Thursday, March 29, 2012

Wachumi waipiga kombora Serikali mbele ya Kikwete

Best Blogger Tips
WACHUMI kutoka China na Vietnam wamesema umasikini unaoikabili Tanzania unatokana pamoja na mambo mengine, viongozi kuwa na maneno mengi kuliko vitendo.Walisema hayo jana mbele ya Rais Jakaya Kikwete na kukosoa mchakato wa ubinafsishaji uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Tatu ambao umebinafsisha na kuua viwanda vingi vya msingi.

Wakichangia mada katika mkutano wa 17 wa mwaka wa Taasisi ya Utafiti wa Kuondoa Umasikini Tanzania (Repoa), wachumi hao waliokuwa wamealikwa kueleza uzoefu wao katika masuala ya kuondoa umasikini, walisema Tanzania haikuwa nchi ya kutegemea misaada kutoka kwa wahisani, bali ilipashwa kujitegemea.

Akitoa uzoefu wake, Profesa Do DucDinh wa Taasisi ya Kimataifa ya Uchumi ya Vietnam alisema inasikitisha kuona Tanzania ina kila rasilimali lakini ni masikini wa kutupwa.

“Nchi imebinafsisha viwanda bila ya umakini na matokeo yake viwanda vingi vimekufa. Kwetu suala la ubinafsishaji tulikuwa makini na Serikali inamiliki viwanda vingi ambavyo vinatoa ajira,” alisema Profesa DucDinh na kuongeza:

“Vietnam hatulimi korosho lakini tuna viwanda vingi vya kubangua korosho, tunategemea malighafi kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania.”

Profesa DocDinh aliishangaa Tanzania ambayo inalima korosho lakini ikabinafsisha viwanda vya kubangua zao hilo ambavyo vingi vimekufa.

“Utabinafsisha vipi viwanda vinavyoongeza thamani ya mazao ya kilimo ambacho kinategemewa na zaidi ya asilimia 80 ya wananchi?” alihoji.

Alisema kama Tanzania ina nia ya dhati ya kupunguza umasikini wa wananchi wake, inatakiwa kujipanga na kusaidia kuikuza sekta ya kilimo.

“Sekta ya kilimo iboreshwe kwa kupewa kipaumbele cha kwanza kwa kujenga miundombinu na wakulima kutumia mbegu bora na mbolea,” alisema.

Kwa upande wake, Profesa Li Xiaoyung wa Kituo cha Kimataifa cha Kuondoa Umasikini cha Beijing alisema maisha magumu yanayolalamikiwa na wananchi yanatokana na mfumuko wa bei hasa vyakula… “Ugali ni chakula kikuu lakini bei ya unga ni kubwa ambayo wengine wanashindwa kumudu, unategemea nini?”

“Nilipokuja mwaka jana nilikuta kilo moja ya mchele inauzwa kwa Sh1,200 lakini nimeshangaa sasa inauzwa kwa Sh2,500! Huu ni mfumko wa ajabu.”

Alisema mfumko huo kwenye bidhaa za chakula ndio unaowasababishia wananchi umasikini kwa sababu ni bidhaa wanazozihitaji katika matumizi ya kila siku.

Mchina huyo alisema sekta za mawasiliano na madini ambazo zinakua kwa kasi haziwezi kuwaondolea umasikini Watanzania kama kilimo hakitapewa kipaumbele.

JK anena
Awali, akifungua mkutano huo wa siku mbili, Rais Kikwete alisema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji kwenye sekta ya kilimo ili kuwanufaisha wananchi na wawekezaji akisema kinachotakiwa ni wananchi kubadili mtizamo wa kudhani kwamba wawekezaji wapo kwa ajili ya kupora mali za wananchi.

“Tukiendelea kudhani kwamba wawekezaji wapo kwa ajili ya kupora mali wakakasirika na kuondoka zao, tutaendelea kuwa masikini,” alisema.

Rais Kikwete alisema Serikali iliamua kuacha kufanya biashara na kuiachia sekta binafsi na yenyewe kubaki na kazi ya kujenga na kuboresha huduma za jamii.

“Serikali ilikuwa inauza viberiti na nyama tukabinafsisha viwanda na sasa tumebaki kuandaa mazingira mazuri ya uwekezaji,” alisema.

Mkurugenzi Mkuu wa Repoa, Profesa Samwel Wangwe alisema mkutano huo utawasaidia watafiti wa masuala ya uchumi kubadilishana mawazo kwa lengo la kufanikisha ajenda muhimu ya kuondoa umasikini nchini.
Chanzo: Mwananchi

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits