Saturday, May 15, 2010

Best Blogger Tips
Kigogo auziwa shangingi la Sh155milioni kwa Sh6 milioni
 
Daniel Mjema, Moshi

KATIBU Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Hilda Gondwe anadaiwa kuomba auziwe kwa Sh6 milioni gari la serikali aina ya Toyota Landcruiser VX maarufu kama shangingi lililonunuliwa miaka mitatu iliyopita kwa Sh96 milioni.

Taarifa za biashara hiyo zimeibua hisia kwa wakazi wa mkoa huo huku wengi wakihoji imekuaje gari hilo la serikali liuzwe kwa bei hiyo ndogo wakati bado liko kwenye hali nzuri.
Mwishoni mwa mwaka jana, gari hilo lenye namba za usajili STK 1867 lililokuwa likitumiwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro (RC), Monica Mbega lilikarabatiwa na kampuni ya Toyota ya jijini Dar es Salaam kwa Sh11 milioni.

Vyanzo vya habari vimedokeza kuwa gari hilo lililonunuliwa miaka mitatu iliyopita kwa Sh96 milioni, halikustahili kuuzwa kwa bei hiyo kutokana na matengenezo makubwa lililofanyiwa Agosti mwaka jana.

Kwa kawaida magari ya serikali huwa hayalipiwi kodi, lakini kama gari hilo lingenunuliwa kwa bei ya soko, kuingizwa nchini na kulipiwa kodi mbalimbali ikiwamo ile ya 0ngezeko la Thamani(VAT), lingekuwa na thamani ya Sh155.7 milioni.

Shangingi lenye bei kama hiyo likiingizwa nchini linatakiwa kulipiwa Sh24 milioni kama kodi ya uagizaji (Import duty), Sh23.7 milioni kama VAT na Sh12 milioni ambazo ni kodi ya ushuru wa forodha.

“Kila mtu ameshangaa sana kwa sababu hilo gari ni kama jipya kwa sababu mwishoni mwa mwaka jana lilifanyiwa matengenezo makubwa kwa Sh11 milioni, leo linauzwaje kwa bei ya kutupa kiasi hicho?” Kimehoji chanzo hicho.

Gari hilo lilifanyiwa ukarabati mkubwa baada ya RC Mbega kukataa kutumia gari lililokuwa likitumiwa na mtangulizi wake, Mohamed Babu ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera.

Alitaka lifanyiwe matengenezo na kurejea katika hali yake ya upya kabla ya kuanza kulitumia.

Kwa sasa serikali imenunua gari jipya aina ya Toyota Landcruicer V8 VX kwa thamani ya Sh190 milioni ambalo ndilo linalotumiwa na RC Mbega ambaye pia ni Mbunge wa Iringa Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Habari zimedai kuwa tayari Katibu Tawala huyo ambaye ndiye mtendaji mkuu wa shughuli za ofisi ya RC, na ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya kabla ya kushushwa cheo na kuwa RAS, ameshalipia gari hilo.

Vyanzo hivyo vya habari vimedai kuwa japo yapo magari mengine ya serikali likiwamo Toyota Landcruiser VX lenye namba STK 2634 ambayo yamechakaa, lakini aliliandikia STK 1867 kuwa limechakaa na halifai tena.

Taarifa hizo zimedai kuwa zipo dalili kuwa kigogo huyo wa serikali ana mpango wa kulitumia gari hilo katika kampeni za kuusaka ubunge katika Jimbo jipya la Tunduru katika Uchaguzi Mkuu ujao utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

Gondwe ambaye anatarajia kustaafu serikalini Novemba mwaka huu, alitumia kikao cha Ushauri cha Mkoa (RCC) kilichofanyika juzi chini ya Uenyekiti wa RC Mbega kutangaza rasmi nia yake hiyo ya kugombea ubunge mwaka huu.

Lakini akizungumza na gazeti hili, Gondwe alisema kwa wadhifa wake, hana mamlaka ya kujiuzia gari la serikali.

Alisema alifuata taratibu zote katika kuomba kununua na hatimaye kupata bali cha kununua gari ambalo amesema hadi sasa hajaanza kulitumia.
Kwa habari zadi utazipata hapa.........

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits