Wednesday, May 30, 2012

Sabodo atoa rai ya ‘kubanana’ na ubadhirifu

Best Blogger Tips
Mustafa Sabodo
 MFANYABIASHARA maarufu nchini, Mustafa Sabodo amewataka mawaziri kutembelea mashirika ya umma, idara, wakala na mamlaka za Serikali zilizo chini yao kwa kushitukiza.

Katika barua ya wazi aliyomuandikia Rais Jakaya Kikwete kwenye gazeti dada la Daily News jana, Sabodo alisema kazi hiyo ifanyike kila mwezi na baadaye kupeleka ripoti ya kila mwezi kwa rais.

Alisema tatizo la rushwa nchini si kubwa katika ngazi ya menejimenti ukilinganisha na idara, mashirika ya umma, wakala na mamlaka za Serikali.

Aidha, Sabodo amemtaka Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kuhakikisha anatembelea kampuni ya madini kwa sababu yanaiibia nchi.

“Waziri wa Nishati na Madini lazima atembelee makampuni ya madini kwani yanatupora. Tafadhali pitia upya ripoti ya Mark Bomani,” ilisema sehemu ya barua hiyo ya Sabodo.

Pamoja na kuwataka mawaziri wote, lakini Sabodo pia ametilia mkazo kwa mawaziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi (Profesa Anna Tibaijuka), wa Fedha (Dk. William Mgimwa) na wa Nishati na Madini kuhakikisha kila mwezi wanaripoti kwa rais na pia kutembelea kwa kushitukiza idara na mamlaka kama vile Mamlaka ya Mapato (TRA), Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na zingine.

Akizungumzia hatua yake ya kukisaidia Chama cha Maendeleo na Demkorasia (CHADEMA), Sabodo ambaye ni kada wa CCM, alisema anafanya hiyo ili kukifanya chama hicho cha upinzani kuwa mwangalizi na kudhibiti matendo maovu ya baadhi ya watu, mawaziri, idara za Serikali ya chama tawala.

“Watu wanasema mimi ni mwanachama wa Chadema, kimsingi siyo, lakini ninakiunga mkono chama hicho kwa sababu ninataka kuwa mwangalizi na kudhibiti matendo mabovu ya baadhi ya watu, mawaziri, Idara za Serikali katika Serikali ya chama tawala,” alisema Sabodo.

“Mwaka 2004 nilishawahi kusema mpinzani si adui, ni mshirika na msaidizi muhimu katika kuleta maendeleo ya Taifa letu,” alisema na kuzungumzia fedha zake, akisema hana fedha haramu za kutoa misaada kwa jamii, na kwamba kipato chake kinatokana na kulipa kodi anazolipa nchini.

“Ukiachilia mbali kodi ninayolipa moja kwa moja Tanzania katika mamlaka husika, sioni ubaya wowote wa mtu kutumia kipato alichokipata nje kwa kushirikiana na masikini wa Tanzania,” alisema.

Aidha, Sabodo alisifu vitendo vya kibinadamu anavyovionesha Rais Jakaya Kikwete na Waziri wa asiye na Wizara maalumu, Profesa Mark Mwandosya hasa kutokana na hatua ya kukataa kupewa msaada wa kuchimbiwa visima katika jimbo lake na kutaka vikachimbwe kwa watu wenye mahitaji zaidi.
Chanzo: HabariLeo

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits