Sunday, August 28, 2011

Wananchi wamepoteza imani na CCM-Msekwa

Best Blogger Tips
Via Majira

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bw. Pius Mseka, amekiri wananchi kupoteza imani na chama hicho, kutokana na
matukio mbalimbali yanayojitokeza, huku viongozi wa chama na serikali wakishindwa kuchukuliwa hatua.

Pia alisema kutokana na hali hiyo, ndio maana katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2010, CCM ilipata ushindi wa asilimia 61 ikilinganishwa na asilimia 82 ambazo chama hicho kilipata mwaka 1995.

Bw. Msekwa, alitoa kauli hiyo jana wakati akuhojiwa na kituo cha televisheni cha Star Tv katika kipindi cha Medani za Siasa na Uchumi.

Alisema chama tawala kinapaswa kutambua kuwa kina wajibu wa kutimiza majikumu yake sasa, kwani inapofika mahala chama kikasahau wajibu wake wananchi wana haki ya kutokukichagua.

"Ili chama kichaguliwe ni lazima kioneshe kwa vitendo nia  na malengo ya kutimiza wajibu kwa wananchi, ili waweze kukiamni," alisema.

Bw. Msekwa alisema kiongozi yoyote anayeficha  ukweli kwamba wananchi wamepoteza imani na CCM, mtu huyo hayuko makini na hatakiwi kuendelea kuwa mwanachama.

Alisema kuwa kutokana na mambo yanavyoendelea  na viongozi wa serikali kushindwa kuchukua hatua ni chanzo cha wananchi kupoteza imani na chama.

Aliongeza kwa kutambua hilo, ndio maana chama kimekuja na dhana ya kujifua gamba kwa kuwataka wanaotuhumiwa kukipotezea mwelekeo chama hicho, wajiondoe wenyewe.

Hata hivyo alijigamba kwamba vyama vya upinzani kama Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) kilipata wabunge wengi bungeni kutokana na wanachama wa CCM waliokuwa wanagombea ubunge kuachwa katika kura za maoni na kukimbili upinzani.

"Ni kweli kabisa kuna baadhi ya makosa tulifanya kwa kuwapitisha wagombea wasiokubalika kwa wananchi na wale waliokubalika tuliwaacha na wao kuhamia CHADEMA na ndio hao wameshinda," alisema Bw.Pius.

Alisema vya upinzani havikuwa na uwezo wa kuwashawaishi wananchi ili wavichague, bali ilitokana na nguvu ya CCM kwa kuwa wananchi walikuwa na imani na CCM na ndio maana walichaguliwa kupitia mgongo wa CCM.

Aliongeza kuwa  CCM iliwaacha watu hao waliokimbilia  vyama vya upinzani kwa kuwa CCM ilikwishawabaini kwamba si watu wema ndani ya chama.

Bw. Msekwa alisema si  jambo jema kwa wananchi kuelekeza matatizo yote yanayotokea hivi sasa kwa chama cha mapinduzi japo kinashika dola.

Alisema kiwango cha uadilifu kwa  watendaji kwa sasa kimepungua tofauti na zamani, kwa kuwa zamani kulikuwa na chama kimoja na watendaji pia walikuwa waaminifu sana tofauti na sasa.

"Zamani uadilifu ulikuwa mkubwa kwa watendaji kwa kuwa kulikuwa na mfumo wa chama kimoja na wanachama wote macho yao yalikuwa yakilinda uadilifu tofauti na sasa", alisema.

Alisema watu wanaotakiwa kujivua gamba wapo kwenye ngazi zote.

Akizungumzia suala la makundi ndani ya chama, alisema hali hiyo inatokea wakati wa kura za maoni, ambapo majungu yanaanzia hapo na siri nyingi kuvuja na hatimaye wale walioachwa kuanzisha makundi na kuwashawishi wanachama kutowapigia kura waliopitishwa.

Alisema wanapaswa kukaa chini na kutafuta njia za kuondoa makundi ndani ya chama. "Changamoto si  kuyafumbia macho kwa kuwa yasipofanyiwa kazi yatapeleka chama pabaya," alisema.
Endelea kusoma habari hii...................
 
No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits