Friday, May 25, 2012

CHADEMA kuwasha moto Jangwani leo

Best Blogger Tips
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), leo kitafanya mkutano mkubwa wa hadhara katika viwanja vya Jangwani, jijini Dar es Salaam ambapo Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk. Wilbord Slaa watahutubia.

Aidha, viongozi wengine wakiwemo wabunge wake 15 ni miongoni mwa watakaoshiriki mkutano huo, akiwemo Mbunge wa Ubungo John Mnyika ambaye juzi, alitangazwa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuwa mbunge halali baada ya kushinda kesi ya kupinga ushindi wake, iliyokuwa ikimkabili.

Joto la mkutano huo limepanda kiasi kwamba, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limetangaza kuweka ulinzi mkali.

Taarifa ya CHADEMA jana imesema kuwa, ingawa Mahakama Kuu imewapatia ushindi wabunge wake, Tundu Lissu, John Mnyika, Gervas Mbasa na wengine waliopingwa, leo katika mkutano huo itaeleza umuhimu wa mabadiliko ya kimfumo katika mhimili huo, na katika utendaji kazi wa Tume ya Uchaguzi (NEC), ambayo chama hicho kinataka iwe chombo huru katika kutekeleza majukumu yake nyeti mbalimbali, ikiwemo kusimamia uchaguzi.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, John Mnyika, alidai kunahitajika mabadiliko ya kimfumo kwa sababu kumekuwa na athari kubwa katika maendeleo ya wananchi, na pia kikwazo cha kuweka madaraka ya uendeshaji wa nchi mikononi mwa umma kama inavyotamkwa katika ibara ya 8 ya katiba ya sasa.

“Tunataka wananchi wajitokeze kwa wingi kusikiliza masuala mbalimbali, zikiwemo hoja juu ya umuhimu wa kufanya mabadiliko ya kimfumo kupitia uandikwaji wa katiba mpya, waje wajue namna ambavyo ubovu wa katiba ya sasa umechangia kwa kiasi kikubwa matatizo makubwa yanayotukabili kama taifa, ikiwemo umaskini, ujinga, maradhi, ufisadi na CCM yenyewe,” alisema Mnyika.

Alidai kuwa katika mkutano huo, watazindua kampeni ya ‘kuiamsha Dar es Salaam’, ikiwemo kaulimbiu ya ‘Vua Gamba, Vaa Gwanda’ inayotarajiwa kuwapokea viongozi na wanachama wengi kutoka CCM.

Aliongeza kuwa, tofauti na CCM ambayo imeanza mchakato wa katiba kwa kujifungia na kutoa misimamo ya mamlaka za chama bila hata maoni ya wanachama wake nchi nzima, CHADEMA itatumia fursa hiyo kutoa elimu ya uraia kwa umma juu ya sheria ya mabadiliko ya katiba, ili kuwezesha umma kumiliki mchakato na hivyo taifa lipate katiba bora.

Mbali na Mnyika, wabunge wengine watakaoonekana leo ni pamoja na Peter Msigwa, Ezekiah Wenje, Tundu Lissu, Grace Kiwelu, Halima Mdee, Rose Kamili, Mhonga Said, Suzan Kiwanga, Joyce Mkya, Godbless Lema na Meya wa Manispaa ya Musoma, Alex Malima Kasurula.

MVUTANO POLISI, CHADEMA
Hata hivyo, pamoja na Jeshi la Polisi kuruhusu kufanyika kwa mkutano huo, kumezuka mvutano kati ya pande hizo mbili kuhusu suala la wanachama kufanya matembezi ya hiyari kutoka kila kona ya Jiji la Dar es Salaam kuelekea Jangwani.

Wakati CHADEMA wakitangaza ramani yatakapopita matembezi hayo, polisi imeyapiga marufuku kwa madai kwamba hakuna sheria yoyote inayoruhusu chama cha siasa kufanya matembezi au maandamano.

Awali, CHADEMA ilituma maombi ya maandishi kwa Jeshi la Polisi kuruhusu matembezi hayo ya amani, kutoka sehemu mbalimbali za jiji hadi viwanja vya Jangwani panapofanyika mkutano wa hadhara leo.

Lakini jana Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema, wanaruhusu kufanyika kwa mkutano huo, na wamejiandaa kikamilifu katika ulinzi, lakini si kwa matembezi.

Kwa mujibu wa Kamanda Kova, CHADEMA iliwasilisha barua ya kuomba kibali cha kufanya mkutano, lakini kabla ya kujibiwa, kilipeleka barua nyingine yenye lengo la kupewa kibali cha matembezi ya amani.

Kova alidai kuwa, mwanachama yeyote atakayekaidi amri hiyo, atachukuliwa hatua za kisheria, na kuonya kuwa watu wasidanganyike kufanya matembezi hayo, ila kila mtu anayo haki ya kwenda katika mkutano kwa namna ya kawaida.

Hata hivyo, CHADEMA imepinga na kudai kuwa hayo si maandamano, bali matembezi maalum kutoka kwenye maeneo ya jiji kwenda viwanja vya Jangwani, ikizingatiwa kuwa hali ni ngumu na si kila mtu mwenye uwezo wa kumudu gharama za usafiri.

Chama hicho kimedai kuwa, Watanzania wanayo haki kikatiba kufanya maandamano na mikusanyiko ili mradi hawavunji sheria, na kimetangaza barabara zitakazotumiwa na watu wa majimbo ya Ilala, Ukonga na Segerea, kuwa ni Buguruni, Uhuru, Msimbazi, Morogoro hadi Jangwani.

Watakaotoka majimbo ya Kinondoni, Kawe na Ubungo, watakutanika katika bustani ya Magomeni, kupitia barabara ya Morogoro hadi Jangwani, wakati wale wa Kigamboni, wataanzia Kivukoni, kupitia Posta ya zamani, Makao Makuu ya Jiji, barabara ya Morogoro hadi Jangwani.

Wale wa Temeke, wataanzia Mwembeyanga, kupitia barabara ya Mandela, Buguruni na kukutana na wale wa majimbo ya Ilala na kuelekea Jangwani.
Chanzo: Tanzania Daima

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits