Friday, October 29, 2010

Best Blogger Tips

Leo ni funga kazi ya kampeni 2010
 
HATIMAYE mbio za kampeni kwa ajili ya uchaguzi mkuu zinahitimishwa leo kwa wagombea kufunga pazia kwenye maeneo mbalimbali kabla ya Watanzania kuamua mustakabali wa nchi yao kesho.
Kampeni hizo zilizinduliwa rasmi Agosti 20 na vyama kuanza kujinadi siku iliyofuata wakati CCM ilipofanya mkutano wake kwenye viwanja vya Jangwani na kufuatiwa na CUF iliyoendesha mkutano wake Agosti 27 kwenye Uwanja wa Kidongo Chekundu na baadaye Chadema ilizindua kampeni zake Agosti 28 kwenye viwanja vya Jangwani.

Vyama hivyo vitatu, ambavyo vinachuana vikali kwenye kinyang'anyiro cha urais, vilifungua pazia kwa vyama vingine kuzindua kampeni zake kwa staili tofauti na viwanja tofauti na leo vitakuwa vikitupa karata ya mwisho baada ya safari ndefu zaa kujaribu kuwafikia wananchi kwenye mikoa tofauti ya Bara na Visiwani.

Wakati vyama hivyo vilitegeana wakati wa uzinduzi, leo vyote vitakuwa majukwaani kuhitimisha kampeni hizo ili kuwaweka sawa wapigakura kabla ya kufanya maamuzi yao kwa siri kesho.
CCM, ambayo inawania kubakia madarakani ili kuendeleza ubabe wake wa takriban miaka 49, itahitimisha kampeni zake kwenye viwanja vya Jangwani ambako mgombea wake wa urais, Jakaya Kikwete atahutubia wafuasi na wanachama wa chama hicho kikongwe.

Chadema, ambayo bila ya kutarajiwa imeonekana kutoa upinzani mkali kwenye kinyang'anyiro cha urais ambacho katika chaguzi zilizopita kilikuwa kati ya CCM na CUF, itahitimisha kampeni zake mkoani Mbeya ambako mgombea wake wa urais, Dk Willibrod Slaa atahutubia.
CUF, ambayo mgombea wake wa urais, Prof Ibrahim Lipumba anawania kwa mara ya nne kuingia Ikulu, itahitimisha kampeni zake kwenye Uwanja wa Kidongo Chekundu jijini Dar es salaam ambako watapokonyana mashabiki na CCM.

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits