Thursday, August 30, 2012

Sitta: Tishio Chadema ni Dk Slaa tu

Best Blogger Tips
 MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya CCM, Samuel Sitta amekiponda Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), akidai kuwa muda wake wa kutawala nchi bado, kwa kuwa hakina viongozi wa kutosha wa kufanya kazi za Serikali ukimwondoa Katibu Mkuu wake, Dk Willibrod Slaa.

Sitta ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na baadhi ya viongozi wa CCM wa Wilaya ya Karagwe, Kagera, alikokuwa katika ziara ya kutembelea ofisi za CCM.

Alisema kuna upungufu mwingi katika safu ya uongozi wa chama hicho, kutokana na kutokuwa na watu wenye uzoefu wa kufanya kazi za Serikali, badala yake akidai kuwa kina baadhi ya viongozi wenye uzoefu wa kuongoza kumbi za muziki... “Wote hapa mnasikia kwamba Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe ni mjuzi wa disko za usiku, sasa huwezi kulinganisha na CCM hata akitoka mtu mmoja chama chetu hakiwezi kuyumba.”

Dk Slaa na Mbowe hawakupatikana jana kuzungumzia kauli hiyo ya Sitta baada ya taarifa kueleza kuwa Mbowe yuko nje ya nchi na alikuwa hapatikani kupitia simu yake ya mkononi kama ilivyokuwa kwa Dk Slaa.

Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe alipinga kauli hiyo akimtaka Sitta aachane na chama hicho kikuu cha upinzani na atumie muda wake kukijenga chama chake ambacho alidai kuwa kina makundi zaidi ya sita.
“Mwaka 2005 tuliweka mgombea Mbowe, mwaka 2010 tukamweka Dk Slaa, mwaka 2015 anaweza akarudi Mbowe, Dk Slaa au mwanachama yeyote wa Chadema,” alisema Zitto.

Alisema Chadema ni taasisi na si chama cha makundi kama ilivyo kwa CCM hivyo hakiwezi kumtegemea mtu mmoja... “Sitta asigombane na Chadema, ajenge chama chake ili tukutane mwaka 2015.”

Akizungumza na viongozi hao wa CCM Karagwe, Sitta alisema hakuna kiongozi mwingine anayeweza kufanya kazi ya kukiongoza Chadema na kukifanya chama kikubalike kwa umma.

“Hawa jamaa hawana hazina ya viongozi kama tulionayo CCM, ambapo tunaweza kusimamisha wagombea 20 wa urais wenye sifa zinazofanana tofauti na wao wanaye Dk Slaa tu ambaye inasemekana aliukimbia upadri.”

Kuhusu CCM
Akizungumzia chama chake, Sitta aliwataka viongozi wa CCM Mkoa wa Kagera kutokaa kimya na badala yake wajitoe na kujibu hoja za upinzani wanazozitoa kuikosoa Serikali iliyopo madarakani ili ionekane haijafanya mambo ya maendeleo tangu kupatikana kwa uhuru.

“Serikali ya CCM imefanikiwa katika maeneo mengi ya huduma za jamii kama elimu, barabara, afya na mawasiliano, sasa inashangaza kuona viongozi wa chama mnashindwa kufanya mikutano ya kuwaeleza wananchi mafanikio yanayotokana na utekelezaji wa sera na ilani ya chama chetu.”

Sitta aliwataka viongozi chama hicho nchini kuepuka mapambano na chuki miongoni mwao lakini akasisitiza kwamba kinaendelea na mkakati wake wa kuwaondoa viongozi wanaodaiwa kuwa ni mafisadi maarufu kwa jina la “magamba”.
Alisema chuki na mapambano yanayoendelea ndani ya chama hicho ndiyo yanayochangia kukidhoofisha na kuwapa la kusema wapinzani na hata kusababisha baadhi ya wanachama kukihama.

“Mapambano ndani ya CCM ndiyo chanzo cha migogoro na mitafaruku inayosababisha viongozi na wanachama wetu kuombeana mambo mabaya na kutoa mwanya kwa watu wetu kuhamia upinzani.”
Sitta yupo katika ziara ya siku tano ya kiserikali mkoani Kagera kukagua miradi mbalimbali inayohusiana na mwingiliano wa uchumi na kijamii kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Chanzo: Mwananchi

Friday, August 24, 2012

Zitto:Kiama walioficha mabilioni Uswisi

Best Blogger Tips
MBUNGE wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe ameahidi kuwataja wanaohusika kuficha mabilioni ya fedha nchini Uswisi katika kikao kijacho cha Bunge Oktoba, mwaka huu iwapo Serikali itashindwa kufanya hivyo hadi muda huo.

Wakati Zitto akisema hayo, kashfa hiyo imechukua sura mpya na sasa fedha hizo zinahusishwa na ufisadi katika Kampuni ya Meremeta.

Kauli ya Zitto ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, imekuja siku chache tangu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta kuwataka wanaowafahamu walioficha fedha hizo kuwataja hadharani ili iwe rahisi kwa Serikali kuwachukulia hatua.

Hata hivyo, Zitto akizungumza na gazeti hili jana alisema: “Mimi ni mbunge makini ninayefahamu taratibu za Bunge na kuheshimu haki za watu wengine, siwezi kukurupuka katika suala hili.

Ninaiachia Serikali na vyombo vyake iendelee kulifanyia kazi na ikiwa watashindwa kuwataja wahusika, basi wasubiri kikao kijacho, nitaweka hadharani majina ya wahusika wote.”

Zitto alisisitiza kuwa Serikali ina uwezo wa kupata taarifa zozote inazozihitaji kutoka Uswisi na kwamba ndiyo maana ameipa muda wa kulifanyia kazi suala hilo kabla yeye hajachukua hatua ya kuwataja wahusika.

“Sikia, lazima tukubaliane jambo moja kwamba mimi siyo Serikali, wala sina dola, ndiyo maana nasema kwamba tusubiri utekelezaji wa ahadi ya Serikali, lakini wakishindwa kuwataja, basi mimi nitatumia nafasi yangu kama mbunge kuwataja na nitafanya hivyo ndani ya Bunge na wala siyo nje ya hapo,” alisema.

Uchunguzi zaidi wa gazeti hili umebaini kuwa kiasi cha Dola za Marekani 186 milioni (takriban Sh300 bilioni) kwa viwango vya sasa vya kubadilishia fedha ambavyo ni Sh1,600 kwa Dola ya Marekani, kimefichwa katika benki tatu tofauti za Uswisi.

Uchunguzi zaidi unabainisha kuwa takwimu hizo ni rasmi kwani zimetolewa na Benki Kuu ya Uswisi, lakini taarifa zaidi zinadai kuwa kuna fedha nyingi zaidi zilizofichwa na Watanzania katika benki nyingine nchini humo ambazo taarifa zake zinaweza kupatikana ikiwa Serikali itasimamia vizuri suala hilo.

Watanzania 27 wameripotiwa kumiliki fedha nchini humo, na mmoja wao anadaiwa kwamba anamiliki Dola za Marekani 56 milioni (wastani wa Sh89.6 bilioni).

Kashfa ya kuwapo kwa vigogo walioficha fedha zao Uswisi iliibuliwa na baadhi ya vyombo vya habari nchini Juni mwaka huu na baadaye mwangwi wake kulitikisa Bunge katika Mkutano wake wa Nane uliomalizika hivi karibuni.

Habari hizo zilikuwa zikinukuu taarifa ya Benki Kuu ya Uswisi iliyoitoa na kuonyesha kuwapo kwa kiasi cha Sh315.5 bilioni zilizotoroshwa Tanzania na kufichwa nchini humo na vigogo ambao ni wanasiasa pamoja na wafanyabiashara.

Suala hilo pia lilijadiliwa katika kikao cha Bunge kilichopita, huku ikidaiwa kwamba fedha hizo zinatokana na biashara (deals) zilizofanywa na watendaji wa Serikali na wafanyabiashara kwenye sekta za nishati na madini na kwamba sehemu kubwa ya fedha zililipwa na kampuni za utafutaji mafuta na gesi katika Pwani ya Mkoa wa Mtwara zilizopewa mikataba kati ya mwaka 2004 na 2006.

Uhusiano na Meremeta

Habari zaidi zinadai kuwa fedha zilizofichwa Uswisi hivi sasa zina uhusiano na ufisadi kupitia Meremeta unaohusisha kiasi cha Dola za Marekani 132 milioni wastani wa Sh211.2 bilioni ambazo zilitoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwenda Benki ya Ned Afrika Kusini.

Fedha hizo zililipwa kama marejesho ya mkopo wa Dola 10 milioni (sawa na Sh1.6 bilioni tu, uliokuwa umechukuliwa na Kampuni ya Meremeta Ltd ambayo ilikuwa mali ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), ikishughulikia uchimbaji wa madini.

Utata katika malipo hayo ni uhalali wa ongezeko la Dola 122 milioni katika malipo hayo, kwani mkopo wa Dola za Marekani 10 milioni ulirejeshwa na faida ya zaidi ya asilimia 1,000.

Uchunguzi unaonyesha kuwa fedha hizo za marejesho tata zilifichwa katika benki moja (jina tunalihifadhi) nchini Mauritius, na baadaye kati ya 2005 na 2006 zilihamishiwa nchini Uswisi, ambako sehemu yake zipo kwenye akaunti ya kigogo ambayo inaongoza kwa kuwa na kiasi kikubwa cha fedha, karibu Sh90 bilioni.

Kashfa ya Meremeta ni ya muda mrefu na mara nyingi Serikali imekuwa ikikataa kuizungumzia kwa maelezo kwamba ni suala ambalo lina masilahi ya usalama kwa taifa.

Awali, Serikali ilisema kwamba Meremeta Ltd ni kampuni ya Kitanzania iliyokuwa ikimilikiwa na JWTZ kwa ajili ya mradi wake wa Nyumbu, Mkoa wa Pwani.

Taarifa za usajili zilizotolewa na Msajili wa Kampuni wa Uingereza na Wales zinabainisha kuwa kampuni hiyo iliandikishwa nchini humo mwaka 1997 na baadaye ilifilisiwa hukohuko Uingereza mwaka 2006.

Taarifa ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) ya Mei 31, 2005 inabainisha kwamba Meremeta Ltd ni tawi la kampuni ya kigeni iliyosajiliwa Tanzania, Oktoba 3, 1997 na kwamba hisa 50 za kampuni hiyo zilikuwa zinamilikiwa na Kampuni ya Triennex (Pty) Ltd. ya Afrika Kusini, wakati hisa 50 zilizobaki zilikuwa zinamilikiwa na Serikali ya Tanzania.

Utata kuhusu umiliki wa Meremeta Ltd unatokana na taarifa ya Brela ambayo pia inazitambua kampuni mbili za Kiingereza ambazo ni London Law Services Ltd na London Law Secretarial Ltd kuwa wamiliki wa hisa moja kila moja ndani ya Meremeta.

Licha ya Serikali kutokuwa mmiliki pekee wa kampuni hiyo, BoT ililipa madeni yote ya Meremeta badala ya kusaidiana na washirika wake ambao kisheria wanaonekana kuwa walikuwa wakimiliki hisa katika kampuni hiyo.

Serikali Tanzania ilikuwa ikimiliki asilimia 50 ya hisa na kwa mujibu wa taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), uhalali wa malipo hayo ulikuwa na walakini kwani kiutaratibu, Nedbank Ltd ilitakiwa iachwe idai fedha zake kutoka kwa mfilisi wa kampuni hiyo kama ilivyo kwa wadeni wengine.

Meremeta bungeni

Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini iliwahi kupewa idhini ya kuchunguza suala hilo, lakini Spika wa Bunge, Anne Makinda alilihamishia katika Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.

Hata hivyo, uchunguzi huo haukuwahi kufanyika na Ofisi ya Spika pia haijawahi kutoa taarifa yoyote. Hivyo suala hilo kubaki kitendawili hadi leo.

Hatua ya Spika kuridhia uchunguzi ilikuja baada ya mvutano wa muda mrefu, uliotokana na hoja zilizokuwa zikitolewa na Serikali kwamba suala la Meremeta lisingeweza kufanyiwa uchunguzi kutokana na “sababu za kiusalama.”

Kumbukumbu za Bunge zinaonyesha kuwa Zitto aliwahi kuwasilisha barua kwa Katibu wa Bunge akitoa taarifa ya hoja ya kutaka kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge kwa ajili ya kuchunguza tuhuma za ufisadi kupitia kampuni hiyo ya uchimbaji wa dhahabu.

Zitto alitoa taarifa ya mdomo bungeni Julai 13, mwaka jana kwa mujibu wa Kanuni ya Bunge Namba 117 (2)-(a) inayomruhusu kutoa taarifa ya kusudio lake la kuwasilisha hoja ya kutaka Bunge liunde kamati teule.

Aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi (sasa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii) aliwahi kusema bungeni kwamba halifahamu suala hilo kwenye majumuisho ya Bajeti ya wizara hiyo ya 2011/12.
Chanzo: Mwananchi

Wednesday, August 22, 2012

Mwili wa Zenawi umewasili Adis Ababa

Best Blogger Tips
 Mwili wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Ethiopia, Melez Zenawi, uliwasili jana usiku katika mji mkuu wa nchi hiyo Adis Ababa na kwa sasa umehifadhiwa katika Ikulu hadi mazishi yake yatakapofanyika.

Maelfu ya raia wa nchi hiyo walimiminika katika barabara za mji huo jana jioni wakati mwili wake ulipowasili kutoka mji mkuu wa Ubelgiji, Brussels.

Meles, ambaye alikuwa na umri wa miaka 57, aliaga dunia ghafla kutokana na maambukizi wakati alipokuwa akitibiwa.

Kifo cha Bwana Zenawi kimezua hofu ya kugombea madaraka hali ambayo ingeweza kuathiri amani ya nchi hiyo.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari, naibu waziri mkuu Hailemariam Desalegn ataliongoza taifa hilo hadi mwaka 2015 wakati uchaguzi mkuu utakapofanyika.

Utawala wa Bwana Zenawi ulishutumiwa kwa kukandamiza upinzani na kuna hofu kuwa Waziri Mkuu mpya huenda asiwe na uzoevu wa kushughulikia na kutatua uhasama wa kisiasa unaoendelea nchini humo.

Zenawi amesifika kwa kuiongoza Ethiopia kufikia mafanikio makubwa ya maendeleo na uchumi, lakini wakosoaji wake wanasema licha ya hayo yote utawala wake haukuruhusu uhuru wa siasa za vyama vingi na kuwa viwango vya ukiukwaji wa haki za binadam bado viko juu.

Bwana Zenawi alikuwa kiongozi wa Ethiopia wakati taifa hilo lilipoingia vitani na nchi jirani ya Eritrea mwaka 1998.

Meles Zenawi aliingia madarakani mwaka 1991 baada ya mapinduzi lakini akapokea sifa kutoka kwa mataifa ya magharibi.
Chanzo: BBC

Monday, August 20, 2012

Sitta:Msiisubiri Serikali kutaja walioficha mabilioni

Best Blogger Tips
 WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amewataka wanaotangaza kuwafahamu vigogo walioficha mabilioni ya fedha nje ya nchi kuwataja mara moja ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao badala ya kuisubiri Serikali kufanya hivyo.Kauli hiyo ya Sitta ambaye pia ni Mbunge wa Urambo Mashariki (CCM), imekuja wakati baadhi ya wanasiasa, wakiwamo wabunge kutishia kuwataja watu hao, lakini wakisisitiza kuwa ni pale tu Serikali itakaposhindwa kufanya hivyo.

Utafiti uliofanywa na Shirika la Kimataifa la Fedha la Global Financial Integrity, unaonyesha kuwa tatizo la utoroshaji wa fedha nchini limekuwapo katika awamu zote za Serikali zilizoiongoza Tanzania, lakini Awamu hii ya Nne imetia fora.

Utafiti huo uliofanywa kuanzia mwaka 1970 hadi 2009, unaonyesha kuwa katika utawala wa Rais Jakaya Kikwete, fedha zilizofichwa nje ya nchi ni Dola za Marekani 7,967.4 milioni (sawa Sh12.7 trilioni).
Akizungumza katika mahojiano maalumu, kuhusu nini kifanyike ili kuiokoa Tanzania isiendelee kufilisiwa na watu wachache, Sitta alisema anasikitishwa na watu hao kuogopa na kuwaficha watu wanaofisadi mali za nchi na hasa pale inapokuwa wahusika ni vigogo wa Serikali.

Alisema vigogo hao ni sababu ya watu kupata kigugumizi katika hili akihoji : “Kwa nini linapokuwa ni suala linalowahusu hawa wanaoitwa vigogo hawatajwi?”

Sitta ambaye ameshika nyadhifa mbalimbali serikalini katika awamu tofauti, alisema haoni kama kuna kosa kumtaja hadharani mtu aliyeficha fedha nje ya nchi huku akisababisha Watanzania kuendelea kukabiliwa na maisha magumu.

“Watajwe! Kama ni Samuel Sitta ameficha fedha nje atajwe. Kwa kweli mimi sioni kama kuna dhambi yoyote kumtaja,” alisema Sitta huku akisisitiza kwamba huo ni msimamo wake binafsi unaotokana na uzoefu wake kwenye uongozi wa nchi na siyo kwa mamlaka aliyonayo ya Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Alisema njia nzuri ya kukomesha tabia hiyo ni kuwataja na vyombo husika kuwafikisha mahakamani kwa kuzingatia kuwa sheria ni msumeno, haipaswi kubagua aliye mdogo au mkubwa kwa maana ya wadhifa katika nchi.Sitta ambaye pia aliwahi kuwa Spika wa Bunge alisema: “Swali la kwa nini hawatajwi, ni jambo la kushangaza.”

Alisema amesikia na kuwasoma baadhi ya wanasiasa wakitishia kuwa watawataja wahusika iwapo Serikali haitafanya hivyo, lakini akasema haoni sababu yoyote ya mtu kusita katika kuokoa taifa dhidi ya wizi wa fedha za umma.

“Haiwezekani kwa mwanasiasa yeyote katika nchi maskini kama Tanzania au kiongozi wa Serikali kuwa na utajiri wa mabilioni ya fedha.”

Alisema hata kama anafanya biashara, siyo rahisi kuwa na utajiri wa kiwango hicho hasa ikizingatiwa kuwa hutumia muda mrefu kulitumikia taifa.
“Sisi tunaofanya kazi serikalini, tunatoka saa moja usiku. Sasa muda huo wa kufanya biashara ni saa ngapi?”

Tuhuma hizo ziliibuka bungeni Jumatano iliyopita baada ya Kambi ya Upinzani kudai kwamba nawafahamu wahusika wa ufisadi huo na kutishia kuwataja ikiwa Serikali haitafanya hivyo.

Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Zitto Kabwe alipokuwa akiwasilisha hotuba ya kambi yake kuhusu Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Fedha alisema miongoni mwa wanaomiliki fedha hizo ni kiongozi wa juu nchini pamoja na aliyepata kuwa waziri katika Serikali ya Awamu ya Tatu iliyoongozwa na Benjamin Mkapa.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili ulibaini kwamba kuna Watanzania 27, wakiwamo wanasiasa na wafanyabiashara walioficha mabilioni ya fedha huko Uswisi, huku mmoja wao akiwa anamiliki Dola za Marekani milioni 56 (sawa na Sh89.6 bilioni).

Katika uchunguzi huo ilibainika pia kuwa kiasi cha fedha kilichothibitishwa kumilikiwa na Watanzania hao ni jumla ya Dola za Marekani 186 milioni (takriban Sh300 bilioni) kwa viwango vya sasa vya kubadilishia fedha ambavyo ni Sh1,600 kwa Dola ya Marekani.

Taarifa hizo zinaeleza kuwa mbali na kigogo anayemiliki Sh90 bilioni, wapo wengine wanne huku anayefuatia akiwa anamiliki Dola 30 milioni (Sh48 bilioni), mwingine dola 20 milioni (Sh32 bilioni) na wengine wawili kila mmoja anamiliki dola milioni 10 (Sh16 bilioni).  

Hiyo inamaanisha kwamba vigogo watano tu katika kundi hilo, wanamiliki Dola milioni 126 (Sh201.6 bilioni) sawa na asilimia 67.74 ya fedha hizo, wakati wengine 22 waliobaki wanamiliki Dola milioni 60 (Sh96 bilioni) sawa na asilimia 32.25.

Kwa hesabu za kawaida, kiasi cha Sh300 bilioni, kinaweza kugharimia ujenzi wa vyumba vya madarasa zaidi ya 33,300, ikiwa chumba kimoja kinagharimu kiasi cha Sh9 milioni.

Katika orodha ya walioweka fedha nchini humo, pia wamo wafanyabiashara wanaomiliki kiasi cha dola kati ya milioni mbili na milioni saba. Kadhalika, wamo wawili waliowahi kuwa mawaziri katika Serikali ya Awamu ya Kwanza ya Mwalimu Julius Nyerere ambao akaunti zao zina kiasi kisichozidi Dola 500,000 kwa kila mmoja.
Chanzo: Mwananchi

Mnyika kinara bungeni

Best Blogger Tips
 MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), kwa sasa ndiye anashikilia rekodi ya ukinara wa kuchangia mara nyingi bungeni, akifuatiwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (CHADEMA) na Godfrey Zambi wa Mbozi Mashariki (CCM).

Kwa mujibu ya rekodi zalizomo kwenye mtandao wa Bunge, Mnyika ambaye ni kipindi chake cha kwanza bungeni, ameonekana kufanya vizuri zaidi sambamba na wabunge wenzake kadhaa wa CHADEMA.

Takwimu hizo hazijawahusisha mawaziri, manaibu wao, Spika, naibu wake, wenyeviti watatu wa Bunge, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa vile nafasi zao zinawapa uwezekano mkubwa wa kuchangia hoja wakati wowote.

Wabunge kumi ambao wameshika nafasi za juu ni Mnyika akiwa amechangia (184), kuuliza maswali ya nyongeza (28) na msingi (7), akifuatiwa na Zitto (79), (25) na (8) wakati Zambi anashika nafasi ya tatu kwa (70), (26) na (9).

Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu anashika nafasi ya nne akiwa amechangia mara 93, maswali ya nyongeza 19 na yale ya msingi 7, akifuatiwa na Diana Chilolo wa Viti Maalumu (CCM) aliyechangia mara 61, maswali ya nyongeza 41 na msingi 9.

Nafasi ya sita inashikiliwa na Halima Mdee wa Kawe (CHADEMA) akiwa na rekodi ya 59, 15 na 6 akifuatiwa na Moses Machali wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi) mwenye michango 57, nyongeza 30 na maswali ya msingi 7.

Magdalena Sakaya wa Viti Maalumu (CUF) amejinyakulia nafasi ya nane akiwa na michango 52, maswali ya nyongeza 13 na ya msingi 4, huku Mbunge wa Kisarawe, Seleman Jafo (CCM) akifuatia kwa 51, 10 na 6.

Anayefunga dimba kwa kumi bora ni Ester Bulaya wa Viti Maalumu (CCM) mwenye michango 47, nyongeza 17 na maswali ya msingi 3, akiwa amefungana na Martha Mlata wa Viti Maalumu (CCM) mwenye rekodi ya michango 47, nyongeza 11 na maswali ya msingi 5.

Ni takriban miaka miwili tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu, ambapo vyama vya upinzani hususan CHADEMA, wabunge wake wameendelea kuonesha umahiri bungeni, kwani hata Bunge la tisa lililopita kwa mujibu wa utafiti wa shirika moja, Zitto na Dk. Willibrod Slaa akiwa mbunge wa Karatu wakati huo, walishika nafasi za juu.

Katika mtiririko huo wa takwimu hizo kwenye mtandao wa Bunge, wabunge wanaoonekana kuwa na alama ndogo wengi ni wale wa Viti Maalumu CCM na baadhi ya CUF.
Chanzo: Tanzania Daima

Mwanasheria Mkuu ampinga Dk Hoseah

Best Blogger Tips
 MWANASHERIA Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema amesema Sheria ya Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru), ni nzuri na kwamba haipaswi kufanyiwa mabadiliko kama ambavyo imekuwa ikidaiwa.

Jaji Werema aliliambia gazeti hili jana kuwa haoni haja ya sheria hiyo kufanyiwa mabadiliko sasa kwa kuwa haina tatizo na ipo kutekeleza misingi ya utawala wa Sheria.

"Mimi nakubaliana na Sheria hii ya (Takukuru) kwamba iendelee kuwapo. Hakuna haja ya kuifanyia mabadiliko sasa. Ni nzuri kwa kuwa inazingatia misingi ya utawala wa sheria," alisema Jaji Werema.

Kauli ya Jaji Werema inapingana na ile iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah kwamba sheria hiyo imekuwa ikiwakwaza kuwashughulikia wala rushwa wakubwa, kwani majalada ya kesi zilizokwishafanyiwa uchunguzi yamekwama kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka (DPP).

Wiki iliyopita Dk Hoseah alilalamikia sheria hiyo, hasa kifungu cha 37 na 57 akisisitiza kuwa ni mbovu kwa kuwa vinamzuia kuwafikisha watuhumiwa wa rushwa kubwa mahakamani. “Tusaidieni sheria hii ibadilishwe ili iweze kuturuhusu kufanikisha kupambana na rushwa nchini,” alisisitiza Dk Hoseah.

Hata hivyo, jana Werema alipinga dhana hiyo na kusema kwamba siyo sahihi kuipa Takukuru mamlaka yote; kutuhumu, kupeleleza na kushtaki kwa kuwa kufanya hivyo ni kinyume na demokrasia, Katiba na utawala wa sheria.

Kumrundikia mtu au taasisi moja mamlaka zote hizo, ni kinyume na misingi ya utawala bora, alisema.

"Haiwezekani mtu (Dk Hoseah) akawa na mamlaka ya kupeleleza na kushtaki, halafu Mahakama ikiwaachia huru watuhumiwa, atasema siyo mimi ni kosa la Mahakama, We can't do that! (hatuwezi kufanya hivyo)," alisema Werema na kuongeza:

"Mimi nakubaliana na kitu kimoja, kila mamlaka iwe na kigingi. Iwe Mamlaka ya Rais, Bunge au Mahakama, lazima kuwe na chombo cha ku-check and balance," alisema Jaji Werema.

Kauli hiyo ya Jaji Werema imekuja siku chache tangu Mkurugenzi wa Mashtaka, (DPP) Eliezer Felishi kukiri kwamba kazi ya kuwafikisha watuhumiwa hao mahakamani ni yake, lakini kesi nyingi zinakwama.

DPP Feleshi alisema ucheleweshaji wa kesi za rushwa kupelekwa mahakamani, unatokana na kukosekana kwa ushahidi wa kutosha. "Ikifikia hapo, nalazimika kuyarudisha mafaili hayo kwa Takukuru," alisema.

"Mimi nafanya kazi kwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa na Serikali. Siwezi kufanya kazi kwa sababu mtu fulani ametaka nifanye. Jambo hilo linaweza kuniletea matatizo baadaye," alisema na kuongeza:

"Kutokana na hali hiyo, siwezi kupeleka mahakamani jalada ambalo halijakamilika. Sheria inanipa siku 60 niwe nimepeleka kesi mahakamani, lakini kama ushahidi haupo cha kufanya ni kurudisha Takukuru faili.”

Madai ya Dk Hoseah
Awali Dk Hoseah alisema anajua matarajio ya wananchi ni makubwa kwa Takukuru, lakini sheria imewafunga mkono kwa kuwa hawawezi kuchukua uamuzi dhidi ya kesi kubwa za ufisadi bila ushauri wa DPP.

“Sina mamlaka ya kumpeleka mtuhumiwa wa rushwa kubwa mahakamani. Uwezo wangu ni kupeleka walarushwa ndogondogo tu na kwamba kazi yangu ni kuchunguza tu,” alisema Dk Hoseah na kuongeza;

“Sheria yetu imetufunga mikono kwa kuwa kumpeleka mtu mahakamani siyo uamuzi wangu, bali ya DPP.”

Awali Dk Hoseah alisema sheria hiyo katika kifungu cha 57 inamzuia kuwapeleka mahakamani watuhuhumiwa wakubwa wa rushwa, mpaka awafikishe kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP).

Kifungu hicho cha 57 (1) kinasema kuwa shtaka lolote la kosa lililoelezwa kwenye Sheria ya Takukuru lazima lifunguliwe kwa ruhusa ya maandishi kutoka kwa DPP. Kifungu cha 57 (2) kinamtaka DPP ndani ya siku 60 kutoa au kukataa ruhusa ya kushtakiwa.

Dk Hoseah alisema, hiyo ni moja ya changamoto zinazoikabili taasisi yake na kwamba wananchi wasubiri mabadiliko ya kiutendaji kama sheria itabadilika na kumruhusu kufanya hivyo.

Maelezo ya Dk Hoseah yanaungwa mkono na sehemu ya taarifa ya awali ya Mpango wa Nchi za Afrika wa Kujitathmini (APRM) ambayo inaeleza kwamba kikwazo cha ufanisi katika vita ya rushwa nchini Tanzania ni sheria inayowazuia Takukuru ipate kibali cha DPP kabla ya kufungua kesi kubwa za rushwa.

“Ni wala rushwa wadogo wadogo tu ndiyo wanaoweza kushtakiwa na Takukuru, lakini makosa makubwa ya rushwa yanayohusu viongozi au watu wa karibu na viongozi wakubwa ni mara chache sana kufunguliwa kesi mahakamani,” inasema sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza:

“Mfumo huu ni kama unainyima mamlaka ya kiutendaji Takukuru na kimsingi, unakandamiza juhudi za chombo hiki kupambana na rushwa”.

Hii siyo mara ya kwanza kwa ofisi hizi mbili kuvutana kuhusu udhaifu katika sheria ya Takukuru, lakini mara zote Serikali imekuwa ikisisitiza kwamba lazima mashtaka kwa watuhumiwa wakubwa wa rushwa wapate yapate kibali cha DPP kabla ya kufikishwa mahakamani.
Chanzo: Mwananchi

Thursday, August 16, 2012

CUF nao wamshukia Nnauye

Best Blogger Tips
 CHAMA cha Wananchi (CUF), kimedai kushangazwa na kauli iliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Bw. Nape Nnauye kwa vyombo vya habari kuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeingia mikataba ya kifisadi na wafadhili wa nje ili kupora rasilimali za nchi.

Taarifa iliyotolewa Dar es Salaama jana na Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF, Bw. Abdul Kambaya, alisema Bw. Nnauye hakupaswa kuishtaki CHADEMA kwa wananchi bali kupitia Serikali yao walipaswa kuzuia fedha hizo na kuwataja wafadhili hao.

“CUF kimeshangazwa na kauli hii ambayo imetolewa na msemaji wa CCM, ambacho ndio chama kinachoongoza nchi, tulitarajia Bw. Nnauye angewataja hao wafadhili wa CHADEMA ambao dhamira yao ni kupora rasilimali za nchi,” alisema Bw. Kambaya.

Aliongeza kuwa, chama hicho kinaamini CCM na CHADEMA ni watoto wa familia moja ambapo wafadhili wao ndani na nje ya nchi pia wa aina moja.

“Kama CHADEMA imeingia mikataba ya kupewa mabilioni ili baadae wataposhika madaraka waweze kulipa mabilioni hayo kupitia rasilimali za nchi basi watakuwa wanaendeleza utaratibu wa CCM kuingia mikataba mibovu isiyo na tija kwa Watanzania,” alisema.

Alisema CUF  inaamini kuwa, tatizo lililopo nchini ni mifumo mibovu inayoendesha Serikali, nchi, kukithiri kwa wizi, matumizi mabaya ya fedha za umma na ukiukwaji wa haki za binaadamu.

Bw. Kambaya alisema, sababu ya Watanzania wengi kuwa maskini wa kutupwa, ukosefu wa huduma bora kwa jamii, kudumaa kwa maendeleo ya nchi na ukosefu wa ajira ni matokeo ya muda mrefu yanayosababishwa na mfumo mbovu uliopo.

Alisema njia sahihi ya kulinda rasilimali zilizopo na zinazoendelea kugunduliwa nchini Serikali ya Umoja wa Kitafa ambayo itashirikisha vyama vyote vyenye wabunge.

Aliongeza kuwa, kwa kuzingatia utaratibu huo hakuna chama ambacho kitakuwa na maamuzi yake katika matumizi ya rasilimali na Maliasili za nchi.

“Sisi tunataka Watanzania waelewe kuwa, mazingira yanaonesha CHADEMA kimeizidi kete chama tawala kwa kuwa na wafadhili wa nje ndio maana CCM Inapiga kelele,” alisema.
Chanzo: Majira

Wednesday, August 15, 2012

Zitto awa mbogo

Best Blogger Tips
 MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (CHADEMA), ameitaka Mamlaka ya Manunuzi ya Umma (PPRA), kufanya uchunguzi wa manunuzi ya mafuta ya kuzalisha umeme ambayo yanagharimu sh bilioni 42 za serikali kila mwezi.

Zitto ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni kwa Wizara ya Fedha, alisema kuwa sakata la mjadala wa ununuzi wa rada haliwezi kuisha kwa kufurahia chenji iliyorudishwa kwani bado taifa linahitaji kujua ukweli.

Akiwasilisha maoni ya kambi hiyo mjini hapa jana, Zitto alisema manunuzi ya mafuta yamejaa mizengwe ya ufisadi uliokithiri, na kwamba licha ya kutaka Spika kuunda tume ya kuchunguza ufisadi huo na Kamati ya Bunge kutaka uchunguzi wa kibunge kufanyika, hakuna hatua zilizochukuliwa.

“PPRA haipaswi kufumbia macho manunuzi yanayotafuna sh bilioni 1.4 kila siku, na yanayoongeza manunuzi ya nchi kutoka nje, hivyo kupoteza fedha za kigeni hovyo,” alisema.

Aliongeza kuwa, Wizara ya Fedha ambayo ndiyo wizara mama ya PPRA ambayo pia inasimamia uchumi wa nchi, inapaswa kuleta bungeni taarifa ya uchunguzi utakaofanywa na PPRA kuhusu manunuzi hayo.

“Takwimu zinaonyesha kuwa serikali inapaswa kutumia zaidi ya sh 42 bilioni kila mwezi kuendesha mitambo ya dharura ya umeme. Manunuzi yenyewe ya mafuta yamejaa mazonge ya ufisadi uliokithiri. Kambi ya upinzani inataka uchunguzi wa kina kuhusu manunuzi ya mafuta kuzalisha umeme, ambayo yanachoma bilioni 42 za serikali kila mwezi,” alisema.

Kuhusu sakata la ununuzi wa rada, Zitto, alisema mjadala huo bado ni mbichi, kwani unahitajika ukweli kuwa taifa lilipata hasara kiasi gani pamoja na hatua stahiki kuchukuliwa dhidi ya wote walioingiza hasara kwa taifa.

Alisema sehemu ya malipo ya deni la taifa ni mkopo wa serikali iliyochukua kununua rada kutoka Kampuni ya BAE ya Uingereza na kuongeza kuwa, suala hilo limejadiliwa kwa upande mmoja wa ufisadi wa kupandisha bei na hatimaye kurejeshwa kwa chenji hiyo.

Zitto, alisema kuwa hiyo ilikuwa nusu ya ukweli kuhusu suala la rada, kwani serikali ilikopa dola milioni 40 kutoka Benki ya Barclays ya Uingereza kwa ajili ya kununua rada hiyo.

“Mkopo huo ulikuwa na riba ya asilimia 4.9 juu ya kiwango cha riba zinazotolewa na Benki ya Dunia au IMF. Kambi rasmi ya upinzani inataka kujua kama mkopo huo umeshalipwa, na jumla tulilipa kiasi gani. Na chenji ya rada ilikuwa na thamani yoyote kifedha?” alihoji.

Zitto pia aligusia suala la udhibiti wa fedha haramu, akisema kambi hiyo imepata taarifa kuwa mmoja wa viongozi wa juu nchini na baadhi ya mawaziri wa serikali za awamu zilizopita, ni miongoni mwa wamiliki wa fedha hizo zipatazo sh bilioni 314.5.

Alisema sehemu kubwa ya fedha hizo zililipwa kampuni ya utafutaji mafuta wa gesi katika Pwani ya Mkoa wa Mtwara zilizopewa mikataba kati ya mwaka 2004 na 2006.

“Tunaitaka serikali kutoa taarifa rasmi ya hatua gani imechukua baada ya taarifa hiyo kutoka Benki ya Taifa ya Uswisi ilipotolewa. Tunataka kuliambia taifa hatua itakazochukua kurejesha fedha hizi na nyingine zozote ambazo zimefichwa ughaibuni. Kambi ya upinzani italazimika kuweka wazi taarifa na majina ya watu wenye umiliki wa fedha katika benki ya Uswisi iwapo serikai haitatoa taarifa rasmi kuhusu suala hili,” alisema.

Hata hivyo msimamo huo wa Zitto, ulimwibua Mbunge wa Simanjiro, Christpher ole Sendeka (CCM), aliyeomba mwongozo na kumtaka Zitto awataje kwa majina viongozi hao, kwani kuacha hivyo ni kuharibu taswira ya serikali na Bunge.

Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lisu, aliingilia kati akisema Sendeka hakupaswa kumkatisha Zitto wakati akizungumza na kusema kuwa iwapo ana wasiwasi na kauli hiyo kwa mujibu wa kanuni anapaswa kuthibitisha maelezo anayoyaona hayana ukweli kabla ya mtoa kauli kuthibitisha.

Aidha, Zitto alisema kuna taarifa nyingine zinazoonesha jinsi taifa linavyoibiwa kupitia kesi mbalimbali ambazo serikali imeshitaki au kushitakiwa kwenye mahakama za kimataifa.

Alitoa mfano wa kesi hizo ni ya IPTL na Standard Chartered Bank ya Hong Kong ambayo imechukua muda mrefu bila kuisha na kuliingiza taifa katika hasara kubwa.

Kuhusu deni la taifa, Zitto alitaka ufanyike ukaguzi maalumu, ili kubaini uhalali wa deni hilo ambalo hadi Juni mwaka huu lilifikia dola milioni 10,354.6.

Alisema ukaguzi ukifanyika, utawezesha kujulikana kama miradi ilitekelezwa kama inavyotakiwa au kuna mazingira yenye utata.

Kuhusu mishahara hewa, Zitto alisema watumishi hewa 9,949 ni wengi na kwamba inaonesha ni jinsi gani serikaki haipo makini katika suala hilo.

Aliitaka serikali kutumia fedha wanazolipwa watumishi hewa kuwalipa walimu na madaktari kwani ni nyingi.

“Siku zote sababu za serikali kutotimiza matakwa ya wafanyakazi katika sekta ya afya na elimu ni kwamba haina fedha. Lakini tunashuhudia sh bilioni 70 kila mwaka zikielekezwa kuwalipa watumishi hewa,” alisema.

Kwa upande wa mashirika ya umma, alisema kambi hiyo inataka kupata maelezo kuhusu sakata la uuzwaji wa hisa za shirika la UDA pamoja na kuhoji serikali imefikia wapi katika pendekezo la kulifanyia marekebisho Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC), ili liweze kumiliki, kusimamia na kuziendesha hisa za serikali katika kampuni binafsi ambao umiliki wa serikali ni chini ya asilimia 50.

Akisoma maoni ya Kamati ya Fedha na Uchumi, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dustan Kitandula (CCM), alisema kuna haja serikali ikadhibiti deni la taifa kabla halijaongezeka zaidi.

Kitandula ambaye ni mbunge wa Mkinga, alisema kuwa serikali inapaswa kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya watumishi wake waliohusika katika ubadhirifu wa ulipaji mishahara hewa.
Chanzo: Tanzania Daima

Monday, August 13, 2012

Dk Ulimboka: Niko tayari kwa lolote

Best Blogger Tips
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Stephen Ulimboka amerejea nchini jana akitokea Afrika Kusini alikokuwa akitibiwa na kulakiwa na mamia ya watu huku akisema haogopi lolote na yupo tayari kwa kazi.

Dk Ulimboka aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere saa 8.15 mchana kwa ndege ya Shirika la South African Airways.

Baada ya kumaliza taratibu zote uwanjani na kutoka nje, Dk Ulimboka alilakiwa na umati mkubwa wa wananchi wakiwemo madaktari na wanaharakati ambao walijaza karibu eneo kubwa la lango la abiria wanaowasili jambo lililoonekana dhahiri kumsisimua kiasi hadi kufikia kububujikwa wa machozi.

Dk Ulimboka ambaye alipelekwa Afrika Kusini akiwa hawezi kutembea wala kula mwenyewe baada ya Juni 27 mwaka huu kutekwa na watu wasiojulikana, kupigwa na kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili, kisha kutupwa katika Msitu wa Pande, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, amerejea akiwa anatembea na mwenye afya njema.

Akizungumza uwanjani hapo, Dk Ulimboka alisema: “Nawashukuru Watanzania kwa kuniombea, nawashukuru madaktari wenzangu, ndugu na jamaa zangu kwa kunisaidia kupata matibabu hadi leo hii narudi nyumbani nikitembea mwenyewe. Hivi sasa niko fiti na niko tayari kwa kazi yoyote.”

Uwanja huo ulikuwa umefurika mamia ya wananchi wakiwemo madaktari ambao walikuwa na shauku ya kumwona Dk Ulimboka, lakini wengi hawakufanikiwa kumwona.

Wingi wa watu ulisababisha kutokea kwa msuguano kati ya madaktari na waandishi wa habari. Wakati wanahabari wakitaka kumwuliza maswali Dk Ulimboka, baadhi ya madaktari walikuwa wakimzuia Dk Ulimboka kujibu maswali licha ya mwenyewe kuonekana kuwa tayari kuulizwa.
Baadhi yao walifikia hatua ya kushika kamera za waandishi huku wengine wakisema... “Mwacheni akapumzike bwana, kwa nini mnamsumbua sumbua.”

Baadhi ya madaktari hao walifikia hatua ya kutumia nguvu dhidi ya wapiga picha wa magazeti na televisheni na hivyo kusababisha vurugu na kelele nyingi katika eneo hilo.

Muda wote wakati Dk Ulimboka akielekea kwenye gari akiwa na maua mkononi aliyokadhibiwa baada ya kuwasili uwanjani hapo, madaktari hao walikuwa wakiimba nyimbo za kuhamasishana ukiwamo Wimbo wa Taifa huku wengine wakisema: “Mtakufa nyie, lakini si Dk Ulimboka.”

Baada ya kupanda gari aina ya Nissan Patrol nyeusi, madaktari hao na wanaharakati na wananchi wengine wakiongozwa, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Ananileya Nkya walilisukuma gari hilo hadi katika lango la kutokea katika uwanja huo.

Wanaharakati
Mbali na Nkya, kulikuwa na idadi kubwa ya wanaharakati wengine wakiongozwa na Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP, Usu Malya.

Wanaharakati hao walikuwa na mabango yaliyoandikwa,  “Dk Ulimboka karibu nyumbani uliumizwa kikatili ukitetea afya bora kwa Watanzania.”

Bango jingine lilisomeka: “Dk Ulimboka damu yako ilimwagika na kuamsha ari kwa wananchi kudai za afya.”
Jingine, “Dk Ulimboka wewe ni mpigania haki ya afya bora kwa wananchi wote Mungu na Watanzania wote tuko nawe.”

Malya akizungumza uwanjani hapo alisema kupona kwa Dk Ulimboka na kurejea nchini ni uthibitisho kwamba Mungu amesikia sauti za wanyonge.

“Dk Ulimboka alisimamia haki za madaktari na za Watanzania wote akitaka huduma bora zipatikane kwenye hospitali za umma kwa ajili ya Watanzania wote,” alisema.

Mkurugenzi wa Tamwa, Nkya alisema amefurahi kumpokea Dk Ulimboka akiwa hai kwa sababu hali yake ilikuwa mbaya wakati akipelekwa kwa matibabu nje ya nchi.

Kwa upande wake, Katibu wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Edwin Chitage alisema kurejea kwa Dk Ulimboka akiwa amepona kunathibitisha kwamba nchi za wenzetu kuna vifaa vya tiba za kisasa na dawa.

“Kurejea kwa Dk Ulimboka ni mapenzi ya Mungu, huu ni uthibitisho kuwa hapa nchini hakuna vifaa tiba na dawa zinazoweza kusaidia wananchi kama ilivyo kwa wenzetu,” alisema Dk Chitage na kuongeza:
“Madaktari tumefarijika na hii imetupa nguvu licha ya vitisho tunavyopata tutaendelea kupigania haki zetu, haya ni mapambano ya muda mrefu, ”alisema.

Dk Chitage alisema kupona na kurejea nchini kwa Dk Ulimboka ni uthibitisho kuwa watu wengi wasio na uwezo wanapoteza maisha kutokana na kukosekana kwa vifaa tiba na dawa hapa nchini... “Madaktari tupo, lakini tatizo ni vifaa na dawa, hiki ndicho tunachopigania ni haki wananchi kupata huduma za afya nchini.”

Katibu Mkuu wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Rodrick Kabangila alisema kurejea kwa Dk Ulimboka kutasaidia kuwatambua watu waliohusika katika tukio la kumteka, kumpiga na kumtupa katika Msitu wa Pande.

“Sisi tumefurahi sana, Dk Ulimboka alisimamia haki za madaktari na sekta ya afya kwa ujumla, kurudi kwake kunatupa nguvu ya kuendelea kudai haki za madaktari na wananchi,” alisema.

Dk Ulimboka anarejea nchini huku Serikali na madaktari wakiwa hawajafikia mwafaka kuhusu madai yao.

Madai ya madaktari hao ni hali bora ya mazingira ya utoaji afya nchini, ongezeko la mishahara, posho za kufanya kazi katika mazingira magumu, posho za kufanya kazi katika mazingira hatarishi na posho za kuitwa kazini.

Safari ya Dk Ulimboka kwenda kwenye matibabu nchini Afrika Kusini ilitawaliwa na usiri mkubwa alipoondoka nchini Juni 31 mwaka huu, akisindikizwa na Dk Pascal Lugajo na kaka yake, Dk Hobakile Ulimboka na mke wake,  Dk Judith Mzovela.

Kutekwa
Dk Ulimboka alitekwa na kufanyiwa vitendi vya ukatili wakati akiratibu mgomo wa madaktari uliokuwa ukiendelea na aliokotwa na msamaria mwema akiwa amefungwa mikono na miguu akiwa katika hali mbaya.

Kutokana na tukio hilo, wanaharakati wa haki za binadamu waliituhumu Serikali kuhusika na tukio hilo, huku Serikali ikikana na kuliagiza Jeshi la Polisi kuwasaka waliohusika.

Akisimulia mkasa huo Dk Ulimboka alisema tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Juni 27 katika Klabu ya Leaders, Dar es Salaam alikokuwa na daktari mwenzake na mtu mwingine aliyekuwa amemwita hapo (Leaders).

“Mara, katikati ya maongezi tukaona huyo mtu aliyeniita anaongea na simu. Ghafla tukiwa tunasema tuagane, wakaja watu kama watano hivi na bunduki, wakasema wewe na yule bwana mko free (huru), tunakuchukua wewe (Dk. Ulimboka). Sijakaa sawa, nikaona nimeshaburutwa nikaanguka kwenye lami, wakaniinua na kuniingiza kwenye gari nyeusi, lakini ilikuwa haina namba.”

Wakati Dk Ulimboka alipokuwa akiendelea na matibabu Afrika Kusini, Rais Jakaya Kikwete alisema Serikali haihusiki na kilichomtokea daktari huyo kwa kuwa alikuwa kiungo muhimu katika majadiliano baina ya Serikali na madaktari.

Rais Kikwete alisema hayo katika hotuba yake ya mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu.
“Dk Ulimboka alikuwa kiungo muhimu katika mazungumzo baina ya Serikali na madaktari. Ni kweli kwamba yeye si mtumishi wa Serikali, hivyo hakustahili kuwa sehemu ya majadiliano haya.

Kulikuwa na rai ya kutaka asiwepo, lakini nilisema wamuache maadam madaktari wanamwamini kuwa anaweza kuwasemea vizuri zaidi kuliko wao wenyewe walioajiriwa na Serikali,” alisema Rais Kikwete.

Alisema alichofanyiwa Dk Ulimboka kimemsikitisha na kumhuzunisha kwa kuwa ni kitendo cha kinyama na kinyume kabisa na mila na desturi za Tanzania.

Kauli ya Rais Kikwete kuhusu mgomo wa madaktari inafanana na ile iliyokuwa imetolewa awali na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akisema wanatambua kuwa Serikali nayo inatajwa katika orodha ya wanaotiliwa shaka kuhusu kilichomtokea Dk Ulimboka, lakini ameshangazwa na hisia hizo akisema haoni sababu ya Serikali kufanya hivyo.

Dk Ulimboka alisafirishwa kwenda Afrika Kusini Juni 31, mwaka huu kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi baada ya jopo la madaktari waliokuwa wakimhudumia, kueleza mabadiliko ya hali ya afya yake, yaliyosababisha figo kushindwa kufanya kazi.

Ulinzi nyumbani
Nyumbani kwao, eneo la Ubungo Kibangu kulikuwa na watu kadhaa waliokuwa nje ya nyumba huku ulinzi ukiwa umeimarishwa.

Vijana wasiopungua watatu wakiwa wamevaa kawaida walikuwa wamekaa jirani na lango la kuingilia wakiratibu nyendo za wanaopita na wanaotaka kuingia katika nyumba hiyo iliyopo karibu na Shule ya Msingi Ubungo Kibangu.

“Watu walikuwa wengi hapa lakini wametakiwa kuondoka ili kutoa nafasi kwa dokta kupumzika na hakuna ambaye anaruhusiwa kuingia kwa sasa labda kama ni daktari mwenzao,” alisema kijana mmoja anayeishi jirani.

Awali, mama mmoja ambaye alifahamika kama ndugu wa familia hiyo anayeishi karibu na nyumba ya Dk Ulimboka alipoulizwa nyumbani kwa kiongozi huyo wa madaktari alihoji anatafutwa na nani na hata mwandishi walipojitambulisha alimtaka aondoke na kurejea alikotoka.

“Baba wewe nenda nyumbani kwako tu, usitake kujua zaidi,” alisema mama huyo majibu ambayo yalionekana kufanana na ya majirani wengi wa daktari huyo.
Chanzo: Mwananchi

Friday, August 10, 2012

Ntagazwa afichua kilichomtoa CCM

Best Blogger Tips
 WAZIRI wa zamani wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Muungano), Arcado Ntagazwa, ameelezea sababu ya kuondoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), akisema ni hofu ya kukosa jibu mbele ya Mwenyezi Mungu juu ya chama hicho kilivyoshindwa kuwatumikia Watanzania licha ya kuongoza nchi yenye utitiri wa rasilimali.

Ntagazwa aliyasema hayo jana wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika Kata ya Mbingu eneo la Tandale katika Wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro.

Alisema, katika mila na desturi za Kiafrika, kiapo kina thamani kubwa na anayeshindwa kukitimiza kiapo chake, basi laana huwa juu yake.

“Mimi nilikuwa CCM, nikiwa mbunge kwa miaka 25 na kushika nafasi mbalimbali za uongozi, ikiwemo ya naibu waziri na uwaziri kamili…Ndani ya ilani ya CCM, kuna ahadi, ahadi ya nne inasema sitopokea wala kutoa rushwa, hii ikiwa ni ahadi ya kila mwana CCM ambayo inakiukwa kwa kiwango kikubwa,” alisema Ntagazwa.

Aliongeza kuwa, shida zote zinazoipata Tanzania kwa sasa, ikiwemo hali ngumu ya maisha, walimu kukosa maslahi bora na ukosefu wa huduma muhimu za kijamii, ni matokeo ya kiapo hicho kukiukwa na viongozi wa CCM.

Alisema, kwa sasa ndani ya CCM hakuna wa kumuonya mwenzake juu ya kuachana na mfumo wa kutoa na kupokea rushwa, hivyo kutokuwa mwokozi kwa tabaka la wanyonge.

Ntagazwa alisema, kutokana na hali hiyo kuwa sugu ndani ya CCM, yeye kama mtu anayehofu ghadhabu za Mwenyezi Mungu, aliamua kujiengua na kuchagua kupigania Watanzania kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

”Nilijua kuwa ipo siku Mwenyezi Mungu ataniita Ntagazwa… Ntagazwa nami nitamuitikia naam, swali litakalofuata ni je, ulitumiaje nafasi yako ya uongozi kwa Watanzania katika kuwatendea haki, ” alisema Ntagazwa huku wananchi wakimshangilia.

Alisema, kwa sababu ya ufisadi unaofanywa na Serikali ya CCM, leo hii kuna hatari kubwa ya vijana kuwa walemavu wa migongo (kibiongo) kutokana na kukaa chini muda mrefu wakiwa darasani  huku wakilazimika kutumia magoti yao kama meza ya kuandikia.
Chanzo: Tanzania Daima

Maelfu wamzika Atta Mills

Best Blogger Tips
 Maelfu ya wananchi wa Ghana jijini Accra wamehudhuria mazishi ya kitaifa ya rais John Atta Mills aliyefariki ghafla mwezi Julai mwaka huu.

Baadhi ya wakuu wa nchi za Afrika wapatao kumi na wanane na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani Hillary Clinton walihudhuria mazishi hayo katika uwanja wa historia ya uhuru mjini Accra.

Mills aliyeugua saratani ya koo kwa muda mrefu amefariki ikiwa imebaki miezi mitano tu kabla ya kufanyika uchaguzi wa urais ambao angegombea tena nafasi hiyo.

Mwandishi wa BBC mjini Accra anasema kifo chake kimewaunganisha Waghana katika majonzi.
Anasema kifo hicho kilionekana kama jaribio kwa demokrasia changa ya nchi hiyo.

Mills aliyeanza kipindi cha miaka minne ya urais mwezi Januari mwaka 2009, amerithiwa na makamu wake rais John Dramani Mahama.

Ghana imepongezwa na jumuiya ya kimataifa kwa namna ambavyo imeshughulikia kipindi cha mpito katika taifa hilo linalofahamika kwa siasa zake za mgawanyiko.

Mazishi

''Leo giza nene limetanda katika anga ya Ghana, Afrika na kwa kweli ulimwengu mzima,'' Bwana Mahama aliuambia umati wa waombolezaji waliokuwa wakifuatilia mazishi hayo kupitia televisheni kubwa zilizowekwa uwanjani hapo.

''Rais Mills alikuwa muhimu sana katika yale ambayo tumekuwa hatuna katika siasa zetu, uzalendo, uvumilivu katika uongozi, uaminifu,'' alisema.

Mwandishi wa BBC Vera Kwakofi anasema watu walianza kukusanyika mapema alfajiri katika uwanja huo wakiwa wamevalia mavazi maalum ya maombolezo rangi nyeusi na nyekundu.

Machifu wengi wa kimila walihudhuria wakiwa na ngoma zao wakipiga midundo ya ujumbe wa kuomboleza.

Mbele ya wapiga ngoma wachezaji walichezesha mikono yao kwa namna ya ishara yenye maana maalum.

Wakati bendi ya jeshi ilipoingia na mwili wa marehemu uwanjani, ngoma, nyimbo za kusifu na za kishujaa zilisimama, mwandishi wetu anasema.

Filimbi za kuomboleza zilichezwa wakati rais Mahama alipowasha moto wa ishara ya kumbukumbu kwa marehemu, ambaye daima alitambulika kama ''Profesa au Mwalimu'', ikiashiria taaluma yake ya muda mrefu ya ualimu, na ''Asumdwoehene'', ikimaanisha mfalme wa amani katika lugha ya Twi.

Misururu ya foleni

Kwa muda wa siku mbili kabla maelfu ya wananchi wa Ghana walisafiri kuelekea Accra kutoa heshima zao za mwisho kwa mwili wa Mills.

Baadhi walipanga foleni kwa saa kadhaa, wengi wao wakilia kwa uchungu, katika mistari ya urefu wa kama kilometa kumi nje ya jengo la Ikulu mjini Accra.

''Nimekuwa hapa kwa saa tatu, ili kumuona, lakini tutamkumbuka sana hapa,'' mwanamke mmoja aliiambia BBC.

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani Hillary Clinton aliwasili Ghana akitokea Nigeria siku ya Alhamisi kuhudhuria mazishi hayo, akikamilisha ziara yake ya siku kumi na moja ya nchi saba za Afrika.

 Amefanya mazungumzo na rais Mahama. Ikionekana kama mfano bora wa demokrasia katika eneo hilo la Afrika, ghana ilichaguliwa na rais wa Marekani Barack Obama katika ziara yake ya nchi zilizo kusini mwa jangwa la sahara mwaka 2009.

Mills aliyefariki akiwa na umri wa miaka 68 alikuwa ni mwanasiasa wa ngazi ya juu kwa miaka mingi.

Kati ya mwaka 1997-2001 alikuwa makamu wa rais kwa aliyekuwa mtawala wa kijeshi Jerry Rawlings, lakini alijiweka mbali na kiongozi huyo.

Aliingia madarakani baada ya ushindi mwembamba dhidi ya mgombea kutoka kilichokuwa chama tawala cha New Patriotic Party, Nana Akufo-Addo
katika uchaguzi wa mwaka 2008.
Chanzo: BBC

Thursday, August 9, 2012

Mahalu:Mungu amejibu

Best Blogger Tips
 MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imewasafisha aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu na Ofisa Utawala wa ubalozi huo, Grace Martin waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya Euro 2 Milioni.

Kutokana na uamuzi huo, Profesa Mahalu amesema anamshukuru Mungu akisema, yaliyotokana ni kwa sababu Mungu amempenda.

“Mungu amenipigania sana na haki imetendeka, sasa hivi nakwenda kanisani kumshukuru Mungu, nanyi nawaambieni mkasome Zaburi 17,” alisema Profesa Mahalu kwa furaha na kukumbatiana na mawakili na ndugu zake.

Profesa Mahalu na Martin walikuwa wakikabiliwa na mashtaka sita yakiwamo ya kula njama na kuiibia Serikali na kuisababishia hasara ya Euro 2,065,827.60, katika mchakato wa ununuzi wa jengo la Ubalozi wa Tanzania nchini Italia.

Hata hivyo,  jana Mahakama hiyo iliwaachia huru ikisema kuwa upande wa mashtaka katika kesi hiyo namba 1 ya mwaka 2007, umeshindwa kuthibitisha mashtaka hayo bila kuacha mashaka.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Ilvin Mugeta aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo alisema kuwa katika ushahidi uliotolewa na mashahidi wote saba wa upande wa mashtaka, hakuna ushahidi wa moja kwa moja unaowatia hatiani washtakiwa hao.

Alisema ushahidi uliopo ni wa mazingira tu ambao ulikuwa umesimamia katika nyaraka mbalimbali zilizowasilishwa mahakamani hapo na upande wa mashtaka kuhusiana na mchakato wa ununuzi wa jengo hilo.

Katika hukumu yake, Hakimu Mugeta alirejea na kusisitiza ushahidi uliotolewa na Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa akimtetea Profesa Mahalu kuwa ni msomi mzuri, mchapakazi, mwadilifu na mwaminifu.

Pia hakimu Mugeta alihoji ilikuwaje hata mshtakiwa wa pili, Martin akaunganishwa katika kesi hiyo kwa kuwa nyaraka zote zilizowasilishwa mahakamani hapo ambazo ndizo upande wa mashtaka ulizitumia katika mashtaka zilikuwa zinamhusisha mshtakiwa wa kwanza tu.

“Mwishowe napenda kusema kwamba nimeshindwa kufahamu ni kwa nini mshtakiwa wa pili alishtakiwa na ndiyo maana katika hukumu hii sikugusia ushahidi wake wa utetezi,” alisema Hakimu Mugeta na kuongeza:

“Kwa kuhitimisha ninasema kwamba upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha mashtaka bila  mashaka yote katika makosa yote sita na washtakiwa wote wanaachiwa huru katika makosa yote.”

Wakati akisoma hukumu hiyo,Hakimu Mugeta alianza kuchambua ushahidi wa upande wa mashtaka na ushahidi wa utetezi kisha akaanza kuainisha ushahidi huo jinsi ulivyoweza au ulivyoshindwa kuwatia hatiani washtakiwa hao kwa kosa moja baada ya lingine.

Kwanza, Hakimu Mugeta alisema anawaachia huru katika kosa la pili la wizi na kwa sababu hiyo hata kosa la kwanza la kula njama ili kutenda kosa hilo likawa limekufa kwa kuwa makosa hayo yote yanategemeana.

Akizungumzia kosa la kula njama, Hakimu Mugeta alisema dhana ya kosa hilo upande wa mashtaka uliegemea kwenye uwepo wa mikataba miwili ya ununuzi wa jengo hilo.

“Siko tayari kutumia dhana yao hiyo isipokuwa kama nitashawishiwa kupita mashaka yote kwamba matumizi ya mikataba miwili kununua jengo la ubalozi lenyewe tu inaunda kosa la jinai,” alisema Hakimu Mugeta.

Aliongeza kuwa upande wa mashtaka ulijielekeza kwenye kutambua kama kulikuwa na kibali cha kutumia mikataba miwili au la.

“Sidhani kama hili linahusiana katika mazingira ya kesi hii. Hii ni kwa sababu kama utumiaji wa mikataba miwili ni kosa la jinai, hakuna kibali ambacho kingeweza kuhalalisha hilo isipokuwa tu kwa kubadilisha sheria husika,”alisisitiza Hakimu Mugeta.

Hakimu Mugeta alirejea ushahidi wa utetezi wa Mkapa kuwa hata kama lengo la muuzaji wa jengo hilo lilikuwa ni kukwepa kodi ya nchi yake, hilo ni tatizo la mwenye jengo na nchi yake na kwamba matakwa ya nchi yalikuwa ni kupata jengo la ubalozi.

Hakimu Mugeta alisema kwa mujibu wa kielelezo cha 5 cha upande wa utetezi [exhibit D5], taarifa ya mthamini kutoka Wizara Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, thamani ya jengo hilo ilikuwa ni Dola za Marekani 5.5milioni.

Alisema hata hivyo, tathmini ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa bei ya jengo hilo ilikuwa ni  Euro 3,098,741.38 na kwamba ndiyo maana ilituma kiasi hicho ambacho ndicho kilicholipwa kwa mnunuzi.

Kuhusu shtaka la wizi, Hakimu Mugeta alisema kuwa hakuna ushahidi unaonyesha kuwa baada ya kiasi hicho  cha pesa kulipwa kwa mwenye jengo kupitia akaunti mbili tofauti za benki za mwenye jengo, baadaye Mahalu alikwenda benki kuzichukua pesa hizo kwa matumizi yake binafsi.

Alisisitiza kuwa mshtakiwa wa kwanza alipewa mamlaka ya kununua jengo hilo kwa bei iliyoonyeshwa katika kielelezo hicho cha 7 cha upande wa mashtaka yaani Euro 3,098,741.38.

Hakimu Mugeta alisema kwa maoni yake ni kwamba ikiwa mshtakiwa baada ya Serikali kukubali bei hiyo ya ununuzi wa jengo hilo, kutoa pesa, na kumpa mshtakiwa wa kwanza nguvu ya kisheria, utaratibu wa malipo ulipaswa kufuata taratibu za Italia.

Alisema hayo ni masharti ambayo muuzaji alimpa mshtakiwa wa kwanza na kwamba shahidi wa pili upande wa utetezi, Mkapa alisema kuwa mahitaji ya nchi yalikuwa ni kupata jengo.

Hakimu Mugeta alisisitiza kwamba kwa mujibu wa ushahidi wa upande wa mashtaka na hata wa utetezi, taratibu zote za ununuzi wa jengo hilo zilifuatwa na kwamba ndiyo maana wataalamu walitumwa kwenda kufanya uthamini.

Kutokana na makosa hayo kutokuthibitishwa na upande wa mashtaka, Hakimu Mugeta pia alitupilia mbali kosa la kuisababishia hasara Serikali akisema kuwa pia upande wa mashtaka umeshindwa kulithibitisha.

Utetezi wa Mkapa

Wakati wa utetezi wao, Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ambaye ununuzi wa jengo hilo ulifanyika wakati wa uongozi wake alipanda kizimbani na kumtetea Mahalu na mwenzake, akidai kuwa mchakato wa ununuzi wa jengo hilo ulifuata sheria.

Mkapa katika ushahidi wake wa utetezi licha ya kudai kuwa mchakato huo ulifuata taratibu na kwamba ni yeye aliyebariki, pia alimmwagia Mahalu sifa nyingi akidai kuwa ni kiongozi mwadilifu na mwaminifu katika historia yake ya utumishi wa umma.

Akiongozwa na mmoja wa mawakili wanaomtetea Mahalu na mwenzake, Wakili Alex Mgongolwa, Mkapa alieleza mchakato wote wa ununuzi wa jengo hilo na malipo yake kwa kuwa lilinunuliwa kwa maagizo Serikali yake.

Wakati upande wa mashtaka ukidai kuwapo kwa uhujumu uchumi kutokana na kuwapo kwa mikataba miwili wakati wa ununuzi wa jengo hilo, Mkapa alidai kuwa aliifahamu mikataba hiyo yote na malipo kufanyika kupitia akaunti mbili tofauti.

Alienda mbali zaidi na kueleza kushangazwa kusikia kuwa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi wakati huo, Martin Lumbanga katika ushahidi wake alidai kuwa hakujua mchakato wa ununuzi wa jengo hilo, akieleza kuwa haujui ni kwa nini Lumbanga alisema hivyo.

Mbali na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambayo wakati wa ununuzi wa jengo hilo, Rais Jakaya Kikwete ndiye aliyekuwa waziri wake, Mkapa alisema wizara nyingine zilizohusika ni Wizara ya Ujenzi na Wizara Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Alidai kuwa wizara zote hizo zilituma wataalamu wake kwenda kufanya tathmini ya thamani ya jengo hilo kabla ya ununuzi wake.

Alisisitiza kuwa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wakati huo, Kikwete bungeni juu ya ununuzi wa jengo hilo ni sahihi.

Pamoja na mambo mengine taarifa hiyo inaeleza kuwa jengo hilo lilinunuliwa kwa Sh2.9 bilioni na kwamba hati za umiliki wake zilishawasilishwa wizarani na kupelekwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali [CAG].

“Maneno hayo ni sahihi. Hayo ndiyo ninayoyajua mimi,”  alidai Mkapa na kuongeza kwamba hajawahi kupata malalamiko kutoka Italia kuhusu ukiukwaji wa sheria wakati wa mchakato wa ununuzi wa jengo hilo wala kwa mmiliki akidai kuwa alilipwa pungufu ya makubaliano.

Akijibu swali la Wakili Mgongolwa kama alishapata malalamiko yoyote kutoka kwa CAG kuhusu ununuzi wa jengo hilo, alijibu kuwa hajawahi kupokea malalamiko hayo.

Akijibu swali la Wakili wa Serikali, Ponsiano Lukosi kama aliwahi kuuliza ni kwa nini mwenye jengo alitaka alipwe kupitia mikataba miwili Mkapa alijibu kuwa hakuuliza kwa kuwa alichokuwa anahitaji ni kupata jengo.

Kuhusu kama lengo la mwenye jengo kutaka kulipwa kwa mikataba miwili lilikuwa ni kukwepa kodi ya Serikali ya nchi yake, Mkapa alijibu:

“Hilo ni tatizo lake na nchi yake, mimi nilikuwa nataka nyumba na nimepata nyumba, nasema Alhamdulilah”.

Pia Mkapa alisema kuwa anamshangaa sana wakili wa Serikali kudai kuwa pesa hizo kulipwa kwa awamu mbili Mahalu alikuwa na lengo za kuzichukua na kuzitumia kwa masilahi yake.

“Mimi nitashangaa sana kusikia hivyo na hasa nitakushangaa wewe maana Profesa [Mahalu] mimi namwamini.”, alisisitiza Mkapa.


Maoni nje ya mahakama

Baada ya hukumu hiyo kutolewa, mawakili waliokuwa wakimtetea Balozi Mahalu na mwenzake, Martin waliizungumzia hukumu hiyo kwa nyakati tofauti.

Wakili Mabere Marando, baada ya Hakimu Mugeta kuwaachia huru wateja wake saa 7:27 mchana alisema  kuwa ana furaha kubwa kwa kuwa Mahakama imetenda haki.

“Hukumu hii iliyotolewa leo kweli ni ya kihistoria kwa sababu ni hukumu ya haki, hakimu amejitahidi kueleza hoja na zote ni za muhimu na kwamba hapakuwepo na sheria ya kumshtaki Mahalu,”alisema Marando huku akiwa ni mwenye tabasamu.

Wakili Alex Mgongolwa ambaye naye pia alikuwa akiwatetea kina Mahalu, alisema kuwa ana furaha  kwa kuwa haki imetendeka.

 “Kwa kweli haki imeonekana kutendeka na imetendeka; Mahakama imetenda haki,”alisema Mgongolwa huku akicheka.

Naye Martin alisema: “Namshukuru Mungu kwa kushinda kesi hii.”

Wakati hayo yote yakiendelea mahakamani hapo, ndugu  wa Mahalu na Martin walikuwa na furaha huku wakituma ujumbe mfupi kweye simu zao za mkononi wakiwajulisha wenzao juu ya tukio hilo.

Katika utetezi wao, upande wa Jamhuri ilileta jumla ya mashahidi saba ambao ni aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Martin Lumbanga, Stewart Migwano, Marco Papi, Kapteni Abubakari Ibrahim, Mkongoti, Kyando kutoka Takukuru na nyaraka mbalimbali.

Utetezi wa Mahalu

Awali akitoa utetezi wake katika mahakama hiyo, Mahalu alidai kuwa alipofika katika Ubalozi huo wa nchini Italia  alikuta ofisi zikiwa na hali mbaya hali iliyosababisha kutoa fedha zake mfukoni na kununua thamani zenye hadhi ya ofisi ya ubalozi. 



Akiongozwa kutoa utetezi wake na wakili wake Marando na Mgongolwa alidai kutokana na kuikuta ofisi hiyo ikiwa na hali hiyo mbaya alilazimika kutoa fedha zake mfukoni kwa ajili ya kununulia samani za ofisini. 



Mahalu alidai kuwa Aprili 1, mwaka 2000 ndiyo siku aliyofika rasmi mjini Rome nchini Italia ikiwa ni siku chache baada ya Mkapa kumteua kuwa Balozi ambapo alieleza majukumu yake yalikuwa ni kulinda na kuyatetea masilahi ya Tanzania na wakati akiwa Balozi wa Italia pia wakati huo huo alikuwa ni balozi wa nchi tisa ambazo ni Greece, Turkey, Serbia, Slovenia,Croatia, Macedonia, Montenegro. 



Alieleza jukumu lake jingine ni kupokea maelekezo kutoka hapa nchini kuhusu kukuza uhusiano baina ya nchini na nchi na kwamba yeye ndiye aliyekuwa mkuu wa masuala yote ya utawala wa ofisi ya ubalozi na kwamba masuala yote ya utawala yalikuwa yakiletwa kwake na maofisa wa ubalozi na Serikali kwa ujumla.

“Nilipofika Italia nilikuta hali ni mbaya inasikitisha kwani ubalozi wa wetu nchini Italia ulikuwa umefungwa tangu mwaka 1994 na nilipoteuliwa mimi kwenda huko ndiyo nikawa nimeenda kuufungua ubalozi huo uanze kufanya kazi. Na wakati nafika hapo kila kitu cha ubalozi kilikuwa kimeondolewa na kurudishwa nchini kikabaki kiofisi kidogo tu kwa ajili ya kushughulikia masuala ya kilimo na mwaka 1997 ndiyo Serikali ilimpeleka msimamizi wa ofisi hiyo.” 



Alidai kuwa baada ya kukuta hali hiyo alichukua hatua ya kumweleza aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa wakati huo, Balozi Kibeloh na kwamba aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo kwa kipindi hicho alikuwa Jakaya Kikwete ambaye kwa sasa ndiye Rais wa nchi ambaye naye alifika katika ofisi za ubalozi huo na kushuhudia hali hiyo mbaya.

Alidia Kikwete aliunga mkono hoja yake kwamba ofisi hiyo ni mbovu na akashauri ipatikane ofisi yenye hadhi ya ubalozi. 



Aliendelea kueleza mbali na Kikwete, pia aliyekuwa Makamu wa Rais , Dk Ali Mohamed Shein naye alitembelea ofisi hizo za ubalozi na kushuhudia ubovu ule na akamuahidi mshtakiwa huyo kuwa akirudi nchini atafikisha tatizo hilo ili taratibu zifanywe za kupatikana jengo kubwa la ubalozi. 



Profesa Mahalu alieleza kuwa baada ya kumweleza matatizo hayo ya ubalozi Katibu Mkuu, Balozi Kibeloh, alikubaliana naye akasema ni muhimu kwa Serikali kutafuta jengo jipya na kwamba Mei 2001, alipewa taarifa na balozi huyo kuwa Rais Mkapa atakwenda Brussels kwa ziara ya kikazi na kwamba yeye mshtakiwa akamwomba tena katibu mkuu huyo amruhusu akamweleze Mkapa matatizo hayo pindi atakapofika Brussels na katibu mkuu huyo alimruhusu.

“Niliporudi mjini Rome Italia, nilimjulisha kwa barua Katibu Mkuu Balozi Kibeloh mazungumzo yangu na Rais Mkapa na balozi huyo naye akanijibu kuwa atazidi kulifuatilia jambo hilo na kuliweka kwenye bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na kwa sababu hiyo ilikuwa ni sera ya wizara yake ya kutaka ofisi za ubalozi wetu nje ya nchi zinunue majengo yao hivyo hoja hiyo itapelekwa bungeni na haitapingwa. ”alidai Profesa Mahalu.

 Mshtakiwa huyo aliendelea kueleza kuwa wakati akisubiri ahadi hiyo ya Katibu Mkuu huyo, mwanzoni mwa Juni 2001, Katibu Mkuu huyo alimpigia simu akimpongeza kwamba maombi ya wizara yao katika bajeti ya kutaka kila ofisi ya ubalozi inunue jengo lake itapitishwa na Bunge na kuongeza kuwa Katibu Mkuu alimtaka mshtakiwa huyo na maofisa wengine wa ubalozi kuanza kutafuta majengo.



Alidai kuwa baada ya kupokea habari hiyo njema kutoka kwa Katibu Mkuu, yeye mshtakiwa alimwandikia barua ya kumshukuru Mei 4 mwaka 2009 ambayo nakala yake aliomba mahakama iipokee kama kielelezo na Hakimu Mugeta aliipokea kama kielelezo cha kwanza.

Utetezi wa Grace
Mei 8, mwaka huu, Martin ambaye alikuwa Ofisa wa Utawala aliieleza mahakama hiyo ya Kisutu kuwa Balozi  Mahalu hakuisababishia Serikali hasara ya Euro 2 milioni, bali alileta faida kwa taifa kwa kuwa na jengo zuri na kwamba anahitaji kupewa shukrani.

Akiongozwa na Wakili Marando kujitetea dhidi ya tuhuma zinazomkabili, Martin alidai kuwa kwa ufahamu wake Balozi Mahalu hakuisababishia Serikali hasara kwa kuwa ununuzi ulileta faida na nchi kupata jengo zuri na  fedha hazikupotea na anastahili shukrani.

Aliendelea kuiomba Mahakama itupilie mbali tuhuma hizo  na kwamba madai ya kuwa Balozi Mahalu alitumia risiti ya ununuzi wa jengo la ubalozi wa Tanzania nchini Italia kuidanganya Serikali kuwa mwenye nyumba amelipwa fedha siyo ya kweli.
Chanzo: Mwananchi

Wednesday, August 8, 2012

NTC yatoa madaraka kwa Congress, Libya

Best Blogger Tips
 Serikali ya mpito nchini Libya imekabidhi madaraka ya kulitawala taifa hilo kwa baraza la Congress lililobuniwa baada ya uchaguzi mkuu wa mwezi uliopita , ikiwa ni hatua muhimu katika kipindi cha mpito katika siasa za taifa hilo.

Mziki wa wa bendi ya jeshi ulichezwa kuwakaribisha wanasiasa na maafisa wa ngazi ya juu katika jeshi waliokuwa wakiwasili tayari kwa sherehe hizo.

Kisha serikali ya mpito nchini Libya ikakabidhi madaraka kwa baraza la Congress ambalo lilibuniwa baada ya uchaguzi wa hivi maajuzi.

Hafla yenyewe ikajawa na taswira ya mwamko mpya katika mji mkuu wa Tripoli.
Hafla hii inaashiria hatua za mpito katika siasa za Libya kutoka utawala wa ki-imla hadi utawala wa kidemokrasia wenye viongozi waliochaguliwa.

Hii haingetokea kama Kanali Muamar Gaddafi angekuwa bado madarakani, wengi wanaamini.
Serikali ya mpito inayovunjwa iliwajumuisha wanamgambo wa upinzani waliomng'oa madarakani na kisha kumuua kanali muamar Gadaffi mwaka mmoja uliopita.

Mustafa Abdel Jalil mwenye kiti wa baraza la kitaifa lililoendesha serikali hiyo ya mpito akihutubu wakati wa sherehe hizo za kukabidhi madaraka, amesema baraza la Congress ndilo pekee lenye haki ya kikatiba kuwaakilisha raia wa Libya.

Waandishi wanasema ingawa kuna utulivu katika mji mkuu, Tripoli, mapigano yanaendelea katika maeneo mengi ya Libya.

Baadhi ya makundi ya wanamgambo yangali yanashikilia madaraka makubwa.
Chanzo: BBC

Tuesday, August 7, 2012

Kipigo cha Dk. Ulimboka chazua balaa Tigo

Best Blogger Tips
 KUTEKWA, kupigwa na kuteswa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Chama cha Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka na hatimaye kufungiwa kwa Gazeti la MwanaHalisi kwa muda usiojulikana, kumeleta kizaazaa katika kampuni ya simu za mkononi ya Tigo, Tanzania Daima Jumatano limebaini.

Habari kutoka ndani ya kampuni hiyo ya simu yenye mtandao mpana nchini, zinasema kuwa zaidi ya wafanyakazi 30 wamefukuzwa kazi na wengine wako kwenye uchunguzi wakituhumiwa kuvujisha mawasilino ya siri ya simu za wateja kwa Gazeti la MwanaHalisi.

Kwa mujibu wa habari hizo, taarifa za mawasiliano za simu zinazodaiwa kuvujishwa na wafanyakazi hao, zilikuwa kati ya Dk. Ulimboka, Afisa Usalama wa Ikulu na watu aliowasiliana nao kabla ya kutekwa.

Rais Jakaya Kikwete amepata kuliambia taifa mara mbili kwa njia ya televisheni, mwishoni mwa Juni na alipozungumza na wahariri wa vyombo vya habari wiki iliyopita, kwamba serikali yake haihusiki kuteka, kutesa na kumtupa daktari huyo porini.

Naye Waziri Mkuu Mizengo Pinda amepata kuliambia Bunge kuwa, serikali yake haihusiki na utekaji, utesaji na kuhoji, “...serikali imteke ili iweje?”

Hivi karibuni serikali ililifungia Gazeti la MwanaHalisi baada ya kuandika habari iliyomtaja ofisa mmoja wa Idara ya Usalama wa Taifa Ikulu (TISS), kuwa ndiye aliyetekeleza mpango wa kumteka, kumpiga na kumtesa hadi kumjeruhi Dk. Ulimboka, ambaye kwa sasa anaendelea na matibabu kwenye hospitali moja nchini Afrika Kusini.

Kwa mujibu wa habari hiyo ambayo serikali inadai kuwa ni ya uchochezi, MwanaHalisi ilianika namba ya simu ya ofisa huyo pamoja na watu wengine wanaodaiwa kuhusika katika tukio hilo linaloendelea kuchunguzwa na kamati maalumu iliyoundwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI).

Vyanzo vya habari kutoka kwa baadhi ya wafanyakazi waliokumbwa na sekeseke hilo, zinasema kuwa waliofukuzwa wengi ni wafanyakazi wa kitengo cha IT ambao wanadaiwa kuhusika kutoa taarifa za siri ya mawasilino kati ya Dk. Ulimboka na watu wanaoaminika kuwa ni wabaya wake.

Mmoja wa wafanyakazi kutoka Kampuni ya Tigo, aliliambia gazeti hili kuwa mbali na kutuhumiwa kutoa siri kwa Gazeti la MwanaHalisi, wafanyakazi wengine wametimuliwa kwa madai ya kufanya udanganyifu kwenye huduma za Tigo Pesa na kujipatia fedha.

“Kweli watu wengi wamefukuzwa wakituhumiwa kutoa siri kwa Gazeti la MwanaHalisi, lakini wengine walikuwa wakishirikiana na mawakala wa Tigo Pesa kuiibia kampuni.

“Kwa mfano mfanyakazi alikuwa anakubaliana na wakala kumwingizia kiasi kama cha sh milioni moja, lakini anaweza kuingiza hadi sh milioni 1.5 na kati ya hizo sh 500,000 ni mali yake,” alisema mfanyakazi huyo.

Akizungumzia na Tanzania Daima Jumatano, Mhariri Mkuu wa Gazeti la MwanaHalisi, Jabir Idrissa alishangazwa na taarifa za Tigo kuwafukuza wafanyakazi wake kwa sababu ya habari iliyochapishwa na gazeti lake.

“Chanzo chetu cha habari hakikutoka kwa wafanyakazi wa Tigo. Kama wamefukuzwa kwa sababu ya MwanaHalisi, wamewaonea bure. Kama Tigo ndio waliotupa taarifa na zile za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), zilitoka wapi?” alihoji Jabir na kusisitiza wafanyakazi hao wameonewa bure.

Ofisa Uhusiano wa Tigo, Edward Shila, alipohojiwa kuzungumzia tukio hilo, hakukubali wala kukataa madai hayo na kumtaka mwandishi kumtumia maswali kupitia e-mail yake ili aweze kuyatolea majibu kiofisi.

“Kama una maswali naomba uniandikie kupitia e-mail yangu ambayo nakutumia sasa hivi…maana siko tayari kutoa kauli yoyote isiyokuwa ya kiofisi,” alisema.

Naye Omary Matulla ambaye amejitambulisha kuwa ni ofisa wa kitengo cha kumbukumbu katika kampuni hiyo, alikanusha kuwapo kwa taarifa za kufukuzwa wafanyakazi wa kampuni hiyo.

Alisema kuwa kila mfanyakazi ana mipaka ya kufanya kazi katika kampuni hiyo, na pia ni wajibu wa kila mtumishi kutunza siri kubwa.

“MwanaHalisi ana mbinu zake za kupata habari wala haiwezekani kupata habari kupitia kampuni yetu na hata hivyo jambo hilo si rahisi hata kidogo kutokea,” alikanusha Omary.

Dk. Ulimboka alitekwa usiku wa Juni 26, kusukumizwa kwenye gari, kupigwa, kufungwa mikono na miguu, kunyofolewa kucha na kutolewa meno na hatimaye kutupwa katika msitu wa Mabwepande nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Tangu kutokea kwa tukio la kutekwa kwa Dk. Ulimboka, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na wanaharakati wa kutetea haki za binadamu, wamekuwa wakiinyoshea kidole serikali kwamba ndiyo iliyohusika.

Kamanda wa Kanda Maalumu ya Polisi mkoani Dar es Salaam, Suleiman Kova, hivi karibuni alitangaza kumfikisha mahakamani mtu mmoja aliyedai kukiri kuhusika na utekaji wa Dk. Ulimboka.
Kova aliwaambia waandishi wa habari kuwa, polisi wamekamata mtu aitwaye Joshua Malundi kutoka Kenya ambaye amekiri kumteka na kumtesa Dk. Ulimboka.

Alidai kuwa mtuhumiwa alikwenda kutubu katika Kanisa la Ufufuo na Uzima, Kawe, Dar es Salaam.
Lakini hata hivyo, mchungaji wa kanisa hilo, Josephat Gwajima alikana kauli ya Kova juu ya mtuhumiwa huyo, akisema hajakwenda kutubu kwao.
Chanzo: Tanzania Daima

Wabunge wa Kenya waketia viti vipya

Best Blogger Tips
Viti Vipya
 Bunge la Kenya lililokarabatiwa na ambalo limekuwa gumzo kubwa kwa sababu ya gharama ya viti vya bunge hilo, hatimaye limefunguliwa rasmi na rais wa nchi hiyo Mwai Kibaki.

Viti hivyo vimegharimu dola 3,000 za kimarekani kwa kila kiti kimoja vikiwa jumla ya 350 vimetengenezwa na kitengo cha magereza nchini humo.

Zabuni ya kwanza ya kutengeneza viti hivyo ilitolewa kwa kampuni moja ya nje lakini ilifutwa baada ya baadhi ya wabunge kugundua kila kiti kingegharimu dola 5000 za kimarekani.

Maafisa wanasema ukarabati huo uliogharimu dola milioni 12 utaliweka bunge katika mfumo mpya wa kisasa wa komputa.

"Mabadiliko tunayoyafanya yataleta mabadiliko chanya katika uongozi," spika wa bunge Kenneth Marende ameiambia BBC.

Amesema mfumo wa kupiga kura wa elektroniki utawawezesha wabunge kupiga kura kwa uhuru wao binafsi kuliko kulazimika kupiga kura kwa kuhofia vyama vyao.

"sasa mbunge atakuwa peke yake, huru kabisa binafsi, atafanya maamuzi yake na kubonyeza tu kitufe."

Mwandishi wa BBC Odeo Sirari mjini Nairobi, anasema baadhi wanaona viti hivyo kuwa ni vya gharama kubwa sana kuliko mabunge mengine katika jumuiya ya madola.

Waziri mkuu wa Kenya Raila Odinga na rais Mwai Kibaki pamoja na wabunge ni miongoni mwa wanaolipwa mshahara wa juu sana barani Africa.

Wabunge walifurika katika jengo hilo lililokarabatiwa wakati rais na spika wakiongoza utaratibu wa sherehe za ufunguzi.

Ukarabati huo ulianza mwezi Aprili mwaka 2010 na ulikuwa umepangwa kuchukua mwaka mmoja kumalizika lakini ulichelewa kwasababu ya utata ulioghubika zabuni yake, mwandishi wetu anasema.

Mbunge John Mbadi, katika kamati ya uwekezaji aliongoza upinzani juu ya zabuni ya kwanza.

"hatukuweza kuelewa ni kwa vipi wabunge wangekuwa wanakaa katika viti vinavyogharimu karibu shilingi 400,000 za Kenya kama dola 5,000, ambazo kwa kiwango chochote cha kawaida zingeweza kujenga nyumba kwa wananchi kadhaa," ameiambia BBC.
"ilikuwa ni upuuzi," amesema.

Mwandishi wetu anasema watu wengi wamelalamika kuwa gharama za sasa bado ni juu.
David Langat, anayesimamia uzalishaji katika magereza nchini Kenya, amesema vifaa vyote vilivyotumika vilitoka nchini Kenya lakini gharama za viti zimekuwa kubwa sana.

Ameiambia BBC kuwa viti hivyo vyenye uzito wa kilo 50 kila kimoja vina kinga dhidi ya moto na vina dhamana ya miaka 30.

Kwa sasa Kenya ina jumla ya wabunge 220 lakini ukumbi huo umewekwa viti 350 idadi ambayo watachaguliwa katika uchaguzi ujao mwezi Machi kwa mujibu wa katiba mpya.
Chanzo: BBC

Shivji, Lwaitama wataka Muungano uvunjwe

Best Blogger Tips
 WASOMI na wanazuoni nchini wametaka Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, uvunjwe kwa kuwa waasisi wake walikuwa na maslahi yao binafsi.

Wakitoa mada kwa nyakati tofauti Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Azaveli Lwaitama, Prof. Abdul Sheriff wa Zanzibar na Prof. Issa Shivji waliushambulia Muungano huo.

Akitoa mada juu ya nguvu ya vyombo vya habari katika kutatua kero za Muungano, Prof Issa Shivji alisema, viongozi wanapindishapindisha historia ya Muungano na kuitumia kama kichaka cha maovu yao.

Aliongeza kuwa, hakuna Msahafu wa Muungano hivyo ulipaswa kuwa na mgawanyo wa madaraka kwa pande zote mbili, hivyo aliitaka tume ya Katiba kutoa fursa kwa wananchi ili watoe maoni yao juu ya suala la Muungano.

Pia alishauri kuwepo na demokrasia ya wazi na ukweli kwa ajili ya Watanzania juu ya suala hilo la Muungano.

Kwa upande wake, Dk. Lwaitama alieleza kuwa sio jambo la hekimu kuyalazimisha makundi ya watu kwa kutumia bunduki.

“Huu Muungano hata waliouanzisha hawakujua namna ya kufanya pale inapotokeza changamoto kama hizi za leo,” alisema na kuongeza kuwa, hakuna haja ya kung’ang’ania Muungano kwa kuwa lengo la waasisi lilikuwa ni kutengeneza taifa ambalo tayari limefanikiwa.

Awali, Prof. Sheriff alisema Zanzibar imepoteza imani na Muungano kutokana na muundo wake kuwa na matatizo tangu ulipoanzishwa.

Alitaka kutumiwa kwa fursa iliyopo ya marekebisho ya Katiba kwa lengo la kuungalia Muungano kwa jicho la tatu.

Alihadharisha vyombo vya habari kuacha kuandika habari za maovu na kuzipamba kama ilivyoripotiwa katika tukio la kikundi cha uamsho, ambapo wengi waliziandika bila kuwa na ufahamu wa kina.
Source: Mwananchi

Monday, August 6, 2012

Ndugai: Baadhi ya wabunge wanalewa wakati wa vikao

Best Blogger Tips
 WAKATI kashfa ya baadhi ya wabunge kuhongwa na kampuni za mafuta ili yatetee mikataba yao haijapoa, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai ameibua tuhuma nyingine nzito kwamba baadhi ya wawakilishi hao wamekuwa wakiingia kwenye vikao wakiwa wamelewa pombe na sigara zisizo za kawaida.

Katika siku karibuni, baadhi ya wabunge wamekuwa wakinaswa na kamera wakiwa wamelala bungeni wakati vikao vinaendelea, kwa maelezo ya uchovu, kauli ambayo huenda sasa ikaongeza mjadala miongoni kama
kinachosababisha walale wakati vikao vinaendelea iwapo ni uchovu wa
kazi au ulevi.

“Kuna wabunge ninavyohisi wanaingia bungeni wakiwa wamevuta sigara fulani kubwa, kulamba vitu fulani au hata kupata bia mbili tatu,” alisema Ndugai akihojiwa jana asubuhi katika kipindi cha medani za

siasa na uchumi cha Star tv.
Ndugai alisema amekuwa akiona hali hiyo hasa Bunge la kuanzia mchana, bila kueleza ni hatua ambazo zimekuwa zikifanyika kupambana na wawakilishi hao wa wananchi wanapobainika wamelewa.
“Wabunge ni watu kama watu wengine, wana tabia kama walivyo wanadamu wengine, wapo ambao kwa namna ninavyohisi wanaingia bungeni hasa vikao vya kuanzia mchana wakiwa wamepiga bia,” alisisitiza
Ndugai ambaye ni Mbunge wa Kongwa, mkoani Dodoma.

Ingawa hakufafanua, inavyofahamika sigara yenye kulevya ni bangi,kulamba vitu fulani vyenye kulewesha maana yake inaweza kuwa kuna baadhi ya wabunge wanatumia dawa za kulevya, pia ulevi mwingine

wa kutumia bia.
Bila kueleza hatua ambazo Bunge linachukua kwa wabunge walevi,
Ndugai aliwataka wabunge kuweka maslahi ya taifa mbele na kujenga
tabia ya kuongea mambo wakiwa na ushahidi.

“Ni kwamba kuna wabunge wamekuwa wakizungumza mambo bila ushahidi,
hili jambo halikubali, wabunge wanapaswa kuzingatia sheria kama
walivyo Watanzania wengine, unapomtuhumu mtu lazima uwe na
ushahidi, lakini inasikitisha sana unakuta mbunge anasema jambo,
anamtaja mtu kwamba anahusika na hili na lile wakati hana hata chembe
ya ushahidi,” alisema.

Pia, aliwataka wanasiasa wote kujenga tabia za kuthamini yale ambayo yanafanywa na wanasiasa wengine.

“Nimekuwa nikifuatilia mambo yanavyokwenda nchini, kuna wanasiasa wanakosea, unakuta mpinzani amekuwa akisema mabaya tu kwa chama tawala, unakuta tunaitwa mafisadi, siyo sahihi, kwa mfano Star tv kukawa na mtu mgoni, ni tatizo la huyo haina maana kwamba wafanyakazi
wote ni wagoni. CCM ni taasisi kubwa, mambo haya yanaweza kutokea.

Lakini pia siyo kweli kwamba wanachama na viongozi wote wa upinzani ni wasafi,” alisema Ndugai na kuongeza:

“Kuna wanasiasa wamekuwa na tabia ya kuona kila kinachofanywa na CCM
ni ushetani, hiyo siyo sawa! Kwa mfano mimi jimboni nimefanya maendeleo mengi. Wakati naingia Bungeni mwaka 2000 kulikuwa na shule chache mno za sekondari, lakini sasa ziko zaidi ya 30, hata zahanati zilikuwa chache sasa ni zaidi ya 40, ni kutokana na jitihada zangu na chama changu, mtu anapokuja kusema hatujafanya kitu tunashindwa kumuelewa.”

Naibu Spika huyo alikwenda mbali zaidi na kuwashauri viongozi wa Serikali akiwamo Msajili wa Vyama vya Siasa kuwa na utaratibu wa kupitia kauli zinazotolewa na wanasiasa, kwa maelezo kuwa baadhi yao
wamekuwa wakitoa kauli nzito, au kukashifiana bila kuchukuliwa hatua.

“Unaweza kukuta mwanasiasa anaibua kashfa nzito, lakini hachukuliwi hatua wala kuulizwa, hiyo siyo sahihi. Wanasiasa tunapaswa kubishana kwa hoja, siyo vinginevyo,” alisema Ndugai.

Ndugai alipoulizwa kuwa wabunge hao hatua watakazochukuliwa kutokana na tabia zao, alisema suala hilo haina haja ya kulizungumzia zaidi ila libaki kama alivyosema.
“Hilo siwezi kulizungumzia zaidi libaki kama nilivyozungumza na walioniomba nizungumze nao,” alisema.
Chanzo: Mwananchi

Sunday, August 5, 2012

Urais 2015 wavuruga chaguzi za CCM

Best Blogger Tips
 MBIO za kuwania nafasi za uongozi wa juu wa Jumuiya za Chama cha Mapinduzi (CCM), imeshika kasi huku taarifa zikionyesha kwamba kambi zinazowania urais wa 2015 ndani ya chama hicho, kila moja inajipanga kuhakikisha inaweka watu wake.

Wakati katika Umoja wa Wanawake (UWT) hadi jana mchuano ulikuwa ukionyesha kuwa mkali kati ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba na Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela hali ni tofauti kwa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM).

Hadi jana katika mbio za kuwania nafasi ndani ya UVCCM, vijana wanne walikuwa wamechukua fomu kuwania nafasi ya uenyekiti na wengine 16 wakiomba nafasi ya makamu mwenyekiti wa jumuiya hiyo ngazi ya taifa huku Katibu Mkuu wa Umoja huo, Martine Shigella akisema wanafahamu mikakati hiyo ya kambi za urais.

Kwa upande wa UWT, Kilango anaonekana kusimama kundi la makada wa CCM wanaojipambanua kupambana na ufisadi, huku Simba akiwa na kundi jingine tofauti na hilo lakini, pia lenye malengo ya urais wa 2015.

Baadhi ya vyanzo vya habari kutoka ndani ya CCM, vilisema mbali ya nafasi hiyo ya juu ya UWT, kinyang’anyiro hicho pia kipo katika nafasi za wenyeviti wa mikoa.

Tayari vita hiyo ya kambi za urais iko pia katika mikoa ambako kila kambi inajipanga kuweka mtu wake, huku katika Mkoa wa Tabora vita ikitarajiwa kuwa kali zaidi kati ya Margareth Sitta na mgombea wa kambi ya watuhumiwa wa ufisadi.

UVCCM
Kwa upande wa umoja huo wa vijana, kambi hizo zimekuwa zikiumana kuhakikisha kila moja inaweka mtu wake katika nafasi ya uenyekiti, makamu na ujumbe wa Baraza Kuu.

Hadi jana waliokuwa wakiwania nafasi za uenyekiti wa UVCCM Taifa ambao tayari walikuwa wamerejesha fomu ni Thabit Jecha Kombo, Sadifa Juma Khamis na Rashid Simai Msaraka.

Katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti ni Paul Makonda, Ally Salum Hapi na Agustino Matefu. Makonda alirejesha jana na kuzungumza na waandishi akiahidi kupambana na mafisadi.

Wanaowania nafasi za Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (Nec), kupitia UVCCM ni Theresia Mtewele, Halima Bulembo, Olivia Sanare, Ahmed Nyangani, Santo Tena, Vaileth Sambilwa, Faidha Salim na Augustino Samwiya.

Katika nafasi za Ujumbe wa Baraza Kuu la Taifa ni, David Mwakiposa, Mteweke Bulembo na Ester Mambali.

UVCCM ni ngome muhimu kimkakati kutokana na kuwa na vijana wengi wanaoweza kufanikisha ajenda mbalimbali ndani na nje ya vikao vya chama na jumuiya.

Uchaguzi huo wa UVCCM unafanyika wakati, kiti cha mwenyekiti kikiwa wazi tangu mwaka 2010 baada ya aliyekuwa mwenyekiti wake, Yusuf Hamad Masauni kuong’olewa akituhumiwa kudanganya umri na tangu wakati huo nafasi yake ilikuwa ikishikiliwa na Makamu wake, Beno Malisa.

Taarifa ya Sekretarieti ya chama hicho iliyowasilishwa katika kikao cha NEC mjini Dodoma mapema mwaka huu ilieleza kuwa makundi ya urais 2015 ndiyo yanayosababisha mpasuko ndani ya chama hicho.

Shigella: Tunajua
Akizungumzia mikakati hiyo ya vigogo wanaotaka urais kumwaga fedha ili kujiweka mazingira mazuri ya kuwa na watu wao ndani ya UVCCM, Shigella alisema wanajua mipango hiyo na kuonya kwamba kama kuna mgombea ambaye ametumwa na genge la watu wanaotarajia kuwania urais 2015, ajue anapoteza muda kwa sababu hatapitishwa.

Alisema jumuiya hiyo haijawahi kuwa na kiongozi aliyepandikizwa na mtu yoyote.
Alisema watatumia njia mbalimbali kuwabaini watu wa aina hiyo, hasa kwa kuitumia Kamati ya Usalama na Maadili ya jumuiya hiyo na kuwafanyia usaili wagombea na kuangalia historia zao.

“Kwa hiyo, kama kuna wanaowania nafasi za urais mwaka 2015 ambao wametuma vijana kutafuta nafasi UVCCM wafahamu kuwa hawatafanikiwa kwa kuwa tumejiandaa kukabiliana nao,” alisema Shigela.

Makonda na ufisadi
Kwa upande wake Makonda ambaye jana alikuwa wa mwisho kurejesha fomu kwa wiki iliyoisha jana, aliwaambia waandishi wa habari kuwa tatizo la rushwa na ufisadi kwa baadhi ya watu ndani ya UVCCM ndilo lililomsukuma kuwania nafasi hiyo.

Alisema historia ya UVCCM kutoka Tanu Youth League imejengeka katika misingi ya uadilifu na uzalendo, lakini katika siku za karibuni kumekuwa na baadhi ya watuhumiwa wa ufisadi ambao wamekuwa wakibomoa misingi hiyo na kujenga ya kwao ya kifisadi.

“Hii ndiyo changamoto ambayo imenifanya nijitose katika  kinyanganyiro hiki, si vizuri kuhama chama kikiwa na matatizo. Njia sahihi ni kutafuta uongozi ili kukabiliana nayo. Tukiwa na viongozi bora tutakuwa na uchungu wa namna ya kutatua matatizo ya vijana, kama uchumi na hata mikakati ya ajira,” alisema.

Alisema wakati rushwa ilitajwa kama adui wa haki katika moja ya ahadi 10 za Mwana-TANU, sasa hivi imekuwa ikitumika kama haki ya kupata uongozi hivyo vijana wanyonge wasiokuwa na fedha za kutoa rushwa kukosa nafasi za kuongoza.

Nape: Tumejipanga
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape Nauye alisema hafahamu kama kuna vijana wanaowania nafasi mbalimbali kwa lengo la kuwasaidia vigogo kwenye mbio za urais mwaka 2015.

“Ndiyo kwanza unaniambia, sina habari hizo. Katika CCM tunachoangalia ni kwamba wanaowania nafasi hizo ni kutojihusisha na rushwa vinginevyo hawatakuwa na sifa za kuchaguliwa,” alisema Nape.
Chanzo: Mwananchi

Makamba: Maisha bora hayawezi kuletwa na JK

Best Blogger Tips
 BAADA  ya kimya cha muda mrefu, Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM, Yusuf Makamba  ameibuka na kusema kuwa maisha bora kwa kila Mtanzania hayawezi kuletwa na Rais Jakaya Kikwete.

Amesema kuwa mbunge mzuri anaweza kutoka chama chochote iwapo Watanzania watashirikiana naye katika kuleta maendeleo ya eneo husika.

Makamba ametoa kauli hiyo ikiwa imepita muda mrefu tangu aibuke katika kikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho (Nec) na kumtuhumu Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye kwamba amekigeuza chama kuwa mali yake binafsi.

Katika kikao hicho Makamba alisema hatua ya Nape kugeuza chama hicho kama taasisi yake binafsi ndiyo ambayo imesababisha kikose mwelekeo.


Lakini jana wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya mwanaye, January ambaye ni Mbunge wa Bumbuli na Naibu Waziri wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia kufungua mkutano wa wakazi wa jimbo hilo, Makamba alisema maendeleo ya Watanzania yataletwa na wao wenyewe, kwa kufanya kazi.

Huku akizungumza baadhi ya maneno kwa lugha ya kisambaa na kunukuu baadhi ya vifungu vya biblia takatifu, Makamba alisema Watanzania wamekuwa wavivu wa kufanya kazi na kwamba kila kitu wanategemea kitafanywa na Rais Kikwete.

Makamba alisema kuwa kwa sasa kumezuka tabia ya baadhi ya Watanzania kuwatupia lawama viongozi kwa kushindwa kuwapa maisha bora.

Makamba, alisema kuwa maendeleo hayawezi kuletwa na mbunge peke yake bali kinachohitajika ni ushirikiano wa pamoja ili kuweza kutimiza lengo na ahadi mbalimbali alizotoa.

Alisema kuwa anashangazwa na baadhi ya Watanzania kuamua kumtupia lawama Rais Kikwete kuwa kashindwa kuleta maisha bora wakati hawana umoja wa kuunganisha nguvu katika kutatua changamoto zinazoikabili nchi.

“Hata kama CCM itaondoka madarakani na kuingia Chadema  bado Watanzania wataendelea kulia umaskini kwa kuwa hatuna tabia ya kushirikiana na kufanya kazi,” alisema Makamba.

Makamba alimwagia sifa mwanaye, January ambaye alikuwa akizindua Shirika la Maendeleo Bumbuli (SMB)ambalo alilianzisha baada ya kuwa mbunge mwaka 2010, kusema kuwa kijana huyo ni mfano wa kuigwa na Watanzania kwa kuwa katika kipindi kifupi cha uongozi wake jimboni humo ameweza kutekeleza ahadi mbalimbali.

Alisema kuwa wananchi wa Bumbuli hawakufanya makosa kumchagua mbunge huyo na kuongeza kwamba wanatakiwa kumpa ushirikiano ili kulifanya jimbo hilo kupiga hatua kimaendeleo.

Kwa upande wake, January wakati akiwakaribisha wakazi wa Bumbuli pamoja na waliotoka mikoa jirani, alisema kuwa wamekutana ili kuangalia namna ya kukabiliana na changamoto zilizopo jimboni humo.

Alisema kuwa siku zote maendeleo huletwa na wakazi waliopo mbali na nyumbani hivyo aliwaomba kuhakikisha kuwa na umoja ili kuondoa matatizo yaliyopo jimboni humo ikiwa ni pamoja elimu, afya, miundombinu na maji.

Alisema kwa upande wake atahakikisha BDC, linawasaidia wakazi hao katika masuala ya ajira na elimu.

Alisisitiza kuwa ili kuinua kiwango cha ufaulu katika jimbo hilo wamebuni njia ya kupandisha ufaulu wa wanafunzi kwani kuanzia sasa wameanzisha kambi ya wanafunzi zaidi ya 150 waliofanya vizuri katika mitihani yao ya mokono ili kuwanoa zaidi, lengo likiwa ni kuhakikisha wanafanya vizru katika mtihani wao wa mwisho.


Januari ambaye ni Naibu Waziri wa Sayansi na Mawasiliano, alisema kuwa wamegundua kuwa baadhi ya wazazi jimboni humo wamekuwa kikwazo cha wanafunzi kushindwa kufanya vema mitihani yao.

aliongeza kuwa  BDC imepata fedha kiasi cha Sh 730 milioni kwa ajili ya kukusanya na kununua mazao ya mboga mboga yaliyopo jimboni humo,  hatua ambayo itasaidia kununuliwa kipato cha wakulima.

Alisema hatua hiyo itakwenda sambamba na kukifufua kiwanda cha matunda cha Maweni ambapo mkulima ataweza kuuza mazao yao huko na kuepukana na madalali na kwamba vijana zaidi ya 120 watapata ajira.
Chanzo: Mwananchi

Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits