Thursday, March 10, 2011

Best Blogger Tips
Askofu abariki tiba ya Loliondo


Via Newhabari

BAADA ya Serikali kupitia Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda, kutangaza kusitisha kwa muda huduma za matibabu yanayotolewa na Mchungaji Ambilikile Mwasapila, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), limepinga hatua yoyote ya kukwamisha huduma hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Arusha jana, Askofu Thomas Laizer wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Kati eneo ambalo pia Mchungaji huyo anaendesha shughuli zake, alisema hatua ya kusitisha huduma hiyo ni kuupinga ukristo.

Kwa sababu hiyo, alisema Kanisa la KKKT halitakubali karama hiyo iliyotolewa na Mungu kupitia mtumishi wake kuhujumiwa.

Badala yake, ameiomba Serikali isaidie kuboresha mazingira ya eneo hilo.

Askofu Laize alisema kujaribu kuizuia kazi hiyo ni kuiingiza jamii katika mfarakano usio na sababu za msingi na huenda ikavuruga jamiii ambayo tayari kupitia huduma hiyo inaonekana kuungana bila kujali taifa, dini kabila wala rangi za watu.

“Si sawa kuzuia huduma ya kiroho kwa kutumia chombo chochote kile bila kuwashirikisha wadau wa kiroho ambao ni sisi viongozi wa dini, na bahati nzuri huduma hii si ya kisayansi kwamba waweza kuichunguza katika maabara,” alisema.

Kuhusu kuitaka Serikali kuingilia kati kusaidia huduma ya Mchungaji Mwasapile, Askofu Laizer alisema kuwa tayari Kanisa la KKKT limeanza mchakato wa kuyaboresha mazingira ya eneo hilo kwa kujenga banda kubwa la watu kupumzikia pamoja na kuchimba mashimo ya vyoo na huduma za maji.

“Tunaomba Serikali ituunge mkono katika hili, tutaanzisha akaunti katika benki ya CRDB, akaunti hiyo kila mtu apitishie mchango wake ili usaidie kuboresha huduma hii muhimu,” alisema.

Aliwashutumu vikali baadhi ya viongozi wa dini hasa wale wa Kikristo wanaopinga huduma ya mchungaji huyo kwa kile alichokiita kuwa ni wivu unaotokana na watu kuyakimbia makanisa ya viongozi hao.

Katika kile kinachonyesha kukerwa na matamshi ya baadhi ya viongozi hao, aliwataka viongozi wa dini, hasa wakristo kusoma na kuuelewa ukristo vizuri badala ya kutoa matamshi yanayoonekana kama wanaotapatapa.
“Wale wanaopinga huduma hii kwanza hawajui theolojia, wanasema mtu ambaye hajaokoka hawezi kutumiwa na Mungu, si kweli. Kwanza hatuokoki, tunaokolewa,” alisema Askofu Laizer.

Aidha aliwatahadharisha waumini wa kikristo na wananchi kuwa makini na viongozi hao aliowaita kuwa ni watu wanaojaribu kumwongoza Mungu kadri ya matakwa yao.

“Hao wanaojiita viongozi wa dini wanaopinga huduma hii wasimshike Mungu pua, kumwendesha na kumpeleleka wanakotaka wao kama farasi, wasifanye monopoly (urasimu) katika kumtumikia Mungu, hilo halipo, yule ni kiumbe dhaifu ambaye Mungu katika mazingira yake ameamua kumtumia yeye na si wao, tumwache afanye kazi yake yeye aliyemteua,” alisema Askofu huyo.

Alitumia fursa hiyo kuwahakikishia wananchi kuwa Mchungaji huyo si mganga wa kienyeji, wala si tapeli kama baadhi ya watu wanavyopotosha, bali ni miongoni mwa watumishi wa KKKT waliostaafu wakiwa waadilifu na ndio wanaoigwa kwa utumishi uliotukuka.

Siku chache baada ya mamia kwa maelfu ya watu kufurika katika Kijiji cha Samunge kupata kikombe cha dawa za mchungaji huyo, wamejitokeza baadhi ya watu kutoa ushuhuda wa kupona.

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits