Friday, September 23, 2011

Waziri amuumbua daktari

Best Blogger Tips
NAIBU Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Lucy Nkya, ameelezea udhaifu wa utoaji huduma za afya kwa baadhi ya hospitali nchini, baada ya kwenda katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru na kuandikiwa dawa bila kujieleza kwa daktari.

Dk. Nkya alisema hayo wakati akizungumza na menejimenti, wafanyakazi na wanafunzi wa uuguzi na udaktari katika Hospitali Teule ya Halmashauri ya Wilaya ya Hai, baada ya kupata hati rasmi ya kutambua kupanda hadhi kwa hospitali hiyo.

Huku akiitaja hospitali hiyo, Naibu Waziri alisema alifika hapo bila kujitambulisha huku amejifunika nguo hadi usoni akaingia kwa daktari ambaye hakumtaja jina, lakini daktari huyo alimwandikia dawa bila kumwuliza tatizo lake.

“Niliingia kwa daktari na kabla sijakaa, akaanza kuniandikia vipimo huku akinihoji kama nina homa na shinikizo la damu (BP), nilimjibu nitajuaje wewe ndiye mtaalamu, akanieleza tena natakiwa kupigwa picha za mionzi (X-ray), nilishangaa sana,” alisema.

Alisema kutokana na hali ile, alimweleza daktari husika kwamba anatakiwa amsikilize kabla ya vipimo, lakini katika hali ya kushangaza, alisisitiza kuwa anatakiwa kwenda kupigwa picha za X-ray.

“Niligundua kuwa daktari yule alikuwa amedhamiria na analosema nilijitambulisha kwamba mimi ni Dk. Lucy Nkya, Naibu Waziri … alipatwa mshtuko, nikamhoji kama ndivyo anavyotoa huduma kwa wananchi wa kawaida, nilimwonya nikaondoka,” alisema.

Alisema aliondoka na kuahidi kurejea wakati mwingine bila kutambulika, ili kuangalia mwenendo wa mtumishi huyo kama anatekeleza wajibu wake kulingana na sheria, kanuni na taratibu za utoaji tiba.

Akizungumza na watumishi wa hospitali hiyo teule, alisema imekuwa miongoni mwa hospitali teule 34 nchini na kuwataka watumishi wake kuzingatia kanuni na taratibu za afya kwa kutoa huduma kulingana na viapo vya taaluma yao.

“Ninyi leo mmepata hati rasmi ya utambuzi kuwa Hospitali Teule ya Wilaya ya Hai, hakikisheni mnatimiza wajibu wenu … hii sasa ni hospitali ambayo inatoa huduma kwa vigezo vya Serikali, nisingependa kusikia malalamiko dhidi yenu,” alionya.

Aliitaka Halmashauri ya Hai kutohamisha watumishi wa hospitali hiyo kwa namna yoyote na badala yake wajitahidi kukabili changamoto zilizopo ili iweze kutekeleza wajibu wake.

“Sasa Serikali itakuwa ikilipa mishahara na marupurupu kwa watumishi wa hospitali hii, tukisikia halmashauri mnahamisha watumishi au kutumia fedha zinazotumwa ili kufanyia vikao, safari za namna yoyote … tutawachukulia hatua kisheria,” alisema.

Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Dk . Saitore Laizer, aliiomba Serikali ianze kutoa ruzuku ya mishahara, dawa, vifaa tiba na vitendanishi kwa hospitali hiyo, ili wananchi wapate huduma kwa gharama nafuu kama ilivyo kwa hospitali zingine za umma.

Alisema changamoto nyingine ni uhaba wa watumishi unaosababishwa na kuhama kwa watumishi kutoka mashirika ya dini na ya binafsi kwenda serikalini, jambo ambalo limeiathiri hospitali hiyo hususani idara za meno na macho.
Chanzo ; HabariLeo

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits