Thursday, February 9, 2012

Wamarekani watafuta uwekezaji katika nishati

Best Blogger Tips
Rais Kikwete akiwa pamoja wageni kutoka Marekani
WAFANYABIASHARA wa sekta ya nishati kutoka nchini Marekani juzi walikutana na Rais Jakaya Kikwete ili kuangalia fursa mbalimbali za uwekezaji katika sekta hiyo.

Ujumbe huo wa wafanyabiashara uliongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anayeshughulikia masuala ya Afrika, Johnnie Carson na ulifanya   majadiliano  na Rais kuhusu sekta ya nishati Tanzania na fursa mbalimbali za uwekezaji kwa kampuni za nishati kutoka Marekani.
Naibu Waziri Carson na ujumbe wake waliwasili jijini Dar es Salaam Februari 8, mwaka huu ikiwa ni sehemu ya ziara ya nchi nne zikiwamo Msumbiji, Nigeria na Ghana ili kuona fursa za uwekezaji hususan katika miradi ya uzalishaji umeme. 

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Ubalozi wa Marekani ilieleza kuwa ujumbe huo ulidhaminiwa pia na Baraza la Wafanyabiashara wa Marekani kwa Afrika (The Corporate Council on Africa) na unathibitisha dhamira ya dhati ya Serikali ya Marekani ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara na Tanzania wakati huo huo ikitangaza fursa nyingi zilizopo hapa nchini.

   "Ujumbe wa Naibu Waziri Carson unajumuisha wawakilishi wa Kampuni za Anadarko Petroleum, Caterpillar, Chevron, Energy International, General Electric, Pike Enterprises, Strategic Urban Development Alliance LLC, Symbion, na Zanbato Group,"ilieleza taarifa hiyo na kuongeza;  "Wajumbe wengine wanaoiwakilisha Serikali ya Marekani ni pamoja na Makamu Mwenyekiti wa U.S. Export-Import Bank, Wanda Felton na viongozi wa Idara ya Rasilimali za Nishati ya Marekani." 

 Ilieeza kuwa juzi, ujumbe huo ulishiriki pia katika majadiliano na maofisa wa sekta ya nishati wa Serikali ya Tanzania na wa sekta binafsi yaliyofanyika katika Hoteli ya Serena na baada ya hapo unatarajiwa kukutana na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO William Mhando.  
Ubalozi huo katika taarifa yake umeeleza kuwa leo, ujumbe wa Naibu Waziri Carson utatembelea Kituo cha Taifa cha Uwekezaji (TIC) ambako watakuwa na majadiliano na wawakilishi wa kituo hicho, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati (EWURA).    mwisho
Chanzo: Mwananchi

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits