Wednesday, September 14, 2011

Rais Kikwete ateua wakuu wapya wa mikoa 15

Best Blogger Tips
RAIS Jakaya Kikwete amewateua wakuu wa mikoa wapya 15, kuwabadilisha vituo vya kazi wakuu wa mikoa watano huku wengine saba wakielezwa kwamba wamestaafu kwa mujibu wa taratibu. Katika uteuzi huo, wa wakuu wa mikoa 21, kati yao 11 walikuwa wakuu wa wilaya na ni Perseko Ole Kone pekee aliyebaki katika kituo chake cha kazi cha Mkoa wa Singida.

Mbali ya idadi kubwa ya wakuu wa wilaya waliopandishwa vyeo, katika uteuzi huo, Rais Kikwete pia amewateua waliokuwa Manaibu Waziri watatu, Mwantumu Mahiza, Ludovick Mwananzila na Joel Bendera, kuwa wakuu wapya wa mikoa.

Taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu iliyotolewa Dar es Salaam jana iliwataja wakuu hao wa wilaya waliopandishwa vyeo na mikoa yao katika mabano kuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, John Tupa (Mara), DC wa Morogoro, Saidi Mwambungu (Ruvuma), Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Chiku Gallawa (Tanga), DC wa Ilala, Leonidas Gama (Kilimanjaro), DC wa Newala, Dk Rehema Nchimbi (Dodoma), Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Elaston Mbwillo (Manyara).

Wengine ni DC wa Karagwe, Kanali Fabian Massawe (Kagera), DC wa Mvomero, Fatma Mwassa (Tabora), DC wa Manyoni, Ali  Rufunga (Lindi), DC wa Kilombero, Mhandisi Ernest Ndikillo (Mwanza), DC wa Bagamoyo, Magesa Mulongo (Arusha). Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Stella Manyanya ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.
Katika uteuzi huo, Mahiza anakwenda Mkoa wa Pwani, Bendera ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na Mwananzila Shinyanga. Kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Mahiza alikuwa ni Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi pamoja na Mwananzila huku Bendera akiwa ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo.

Waliobadilishwa vituo vya kazi ni Abbas Kandoro anayekwenda Mbeya akitokea Mwanza, Said Mecky Sadiki anayehamia Dar es Salaam akitokea Lindi, Christine Ishengoma anayekwenda Iringa akitokea Ruvuma, Luteni Kanali Issa Machibya kutoka Morogoro kwenda Kigoma na Kanali Joseph Simbakalia anakwenda Mtwara akitokea Kigoma.

Wakuu wa mikoa waliostaafu ni Mohammed Babu aliyekuwa Kagera; Isidore Shirima (Arusha), Kanali Anatory Tarimo (Mtwara), John Mwakipesile (Mbeya), Kanali Enos Mfuru (Mara), Brigedia Jenerali Dk Johanes Balele (Shinyanga) na Meja Jenerali   Said Kalembo (Tanga).

Wakuu wa wanne wa mikoa waliostaafu ambao watapangiwa vituo vingine vya kazi ni Amina Mrisho aliyekuwa Pwani, Dk James Msekela aliyekuwa Dodoma, Abeid Mwinyimusa aliyekuwa Tabora na Daniel Ole Njoolay wa Rukwa.

Taarifa hiyo ya Ofisi ya Waziri Mkuu imesema: “Wakuu wa mikoa mipya minne ya Simiyu, Geita, Katavi na Njombe itakayoundwa baada ya taratibu kukamilika watatangazwa baadaye.”

Taarifa hiyo iliongeza: "Wakuu wote wa mikoa waliopo sasa wameagizwa kuandaa hati za makabidhiano katika muda wa siku 14 kuanzia siku ya kuapishwa kwa wakuu wapya wa mikoa. Aidha, wakuu wa wilaya ambao wamepandishwa vyeo kuwa wakuu wa mikoa nao wanapaswa kufanya hivyohivyo kwa ajili ya wakuu wa wilaya watakaopangiwa vituo vitakavyokuwa vimeachwa wazi kutokana na uteuzi wao.”

"Makabidhiano hayo lazima yahusishe pia kutembelea kwa pamoja baadhi ya maeneo na miradi ambayo ni muhimu kama sehemu ya makabidhiano yao," ilisisitiza taarifa hiyo na kuongeza:

"Wakuu wote wa mikoa walioteuliwa na wakuu wa mikoa minne mipya watakaoteuliwa pamoja na wakuu wote wa wilaya watakaoteuliwa baada ya zoezi kukamilika watatakiwa kuhudhuria mafunzo ya wiki tatu kwenye Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo, Dodoma kwa lengo la kuwajengea uwezo zaidi wa kiuongozi na kiutendaji.”

Wakuu hao wapya wa mikoa wataapishwa na Rais Kikwete kesho saa 4.00 asubuhi kwenye Viwanja vya Ikulu, Dar es Salaam.
Chanzo: Mwananchi

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits