Tuesday, January 17, 2012

Wabunge 100 kumzika Mtema

Best Blogger Tips
 WABUNGE zaidi ya 100 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wanatarajia kushiriki maziko ya marehemu Regia Doto Mtema (32), Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema) yanayotarajia kufanyika leo nyumbani kwao Ifakara, Morogoro.

Pia Rais Jakaya Kikwete ambaye yuko katika ziara ya kikazi mkoani humo, anatarajia kushiriki maziko hayo.

Hayo yalibainika jana wakati wa utoaji heshima za mwisho kwa mwili wa marehemu katika ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam ulioongozwa na Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliiwakilisha Serikali huku upinzani ukiwakilishwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe. Viongozi mbalimbali wa Serikali akiwamo Mwanasheria Mkuu Frederick Werema, mawaziri na wabunge walishiriki.

Kati ya wabunge hao 50 waliteuliwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda na watahudumiwa na Serikali wakiwemo wajumbe wote wa Kamati ya Uongozi, wenyeviti wa kamati zote na wajumbe 10 wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu.

Wengine ni wabunge wote wa Mkoa wa Morogoro, wabunge sita waliowakilisha CCM, wanne Chadema, watatu CUF na mmoja mmoja kutoka NCCR-Mageuzi, UDP na TLP.

Wabunge wengine 50 walitokana na vyama vyao, makundi na taasisi mbalimbali wakiongozwa na Makinda, Naibu Spika Job Ndugai na Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Kabwe Zitto .

Akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Serikali, Pinda aliwapa pole Chadema kwa kuondokewa na Mbunge wao mwanamke mwenye uwezo mkubwa.

Alisema atamkumbuka sana kwani kila Alhamisi wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu aliuliza maswali, huku akisisitiza kuwa si rahisi kwa Chadema kuziba pengo hilo la Mbunge aliyekuwa na karama za pekee.

Alisema Rais Kikwete kabla ya kuanza ziara Morogoro alionesha nia ya kushiriki maziko hayo na kama ratiba haitambana atashiriki.

Makinda aliwataka wanawake kumuenzi Regia kwa kuthubutu kugombea nafasi za uongozi bila uoga.

“Regia ametuunganisha Watanzania kwa kutimiza upendo wa asili wa Watanzania, kwani ni nyota iliyomulika Tanzania … kuishi wamoja licha ya tofauti za kisiasa ambazo ni mapambio tu,” alisisitiza.

Makinda alisema Regia aliishi kwa upendo mpaka kwenye nyumba yake ya Mbezi ambako alihifadhi watu wenye shida jambo lililoonesha kuwa alikuwa Mbunge aliyejali matatizo ya watu na ndivyo wabunge wanavyotakiwa kuishi.

“Katika mkutano uliopita wa Bunge ilikuwa kama ananiaga kwani alinitumia karatasi ikisema ‘mama nakupenda … I love you so much’,” alisema Makinda.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, alisema Regia alijiunga na chama hicho mwaka 2001, akiwa chuoni, huku akiamini na kusimamia ukweli kwamba hakuna kazi mwanamume anaweza na mwanamke asiiweze.

Alisema ulemavu wake haukuwa kikwazo katika mapambano ndani ya chama, ujasiri aliouonesha tangu awali alipofanya kazi makao makuu ya chama kwa miezi miwili bila wazazi wake kujua.

Regia alikufa kwa ajali ya gari alilokuwa akiendesha eneo la Ruvu, mkoani Pwani akitokea nyumbani kwake Mbezi-Makabe, Dar es Salaam, kwenda Vigwaza akiwa na watu wengine saba akiwamo mama yake mdogo, Bernadeta Mtema.

Taarifa za polisi wa Pwani zilidai kuwa alilipita lori na ghafla kukutana uso kwa uso na lori lingine na alipojaribu kurudi upande wake, alikosa mwelekeo na kupinduka na kupoteza maisha papo hapo huku wenzake wakijeruhiwa.
Chanzo: HabariLeo

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits