Friday, December 3, 2010

Best Blogger Tips
Mtoto wa Kwanza wa Jumbe afariki dunia

*Rais Kikwete atuma salamu za rambirambi 

MTOTO wa kwanza wa Rais mstaafu wa Zanzibar, Alhaji Aboud Jumbe, Dk. Suleiman Aboud Jumbe (62) amefariki dunia nchini India.
 
Dk. Suleiman alifariki dunia Jumatatu wiki hii nchini humo alikokwenda kumsindikiza baba yake Rais mstaafu Jumbe kwa ajili ya matibabu. Haikufahamika mara moja chanzo cha kifo chake, na mwili wake ulitarajiwa kuwasili Zanzibar jana kwa mazishi. Kutokana na kifo hicho, Rais Jakaya Kikwete, amemtumia rambirambi Mzee Jumbe kutokana na kifo hicho cha ghafla cha mtoto wake.
 
Dk. Suleiman alifariki katika Hoteli ya MDS Lodge iliyoko Sarita Vihar mjini New Delhi,  ambako alikuwa amefikia kwa ajili ya matibabu ya baba yake katika Hospitali ya Apollo. Kwa mujibu wa habari kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini India, alifariki dunia akiwa chumbani kwenye hoteli hiyo aliyofikia na mwili wake utarajiwa kuwasili jana kwa ndege. Katika rambirambi zake, Rais Kikwete alisema: Nashindwa kuelezea kiasi cha majonzi na huzuni niliyopata baada ya kutaarifiwa kuhusu kifo cha ghafla cha mwanao, Dk. Suleiman Aboud Jumbe Mwinyi, na msiba huo mkubwa uliokufika. Napenda kutuma rambirambi za dhati ya moyo wangu kwako kufuatia msiba huu mkubwa. Napenda kukuthibitishia kuwa mimi na wenzangu katika Serikali tuko nawe katika msiba huu mkubwa na katika kipindi hiki kigumu na cha majonzi makubwa.
 
Aliongeza Rais Kikwete: Nakuomba pia kwa kupitia kwako uwasilishe salamu zangu za rambirambi na wenzangu katika Serikali kwa familia yako yote na kwa jamaa na marafiki ambao kwa namna moja ama nyingine wameguswa na msiba huu.
ìTunajua kuwa mnapitia kipindi kigumu. Tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu awapeni nguvu, subira na uvumilivu wa kubeba majonzi ya kipindi hiki kwa sababu yote ni mapenzi yake, alisema.
Wakati wa uhai wake, Dk. Jumbe alikuwa miongoni mwa madaktari bingwa wazalendo katika Hospitali ya Mnazi Mmoja mjini Zanzibar baada ya kuhitimu masomo yake nchini China.
Source: Uhuru
 

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits