Sunday, September 16, 2012

UWT kwawaka moto

Best Blogger Tips
MAPENDEKEZO ya Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya ya Umoja wa Wanawake (UWT) wa CCM ya majina ya wagombea nafasi ya uenyekiti wa jumuiya hiyo ngazi ya taifa, yameibua mlolongo wa tuhuma kuwa yalifikiwa kwa upendeleo, rushwa na woga.

Tuhuma hizo zimetolewa na baadhi ya walioomba kuteuliwa kuwania nafasi hiyo, ambao majina yao hayakupendekezwa na kamati wanayodai kuwa ilifanya kazi kwa woga na kuwapendelea baadhi ya wagombea baada ya kushawishiwa kwa rushwa.

Mbali ya malalamiko ya wagombea, taarifa kutoka ndani ya UWT zinaeleza kuwa, uteuzi wa majina yaliyopendekezwa na kamati ya utekelezaji na kupelekwa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM umeibua ufa baina ya wanajumuiya hiyo kwa kile kinachoelezwa baadhi yao kujiona wanatengwa kwa sababu hawana watu wa kuwapigania dhidi ya wake wa vigogo wanaodaiwa kuogopwa na kutetewa na waume zao.

Mmoja wa wagombea ambaye jina lake halikupendekezwa, Hamida Thabit, katika mahojiano yake na gazeti hili kuhusu mwenendo wa mchakato wa uteuzi alisema ulikuwa wa hovyo kwa sababu haukuzingatia sifa na uwezo wa waombaji.

Alisema waombaji wenye sifa majina yao hayakupendekezwa kwa sababu hawakuwa na pesa za kuwafurahisha wajumbe, na majina ya waombaji ambao waume zao wana sauti ndani ya chama yalipitishwa kwa woga.

“Sijaridhika na mapendekezo ya kamati. Siyo kwamba nina uchu wa madaraka, lakini wakati mwingine ukiona mambo yanakwenda kombo kiasi cha kutisha ni lazima kusema. Na ninasema ili NEC ilione hili, itende haki kwa sababu UWT ni waoga.

“Baadhi yetu majina yetu hayakupendekezwa kwa sababu hatuna pesa, hatuna watu wa kututetea, hatuna wanaume wenye nyadhifa au sauti ndani ya chama. Ni aibu kwa jumuiya iliyokomaa kama UWT kuchagua watu kwa kuwaogopa, eti wasipochaguliwa watapiga kelele.

“Wabunge wenye majimbo, wana kazi za kila siku za kusimamia majimbo yao, bado wanataka na kazi ngumu ya kuongoza umoja huu na majina yao yanapitishwa, hiyo maana yake nini? Wanaachwa watu wenye sifa, wanaoijua UWT,” alisema Hamida.

Alisema mwenendo wa sasa wa CCM unaonekana kuwa wa kifamilia zaidi kwa sababu licha ya kuwa na wanachama wengi wenye sifa na uwezo wa kushika nafasi za uongozi, bado nafasi hizo zinatolewa kwa kujuana na hasa kwa kuangalia wake wa vigogo.

Alitolea mfano wa Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango, kuwa ni mbunge wa jimbo ambaye ana jukumu la kuwatumikia wapiga kura wake, hivyo hapaswi kukabidhiwa jukumu lingine la kuongoza UWT kwa sababu majukumu yote ni mazito.

Pia alisema Maryrose Majinge hakupaswa kupendekezwa kwa sababu hana sifa zinazostahili kuwa kiongozi wa juu wa umoja huo.

“Anne Kilango ni mbunge wa jimbo, anawajibika kwa karibu sana kwa wananchi wa jimbo lake, lakini bado anataka uenyekiti wa jumuiya. Majukumu yote ni mazito, kwanini yeye tu majukumu hayo?

“Sophia Simba ni sawa kwa sababu yeye ni mwenyekiti hivyo anatetea kiti chake na anao uzoefu wa uongozi ndani ya jumuiya, lakini hata huyu Maryrose, ametokea umoja wa vijana moja kwa moja amerushwa hadi kwenye uenyekiti, aanzie chini ajifunze na kupata uzoefu.

“Huu ni upendeleo wa wazi kabisa, unajua ukiwa na watoto watatu halafu ukawa unampendelea mmoja tu, wengine lazima watalalamika na itafika mahali watapachukia nyumbani, huko ndiko tunakokwenda.

“Kwa sababu lazima ieleweke kuwa kujua kupiga kelele siyo ujuzi wa kiutendaji, kupiga kelele bungeni siyo kigezo cha kuwa kiongozi bora,” alisema.

Alipoulizwa kama ana mpango wa kukata rufaa kupinga mapendekezo hayo, alisema hana mpango huo kwa sababu anaamini hakuna kitakachofanyika isipokuwa anabaki na matumaini NEC itatenda haki.

Mgombea mwingine aliyelalamikia mapendekezo ya kamati ya utekelezaji ya UWT ni Hilder Kitana, ambaye alisema ingawa anayaheshimu maamuzi ya kamati hiyo, amesikitishwa na kitendo chake cha woga.

Kitana alisema kamati hiyo imewaacha baadhi ya waombaji wenye sifa na kuchukua majina ya watu ambao hawana rekodi ya uongozi ndani ya jumuiya, lakini pia wenye majukumu ya kila siku kwa nafasi ambazo tayari wanazo.

“Wameamua wamependekeza majina hayo sawa, nayaheshimu. Lakini nimesikitishwa na woga wa kamati hii. Tukienda kwa kuogopana kama walivyokuwa wanasema ndani ya kamati hiyo hatutafika, tunaiua jumuiya.

“Mimi nimekuwa Mjumbe Kamati Kuu ya UWT, nimekuwa Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Dar es Salaam, ninaijua jumuiya, sina jukumu kwa sasa linalonibana moja kwa moja zaidi ya biashara zangu, halafu jina langu linakatwa kwa sababu wanasema wakimuacha Kilango, anaongea sana na mke wa mtu mkubwa itakuwa matatizo, atapiga kelele hadi kwenye vyombo vya habari, huu ni udhaifu mkubwa,” alisema Kitana.

Kwa upande wake, Maryrose Majinge, alisema licha ya jina lake kupendekezwa, anasubiri maamuzi ya NEC.
Alisema nafasi za uongozi ndani ya CCM zinapaswa kuzingatia uwezo wa utendaji badala ya kuchagua watu kwa sifa ya kuzungumza au kwa majina ya wenzi wao.

Wiki iliyopita, kamati ya utekelezaji ya UWT iliyoketi mjini Dodoma ilipendekeza majina ya wanachama wake watatu kwenda NEC ya CCM kwa ajili ya kuwania uenyekiti wa jumuiya hiyo. Waliopendekezwa ni Mwenyekiti wa sasa, Sophia Simba, Anne Kilango na Maryrose Majinge.
Chanzo: Tanzania Daima

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits