Sunday, January 22, 2012

Dk. Slaa atinga Ikulu

Best Blogger Tips
 CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), jana kilikutana tena na Rais Jakaya Kikwete katika Ikulu ya Magogoni, Dar es Salaam, kujadili masuala mbalimbali, ukiwamo mchakato wa uanzishaji wa Katiba mpya.

Miongoni mwa wajumbe wa CHADEMA waliokwenda Ikulu ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, ambaye alichuana na Rais Kikwete katika kinyang’anyiro cha urais mwaka 2010, na tangu hapo wawili hao hawajakutana ana kwa ana.

Habari za ndani kutoka Ikulu na CHADEMA zilieleza kuwa Kikwete na Dk. Slaa walikutana katika kikao kilichowashirikisha viongozi wengine wa CHADEMA wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe.

Tanzania Daima Jumapili, liliwasiliana na Mbowe kwa njia ya ujumbe mfupi wa maneno (sms) kujua kuhusu safari hiyo, akajibu: “Tunakutana leo in the next 30 minutes (ndani ya dakika 30 zijazo).”

Hata hivyo, Mbowe hakutaja watu walioongozana naye kukutana na Rais Kikwete, ambaye mwishoni awali walikutana naye mwaka jana kuzungumzia upungufu mkubwa kwenye sheria ya uundwaji wa Katiba mpya.

Habari zilizolifikia gazeti hili ni kwamba Rais Kikwete ndiye aliyefanya jitihada za kutaka kukutana na CHADEMA jana, ili kuwaeleza hatua aliyochukua baada ya makubalino yao ya awali.

Tanzania Daima linajua fika kwamba ujumbe wa CHADEMA ulipokutana na rais mwaka jana, ulimwomba asikubali kusaini muswada wa kurekebisha Katiba mpya kuwa sheria, kwa kuwa ulikuwa na upungufu mkubwa.

Hata hivyo, Rais Kikwete alisaini muswada huo kuwa sheria. Watu walio karibu naye wameliambia gazeti hili kuwa alisaini ili kuepusha upinzani mkubwa kutoka kwa wabunge wa CCM ambao walikuwa wamepitisha muswada huo kwa kutekeleza agizo la chama ambacho yeye ni mwenyekiti wake.

Kama asingesaini muswada huo kuwa sheria, ingebidi urejeshwa bungeni kufanyiwa marekebisho kadiri ya mapendekezo ya CHADEMA, lakini wabunge wake wangetafsiri kwamba amewadharau, na wangeweza hata kuleta hoja ya kutokuwa na imani naye, jambo ambalo lingemtikisa zaidi rais ambaye tayari amekuwa anakabiliwa na makundi hasimu ndani ya chama chake.

Habari kutoka kwa watu walio karibu na Ikulu zinasema Rais Kikwete alisema kwamba kutokana na mazingira ya kisiasa yanayomkabili ndani ya chama chake, asingeacha kusaini muswada huo, lakini angehakikisha kwamba sheria hiyo haitumiki hadi baada ya kufanyiwa marekebisho muhimu kwa mujibu wa mapendekezo ya CHADEMA, ambayo Rais Kikwete aliridhika kwamba ni muhimu.

Mbunge mmoja amelidokeza gazeti hili kuwa tayari wamepewa makabrasha yenye marekebisho ya sheria hiyo, na wanatarajia kuyajadili kwenye vikao vya Bunge vinavyotarajiwa kuanza Januari 30, mwaka huu.

Hata hivyo, jitihada za kuwapata viongozi wa Bunge kuzungumzia jambo hilo ziligonga mwamba.
Tanzania Daima Jumapili limedokezwa na baadhi ya wasaidizi wa rais kuwa tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Rais Kikwete amekuwa akifanya jitihada za kukutana na Dk. Slaa, lakini jitihada zake ziligonga mwamba mara kadhaa kutokana na sababu mbalimbali.

Inadaiwa kwamba hata mwaka jana CHADEMA walipoomba kukutana na rais kujadili suala hilo, alikubali mara moja baada ya kuona jina la Dk. Slaa likiwa miongoni mwa wajumbe waliotarajia kwenda Ikulu. Hata hivyo, Dk. Slaa hakwenda Ikulu, kwani alipata udhuru.

Viongozi hao pia walishindwa ‘kuteta’ katika msiba wa Mbunge wa Viti Maalumu, Regia Mtema (CHADEMA) walipoonana kwenye mazishi Ifakara.

Licha ya mahasimu hao kushiriki mazishi pamoja, bado hawakuonana ana kwa ana, jambo ambalo liliibua hoja kwamba Dk. Slaa alimkwepa Rais Kikwete.

Hoja ya Dk. Slaa kumkwepa Rais Kikwete ilizua mjadala wiki iliyopita, huku mwenyewe akisisitiza kuwa asingependa kutumia msiba wa marehemu Regia kutafuta umaarufu wa kisiasa. Alisisitiza kuwa kutokutana kwake na rais lilikuwa tatizo la kiitifaki.

Awali kabla ya CHADEMA kwenda kuonana na Rais Kikwete mwishoni mwa mwaka jana, wabunge wake walisusia kujadili muswada huo kwa madai kuwa utaratibu wa utungaji wa sheria hiyo haukufuatwa, na kwamba Spika wa Bunge, Anne Makinda, alikuwa amekula njama na CCM kuharibu mchakato wa utungaji wa sheria hiyo, ili kuharibu mchakato na matokeo yake.
Chanzo: Tanzania Daima

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits