa na Bunge na tayari
ameleta mashine kuanza kazi ya mradi huo uliosubiriwa kwa zaidi ya miaka 15 sasa na kugubikwa na maneno mengi katika mchakato wake.
Chanzo: HabariLeo

Wednesday, December 7, 2011

Saadi Gaddafi 'ajaribu kupenya Mexico'

Best Blogger Tips
Saad Gaddafi
Serikali ya Mexico imesema imezuia njama iliyokuwa ifanywe na kundi la wahalifu la kumpenyeza kwa magendo mmoja wa watoto wa aliyekuwa kiongozi wa Libya Kanali Muammar Gaddafi nchini Mexico. 

Saadi Gaddafi amekuwa kwenye kifungo cha nyumbani nchini Niger iliyopo Afrika Magharibi tangu alipoikimbia Libya mwezi Septemba.

Msemaji wa serikali ya Mexico alisema Saadi Gaddafi na baadhi ya wanafamilia wake walizuiwa kutokana na matokeo ya ripoti za kijasusi.

Watu wengi wamekamatwa kutokana na tukio hilo.

Maafisa wa Mexico wamsema jaribio hilo- lililoibuliwa Septemba 6- lilihusisha majina na nyaraka za uongo.

Nyumba salama

Waziri wa mambo ya ndani Alejandro Poire alisema mpango huo unahusisha mtandao wa uhalifu " mkubwa wa kimataifa", lakini ikagundulika mwezi Septemba kabla ya mpango huo kukamilika.

Mtandao huo ulihusisha watu kutoka nchi mbalimbali, ikiwemo Mexico, Denmark na Canada, Bw Poire aliuambia mkutano wa waandishi wa habari huko Mexico.

Alisema, walikuwa wakinunua nyumba zenye salama na kufungua akaunti za benki.

Tarehe 14 Septemba- siku nane baada ya njama hiyo kugundulika- Niger ilisema Saadi Gaddafi, mwenye umri wa miaka 38, aliwasili mjini Niamey.

Iliripotiwa kuwa alisafirishwa kwa ndege ya kijeshi kutoka mji wa Agadez kaskazini mwa nchi hiyo.

Septemba 29, Shirika la polisi la kimataifa, Interpol lilitoa " hati ya kukamatwa" kwa Saadi Gaddafi, wakitaka nchi wanachama imkatae iwapo atatokea kwenye nchi zao.

Wakala wa polisi wa kimataifa wamesema anatakiwa kwa madai ya kutoa vitisho kwa kutumia silaha alipokuwa mkuu wa shirikisho la mpira la Libya.

Saadi Gaddafi, ambaye alikuwa akicheza soka katika ligi kuu ya Italia Serie A, pia amewekewa vikwazo vya kusafiri na mali zake kutiwa tanji chini ya azimio la baraza la usalama la umoja wa mataifa lililopitishwa mapema mwaka huu.
 Chanzo: BBC

Tuesday, December 6, 2011

Jose Chameleone adhihirisha ubilionea

Best Blogger Tips
Jose Chameleone
 HAKUNA ubishi kwamba, unapotaja jina la Jose Chameleone, moja kwa moja akili itakuelekeza kwa msanii anayeporomosha muziki wenye mvuto, uliochanganywa na vionjo vya kiasili kutoka kwa nyota huyo raia wa Uganda.

Amekuwa akikonga nyoyo za mashabiki wa ndani na nje ya Afrika Mashariki kwa takribani miaka 12 sasa.

Bila kutafuna maneno, yafaa kueleza kuwa, ndani ya kipindi hicho Chameleone ambaye jina lake halisi ni Joseph Mayanja, hajachuja.

Na ndiyo maana kila kukicha, nyota ya msanii huyo inazidi kung’ara, hali kadhalika kipato chake kikizidi kuimarika kiasi cha kumfanya mmoja wa vijana wenye uwezo mkubwa kifedha nchini Uganda.

Nyota huyo aliyezaliwa miaka 33 iliyopita ameshavuka katika daraja la umasikini, sasa akiogelea fedha.

Ndiyo, kwa asiyeamini, hebu angalau baadhi ya mambo yanayothibitisha utajiri wa nyota huyo.

Anamiliki jumba la kifahari katika vilima vya Sekuku jijini Kampala, pia ana nyumba huko Arizona, Marekani, achilia ile ya Kigali, Rwanda aliyoinunua hivi karibuni kwa mamilioni ya shilingi.

Ukiachilia mbali gari la kisasa aina ya Cadillac Escalade lililomgharimu zaidi ya Sh milioni 100, Chameleone ambaye ni baba wa watoto watu, pia anamiliki Mercedes Benz, BMW na aina nyingine za magari.

Kwa ujumla, anakadiriwa kuwa na utajiri unaofikia Sh bilioni 1.5 kwa fedha za Tanzania. Na anasema bado anazisaka, kwani bila ya kuwa na tamaa ya kusaka mafanikio zaidi, ndoto huenda zisitimie.

Anayasema hayo akisisitiza kuwa, baada ya nyumba, magari na akaunti nono benki, sasa ana ndoto za kumiliki helikopta yake, baada ya kuwa amekuwa akikodi mara kadhaa ama kwenda katika matamasha au kama alivyofanya wakati anamuoa mkewe Daniela Atim.

Je, ni nini siri ya mafanikio ya nyota huyu kipenzi cha wengi Afrika Mashariki na Kati? Mwenyewe, amekaririwa mara kadhaa akisisitiza kuwa, ni kujituma na kuuchukulia muziki kuwa ni kazi.

“Bila kujituma, hakuna maendeleo. Nimehangaika sana kuyatafuta maendeleo, na hata baada ya kuyapata, sijabweteka. Nafanya kazi usiku na mchana huku nikihakikisha kila shilingi ninayoingiza inazidi kuniinua kimaisha,” anasema nyota huyo mwenye utitiri wa tuzo za ndani na nje ya Uganda.

Ubora wa nyimbo kama Kipepeo, Mama Rhoda, Jamila, Mambo Bado, Mama Mia, Shida za Dunia, Fitina Yako, Haraka Haraka, Ndivyo Sivyo aliomshirikisha Joseph Haule `Profesa Jay’ wa Tanzania, ni baadhi ya kielelezo cha kipaji cha kipekee cha muziki kwa Chameolen, msanii mwenye umbo dogo lakini anayetajwa kuwa mkorofi.

Je, mwenyewe anazungumziaje kuhusu ukorofi? Anasema: “Hata wewe ukiniangalia utaamini kuwa mimi ni mkorofi?

Mara nyingi nasingiziwa ili watu wengine wafanye biashara…” Je, alitokea wapi kimuziki? Ni historia ndefu, lakini kwa kifupi itoshe kusema kwamba, alianzia mwaka 1994 akiwa mchezesha disko katika klabu ya usiku ya Maganjo Mizuri, wakati huo akiwa mwanafunzi wa sekondari jijini Kampala.

Na aliwahi kuajiriwa Rwanda katika klabu ya usiku ya Cadillac mara tu baada ya kuhitimu elimu ya sekondari.

Kwa umahiri wake , mbali ya kumwingizia fedha nyingi, amebahatika pia kuzuru Ulaya, Marekani na hata Mashariki ya Mbali kwa shughuli za kimuziki, achilia heshima ya kutumbuiza wakati wa fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Afrika Kusini mwaka jana.

Katika familia yao, Jose ni mtoto wa nne kati ya saba ambayo ina msichana mmoja. Anakumbuka alisoma Shule ya Msingi Nakasero, Sekondari ya Mengo na Sekondari ya Kiislamu ya Kawempe.

“Ingawa nilifaulu kiasi cha kutakiwa kujiunga chuo kikuu, niliamua kuzama katika muziki. Na sijakata tamaa au kuahirisha, ipo siku nitasoma chuo kikuu na kuitwa msomi,” anasema nyota huyo ambaye wazazi wake walitaka asome na kuwa daktari, lakini akakacha masomo kwa muda.

Hata hivyo anasema kuwa, ingawa aliwaudhi wazazi wake, bado anashukuru kwamba yeye ni daktari wa muziki anayewakuna wengi, ikiwa pamoja na wazazi wake.

“Hatuna uhasama tena kwa sababu kama ni maisha nimeyashika, kwa hivyo nimewafuta machozi wazazi wangu ambao awali waliamini labda ndiyo nilikuwa napotea kimaisha.”

Baadaye alihamishia makazi yake Nairobi, Kenya alikoishi maisha ya kubahatisha, alilazimika kulala studio hadi alipookolewa na Dorotea ambaye jina lake halisi ni Griet Onsia.

Anakumbuka akiwa na Bebe Cool na Redsun alipata fursa ya kutumbuiza katika shindano la kumsaka Mrembo wa Kenya.

Anakiri hapo ndipo milango ya neema ilipoanza kufunguka. Anasema Dorotea, baada ya kuzoeana alimshawishi ahamie nyumbani kwake badala ya kuendelea kulala studio, ushawishi ambao ulimchukua zaidi ya wiki moja kumkubalia.

“Nilipohamia tulikuwa marafiki, lakini mengine yaliibuka tukiwa katika nyumba moja. Mara nyingi kila akitoka, alinikuta nimetulia naandika nyimbo, huku akihoji ni lini nitarekodi. Nilikosa jibu kwa kuwa siku wa na fedha.

“Siku moja akiwa safarini huko Afrika Magharibi aliniachia bahasha yenye dola za Kimarekani 1,000 (karibu Sh milioni 1.8 za Tanzania kwa sasa), akaniambia niingie studio.

“Huo ukawa mwanzo wa kibao Mama Mia na sikuamini kama fedha ile ingebadilisha maisha yangu na kunifikisha hapa nilipo. Mengine yanabaki kuwa historia,” anasema.

Pamoja na utajiri aliovuna kupitia muziki, nyota huyo anasema historia ya kushuhudiwa `Live’ na watu zaidi ya bilioni 9 akitumbuiza wakati wa Kombe la Dunia kwake ni kitu cha kipekee.

“Mtoto wa Afrika tena Afrika Mashariki kupewa heshima ile haikuwa kitu kidogo. Najiona mwenye bahati na ni mastaa wachache wanaweza kuingia katika kundi la bahati hata wangeishi kwa miaka 1000.”

Anasema kutokana na baraka alizopata maishani, ameamua kuanzisha taasisi ya Chameleone ili aweze kuwasaidia wasiojiweza.

“Nikiwa mdogo sikuwa na maisha mazuri, sikutoka katika familia bora, kwa hiyo ninajiona mwenye wajibu wa kuwasaidia wengine wakianzia katika misingi mizuri ya kielimu. “Nimeshanunua eneo kwa ajili ya kujenga kituo.

Nataka jamii siku moja inikumbuke kwamba niliwika na kuitangaza nchi yangu, lakini pia sikuwa mchoyo, bali niliyatumia vyema matunda ya muziki.

Kwa kufanya hivi, naamini ipo siku nitawashawishi wengi kufanya mambo makubwa kwa ajili ya jamii wanayotoka.”

Huyo ndiye Joseph Mayanja ambaye pamoja na misukosuko ya maisha tangu akiwa shule hadi sasa akiwa staa, bado nyota yake inang’ara.

Je, atazidi kupata mafanikio? Bila shaka ni jambo la kusubiri na kuona, hasa ikizingatiwa kuwa, mwenyewe amejijengea falsafa ya kutolewa sifa, bali kazi kwa kwenda mbele.

Pamoja na yote, Chameleone anapaswa mfano wa kuigwa kwa wasanii wengi wa Kitanzania ambao huvuma kwa muda mfupi, lakini wakishazikamata fedha hupotelea kwenye ulimwengu wa anasa na baadaye kujikuta wakiwa `choka mbaya’, tena wakiwa hawana akiba benki wala hawajawekeza.
Chanzo: HabariLeo


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits