Wednesday, September 21, 2011

Msuya aonya Serikali isicheze na mgawo umeme

Best Blogger Tips
WAZIRI Mkuu Mstaafu, Cleopa Msuya ameitahadharisha Serikali kuwa makini na suala la mgawo wa umeme ambao amesema unaongeza ugumu wa maisha kwa wananchi, kwani unaweza kusababisha matatizo makubwa kiasi cha nchi kushindwa kutawalika.“Hali ikiendelea hivi tusishangae kutokea kwa mambo kama yaliyotokea kwa nchi za Kiarabu ambazo wananchi wake wameshindwa kuvumilia ugumu wa maisha na kuamua kuandamana.”  Msuya alitoa tahadhari hiyo, Dar es Salaam jana wakati wa mjadala wa kitaifa  kuhusu miundombinu, nishati na madini kwenye Wiki ya Maonyesho ya Miaka 50 ya Uhuru yaliyoandaliwa na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).

Angalizo la Msuya inakuja kipindi ambacho nchi ipo katika mgawo wa umeme kutokana na uhaba mkubwa wa nishati hiyo hali ambayo inaathiri sekta mbalimbali za uzalishaji na watumiaji wa kawaida.

Msuya alikuwa Waziri Mkuu kati ya Novemba 7, 1980 hadi Februari 24, 1983 na kushika tena wadhifa huo Desemba, 1994. Pia aliwahi kuwa Waziri wa Fedha, Viwanda katika vipindi tofauti.

Ili kukabiliana na tatizo hilo, Serikali kupitia kwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja ilitangaza mpango wa dharura wa Sh1.2 trilioni kukabiliana na mgawo, lakini hadi sasa hakuna mabadiliko yoyote yanayoonekana tangu ulipoasisiwa Agosti, mwaka huu.

Kauli ya Msuya
Msuya alisema Tanzania inahitaji uchumi unaokua na kwamba Serikali isipoangalia, tatizo la kushindwa kukua kwa uchumi, maendeleo ya nchi hayatafanikiwa.  “Kabla ya uhuru idadi ya watu ilikuwa milioni nane na sasa tuko zaidi ya watu 53 milioni, kuna haja ya kuwa na uchumi unaokua badala ya kuzalisha bila mafanikio, Serikali iwe makini katika kuimarisha mambo muhimu kama nishati,” alisema na kuongeza:

“Serikali inatakiwa kufikiri juu ya kuimarisha masuala ya umeme nchini wakati wawekezaji wanapoingia ili kusaidia uchumi kukua haraka na kuepusha kutokea kwa mambo yaliyozikumba nchi za Kiarabu.”  Ingawa hakuzitaja nchi hizo, lakini Misri, Tunisia, na Yemen ndizo zilikumbwa na maandamano kupinga hali ngumu ya kiuchumi na kusababisha viongozi wa Misri na Tunisia na kung’olewa madarakani.

Msuya alisema Serikali ina jukumu la kuimarisha mazingira yatakayoendeleza uchumi na kwamba ipo changamoto kubwa ya kuziunganisha sekta binafsi ili kuinua uchumi.  “Tatizo ni namna Serikali itakavyokubaliana na sekta binafsi katika kuimarisha uchumi wake na kuwainua wananchi kibiashara kwa sababu miundombinu ya uzalishaji hasa umeme bado haijasambaa katika mikoa yote,” alisema.

Alisema Serikali itakapoiunganisha mikoa 26 katika kuzalisha biashara na kuipatia nguvu ya umeme, itakuwa njia mojawapo ya kuimarisha mafanikio ya kila mwananchi na kuondokana na umaskini. “Sasa hivi tunaambiwa kuwa kuna fungu la fedha la kutekeleza kilimo, lakini bado kuna maswali mengi ya kujiuliza juu ya uwezeshwaji wa kilimo, kwa sababu maeneo ya vijijini ambayo ndiyo yanayojishughulisha na kilimo hayana umeme, Kilimo Kwanza kitatekelezwaje?,” alihoji Msuya.  Msuya alisema, ipo haja kwa Serikali kuangalia namna ya kuboresha mazingira ya kiutendaji ya halmashauri mikoani ili kila mkoa uunganishiwe umeme kirahisi.
 
Kauli ya Ngeleja

Ngeleja akizungumza kwenye hafla hiyo alisema, Serikali imetoa fursa kwa sekta binafsi kuwekeza hasa katika masuala ya nishati ili kuzalisha, kusambaza na kusafirisha.Alisema sekta binafsi imepewa jukumu hilo ili kuzalisha zaidi na kuimarisha uchumi wa nchi kwa kiwango kinachotakiwa na kuboresha miundombinu yake.

“Tangu Serikali ilipofanya mageuzi ya kisera katika uendeshaji uchumi wa nchi, sekta binafsi imekuwa ikiongezewa nguvu ya biashara hivyo ni vyema sekta hiyo ikatumia fursa ya kuwekeza zaidi katika sekta muhimu na kuzingatia sera ya nishati ya mwaka 2008,” alisema.

Alisema matatizo ya umeme yaliyopo yanatokana na mfumo wa kuunganisha umeme na kiwango kikubwa kinachopotea kutokana na usambazaji kuanzia katika chanzo cha umeme.

“Uwekezaji mdogo katika umeme unaochukua muda mrefu pia ni chanzo kikubwa katika kuchangia umeme, tozo zinazotozwa hazikidhi mahitaji yaliyopo na gharama kubwa za mafuta katika soko la dunia zinaongeza gharama za uzalishaji,” alisema.  Akizungumzia tatizo la mgawo wa umeme, Ngeleja alisema uchumi wa nchi umeporomoka kwa asilimia 6.9 na kuwa megawati 236 za mgawo huo kwa siku moja zinagharimu Dola za Marekani 400 milioni (takriban Sh500 bilioni).

 Mgawo wa umeme umekuwa ukiitikisa nchi zaidi tangu mwaka 2006 na hadi sasa Serikali imekuwa na mipango mingi ukiwamo ule uliopitishwa na Bunge hivi karibuni, kuonekana kukosa tija.  Katika mpango huo wa dharura, Serikali ilitangaza kuwa itatumia kiasi hicho cha Sh1.2 trilioni kwa ajili ya  mpango huo wa ili kunusuru uchumi wa nchi kuanzia Agosti hadi Desemba mwaka huu na Januari hadi Desemba mwakani. 

 Wiki moja iliyopita, Waziri Ngeleja alitoa ahadi ya kupungua makali ya mgawo huo lakini hadi sasa, hakuna nafuu iliyojitokeza.
Chanzo: Mwananchi

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits