Wednesday, September 28, 2011

Helkopta Chadema yavuruga Igunga

Best Blogger Tips
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jana kilianza kutumia helkopta katika mikutano yake ya
kampeni za ubunge katika Jimbo la Igunga na kusababisha baadhi ya mikutano ya vyama vingine vinavyoshiriki kampeni hizo kuvunjika.

Helkopta hiyo inayoendeshwa na Kapteni Paul Denge iliwasili saa 6:00 mchana katika kiwanja cha Shule ya Msingi Choma cha Nkola na kusababisha walimu na wanafunzi kuvunja vipindi vya masomo kushuhudia chopa, pia wananchi waliikimbilia kwa baiskeli na pikipiki, kitendo kilicholazimisha walinzi wa Chadema kufanya kazi ya ziada kuzuia wananchi walionekana kutaka kuishika na kupiga picha.

Wakati Chadema kikianza kutumia helkopita hiyo na kupata wananchi wengi kwenye mikutano yao, Chama Cha Mapinduzi (CCM) jana kilikuwa kimesimamisha kampeni kusubiri helkopita zake mbili ambazo zilitarajiwa kuwasili muda wowote, zikitokea Dar es Salaam.

Nacho Chama cha Wananchi  (CUF), kilikutana na waandishi wa habari na kuwaeleza nia ya kuleta chopa kama hiyo, ili kuwafikia wananchi katika maeneo ya jimbo hilo ambalo kijiografia limekuwa na miundombinu isiyopitika kirahisi.

Mara baada ya helkopita hiyo kuwasili, iliwachukua viongozi wa Chadema, akiwemo Mwenyekiti, Bw. Freeman Mbowe, mgombea ubunge Bw. Joseph Kashindye na mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Morogoro, Bi. Susan Kiwanga pamoja na waandishi wa habari na kuelekea katika kijiji cha Chabiso.

Katika Kijiji cha Chabiso, CUF walikuwa wafanye mkutano eneo hilo lakini baada ya kukimbiwa na wananchi wote waliamua kuvunja mkutano na kuondoka.

Akizungumza katika mkutano kijijini hapo, Bw. Mbowe alisema CCM imekabwa kila kona na safari hii haitatoka, kisha akawataka wananchi kufumbua macho kwa kuwa saa ya ukombozi imefika kwani wameteseka ndani ya miaka 50 bila mafanikio.

“Nawaambia ndugu zangu Chadema imeikamata CCM kweli kweli hadi kufikia hatua ya kutuogopa, safari hii tutabanana na ninawahakikishia hawatoki, tumejipanga kupambana nao. CCM inaogopa sana Chadema ndiyo maana mnasikia kila siku kwamba wanasema chama chetu ni cha fujo, siyo kweli wameona tunakubarika kwa Watanzania roho imeanza kuwadunda,” alisema.

Aliwataka wananchi hao kuwa wanakabiliwa na mtihani mkubwa ambao hivi sasa Watanzania wote wameelekeza macho na masikio yao kwao, kusikia wataamua nini juu ya hatma ya kupata kiongozi atakayewasaidia matatizo yanayowakabili.

“Nimepata taarifa kwamba kuna matatatizo makubwa yakiwemo maji, zahanati na barabara, lazima mfanye maamuzi mazuri, CCM hii ni ya matajiri ambao wanawakumbuka kila uchaguzi unapofika lazima muonyesha miaka 50 ya uhuru wa Tanzania wameshindwa kumaliza kero zenu.

…Lakini pia nimesikia hapa kuna chakula cha msaada kinagawiwa, hizi ni fedha zenu si za CCM, kama wanavyopita humo wanawadanganya…kama kuna mwanachama wetu yeyote atakayenyimwa atoe taarifa kwa viongozi wetu haraka, kwa sababu ni haki yenu kupata chakula,” alisema.
Endelea kusoma habari hii.................

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits