Tuesday, December 21, 2010

Best Blogger Tips
Gbagbo atoa hotuba kupitia televisheni


 Mtu anayedhaniwa na wengi kwamba alishindwa katika uchaguzi wa urais uliofanyika hivi maajuzi nchini Ivory Coast rais wa sasa Laurent Gbagbo ametoa hotuba yake ya kwanza kwenye televisheni ya kitaifa akijitangaza kuwa yeye ndiye rais wa halali nchini humo.

Bwana Gbagbo alifutilia mbali uwezekano wa taifa hilo kurejea katika vita vya wenyewe kwa wenyewe, na kutoa wito wa kufanyika mazungumzo baina ya pande zote mbili, akipendekeza jopo litakalowashirikisha wapatanishi kutoka jamii ya kimataifa kusuluhisha mgogoro huo.

Lakini mpinzani wake Alassane Ouattara, ambaye ametambuliwa na jamii ya kimataifa kuwa ndiye aliyeshinda uchaguzi huo amejibu kwa kusema kuwa wamekuwa na mikutano kwa kipindi cha miaka mitano na hakuna yeyote aliyetilia shaka kuhusu ni nani aliyeshinda uchaguzi huo.

Wakati huo huo umoja wa mataifa umeonya kuhusu uwezekano wa kuzuka vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Ivory Coast na kuwashutumu wafuasi wa bwana Laurent Gbagbo kwa kuwasajili mamluki kutoka taifa jirani la Liberia kuzua vurugu nchini humo.

Katibu mkuu wa umoja huo, Ban Ki-moon, amesema mrengo wa bwana Gbagbo unajaribu kuwazuia wanajeshi wa kulinda amani wa umoja wa mataifa nchini humo, ambao wanamlinda mpinzani wake , Alessane Ouattara.

Bwana Ban amesema hali huenda ikawa mbaya zaidi katika siku kadhaa zijazo.

Alitoa wito kwa mataifa mengine kuusaidia ujumbe wa umoja wa mataifa nchini Ivory Coast.

Wiki mbili zilizopita rais wa Liberia, Ellen Johnson-Sirleaf, alisema kuwa wapiganaji wa zamani kutoka nchini mwake wametakiwa kushiriki katika mapambano nchini Ivory Coast.
Source: BBC

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits