Thursday, February 24, 2011

Best Blogger Tips
Gaddafi amlaumu Osama

Kiongozi wa Libya Kanali Muammar Gaddafi amekiambia kituo cha televisheni cha taifa kuwa Osama Bin Laden na wafuasi wake, ndio wa kulaumiwa kwa maandamano yanayotikisa nchi yake.

Katika hutuba aliyotoa kupitia simu, mahsusi kwa ajili ya wakazi wa mji wa al-Zawiya, Kanali Gaddafi amesema vijana wanadanganywa kwa kupewa dawa za kulevya na pombe ili washiriki katika "uharibifu na hujuma".

Kanali Ghaddafi anajitahidi kurejesha udhibiti wa mji mkuu Tripoli na maeneo ya magharibi.
Waandamanaji wamekuwa wakipata nguvu katika miji ya mashariki.

Wanasiasa wa upinzani na viongozi wa kikabila wamefanya mkutano muhimu katika mji wa mashariki wa al-Badya, kuonesha umoja dhidi ya Kanali Gaddafi.

Hotuba hiyo ililenga mji wa al-Zawiya uliopo kilomita 50 magharibi mwa mji mkuu, ambapo kumekuwa na ripoti za milio ya risasi mitaani.

Kanali Ghaddafi amesema waandamanaji hawana madai yenye msingi, na walikuwa wakiongozwa na kiongozi wa al-Qaeda.

"Bin Laden.... huyu ndio adui anayewadanganya watu. Msidanganywe na Bin Laden," amesema.

"Ni wazi kuwa sasa jambo hili linaongozwa na al-Qaeda. Vijana wenye silaha, watoto wetu, wanachochewa na watu ambao wanatafutwa na Marekani na nchi za Magharibi.

"Wale wanaochochea ni wachache, na hatuna budi kuwakamata."

Amesema vijana hao waandamanaji "wanafurahia kupiga risasi hasa wakiwa wamelewa".

Amesema Libya sio kama Misri na Tunisia, ambazo zimeshuhudia viongozi wao wakiondolewa madarakani, kwa sababu watu wa Libya wana uwezo wa kubadili maisha yao kwa kupitia kamati.
Source: BBC

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits