Saturday, February 26, 2011

Best Blogger Tips
Posh wa Beckam mjamzito

LONDON, England
WAKATI wadau wa soka na muziki wanasubiri kuona Posh Beckham anajifungua mtoto wa nne, mume wake David ametoboa siri ya moyoni. Akitoa siri hiyo, amesema pamoja na furaha ya kupata mtoto mwingine, ambaye anatarajiwa kuwa wa kwanza mwanamke kwao, mkewe alimliza alipojua ukweli huo.

Anakiri kuwa mkewe ambaye ni mwanamuziki wa zamani wa kundi la Spice Girls na sasa ni mwanamitindo mashuhuri, Victoria, amekuwa mtu mwenye kuficha siri, na mara nyingi amekuwa akimchanganya katika baadhi ya mambo. "Kuna mambo ananificha hadi dakika za mwisho, ananishangaza mno," anasema. Gwiji huyo wa soka alieleza kuwa mkewe anapenda maendeleo ya familia yao na ndio maana hufanya vitu kwa kufikiria kabla ya kumueleza.

Katika maisha yake ya ndoa, anasema hakuna jambo ambalo limeweza kumchanganya hadi sasa, kama suala la mimba hii aliyonayo mkewe maarufu kwa jina la Posh. "Sikuwa nikijua juu ya ujauzito huo, Posh hakunieleza, hadi siku moja ambayo aliamu kunishangaza. "Siku hiyo alinieleza anataka kunipa ofa. Nilimkubalia na tukatoka kwenda kula chakula cha usiku nje kwenye mgahawa.  "Nikiwa sina hili wala lile, tukiendelea kula na kunywa kwa furaha, ndipo alipoamua 'kunitupia bomu'. "Becks, aliita. Nikamuangalia usoni. Kuna kitu nataka nikwambie," alinieleza na nikiwa sina hakika na alilokuwa nalo moyoni, nikamjibu "niambie mpenzi." Huko ndio aliniambia suala la uja uzito,"alisema mchezaji huyo. "Nina mimba!" alitamka huku akiniangalia machoni bila kupepesa. "Nilianza kutokwa na machozi. Si kwamba nilikuwa nalia, bali yalikuwa machozi ya furaha ya kusikia habari hiyo nzuri," alisema Beckham ambaye tayari ni baba wa watoto watatu wa kiume, aliozaa na mkewe huyo. Watoto hao ni  Brooklyn, Romeo na Cruz. "Niliiona hiyo ni habari njema, kwani nilikuwa ninatamani sana kupata mtoto mwingine, matumaini kwamba tutapata mtoto wa kike." Anasema furaha yake hiyo imetokana na ukweli kuwa alijua pia mkewe alikuwa akitaka mtoto mwingine, na niligundua alipokuwa akinieleza habari hizo, hata yeye alikuwa katika furaha.

Furaha yangu anasema, ni kwamba tutaongeza binadamu mwingine katika familia yetu, na anataka kuona familia yake inaongezeka, akitaraji mmoja  wa watoto wake, hasa wa kiume, akirithi kazi yake ya kucheza soka. Hata hivyo, gwiji huyo wa soka anaeleza anapenda kuona familia yake ikitoa wataalamu mbalimbali ambao wataweza kuisaidia nchi yao ya Uingereza, siku zijazo. "England inahitaji wataalamu mbalimbali, hawa watoto Mungu akiwajalia watasoma na kuanza maisha yao huku wakisaidia maendeleo ya nchi hii na ulimwenguni mzima," alisema mchezaji huyo wa zamani wa Manchester United, ambaye sasa amesajiliwa na timu ya Los Angeles Galaxy ya Marekani. Becks ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 35 na mkewe Victoria akiwa na miaka 36, tayari wameanza kufanya maandalizi ya kumpokea mtoto huyo mpya.

Wanandoa hao wameweza wameshawarifu watoto wao watatu kuwa watarajie kumuona mtoto mchanga kabla ya sikukuu ya Krismasi mwaka huu. David na Victoria wameanza kupokea taarifa za kupongezwa na marafiki zao huku wakimuombea kwa Mwenyezi Mungu, Victoria ajifungue salama. Miongoni mwa watu ambao wametuma ujumbe huo ni pamoja na mwanamuziki maarufu duniani, Kylie Minogue. Hata hivyo, msemaji wa Victoria Beckham, Jo Milloy, ameeleza kuwa mipango mingine kuhusu jambo hilo inaendelea. Lakini baadhi ya vyombo vya habari nchini humo vikiwemo vituo vya luninga, vinahaha kutaka kuingia mkataba na familia hiyo kutangaza wakati mrembo huyo akijifungua.

Vyombo hivyo  vya habari vimekuwa vikijaribu kuteta na watendaji wa wanandoa hao ili waweze kuwashawishi wakubaliane nao, na ikiwezekana waweze kurekodi kipindi cha kuonyesha wakati mwanamuziki huyo wa zamani akijifungua.

Lakini hadi juzi hakuna taarifa yoyote iliyotolewa na familia hiyo kama itakubali jambo hilo au la.

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits