Friday, December 23, 2011

Hameni -JK

Best Blogger Tips
Mafuriko Jijini Dar-es-salaam
 RAIS Jakaya Kikwete amewahakikishia waathirika wa mafuriko ya mvua zinazoendelea kunyesha kwa siku tatu mfululizo sasa, kuwa Serikali itawapa msaada wa hali na mali, lakini
lazima wahame mabondeni.

Amesema Serikali ipo tayari kuwatafutia maeneo ya kujenga makazi ya kudumu na kwa dharura iliyopo kuwapa hifadhi ya mahema, vyakula, magodoro, vyoo, maji na huduma ya afya kama ilivyofanyika, lakini haina msamaha juu ya wao kuendelea kuishi mabondeni.

“Wenzetu wa hali ya hewa wanasema mvua hizi zinaendelea, Makamba (Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kabla ya Abbas Kandoro) aliwahamisha kwa helikopta, sasa Sadiki (Said Mecky-Mkuu wa Mkoa wa sasa) naye anawahamisha vivyo hivyo, hivi hali hii tutaiacha ijirudie mpaka lini?.....

“Ni vizuri mjiondoe kwenye maisha ya mashaka, nawahakikishia Serikali yenu ipo nanyi katika hali ngumu hii, lakini ni vizuri muondoke maeneo hayo ya hatari, suala kubwa ni mnahamaje?

Kamati ya Maafa ya Mkoa ihakikishe hilo linatekelezwa kwa ubora na mapema,” alisema Kikwete akizungumza na waathirika hao.

Alizungumza na waathirika walio katika Kambi ya Mchikichini, wilayani Ilala, wapatao 1,900 kwa niaba ya waathirika wengine wa kambi nyingine saba zilizowekwa katika shule za sekondari na msingi kwa hifadhi.

Kabla ya kuzungumza nao, Rais Kikwete alipata nafasi ya kuzunguka kwa helikopta kuona athari za mafuriko hayo katika jiji na pia kutembelea kambi hiyo.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, watu zaidi ya 20 wamepoteza maisha na 4,900 wameathirika kwa kukosa makazi.

Aidha, vifo zaidi havijaripotiwa kwa kuwa bado baadhi ya nyumba zimezingirwa na maji na matope.

Akihutubia hadhara hiyo, Rais alisisitiza watu kuheshimu mikondo ya maji kwa kuwa hakuna mwanadamu anayeweza kuzuia maji, upepo au moto na kutolea mfano kwa Marekani, Australia na nchi zenye teknolojia ya juu, lakini maji huwashinda.

Rais Kikwete aliwaagiza Mipango Miji wafanye kazi ipasavyo kwa kuwa wao ndio wamekuwa vinara wa kugawa maeneo kwa hati halali wakati wakijua wazi ni maeneo hatari kwa maisha ya watu, mabondeni na kwenye mikondo ya maji.

“Maji hayana tajiri wala masikini, nilikuwa napita kwa helikopta nikaona hata kwenye kampuni ile Jangwani (Kajima) ukuta umeenda, Mipango Miji fanyeni kazi vizuri kuepusha yanayoweza kuepukika, mikondo ya maji iachwe nafasi, baadhi ya hawa watu wana hati halali, mmewapa ninyi,” alisema Rais.

Aidha, aliwahakikishia waathirika hao kufuatiliwa kwa karibu suala lao na kuwaahidi kuwa viongozi wakiwemo mameya, wabunge, madiwani na watendaji wahakikishe usiku na mchana watawahudumia mpate makazi maeneo yafaayo.

Awali, akihutubia, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sadiki alisema walioathirika ni 4,900 na vifo vilivyoripotiwa mpaka jana asubuhi ni 20 ambapo miili 18 imetambuliwa na miwili bado ipo Hospitali ya Taifa Muhimbili, aliwataka watu wakatambue miili hiyo.

Katika hotuba yake, Sadiki alisema uongozi wa mkoa kwa kushirikiana na viongozi wa kisiasa wamefikia hitimisho la kuwataka wakazi hao wa mabondeni kuridhia kuhama baada ya kutenga eneo katika Wilaya ya Kinondoni la ekari 2,000 linalotoa viwanja 2,800 ili wakazi hao waanze kujenga makazi mapya.

“Lakini tuna taarifa huko nyuma kwamba kuna waliopewa maeneo Wazo Hill, Yombo Dovya, hawakuhamia huko, wakauza na hata hizi huku wakauza, muda si mrefu shule zitafunguliwa hivyo tutahakikisha mnapata hifadhi ya dharura huko ili tuwapishe wanafunzi huku,” alisema Sadiki.

Kwa mujibu wake, kuna kambi zaidi ya saba jijini Dar es Salaam na vitu mbalimbali vimetolewa na wasamaria wema, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi yakiwemo mahema, vyakula, nguo, dawa na mikeka. Mbunge wa Ubungo, John Mnyika ametoa vitu vyenye thamani ya Sh milioni moja kwa kambi tano.

Gazeti hili lilitembelea katika baadhi ya kambi hizo kwa lengo kujionea hali ilivyo ambapo katika kituo cha Rutihinda, hadi saa 5.45 asubuhi, waathirika 52 waliokuwa wameandikishwa walilalamika kutokuwepo kwa huduma yoyote ikiwemo ya chakula, na magodoro tangu wafike kambini hapo juzi asubuhi.

Akizungumzia suala hilo, msimamizi wa kambi hiyo ambaye pia ni Mtendaji wa Kata ya Kigogo, Kassim Mbezi, alisema iliwalazimu baadhi ya waathirika kuondoka na kujitafutia hifadhi na chakula.

Walikuwa zaidi ya 100 kambini hapo na kubaki hao 52. “Hadi hivi sasa watu waliopo hapa ni 52, awali waliokuwepo wengi lakini wanapokuja na kukuta hali ya kambi ilivyo wanaamua
kuondoka na kurudi katika maeneo waliyotoka na wengine kwenda kujitafutia chakula kwa kuwa wana watoto,” alisema Mbezi.

Alipotafutwa Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuf Mwenda kwa lengo la kuzungumzia tatizo la kambi hiyo, alisema idadi kamili ya waathirika ndiyo kikwazo cha kufikishwa mapema kwa misaada hiyo na hadi kufikia muda huo, tayari walishaipata idadi yao hivyo utaratibu wa kuwafikishia misaada ulikuwa ukiendelea.

Kambi ya Azania iliyopo Manispaa ya Ilala iliyo na waathirika 426, hali ilikuwa ikiendelea vizuri na waathirika wote kupata mahitaji yao muhimu ikiwemo ya vyakula vilivyotolewa na taasisi mbalimbali na wasamaria.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa ya Kata ya Kariakoo, Mathias Muyenjwa, alisema ukiacha kituo hicho vituo vingine vilivyopo katika Kata ya Kariakoo na idadi ya waathirika katika mabano ni Mtambani A (343), Mtambani B (1,340) pamoja na Kariakoo Kaskazini yenye waathirika 302.

Kuhusu hali ya kambi hiyo, Muyenjwa alisema huduma mbalimbali zinaendelea kutolewa kwa waathirika ikiwemo ya afya huku akiitaja misaada iliyotolewa na kuwa ni michele, mikate, maji ya kunywa, juisi, mafuta ya kula, sabuni, mablangeti, mashuka pamoja na nguo za kawaida.

Baadhi ya waliotajwa kufa kutokana na mvua hizo ni Tulihama (65) mkazi wa Ubungo Msewe, Maganga Said (8) mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kanjenje Tabora, Gathi Mseti (30) na mwanawe Thomas Rashid (8) wakazi wa Kipunguni, Vian Maxmilian (13) mkazi wa Mburahati, Magreth Makwaya (6), mkazi wa Luhanga, Ibrahim Lusuma(60), mkazi wa Ubungo Msewe.
Chanzo: HabariLeo

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits