Sunday, October 31, 2010

Best Blogger Tips

Jina langu lilikatwa nisigombee ubunge - Dk. Mwakyembe

Via Ippmedia

  Mgombea Ubunge Jimbo la Kyela kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Dk.Harrison Mwakyembe, amevunja ukimya kwa kutoboa siri kwamba Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Mbeya ilikata jina lake ili asiwe mgombea.

Lakini akasema pamoja na mbinu hiyo, Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete, ndiye aliyeokoa jahazi kwa kuamuru jina lake lirejeshwe ili kulinda heshima na maamuzi ya wananchi wa Kyela waliompa kura nyingi wakati wa mchakato wa kura za maoni.

Dk. Mwakyembe alitoa madai hayo mazito wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika kijiji cha Mpunguti, kata ya Makwale, alipokuwa akieleza sababu zinazomfanya aendelee kumnadi mgombea urais kupitia CCM, Dk. Kikwete, licha ya mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Dk.Wilbroad Slaa, kumtaka asimnadi mgombea huyo ili chama chake kisiweke mgombea ubunge wa kupambana naye jimbo la Kyela.

“Nawajibika na nalazimika kumpigia debe Rais Kikwete kwa sababu bila ya JK nisingesimama kuongea nanyi hapa, Kamati ya Siasa Wilaya walinipa alama A kwa maana ya kwamba nafaa kugombea kwa tiketi ya CCM, lakini jina lilipopelekwa kwenye kikao cha Kamati ya Siasa ya Mkoa ambayo miongoni mwa wajumbe wake ni Mkuu wa Mkoa walikata jina langu,” alisema.

Dk. Mwakyembe ambaye alipata kura 15,336 wakati wa mchakato wa kura za maoni, alidai kuwa wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Mbeya walichukua uamuzi wa kukata jina lake na kumpa mgombea aliyeshika nafasi ya pili katika kura za maoni kwa madai kuwa “yeye ni mkorofi, amewaumiza wenzake hasa katika suala la mkataba tata wa kampuni ya Richmond”.

"Kamati ya siasa ya Mkoa imekata jina langu, wengine tunapenda kutoa hoja za msingi na siyo hadithi, walikata jina langu na leo nalazimika kusema hivyo, kisa eti mimi ni mkorofi nilishawaumiza wenzangu, mimi nashangaa watu wanaozungumzia mambo hayo, unajua tunaanza kuwa taifa linalokosa maadili, umeumiza nini, mwizi umwangalie umchekee chekee?" alihoji.

Hata hivyo, alisema baada ya matokeo ya maamuzi hayo kupelekwa Dodoma kwenye kikao cha Kamati Kuu ya CCM kilichoketi chini ya Mwenyekiti wake Rais Jakaya Kikwete, kiongozi huyo wa CCM aliamuru jina lake lirejeshwe haraka ili kuzingatia demokrasia ya wananchi wa wilaya ya Kyela ambao walimpa kura nyingi wakati wa mchakato wa kura za maoni.

Alisema kutokana na upendo alionao Rais Kikwete kwa wananchi wenzake, kuna kila sababu kwa wana- Kyela kuhakikisha leo wanamchagua mgombea huyo wa urais wa CCM ili aweze kuendeleza mipango ya maendeleo katika jimbo hilo.

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits