Thursday, October 14, 2010

Best Blogger Tips
Gari la Chenge lagonga tena, laua


MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Bariadi Magharibi mkoani Shinyanga (CCM), Andrew Chenge ameingia matatani tena baada ya gari lake kudaiwa kumgonga mwendesha pikipiki na kusababisha kifo wakati akitoka kwenye kampeni.

Tukio hilo limetokea wakati mwanasheria huyo wa zamani akiendelea na kesi ya mashtaka mawili ya kuendesha kizembe na kugonga pikipiki ya matairi matatu na kusababisha vifo vya watu wawili na jingine la kuendesha gari ambalo bima yake ilishaisha.

Hata hivyo, imeelezwa kuwa katika ajali ya jana waziri huyo wa zamani wa Miundombini hakuwa akiendesha gari hilo, bali alikuwa ndani.

Habari zilizopatikana jana kutoka wilayani Bariadi zimeeleza kuwa Chenge akiwa anatokea Kijiji cha Namisagusa na Kilalo alikokuwa na mkutano wa kampeni kuelekea mjini Bariadi, alipata ajali hiyo katika Kijiji cha Mbiti kilicho Kata ya Mhango, Tarafa ya Ntunzu.

“Hii ajali imetokea majira ya saa 1:00 usiku, Chenge baada ya kuona gari lake limegonga alishuka na kuhamia katika gari jingine na kuondoka eneo hilo. Wananchi walipofika hapo walilizuia gari hilo, lakini baadaye wakatimuliwa na polisi ambao waliliondoa gari hilo,” alieleza Patrick Liyuba mmoja wa wananchi wanaodai kushuhudia ajali hiyo.
Source: Mwananchi

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits