Thursday, May 19, 2011

Best Blogger Tips
CCM Arusha kwachafuka

 HALI si shwari chama tawala mkoani Arusha mara baada ya gari la Katibu wa CCM hapa, Mary Chatanda kunusurika kuchomwa moto na baadhi ya wanachama wa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM).Wanachama wa umoja huo kutoka wilaya mbalimbali za Mkoa wa Arusha waliandamana katika Jengo la Makao Makuu ya CCM Mkoa wa Arusha, wakishinikiza Chatanda pamoja na Mjumbe wa Baraza la Vijana mkoani Arusha, Mrisho Gambo "wajivue gamba".

Hali hiyo ilijitokeza jana katika jengo la makao makuu ya chama hicho wakati Kikao cha Kamati ya Siasa Mkoa kikiendelea ambapo, hali iliyosababisha dereva wa gari la katibu huyo wa CCM kulitoa nje ya jengo hilo na kisha kulikimbiza mahali kusikojulikana.

Vijana hao walikuwa wameshika mabango yenye ujumbe mbalimbali huku wakipaza sauti zilizokuwa zikimtaka Chatanda kuondoka katika nafasi yake ya uongozi kwa madai kwamba amekuwa akikivuruga CCM mkoani Arusha.

Wakizungumza na waandishi wa habari, wanachama hao kutoka wilaya za Monduli, Longido, Arusha, Arumeru, Karatu na Ngorongoro walisema pamoja na wao kutoa malalamiko mbalimbali juu ya Chatanda na Gambo, lakini uongozi wa CCM taifa umekuwa ukiwakumbatia viongozi hao na kudai sasa wamechoka.

Walisema malaliko yao kuwa Chatanda amekuwa akikivuruga chama chao ikiwa ni pamoja na kusababisha kukosa ushindi wa Jimbo la Arusha Mjini lililoenda kwa Chadema huku wakisema kwamba ikiwa atakataa kung'oka watajua cha kufanya.

“Hatumtaki Chatanda na hatumtaki Mrisho Gambo hawa watu kwanza ni wasaliti, lakini pia wamechangia sisi kushindwa kuchukua jimbo hili kwani walikuwa wanaiunga mkono Chadema tunataka waondoke mara moja hadi kieleweke,” ilisikika sauti ya mmoja wa vijana hao.

Miongoni mwa jumbe ambazo zilikuwa zimeandikwa kwenye mambango hayo ni "Chatanda umehujumu uchaguzi kwa siasa zako za makundi zilizojaa chuki, ubinafsi na ubabe usio na manufaa kwa Chama Cha Mapinduzi", "Chatanda kwa siasa zako za ubabe umetuchonganisha na viongozi wa dini”, na nyingine kadha wa kadha.

Hali hiyo ilisababisha Mwenyekiti wa UVCCM mkoani Arusha, James Ole Millya aliyekuwa kwenye kikao cha kamati ya siasa kutoka nje na kwenda ukumbini kuwatuliza wanachama hao, lakini juhudi zake ziligonga mwamba.

Akizungumza na wanachama hao, Milya aliwataka wapunguze jazba na kusema kuwa yeye ni mjumbe ametumwa kusikiliza madai yao hivyo wampatie na kisha taufikisha ujumbe huo.

“Jamani ninawaomba mtulie sidhani kama mtafanya fujo ninaomba mnipatie ujumbe mnitume niufikishe jamani nami nitaufikisha tulieni jamani,” alisema Milya

Hata hivyo, ushawishi wa Milya haukuzaa matunda na kuamua kurudi kikaoni kwani wanachama hao waliendelea kupaza sauti zao kwa wakidai kuwa wanamtaka katibu huyo aondolewe mkoani Arusha kwa kuwa amekuwa akiingilia uamuzi wa umoja wao na kuendelea kumkubatia Gambo.

“Mheshimiwa tunakipenda sana chama chetu na tunakuheshimu sana, tunaomba Chatanda aondoke la sivyo tutachoma gari lake, tukikutana nalo tutamondoa kwa nguvu,” alisema kwa jazba mmoja wa vijana hao.
Endelea kusoma habari hii......................

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits