Saturday, August 13, 2011

Kikwete aongoza maziko ya Mayunga

Best Blogger Tips
RAIS Jakaya Kikwete ameongoza mamia ya waombolezaji kumzika Luteni Jenerali (mst) Silas Mayunga kwenye makaburi ya Wasabato ya Unyanyembe mjini hapa.

Jenerali Mayunga, shujaa wa Operesheni Chakaza ya kumng’oa Iddi Amin baada ya kuwa ameivamia Tanzania mwaka 1978, alifariki dunia mwishoni mwa wiki iliyopita katika Hospitali ya Apollo jijini New Delhi, India, ambako alikuwa anatibiwa.

Alikuwa na umri wa miaka 71.

Jenerali Mayunga alizikwa juzi kwa taratibu zote za Kanisa la Wasabato na za kijeshi ikiwa ni pamoja na kupigiwa mizinga 15 na gwaride la heshima la Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Rais Kikwete aliungana na viongozi wa kitaifa katika maziko hayo ambao ni pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Edward Lowassa ambaye ni Waziri Mkuu wa zamani na Waziri wa Ulinzi Hussein Mwinyi.

Wengine ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Amina Masenza, wenyeviti wa CCM wa mikoa ya Shinyanga na Mwanza, wabunge wa Mkoa Shinyanga akiwamo Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davies Mwamunyange na viongozi wengine waandamizi wa Jeshi na wapiganaji.

Rais Kikwete akifuatana na mkewe Mama Salma, aliwasili makaburini saa 9.56 alasiri akitokea Dar es Salaam ambapo pia alikuwa na ziara ya siku mbili Shinyanga ikiwa ni pamoja na kuhudhuria maziko hayo.

Mara baada ya Rais kuwasili makaburini, gwaride la Jeshi lililobeba mwili wa marehemu, liliingia eneo la makaburi saa 10.12 jioni na mwili wa marehemu kuteremshwa kaburini saa 10.30.

Mjane wa marehemu na watoto wake walikuwa wa kwanza kuweka udongo kaburini wakifuatiwa na Rais na Mama Salma, Lowassa, Mwinyi, Masenza, Jenerali Mwamunyange na Naibu Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Uganda, Luteni Jenerali Colleta Ivan, ambaye baadaye
aliwasomea waombolezaji salamu za rambirambi za Rais Yoweri Museveni.

Katika salamu zake, Rais Museveni alielezea mchango wa Jenerali Mayunga katika Operesheni Chakaza akisema alikuwa Jenerali ambaye alimpokea Museveni na wapiganaji wake 28 wa awali kwenye Shule ya Msingi ya Nyamiyanga mkoani Kagera Desemba 23, 1978.

Alisema: “Wakati Kampala inatekwa kutoka mikononi mwa majeshi ya Iddi Amin na kufikia hatua muhimu ya kuikomboa Uganda Aprili 11, 1979, askari wapiganaji katika kikosi hicho cha Waganda walikuwa 9,000 na yote hii ilikuwa kazi ya Jenerali Mayunga ambaye alitoa
mchango mkubwa sana kuongeza askari hao kwa kiwango hicho kikubwa. Tumepotelewa na mpiganaji na Kamanda hodari.”
Source: HabariLeo
 

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits