Wednesday, September 28, 2011

Helkopta Chadema yavuruga Igunga

Best Blogger Tips
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jana kilianza kutumia helkopta katika mikutano yake ya
kampeni za ubunge katika Jimbo la Igunga na kusababisha baadhi ya mikutano ya vyama vingine vinavyoshiriki kampeni hizo kuvunjika.

Helkopta hiyo inayoendeshwa na Kapteni Paul Denge iliwasili saa 6:00 mchana katika kiwanja cha Shule ya Msingi Choma cha Nkola na kusababisha walimu na wanafunzi kuvunja vipindi vya masomo kushuhudia chopa, pia wananchi waliikimbilia kwa baiskeli na pikipiki, kitendo kilicholazimisha walinzi wa Chadema kufanya kazi ya ziada kuzuia wananchi walionekana kutaka kuishika na kupiga picha.

Wakati Chadema kikianza kutumia helkopita hiyo na kupata wananchi wengi kwenye mikutano yao, Chama Cha Mapinduzi (CCM) jana kilikuwa kimesimamisha kampeni kusubiri helkopita zake mbili ambazo zilitarajiwa kuwasili muda wowote, zikitokea Dar es Salaam.

Nacho Chama cha Wananchi  (CUF), kilikutana na waandishi wa habari na kuwaeleza nia ya kuleta chopa kama hiyo, ili kuwafikia wananchi katika maeneo ya jimbo hilo ambalo kijiografia limekuwa na miundombinu isiyopitika kirahisi.

Mara baada ya helkopita hiyo kuwasili, iliwachukua viongozi wa Chadema, akiwemo Mwenyekiti, Bw. Freeman Mbowe, mgombea ubunge Bw. Joseph Kashindye na mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Morogoro, Bi. Susan Kiwanga pamoja na waandishi wa habari na kuelekea katika kijiji cha Chabiso.

Katika Kijiji cha Chabiso, CUF walikuwa wafanye mkutano eneo hilo lakini baada ya kukimbiwa na wananchi wote waliamua kuvunja mkutano na kuondoka.

Akizungumza katika mkutano kijijini hapo, Bw. Mbowe alisema CCM imekabwa kila kona na safari hii haitatoka, kisha akawataka wananchi kufumbua macho kwa kuwa saa ya ukombozi imefika kwani wameteseka ndani ya miaka 50 bila mafanikio.

“Nawaambia ndugu zangu Chadema imeikamata CCM kweli kweli hadi kufikia hatua ya kutuogopa, safari hii tutabanana na ninawahakikishia hawatoki, tumejipanga kupambana nao. CCM inaogopa sana Chadema ndiyo maana mnasikia kila siku kwamba wanasema chama chetu ni cha fujo, siyo kweli wameona tunakubarika kwa Watanzania roho imeanza kuwadunda,” alisema.

Aliwataka wananchi hao kuwa wanakabiliwa na mtihani mkubwa ambao hivi sasa Watanzania wote wameelekeza macho na masikio yao kwao, kusikia wataamua nini juu ya hatma ya kupata kiongozi atakayewasaidia matatizo yanayowakabili.

“Nimepata taarifa kwamba kuna matatatizo makubwa yakiwemo maji, zahanati na barabara, lazima mfanye maamuzi mazuri, CCM hii ni ya matajiri ambao wanawakumbuka kila uchaguzi unapofika lazima muonyesha miaka 50 ya uhuru wa Tanzania wameshindwa kumaliza kero zenu.

…Lakini pia nimesikia hapa kuna chakula cha msaada kinagawiwa, hizi ni fedha zenu si za CCM, kama wanavyopita humo wanawadanganya…kama kuna mwanachama wetu yeyote atakayenyimwa atoe taarifa kwa viongozi wetu haraka, kwa sababu ni haki yenu kupata chakula,” alisema.
Endelea kusoma habari hii.................

Monday, September 26, 2011

Prof Wangari Maathai afariki dunia

Best Blogger Tips
Mtunukiwa wa tuzo ya Amani ya Nobel Prof Wangari Maathai ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 71.

Mwanaharakati huyo mashuhuri wa mazingira na haki za binadamu wa Kenya Profesa Wangari Maathai amefariki dunia mjini Nairobi usiku wa kuamkia , Jumatatu kutokana na maradhi ya saratani.

Prof Karanja Njoroge ambaye ni mkurugenzi wa Green Belt Movement, shirika ambalo Prof Maathai alilianzisha amethibitisha kifo hicho.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari Prof Njoroge amesema wakati wa kifo chake Wangari alikuwa na wanafamilia na marafiki.

Marehemu ameacha watoto watatu, wawili wakiume na mmoja wa kike.

Profesa Wangari Maathai alipata tuzo la amani ya Nobel mwaka 2004, kufuatia juhudi za kupigania uhifadhi wa mazingira nchini Kenya.

Mbali ya kuwa Mwanaharakati wa Maswala ya Mazingira na haki za binadamu , Wangari Maathai pia alikuwa mwanasiasa shupavu.

Amewahi kuhudumu kama Mbunge na Naibu waziri wa Mazingira nchini Kenya.

Prof Maathai pia katika uhai wake alipata tuzo mbalimbali za kimataifa kwa kutambua mchango wake.

Prof. Wangari Muta Maathai alianzisha vuguvugu la Green Belt mnamo mwaka 1977, ambapo alifanya kazi na wanawake kote nchini kuboresha maslahi yao na kuhifadhi mazingira.

Alikuwa mtetezi mashuhuri wa matumizi bora ya mali asili .Shughuli zake zilitambuliwa mara kwa mara kote duniani.
Chanzo: BBC

Saturday, September 24, 2011

Liyumba atoka jela

Best Blogger Tips
Hatimaye aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu Tanzania (BoT), Amatus Liyumba (63), jana aliachiwa huru na Jeshi la Magereza, baada ya kumaliza kifungo chake cha miaka miwili kwa kosa la matumizi mabaya ya ofisi.

Liyumba aliachiwa jana asubuhi baada ya kutumikia kifungo cha miaka miwili alichohukumiwa na jopo la mahakimu wawili kati ya watatu waliosikiliza kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na NIPASHE jana majira ya saa 4:42 asubuhi, kwa njia ya simu, msemaji wa jeshi hilo, Kamishna Mwandamizi, Omary Mtiga, alisema kuwa Liyumba aliachiwa baada ya kumaliza kifungo chake mapema saa 3:00 asubuhi na kuongeza kuwa alikuwa huru rasmi nje ya gereza la Ukonga jijini Dar es Salaam. 

“Ndiyo Liyumba ameachiwa leo (jana) asubuhi kwa sababu ameshamaliza kutumikia adhabu ya kutumikia kifungo cha miaka miwili katika gereza la Ukonga, jijini Dar es Salaam,” alisema Kamishna Mtiga.

Mei 24, mwaka jana, mahakimu wawili, Lameck Mlacha na Benedict Mwingwa kati ya watatu walitoa hukumu iliyomtia hatiani bosi huyo wa zamani wa BoT, ambaye alihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela.

Liyumba alituhumiwa kutumia madaraka yake vibaya na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh. bilioni 221 kupitia kwenye mradi wa ujenzi wa majengo pacha ya benki hiyo.

Hukumu ya Hakimu Edson Mkasimongwa ilimuona Liyumba ana hatia katika kosa hilo.

Mbali na kuachiwa huru, Liyumba yuko nje kwa dhamana kwa shtaka la kukutwa na simu gerezani kinyume na kifungu namba 86 kidogo cha kwanza na cha pili cha Sheria ya Jeshi la Magereza.

Ilidaiwa kuwa Julai 27, mwaka huu kinyume cha sheria hiyo ya magereza, Mkurugenzi huyo wa zamani, alikutwa na simu ya mkononi aina ya Nokia 1280 ya rangi nyeusi iliyokuwa inatumia laini namba 0653-004662 pamoja na namba ya utambulisho ya simu (IMEI) 356273/04/276170/3.

Ilidaiwa kuwa mshtakiwa alikutwa na simu hiyo katika chumba chake cha magereza bila kuwa na kibali cha kufanya hivyo huku akijua ni kosa.

Mshtakiwa alikana shtaka hilo na mahakama ilimtaka kujidhamini kwa hati ya dhamana ya Sh. 50,000 na mdhamini mmoja ambaye ni mtumishi wa serikali au kutoka kwenye taasisi inayotambulika.

Mshtakiwa alitimiza masharti hayo na mahakama ilimuachia kwa dhamana hadi Septemba 29, mwaka huu.

Friday, September 23, 2011

Waziri amuumbua daktari

Best Blogger Tips
NAIBU Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Lucy Nkya, ameelezea udhaifu wa utoaji huduma za afya kwa baadhi ya hospitali nchini, baada ya kwenda katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru na kuandikiwa dawa bila kujieleza kwa daktari.

Dk. Nkya alisema hayo wakati akizungumza na menejimenti, wafanyakazi na wanafunzi wa uuguzi na udaktari katika Hospitali Teule ya Halmashauri ya Wilaya ya Hai, baada ya kupata hati rasmi ya kutambua kupanda hadhi kwa hospitali hiyo.

Huku akiitaja hospitali hiyo, Naibu Waziri alisema alifika hapo bila kujitambulisha huku amejifunika nguo hadi usoni akaingia kwa daktari ambaye hakumtaja jina, lakini daktari huyo alimwandikia dawa bila kumwuliza tatizo lake.

“Niliingia kwa daktari na kabla sijakaa, akaanza kuniandikia vipimo huku akinihoji kama nina homa na shinikizo la damu (BP), nilimjibu nitajuaje wewe ndiye mtaalamu, akanieleza tena natakiwa kupigwa picha za mionzi (X-ray), nilishangaa sana,” alisema.

Alisema kutokana na hali ile, alimweleza daktari husika kwamba anatakiwa amsikilize kabla ya vipimo, lakini katika hali ya kushangaza, alisisitiza kuwa anatakiwa kwenda kupigwa picha za X-ray.

“Niligundua kuwa daktari yule alikuwa amedhamiria na analosema nilijitambulisha kwamba mimi ni Dk. Lucy Nkya, Naibu Waziri … alipatwa mshtuko, nikamhoji kama ndivyo anavyotoa huduma kwa wananchi wa kawaida, nilimwonya nikaondoka,” alisema.

Alisema aliondoka na kuahidi kurejea wakati mwingine bila kutambulika, ili kuangalia mwenendo wa mtumishi huyo kama anatekeleza wajibu wake kulingana na sheria, kanuni na taratibu za utoaji tiba.

Akizungumza na watumishi wa hospitali hiyo teule, alisema imekuwa miongoni mwa hospitali teule 34 nchini na kuwataka watumishi wake kuzingatia kanuni na taratibu za afya kwa kutoa huduma kulingana na viapo vya taaluma yao.

“Ninyi leo mmepata hati rasmi ya utambuzi kuwa Hospitali Teule ya Wilaya ya Hai, hakikisheni mnatimiza wajibu wenu … hii sasa ni hospitali ambayo inatoa huduma kwa vigezo vya Serikali, nisingependa kusikia malalamiko dhidi yenu,” alionya.

Aliitaka Halmashauri ya Hai kutohamisha watumishi wa hospitali hiyo kwa namna yoyote na badala yake wajitahidi kukabili changamoto zilizopo ili iweze kutekeleza wajibu wake.

“Sasa Serikali itakuwa ikilipa mishahara na marupurupu kwa watumishi wa hospitali hii, tukisikia halmashauri mnahamisha watumishi au kutumia fedha zinazotumwa ili kufanyia vikao, safari za namna yoyote … tutawachukulia hatua kisheria,” alisema.

Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Dk . Saitore Laizer, aliiomba Serikali ianze kutoa ruzuku ya mishahara, dawa, vifaa tiba na vitendanishi kwa hospitali hiyo, ili wananchi wapate huduma kwa gharama nafuu kama ilivyo kwa hospitali zingine za umma.

Alisema changamoto nyingine ni uhaba wa watumishi unaosababishwa na kuhama kwa watumishi kutoka mashirika ya dini na ya binafsi kwenda serikalini, jambo ambalo limeiathiri hospitali hiyo hususani idara za meno na macho.
Chanzo ; HabariLeo

Thursday, September 22, 2011

Michael Sata ashinda uchaguzi Zambia

Best Blogger Tips
Mshindi wa uchaguzi wa Zambia Michael Sata
Kiongozi wa chama cha Patriotic Front, Micheal Sata ametangazwa kwa mshindi wa uchaguzi wa urais nchini Zambia

Bw Sata alipata asilimia 43 ya kura zilizopigwa na kumshinda Rais Rupiah Banda wa chama tawala cha MMD ambacho kimekuwa mamlakani kwa muda wa miaka 20.

Tangazo hilo lilitolewa na Jaji Mkuu wa Zambia Ernest Sakala.

Awali watu wawili waliuawa kufuatia ghasia katika maeneo ambayo ni ngome ya upinzani.

Mkuu wa Polisi wa jimbo hilo maafuru kwa uzalishaji Shaba ameliambia shirika la habari la Reuters watu wamejitokeza katika barabara za mji wa Kitwe na Ndola wakivurumisha mawe.

Mwandishi wa BBC anasema ghadhabu hizi zimechochewa na agizo la serikali kupiga marufuku vyombo vya habari kutangaza matokeo bila ya idhini ya tume ya uchaguzi ya nchi hiyo.

Mwandishi wa BBC Mutuna Chanda akiwa Lusaka kilomita 300 kusini mwa Kitwe, anasema huko Kitwe, waandamanaji waliteketeza soko moja usiku na Polisi wameweka vizuwizi katika mji wa Wusaikile.

Rais Banda alimshinda Bw Sata kwa kura 35,000 katika uchaguzi wa mwaka 2008, matokeo yaliozusha ghasia kutoka upande wa upinzani katika ngome zao za mijini.

Tangu uchaguzi wa mwaka 2008, watu wengine milioni moja wamejiandikisha kuwa wapiga kura,wengi wao vijana wasio na ajira.
Chanzo: BBC

Upinzani waelekea kushinda Zambia

Best Blogger Tips
Bwana Michael Sata
 KIONGOZI wa upinzani nchini Zambia, Michael Sata, anaelekea kushinda katika Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo, uliofanyika Jumanne wiki hii katika nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa madini ya shaba.

Hata hivyo, ghasia kubwa ziliripotiwa kuibuka katika Jimbo la Kaskazini mwa Zambia la Ukanda wa Shaba, kwenye ngome kuu ya Sata, kufuatia kusitishwa kwa matokeo ya awali ya uchaguzi, yaliyokuwa yakionyesha kwamba kiongozi huyo anaongoza dhidi ya Rais anayemaliza muda wake, Rupiah Banda.

Matokeo ya awali ya uchaguzi huo uliofanyika Jumanne wiki hii, yalitangazwa jana jioni na Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo, yakionyesha kuwa Sata alikuwa akiongoza kwa kura 639,787 dhidi ya 542,362 za Banda, ambaye ni kiongozi wa Chama cha The Movement for Multi-party Democracy (MMD) kilichotawala taifa hilo tangu 1991.
Matokeo yaliyotangazwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zambia, Irene Mambilima yalikuwa ni yale yaliyokusanywa katika majimbo 85 kati ya 150.

Hatua ya kusitishwa kwa matokeo yaliyokuwa yakimpa matumaini Sata (74) maarufu kwa jina la "King Cobra" kutokana na kauli zake kali, kumezusha ghasia kubwa kutokana na kuwapo kwa hisia za wizi wa kura.
Wakati matokeo ya uchaguzi huo yakisubiriwa kwa hamu, Mahakama Kuu ya nchi hiyo imevizuia vyombo vya habari kutangaza matokeo kabla ya kutolewa na Tume ya Uchaguzi.

Amri ya Mahakama Kuu ilitolewa kufuatia ombi lililowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Zambia. Jaji wa Mahakama Kuu, Jane Kabuka, alisema wanavizuia vyombo vya habari kutangaza au kuchapisha matokeo yasiyo rasmi hadi yapate idhini ya Tume ya Uchaguzi.

Katika toleo lake la juzi, gazeti binafsi la The Post lilikuwa na kichwa cha habari kuwa Satta ameshinda uchaguzi huo. Na hata baada ya pingamizi hilo la Mahakama Kuu, jana tena gazeti hilo liliandika kuwa kiongozi huyo wa upinzani anaongoza kwa 59%.

Hatua hiyo ya Mahakama Kuu  imekuja huku Tume ya Uchaguzi  ikisema kuwa wezi wa mitandao wameingilia mtandao wao na kuweka matokeo ya uongo yanayoonyesha kuwa kiongozi wa chama cha upinzani cha Patriotic Front, Satta, anaongoza.

Msemaji wa Tume hiyo, Cris Akufuna, alisema kutokana na hitilafu hiyo maofisa wake wanafanya kazi kuhakiki zaidi ya mara mbili matokeo kutoka maeneo mbalimbali.Alisema mchakato huo umesababisha kuchelewa kutolewa kwa matokeo, hali ambayo imeanza kuzua hofu ya kwamba matokeo ya uchaguzi huo yamefanyiwa hila.

Katika maeneo kadhaa tayari washabiki wa kiongozi huyo wa upinzani wameanza kusherehekea wakiamiani kuwa kiongozi wao ameshinda.Rais Banda anatarajiwa kupata kura nyingi katika maeneo ya mikoani, ambako kuna uwezekano wa matokeo kutolewa taratibu, kuliko maeneo ambayo ni ngome ya  upinzani, ambayo ni mji mkuu Lusaka na maeneo ya Ukanda wa Shaba, ambako ndiko kitovu cha uchumi wa Zambia.

Hata hivyo, kwa mujibu wa duru za habari ni mapema mno kusema iwapo Satta, yuko katika nafasi nzuri ya kushinda na kukiondoa madaraka chama tawala kwa mara ya kwanza tokea kumalizika kwa mfumo wa chama kimoja mwaka 1991.Akufuna alisema bado wanaendelea kupokea matokeo kutoka maeneo mbalimbali na kwamba mpaka itakapofika leo jioni watatangaza matokeo rasmi.

Vurugu mpaka Mbeya
Mpaka wa Zambia na Tanzania katika eneo la Tunduma mkoani Mbeya umefungwa upande wa Zambia kutokana na vurugu zinazoendelea maeneo mbalimbali ya nchi hiyo. Maeneo hayo ni pamoja na mji wa Nakonde  katika mpaka huo upande wa Zambia, ambako  magari yanadaiwa kupigwa mawe.

 Habari kutoka ndani ya  vyombo vya usalama Mkoa wa Mbeya zinadai kuwa katika mji huo unaopakana na Tunduma,  kumezuka vurugu ambapo wananchi wa Nakonde wamekuwa wakifanya vurugu kwa kupiga mawe magari, huku polisi nao wakituliza vurugu hizo kwa kurusha mabomu ya machozi.

 "Vurugu hizi zipo mpakani  upande wa Zambia kwani hata  wenzetu Zambia wameamua kufunga mpaka, lakini siyo kiofisi ni kienyeji kwa ajili ya kuzuia vurugu zisiweze kuvuka upande wetu wa Tanzania na  kuepusha mali, yakiwamo magari kuharibiwa na vurugu hizo,"inadai taarifa hiyo.

 Taarifa hizo zilisema kuwa, magari yaliyopigwa mawe ni pamoja na basi aina ya Taqwa linalofanya safari zake kutoka Tanzania kwenda Zambia na lori la mkoani Iringa  la kampuni ya Asasi ambapo yalipigwa mawe yakiwa  mpakani upande wa Zambia.

 Aidha, kwa upande wa Tanzania katika mji wa Tunduma hakuna kinachoendelea, kwani malori yote yaliyopo Tunduma yamezuiwa kuvuka mpaka hadi hapo vurugu hizo zitakapotulia.
Chanzo: Mwananchi

Wednesday, September 21, 2011

Msuya aonya Serikali isicheze na mgawo umeme

Best Blogger Tips
WAZIRI Mkuu Mstaafu, Cleopa Msuya ameitahadharisha Serikali kuwa makini na suala la mgawo wa umeme ambao amesema unaongeza ugumu wa maisha kwa wananchi, kwani unaweza kusababisha matatizo makubwa kiasi cha nchi kushindwa kutawalika.“Hali ikiendelea hivi tusishangae kutokea kwa mambo kama yaliyotokea kwa nchi za Kiarabu ambazo wananchi wake wameshindwa kuvumilia ugumu wa maisha na kuamua kuandamana.”  Msuya alitoa tahadhari hiyo, Dar es Salaam jana wakati wa mjadala wa kitaifa  kuhusu miundombinu, nishati na madini kwenye Wiki ya Maonyesho ya Miaka 50 ya Uhuru yaliyoandaliwa na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).

Angalizo la Msuya inakuja kipindi ambacho nchi ipo katika mgawo wa umeme kutokana na uhaba mkubwa wa nishati hiyo hali ambayo inaathiri sekta mbalimbali za uzalishaji na watumiaji wa kawaida.

Msuya alikuwa Waziri Mkuu kati ya Novemba 7, 1980 hadi Februari 24, 1983 na kushika tena wadhifa huo Desemba, 1994. Pia aliwahi kuwa Waziri wa Fedha, Viwanda katika vipindi tofauti.

Ili kukabiliana na tatizo hilo, Serikali kupitia kwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja ilitangaza mpango wa dharura wa Sh1.2 trilioni kukabiliana na mgawo, lakini hadi sasa hakuna mabadiliko yoyote yanayoonekana tangu ulipoasisiwa Agosti, mwaka huu.

Kauli ya Msuya
Msuya alisema Tanzania inahitaji uchumi unaokua na kwamba Serikali isipoangalia, tatizo la kushindwa kukua kwa uchumi, maendeleo ya nchi hayatafanikiwa.  “Kabla ya uhuru idadi ya watu ilikuwa milioni nane na sasa tuko zaidi ya watu 53 milioni, kuna haja ya kuwa na uchumi unaokua badala ya kuzalisha bila mafanikio, Serikali iwe makini katika kuimarisha mambo muhimu kama nishati,” alisema na kuongeza:

“Serikali inatakiwa kufikiri juu ya kuimarisha masuala ya umeme nchini wakati wawekezaji wanapoingia ili kusaidia uchumi kukua haraka na kuepusha kutokea kwa mambo yaliyozikumba nchi za Kiarabu.”  Ingawa hakuzitaja nchi hizo, lakini Misri, Tunisia, na Yemen ndizo zilikumbwa na maandamano kupinga hali ngumu ya kiuchumi na kusababisha viongozi wa Misri na Tunisia na kung’olewa madarakani.

Msuya alisema Serikali ina jukumu la kuimarisha mazingira yatakayoendeleza uchumi na kwamba ipo changamoto kubwa ya kuziunganisha sekta binafsi ili kuinua uchumi.  “Tatizo ni namna Serikali itakavyokubaliana na sekta binafsi katika kuimarisha uchumi wake na kuwainua wananchi kibiashara kwa sababu miundombinu ya uzalishaji hasa umeme bado haijasambaa katika mikoa yote,” alisema.

Alisema Serikali itakapoiunganisha mikoa 26 katika kuzalisha biashara na kuipatia nguvu ya umeme, itakuwa njia mojawapo ya kuimarisha mafanikio ya kila mwananchi na kuondokana na umaskini. “Sasa hivi tunaambiwa kuwa kuna fungu la fedha la kutekeleza kilimo, lakini bado kuna maswali mengi ya kujiuliza juu ya uwezeshwaji wa kilimo, kwa sababu maeneo ya vijijini ambayo ndiyo yanayojishughulisha na kilimo hayana umeme, Kilimo Kwanza kitatekelezwaje?,” alihoji Msuya.  Msuya alisema, ipo haja kwa Serikali kuangalia namna ya kuboresha mazingira ya kiutendaji ya halmashauri mikoani ili kila mkoa uunganishiwe umeme kirahisi.
 
Kauli ya Ngeleja

Ngeleja akizungumza kwenye hafla hiyo alisema, Serikali imetoa fursa kwa sekta binafsi kuwekeza hasa katika masuala ya nishati ili kuzalisha, kusambaza na kusafirisha.Alisema sekta binafsi imepewa jukumu hilo ili kuzalisha zaidi na kuimarisha uchumi wa nchi kwa kiwango kinachotakiwa na kuboresha miundombinu yake.

“Tangu Serikali ilipofanya mageuzi ya kisera katika uendeshaji uchumi wa nchi, sekta binafsi imekuwa ikiongezewa nguvu ya biashara hivyo ni vyema sekta hiyo ikatumia fursa ya kuwekeza zaidi katika sekta muhimu na kuzingatia sera ya nishati ya mwaka 2008,” alisema.

Alisema matatizo ya umeme yaliyopo yanatokana na mfumo wa kuunganisha umeme na kiwango kikubwa kinachopotea kutokana na usambazaji kuanzia katika chanzo cha umeme.

“Uwekezaji mdogo katika umeme unaochukua muda mrefu pia ni chanzo kikubwa katika kuchangia umeme, tozo zinazotozwa hazikidhi mahitaji yaliyopo na gharama kubwa za mafuta katika soko la dunia zinaongeza gharama za uzalishaji,” alisema.  Akizungumzia tatizo la mgawo wa umeme, Ngeleja alisema uchumi wa nchi umeporomoka kwa asilimia 6.9 na kuwa megawati 236 za mgawo huo kwa siku moja zinagharimu Dola za Marekani 400 milioni (takriban Sh500 bilioni).

 Mgawo wa umeme umekuwa ukiitikisa nchi zaidi tangu mwaka 2006 na hadi sasa Serikali imekuwa na mipango mingi ukiwamo ule uliopitishwa na Bunge hivi karibuni, kuonekana kukosa tija.  Katika mpango huo wa dharura, Serikali ilitangaza kuwa itatumia kiasi hicho cha Sh1.2 trilioni kwa ajili ya  mpango huo wa ili kunusuru uchumi wa nchi kuanzia Agosti hadi Desemba mwaka huu na Januari hadi Desemba mwakani. 

 Wiki moja iliyopita, Waziri Ngeleja alitoa ahadi ya kupungua makali ya mgawo huo lakini hadi sasa, hakuna nafuu iliyojitokeza.
Chanzo: Mwananchi

Wednesday, September 14, 2011

Rais Kikwete ateua wakuu wapya wa mikoa 15

Best Blogger Tips
RAIS Jakaya Kikwete amewateua wakuu wa mikoa wapya 15, kuwabadilisha vituo vya kazi wakuu wa mikoa watano huku wengine saba wakielezwa kwamba wamestaafu kwa mujibu wa taratibu. Katika uteuzi huo, wa wakuu wa mikoa 21, kati yao 11 walikuwa wakuu wa wilaya na ni Perseko Ole Kone pekee aliyebaki katika kituo chake cha kazi cha Mkoa wa Singida.

Mbali ya idadi kubwa ya wakuu wa wilaya waliopandishwa vyeo, katika uteuzi huo, Rais Kikwete pia amewateua waliokuwa Manaibu Waziri watatu, Mwantumu Mahiza, Ludovick Mwananzila na Joel Bendera, kuwa wakuu wapya wa mikoa.

Taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu iliyotolewa Dar es Salaam jana iliwataja wakuu hao wa wilaya waliopandishwa vyeo na mikoa yao katika mabano kuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, John Tupa (Mara), DC wa Morogoro, Saidi Mwambungu (Ruvuma), Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Chiku Gallawa (Tanga), DC wa Ilala, Leonidas Gama (Kilimanjaro), DC wa Newala, Dk Rehema Nchimbi (Dodoma), Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Elaston Mbwillo (Manyara).

Wengine ni DC wa Karagwe, Kanali Fabian Massawe (Kagera), DC wa Mvomero, Fatma Mwassa (Tabora), DC wa Manyoni, Ali  Rufunga (Lindi), DC wa Kilombero, Mhandisi Ernest Ndikillo (Mwanza), DC wa Bagamoyo, Magesa Mulongo (Arusha). Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Stella Manyanya ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.
Katika uteuzi huo, Mahiza anakwenda Mkoa wa Pwani, Bendera ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na Mwananzila Shinyanga. Kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Mahiza alikuwa ni Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi pamoja na Mwananzila huku Bendera akiwa ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo.

Waliobadilishwa vituo vya kazi ni Abbas Kandoro anayekwenda Mbeya akitokea Mwanza, Said Mecky Sadiki anayehamia Dar es Salaam akitokea Lindi, Christine Ishengoma anayekwenda Iringa akitokea Ruvuma, Luteni Kanali Issa Machibya kutoka Morogoro kwenda Kigoma na Kanali Joseph Simbakalia anakwenda Mtwara akitokea Kigoma.

Wakuu wa mikoa waliostaafu ni Mohammed Babu aliyekuwa Kagera; Isidore Shirima (Arusha), Kanali Anatory Tarimo (Mtwara), John Mwakipesile (Mbeya), Kanali Enos Mfuru (Mara), Brigedia Jenerali Dk Johanes Balele (Shinyanga) na Meja Jenerali   Said Kalembo (Tanga).

Wakuu wa wanne wa mikoa waliostaafu ambao watapangiwa vituo vingine vya kazi ni Amina Mrisho aliyekuwa Pwani, Dk James Msekela aliyekuwa Dodoma, Abeid Mwinyimusa aliyekuwa Tabora na Daniel Ole Njoolay wa Rukwa.

Taarifa hiyo ya Ofisi ya Waziri Mkuu imesema: “Wakuu wa mikoa mipya minne ya Simiyu, Geita, Katavi na Njombe itakayoundwa baada ya taratibu kukamilika watatangazwa baadaye.”

Taarifa hiyo iliongeza: "Wakuu wote wa mikoa waliopo sasa wameagizwa kuandaa hati za makabidhiano katika muda wa siku 14 kuanzia siku ya kuapishwa kwa wakuu wapya wa mikoa. Aidha, wakuu wa wilaya ambao wamepandishwa vyeo kuwa wakuu wa mikoa nao wanapaswa kufanya hivyohivyo kwa ajili ya wakuu wa wilaya watakaopangiwa vituo vitakavyokuwa vimeachwa wazi kutokana na uteuzi wao.”

"Makabidhiano hayo lazima yahusishe pia kutembelea kwa pamoja baadhi ya maeneo na miradi ambayo ni muhimu kama sehemu ya makabidhiano yao," ilisisitiza taarifa hiyo na kuongeza:

"Wakuu wote wa mikoa walioteuliwa na wakuu wa mikoa minne mipya watakaoteuliwa pamoja na wakuu wote wa wilaya watakaoteuliwa baada ya zoezi kukamilika watatakiwa kuhudhuria mafunzo ya wiki tatu kwenye Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo, Dodoma kwa lengo la kuwajengea uwezo zaidi wa kiuongozi na kiutendaji.”

Wakuu hao wapya wa mikoa wataapishwa na Rais Kikwete kesho saa 4.00 asubuhi kwenye Viwanja vya Ikulu, Dar es Salaam.
Chanzo: Mwananchi

Monday, September 12, 2011

Miss Universe 2011 ni Leila Lopes Kutoka Angola

Best Blogger Tips
Miss Universe 2011 Leila Lopes
Miss Angola Leila Lopes amevishwa taji la Miss Universe 2011 katika mchuano uliofanyika siku ya jumanne katika jiji la Sao Paulo nchini Brazil.

Lopez, alikuwa katika la watu watano walioweza kufika katika fainali za mashindano hayo. Wengine walikuwa ni kutoka China, Brazil, Philippines, Ukraine na Panama.

Nchi zilizoingia katika kumi bora ni Australia, Costa Rica, France, Ukraine, Portugal, Panama, Philippines, Angola, China na Brazil.

Lopez ameweza kuwashinda washiriki wengine 88 kutoka nchi mbambali duniani zilizoshiriki mashindano hayo ikiwamo Tanzania.

Mashindano hayo yalikuwa ni ya 60 kufanyika tangu yaanzishwe 1952.




Boma la mafuta lalipuka Kenya na kuua zaidi ya 100

Best Blogger Tips
Waokozi wakisaidia watu baada ya Bomba kulipuka mjini Nairobi
 Zaidi ya watu mia moja wamekufa baada ya bomba la mafuta kupasuka na kulipuka katika katika mji mkuu wa Kenya Nairobi, polisi wamesema.

Mlipuko huo umetokea katika eneo la viwandani la Lunga Lunga na askari wa zima moto walipambana na moto mkali ambao ulikuwa ukitishia makazi ya watu mjini humo.

Bomba hilo la mafuta limepita katika makazi ya watu wengi kwenye mitaa ya mabanda katikati ya mji wa Nairobi na Uwanja wa ndege.

Zaidi ya majeruhi 100 wamepelekwa hospitali, maafisa wanasema.

Msemaji wa magari ya huduma za dharura alisema waathirika wengi waliungua kiasi cha kutokufatambulika.

Taarifa zinasema mlipuko huo huenda umesababishwa na kishungi cha sigara kilichotupwa katika mtaro wa maji ambao ulikuwa ukielea mafuta.

Mafuta hayo yalivuja kutoka kwenye tangi moja katika ghala linalomilikiwa na Kampuni ya Mafuta ya Kenya, msemaji wa polisi Charles Owino ameliambia shirika la habari la Reuters.

‘Miili yaelea

Polisi na jeshi wameweka vizuizi katika eneo hilo, ambapo wakazi walisema kuvuja kwa mafuta kwenye bomba hilo na kusababisha watu wengi kukimbilia kuchota mafuta yaliyovuja.

"Kulikuwa na sauti kubwa ya mlipuko, mlipuko mkubwa, na moshi na moto ukiwaka juu angani," mkazi mmoja Joseph Mwego aliliambia shirika la habari la AFP.

Sehemu ya miili ilionekana ikiungua kiasi cha mita 300 (futi 1,000) karibu na eneo la tukio, wenyeji walisema.

Miili mingine likuwa inaelea katika mto karibu na eneo hilo ambapo watu walioungua iliripotiwa waliruka baada ya kushika moto.

Vibanda vilivyoezekwa kwa mabati vimejengwa karibu kabisa na bomba hilo, wakazi walisema.

Kumekuwa na vifo vingine ambavyo vimetokana na watu kuchota mafuta yanayovuja: Zaidi ya watu mia moja walikufa eneo la Molo, magharibi mwa Kenya mwaka 2009 baada ya lori la mafuta kupinduka na moto kulipuka.
Chanzo: BBC

Saturday, September 10, 2011

Ajali ya meli Zanzibar: Mamia wafariki

Best Blogger Tips
Watu wasiopungua 187 wamekufa baada ya meli iliyokuwa imezidisha mizigo kuzama katika pwani ya kisiwa cha Zanzibar ikiwa na watu takriban 800.

Msemaji wa serikali amesema watu 620 walionusurika wameokolewa. Serikali imetangaza siku tatu za maombolezo.

Inadhaniwa kuwa meli hiyo ilizama baada ya injini yake kukosa nguvu.

Shughuli za uokoaji zilikwazwa kwa kuwa meli hiyo ilizama usiku.

Zaidi ya watu 100 bado hawajulikani walipo, lakini watu 325 walionusurika wameokolewa, kwa mujibu wa waziri wa masuala ya dharura wa Zanzibar.

Meli hiyo, MV Spice Islander ilikuwa ikisafiri kati ya Kisiwa kikuu cha Unguja kuelekea Pemba.
Meli hiyo ilikuwa ikirejesha watu baada ya kumalizika kwa mfungo wa Ramadhani.

Msaada

Mamlaka za huko zimezidiwa na tukio hilo na zimeomba msaada kutoka nje.

Serikali ya Zanzibar imeunda kituo cha uokoaji na kutoa wito kwa taasisi zote kusaidia katika shughuli za uokozi. Serikali hiyo pia imeomba msaada kutoka nchi nyingine za nje, kama vile Kenya na Afrika Kusini.

Walionusurika walichukuliwa na boti za kibinafsi na kupelekwa katika bandari ya Zanzibar, amekaririwa kamishna wa polisi wa Zanzibar Mussa Hamis.

Miili ya watu imekuwa ikisukumwa katika pwani ya Zanzibar na mawimbi. Mpaka sasa miili ya watu 100 wamepatikana, amesema mwandishi wa BBC Ali Saleh akiwa Zanzibar.

Maelfu ya ndugu na jamaa wanasubiri kusikia taarifa za ndugu zao ambao walikuwa ndani ya meli hiyo, anasema mwandishi wetu.

Mohhamed Aboud, waziri wa masuala ya dharura wa Zanzibar anasema watu 259 walionusurika wameokolewa lakini 40 kati yao wamejeruhiwa sana.

Catherine Purvis, mtalii kutoka Uingereza aliyepo Zanzibar, akisubiri boti ya kwenda Dar es Salaam amesema ameshuhudia miili ya watu wengi ikitolewa ndani ya maji.

"Nimesimama katika bandari ya Zanzibar nikiwa na watalii wengine kama 10 wa Marekani na Uingereza.

"Boti yetu imechelewa kwa sababu wanatumia vyombo vyote vya baharini kuokoa watu".

Rubani mmoja wa helikopta Kapteni Neels van Eijk alipita juu ya eneo la tukio.

"Tuliona walionusurika wakiwa wameshikilia magodoro na majokofu au chochote kile kinachoweza kuelea. Ni vigumu kusema idadi kamili, lakini naweza kusema walikuwepo zaidi ya watu 200 walionusurika ndani ya maji na miili ya watu pia," ameiambia BBC.

"Wakati huo, kulikuwa na boti chache zilizofika katika eneo hilo. Walikuwa wakitafuta walionusurika, ingawa bahari haikuwa imechafuka sana, mawimbi walikuwa makubwa, kwa hiyo ilikuwa vugumu kuona walionusurika.

"Tulirusha ndege yetu na kuziongoza boti hadi kwa watu walionusurika ili waweze kuwachukua. Kulikuwa na miili kadhaa ndaniya maji."

Meli hiyo iliondoka Unguja takriban saa tatu usiku saa za Afrika Mashariki na inadhaniwa kuwa ilizama majira ya saa saba usiku.

Ilikuwa imebeba abiria wengi kiasi kwamba baadhi ya abiria waligoma kupanda, amekaririwa abiria mmoja aliyenusurika Abdullah daid, akizungumza na shirika la habari la AP.
Chanzo: BBC



Friday, September 9, 2011

Hatimaye BAE yakubali kuilipa Tanzania fedha za Rada

Best Blogger Tips
Kampuni ya kutengeneza silaha za kijeshi ya Uingereza BAE Systems, hatimaye imekubali kuilipa moja kwa moja serikali ya Tanzania dola milioni 47.

Fedha hizo ni malipo ya ziada yaliyotokana na mauzo ya Rada ambayo yalikuwa ni zaidi ya fedha halisi ya ununuzi wa rada hiyo .

Uamuzi huo unahitimisha mvutano wa muda mrefu kuhusu ununuzi wa rada hiyo ambao ulifanyika katika mazingira ya rushwa na kusababisha mahakama nchini Uingereza kuamuru fedha hizo zirejeshwe Tanzania
Kampuni ya BAE Systems ilishutumiwa na wabunge wa Uingereza kwa kujivuta kutekeleza amri ya mahakama iliyotolewa zaidi ya mwaka mmoja uliopita .

Serikali ya Uingereza ilisema imeiambia BAE kuwa hawana budi kulipa malipo hayo na kutarajia kuwa suala hilo lingefikiwa muafaka kwa faida ya watanzania.

Awali katika taarifa yake rasmi BAE ilisema inafanya kazi na serikali ya Uingereza kupitia wizara yake ya Maendeleo ya Kimataifa (DFID) kutoa malipo hayo kulingana na utaratibu wao.

BAE haikuwa tayari kuilipa serikali ya Tanzania fedha hizo na ilitaka ilipe kupitia misaada yake kwa mashirika ya hisani ya Uingereza yanayofanya kazi nchini Tanzania.

Akizungumza na BBC Idhaa ya Kiswahili kutoka Kongwa Dodoma, Naibu Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai alisema ‘huku Tanzania tumeupokea uamuzi huo kwa furaha kubwa sana sana sana, kwa sababu ni jambo ambalo kwa upande wetu tukuwa tunaona kuwa si haki na kwa kuwa sasa fedha hizo zinarudi Tanzania,
‘Ni matumaini yetu kuwa fedha hizi zitatumika vizuri, kupitia serikali yetu kwa manufaa ya watanzania wote kama ilivyokusudiwa.’ Aliongeza Bw Ndugai.

Naibu Spika Job Ndugai miezi michache iliyopita aliongoza ujumbe wa wabunge wa Tanzania mjini London kufuatilia malipo hayo, baada ya kutokea mvutano wa muda mrefu kati ya serikali Tanzania na kampuni hiyo ya BAE.
Chanzo: BBC

Thursday, September 8, 2011

Chadema yazindua kampeni, Mkapa atua Igunga

Best Blogger Tips
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimezindua kampeni zake za kuwania Jimbo la Igunga huku Katibu Mkuu wake, Dk. Willibrod Slaa, akiwataka wananchi kumchagua mgombea wa chama hicho, Joseph Kashindye ili alinde rasilimali za wana Igunga.

Wakati Chadema wakizindua kampeni hizo kwa mtindo wa kumwaga tuhuma na kashfa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Rais wa Awamu ya Tatu, alitua Igunga tayari kwa uzinduzi wa kampeni za chama hicho na kuelezea furaha aliyonayo ya kusafiri kwa lami kutoka Dar es Salaam hadi Igunga.

Katika uzinduzi wa Chadema, Dk. Slaa aliwataka wananchi waliokuwa wamefurika katika Uwanja wa Sokoine mjini hapa, kumchagua Kashindye ili alinde rasilimali hizo na kupunguza aliowaita panya wanaozitafuna.

Alidai kuwa mgombea wa CCM, Dk. Peter Kafumu, hawezi kuleta mabadiliko yoyote Igunga na kwa Taifa kutokana na alichoita kuwepo kwa mfumo mbovu wa CCM katika kusimamia maslahi ya wananchi.

Dk. Slaa alisema kuwa nchi inahitaji kutetewa na makamanda, ili ifanikiwe kwa kuwa CCM imeshindwa kazi ya kuwasaidia wananchi.

Aliwaambia polisi aliowaita wanaoagizwa kuwapiga mabomu wananchi, wasifanye hivyo kwa kuwa kazi ya Chadema, ni kuwatetea polisi wa vyeo vya chini ambao alidai wanapewa posho ndogo isiyokidhi mahitaji yao.

Naye Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema kuwa Serikali ya CCM imeshindwa kazi hivyo haifai kuwa madarakani wala kuongezewa wabunge kwa kuwa itazidi kuwadidimiza wananchi.

Kwa upande wake Kashindye alijinadi mbele ya wananchi hao kuwa wakiona mwalimu anaachia chaki na kwenda kwenye siasa, basi wajue hali ni mbaya kwa kuwa Taifa linahitaji ukombozi.

“Hata Mwalimu Nyerere (Baba wa Taifa Mwalimu Julius), aliachia chaki alipoona hali ni mbaya na akaamua kuingia kwenye siasa na kuikomboa Tanzania tunayoishi leo,” alisema.

Alidai kuwa CCM wanadhani kuwa watumishi wa Serikali ni mali yao kitu ambacho si kweli na ameamua kuingia Chadema ili awatetee wananchi wa Igunga na Taifa kwa ujumla.

“CCM ni chama kinachokufa nisingeweza kuondoka na kuingia CCM kuwa mbunge wa kusinzia kwa kuwa hawana hoja,” alidai.

Alidai kuwa fedha nyingi za kujenga barabara zimeliwa kitu ambacho kimesababisha wananchi kuteseka kutokana na mfumo mbovu wa CCM.

“Nawaombeni mnitume niende huko bungeni niende nikawe Spika ya Igunga; nikaseme yote na tupate mafanikio wote,” alisema.

Mbunge wa Viti Maalumu Chadema, Susan Kiwanga alisema ni lazima Igunga wahakikishe chama hicho kinashinda kwa kumchagua Kashindye ili awatetee bungeni.

Alisema, ataweka kambi Igunga na kuhakikisha chama hicho kinashinda kwa kuwa Chadema ni chama cha kutetea wanyonge ambao wamekuwa wakinyonywa na CCM kwa miaka nenda rudi.

Mkapa atua Igunga Lakini Mkapa baada ya kutua Igunga, aliweka bayana kuwa amefika kupambana na kumnadi mgombea wa CCM kwa kuwa anajisikia faraja na matunda ya CCM yakiwemo kutembelea barabara ya lami kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanza.

Akiwahutubia wananchi katika Kitongoji cha Makomero alisema kuwa ni muhimu kwa wana Igunga kupuuza vyama vingine kwa kuwa CCM ikitoa ahadi, inatimiza na viongozi wake ni makini.

“Kazi yetu ni moja tu, kila mtu ahakikishe Dk. Kafumu anashinda na kila mtu ambaye amejiandikisha aende kupiga kura ili mambo yawe poa,” alisema Mkapa.
Chanzo: HabariLeo

Mbuzi mwenye miguu nane azaliwa Bunda

Best Blogger Tips
KATIKA  hali isiyokuwa ya kawaida mbuzi mmoja katika Kijiji cha Nafuba kilichoko Kata ya Nansimo wilayani hapa, amezaa mapacha  huku mmojawao akiwa na miguu minane, mikia miwili na kichwa kimoja.

Habari zilizopatikana kutoka kijijini hapo na kuthibitishwa na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kilomo, kulikotokea tukio hilo, Fabian Kamanyi zinasema tukio hilo la kustaajabisha lilitokea jana mnamo  saa 1:45 asubuhi wakati mbuzi huyo aliyekuwa ametimiza miezi tisa ya ujauzito wake kuzaa mapacha hao kikiwamo kiumbe hicho ambacho hata hivyo kilikufa saa mbili baadaye.

Fabian alisema kabla ya kuzaa mbuzi huyo ambaye hiyo ni mara yake ya tatu kuzaa usiku, alikuwa akilia kama ishara ya kutaka kuzaa  hali iliyomfanya mmiliki wake Silvanus Bernado, asubuhi yake  kumtenganisha na wenzake kwa kumfunga jirani na nyumbani ili ampatie uangalizi wa pekee.

Alisema hatimaye ulipotimia muda wake wa kuzaa (usiku), mbuzi huyo alizaa mapacha hao akiwamo huyo mmoja wa ajabu ambaye alikuwa wa kwanza kuzaliwa akiwa haonyeshi jinsi  ya aina yoyote tofauti  na mwenzake ambaye alikuwa ana jinsi ya kiume.

Ingawa mwenye mbuzi huyo (Bernado), alilielezea tukio hilo kama kitu cha kawaida, lakini baadhi ya wakazi wa kijiji hicho ambacho ni moja ya Visiwa ndani ya Ziwa Victoria eneo la Wilaya ya Bunda wanaliona kama moja ya matendo ya ushirikina hali iliyosababisha wazee wa kisiwa hicho kulikemea kwa kumtaka aliyefanya hivyo aache mara moja.

Kwa upande wake daktari wa mifugo wa wilaya hiyo, Dk Ndyanabo Tibaijuka alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo licha ya kusema hakuwa hajapata taarifa rasmi, lakini alisema kama limetokea ni jambo la kawaida katika maisha ya viumbe linalojitokeza wakati wa hatua za awali za uchanga wa mimba pindi viungo mbalimbali vya mwili vinapogawanyika ili kujiumba katika umbo linalotakiwa.

“Sijapata taarifa rasmi za tukio hilo; lakini kama limetokea hilo ni jambo la kawaida linalotokea katika hatua za awali za uchanga wa mimba viungo vinapojigawanyisha,”alisema Dk Ndyanabo.
Chanzo: Mwananchi

Wednesday, September 7, 2011

Wakutwa na heroine za bilioni 4/-

Best Blogger Tips
JESHI la Polisi Kitengo cha Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini, limewakamata watu watano akiwemo raia wa Iran, Ali Mirzael Pirbaksh, kwa tuhuma za kukutwa na kilo 97 za dawa hizo aina ya heroine zenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 4.4.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkuu wa Kitengo hicho Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Godfrey Nzowa, alisema kukamatwa kwa watuhumiwa hao kumetokana na taarifa walizopewa na raia wema.

Aliwataja watuhumiwa wengine kuwa ni Said Mrisho (31) wa Tandale, Aziz Kizingiti (32) wa Magomeni Mapipa, Abdul Lukongo (36) wa Kariakoo na Hamidu Karimu (43), wa Tandale.

Nzowa alisema watuhumiwa hao waliokuwa wamepakia dawa hizo ndani ya magari mawili, Toyota Carina namba T 954 BGT na Caldina namba T 107 BAS, walikamatwa jana saa 9.30 alifajiri eneo la Afrikana Mbuyuni, Kinondoni.

“Baada ya mimi kupewa taarifa za watu hao, nilichukua vijana wangu na kuwafuatilia taratibu katika maeneo waliyokuwa wakienda na hatimaye kuwakamata eneo hilo,” alisema Nzowa.

Alisema baada ya kuwahoji watuhumiwa hao, isipokuwa raia huyo wa Iran, ambaye ndiye anadaiwa kuingiza dawa hizo nchini, walidai kuwa zilikuwa mali ya Pirbaksh, ambaye hata hivyo hakuhojiwa baada ya kukosekana mkalimani.

Nzowa alisema watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani wakati wowote upelelezi wa tukio hilo utakapokamilika, huku akiwataka wananchi wanaojihusisha au kutumiwa kufanya biashara hiyo kuacha, ili kuepuka mkono wa sheria.

Aidha, aliwashukuru wananchi kwa ushirikiano wanaolipa Jeshi hilo katika kupambana na biashara hiyo haramu, huku akiwataka kuendelea kudumisha uhusiano huo hadi mapambano hayo yatakapofanikiwa.
Chanzo: HabariLeo

 

Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits