Tuesday, December 6, 2011

Jose Chameleone adhihirisha ubilionea

Best Blogger Tips
Jose Chameleone
 HAKUNA ubishi kwamba, unapotaja jina la Jose Chameleone, moja kwa moja akili itakuelekeza kwa msanii anayeporomosha muziki wenye mvuto, uliochanganywa na vionjo vya kiasili kutoka kwa nyota huyo raia wa Uganda.

Amekuwa akikonga nyoyo za mashabiki wa ndani na nje ya Afrika Mashariki kwa takribani miaka 12 sasa.

Bila kutafuna maneno, yafaa kueleza kuwa, ndani ya kipindi hicho Chameleone ambaye jina lake halisi ni Joseph Mayanja, hajachuja.

Na ndiyo maana kila kukicha, nyota ya msanii huyo inazidi kung’ara, hali kadhalika kipato chake kikizidi kuimarika kiasi cha kumfanya mmoja wa vijana wenye uwezo mkubwa kifedha nchini Uganda.

Nyota huyo aliyezaliwa miaka 33 iliyopita ameshavuka katika daraja la umasikini, sasa akiogelea fedha.

Ndiyo, kwa asiyeamini, hebu angalau baadhi ya mambo yanayothibitisha utajiri wa nyota huyo.

Anamiliki jumba la kifahari katika vilima vya Sekuku jijini Kampala, pia ana nyumba huko Arizona, Marekani, achilia ile ya Kigali, Rwanda aliyoinunua hivi karibuni kwa mamilioni ya shilingi.

Ukiachilia mbali gari la kisasa aina ya Cadillac Escalade lililomgharimu zaidi ya Sh milioni 100, Chameleone ambaye ni baba wa watoto watu, pia anamiliki Mercedes Benz, BMW na aina nyingine za magari.

Kwa ujumla, anakadiriwa kuwa na utajiri unaofikia Sh bilioni 1.5 kwa fedha za Tanzania. Na anasema bado anazisaka, kwani bila ya kuwa na tamaa ya kusaka mafanikio zaidi, ndoto huenda zisitimie.

Anayasema hayo akisisitiza kuwa, baada ya nyumba, magari na akaunti nono benki, sasa ana ndoto za kumiliki helikopta yake, baada ya kuwa amekuwa akikodi mara kadhaa ama kwenda katika matamasha au kama alivyofanya wakati anamuoa mkewe Daniela Atim.

Je, ni nini siri ya mafanikio ya nyota huyu kipenzi cha wengi Afrika Mashariki na Kati? Mwenyewe, amekaririwa mara kadhaa akisisitiza kuwa, ni kujituma na kuuchukulia muziki kuwa ni kazi.

“Bila kujituma, hakuna maendeleo. Nimehangaika sana kuyatafuta maendeleo, na hata baada ya kuyapata, sijabweteka. Nafanya kazi usiku na mchana huku nikihakikisha kila shilingi ninayoingiza inazidi kuniinua kimaisha,” anasema nyota huyo mwenye utitiri wa tuzo za ndani na nje ya Uganda.

Ubora wa nyimbo kama Kipepeo, Mama Rhoda, Jamila, Mambo Bado, Mama Mia, Shida za Dunia, Fitina Yako, Haraka Haraka, Ndivyo Sivyo aliomshirikisha Joseph Haule `Profesa Jay’ wa Tanzania, ni baadhi ya kielelezo cha kipaji cha kipekee cha muziki kwa Chameolen, msanii mwenye umbo dogo lakini anayetajwa kuwa mkorofi.

Je, mwenyewe anazungumziaje kuhusu ukorofi? Anasema: “Hata wewe ukiniangalia utaamini kuwa mimi ni mkorofi?

Mara nyingi nasingiziwa ili watu wengine wafanye biashara…” Je, alitokea wapi kimuziki? Ni historia ndefu, lakini kwa kifupi itoshe kusema kwamba, alianzia mwaka 1994 akiwa mchezesha disko katika klabu ya usiku ya Maganjo Mizuri, wakati huo akiwa mwanafunzi wa sekondari jijini Kampala.

Na aliwahi kuajiriwa Rwanda katika klabu ya usiku ya Cadillac mara tu baada ya kuhitimu elimu ya sekondari.

Kwa umahiri wake , mbali ya kumwingizia fedha nyingi, amebahatika pia kuzuru Ulaya, Marekani na hata Mashariki ya Mbali kwa shughuli za kimuziki, achilia heshima ya kutumbuiza wakati wa fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Afrika Kusini mwaka jana.

Katika familia yao, Jose ni mtoto wa nne kati ya saba ambayo ina msichana mmoja. Anakumbuka alisoma Shule ya Msingi Nakasero, Sekondari ya Mengo na Sekondari ya Kiislamu ya Kawempe.

“Ingawa nilifaulu kiasi cha kutakiwa kujiunga chuo kikuu, niliamua kuzama katika muziki. Na sijakata tamaa au kuahirisha, ipo siku nitasoma chuo kikuu na kuitwa msomi,” anasema nyota huyo ambaye wazazi wake walitaka asome na kuwa daktari, lakini akakacha masomo kwa muda.

Hata hivyo anasema kuwa, ingawa aliwaudhi wazazi wake, bado anashukuru kwamba yeye ni daktari wa muziki anayewakuna wengi, ikiwa pamoja na wazazi wake.

“Hatuna uhasama tena kwa sababu kama ni maisha nimeyashika, kwa hivyo nimewafuta machozi wazazi wangu ambao awali waliamini labda ndiyo nilikuwa napotea kimaisha.”

Baadaye alihamishia makazi yake Nairobi, Kenya alikoishi maisha ya kubahatisha, alilazimika kulala studio hadi alipookolewa na Dorotea ambaye jina lake halisi ni Griet Onsia.

Anakumbuka akiwa na Bebe Cool na Redsun alipata fursa ya kutumbuiza katika shindano la kumsaka Mrembo wa Kenya.

Anakiri hapo ndipo milango ya neema ilipoanza kufunguka. Anasema Dorotea, baada ya kuzoeana alimshawishi ahamie nyumbani kwake badala ya kuendelea kulala studio, ushawishi ambao ulimchukua zaidi ya wiki moja kumkubalia.

“Nilipohamia tulikuwa marafiki, lakini mengine yaliibuka tukiwa katika nyumba moja. Mara nyingi kila akitoka, alinikuta nimetulia naandika nyimbo, huku akihoji ni lini nitarekodi. Nilikosa jibu kwa kuwa siku wa na fedha.

“Siku moja akiwa safarini huko Afrika Magharibi aliniachia bahasha yenye dola za Kimarekani 1,000 (karibu Sh milioni 1.8 za Tanzania kwa sasa), akaniambia niingie studio.

“Huo ukawa mwanzo wa kibao Mama Mia na sikuamini kama fedha ile ingebadilisha maisha yangu na kunifikisha hapa nilipo. Mengine yanabaki kuwa historia,” anasema.

Pamoja na utajiri aliovuna kupitia muziki, nyota huyo anasema historia ya kushuhudiwa `Live’ na watu zaidi ya bilioni 9 akitumbuiza wakati wa Kombe la Dunia kwake ni kitu cha kipekee.

“Mtoto wa Afrika tena Afrika Mashariki kupewa heshima ile haikuwa kitu kidogo. Najiona mwenye bahati na ni mastaa wachache wanaweza kuingia katika kundi la bahati hata wangeishi kwa miaka 1000.”

Anasema kutokana na baraka alizopata maishani, ameamua kuanzisha taasisi ya Chameleone ili aweze kuwasaidia wasiojiweza.

“Nikiwa mdogo sikuwa na maisha mazuri, sikutoka katika familia bora, kwa hiyo ninajiona mwenye wajibu wa kuwasaidia wengine wakianzia katika misingi mizuri ya kielimu. “Nimeshanunua eneo kwa ajili ya kujenga kituo.

Nataka jamii siku moja inikumbuke kwamba niliwika na kuitangaza nchi yangu, lakini pia sikuwa mchoyo, bali niliyatumia vyema matunda ya muziki.

Kwa kufanya hivi, naamini ipo siku nitawashawishi wengi kufanya mambo makubwa kwa ajili ya jamii wanayotoka.”

Huyo ndiye Joseph Mayanja ambaye pamoja na misukosuko ya maisha tangu akiwa shule hadi sasa akiwa staa, bado nyota yake inang’ara.

Je, atazidi kupata mafanikio? Bila shaka ni jambo la kusubiri na kuona, hasa ikizingatiwa kuwa, mwenyewe amejijengea falsafa ya kutolewa sifa, bali kazi kwa kwenda mbele.

Pamoja na yote, Chameleone anapaswa mfano wa kuigwa kwa wasanii wengi wa Kitanzania ambao huvuma kwa muda mfupi, lakini wakishazikamata fedha hupotelea kwenye ulimwengu wa anasa na baadaye kujikuta wakiwa `choka mbaya’, tena wakiwa hawana akiba benki wala hawajawekeza.
Chanzo: HabariLeo

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits