Friday, May 27, 2011

Best Blogger Tips
Hospitali kubwa ya moyo kujengwa Mlimani City

Via HabariLeo

HOSPITALI kubwa ya moyo itaanza kujengwa eneo la Mlimani City Dar es Salaam wakati wowote kuanzia sasa na kukamilika ndani ya miezi 30 ijayo, ili kutoa huduma ya upasuaji na tiba ya moyo.

Ujenzi huo utafanywa na Shirika la Hifadhi ya Jamii Nchini (NSSF) kwa ushirikiano na Hospitali ya Apollo za India, chini ya usimamizi wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ya Tanzania.

Mkataba wa ujenzi huo ulisainiwa Ikulu Dar es Salaam jana mbele ya Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu wa India, Dk. Manmohan Singh na umelenga kuimarisha uwezo wa Tanzania kukabili magonjwa ya moyo, saratani na figo yanayohitaji utaalamu zaidi.

Akizungumza baada ya kusainiwa kwa mkataba huo, Rais Kikwete alisema hayo ni matunda ya ujio wa Dk. Singh nchini.

Rais alisema, ujenzi wa hospitali hiyo utaokoa mabilioni ya fedha za Serikali yanayotumika kupeleka wagonjwa wa moyo nchini India kwa ajili ya upasuaji na tiba nyingine pamoja na gharama za mafunzo ya madaktari.

Madaktari hao wamekuwa wakitumwa kupata utaalamu zaidi katika Hospitali ya Apollo nchini India lakini Rais Kikwete alisema fedha hizo za mafunzo zitaokolewa kwa kuwa wanachokifuata huko kitapatikana nchini.

Rais Kikwete alitoa mfano wa mwaka jana amabo Serikali ilitumia Sh. bilioni 11 kupeleka wagonjwa wake India kwa ajili ya matibabu ya ugonjwa wa moyo wakati gharama hizo zingeweza kupungua zaidi kama huduma hiyo ingepatikana nchini.

“Kwa kuanzia, tutahakikisha hospitali hiyo mpya inakuwa na wataalamu bora wa kutosha wa kutibu ugonjwa wa moyo ndipo tuendelee na ule wa saratani na figo. Wenzetu wa Apollo wamekubali kuja kutumegea utaalamu kwa kutoa mafunzo hapa hapa nchini hospitali hiyo itakapo anza kazi miaka miwili na nusu ijayo.

“Hatutakuwa na sababu ya kuhamishia wagonjwa wetu wa moyo India tena kwa sababu mkataba tulio saini unaeleza wazi kuwa hospitali hiyo itatoa huduma kama tunayoifuata katika nchi hiyo. Vifaa vya tiba na wataalamu watakao wapa ujuzi wataalamu wa nchini pia watatoka India kwa makubaliano ya ushirikiano,” alisema Rais Kikwete.

Kwa mujibu wa Kikwete, baada ya kusainiwa kwa mkataba huo wagonjwa wanaotakiwa kuhudhuria kliniki za moyo nchini humo kila baada ya miezi mitatu, hawatafanya hivyo kwa sababu madakitari wao watakuja nchini mara kwa mara kuwaona.

“Utaratibu huu upo kwenye makubaliano yetu na utatuondolea gharama tunazozipata sasa. Madaktari wa India wataanza kuwafuata wagonjwa wao nchini. Huu ni ushirikiano wenye faida,” alisema.

Akizungumzia uwezo wa madaktari wanaopata mafunzo kutoka kwa wataalamu wa India, Rais Kikwete alisema umedhihirika pale walipofanikisha operesheni 155 za moyo nchini.

Alisema, madaktari na wauguzi 29 wa magonjwa ya moyo na mengine yanayoambatana na ugojwa huo walipata mafunzo India na kufaulu kwa kiwango kizuri cha kuendesha huduma hiyo kwa upana zaidi nchini.

Mbali na hilo, Rais alimweleza Dk. Sigh kuwa uwekezaji wa nchi yake Tanzania ni Sh. bilioni 1.3 tu, kiasi alichosema kuwa ni kidogo sana ikilinganishwa na uzuri wa uhusiano wa nchi hizo mbili.

Alisema anaamini baada ya kusainiwa kwa mkataba huo kuhusu ukataji kodi, uwekezaji utaimarika maradufu kwa sababu kampuni iliyowekeza katika nchi hizo mbili itawajibika kulipa kodi kwenye nchi moja pekee.

Dk. Singh alimuhakikishia Rais Kikwete kuwa atafanya ushawishi wa kutosha kuuimarisha wawekezaji kuwekeza nchini.

Mbali makubaliano ya ushirikiano katika uwekezaji na ulinzi, Dk. Singh alimhakikishai Rais Kikwete kuwa nchi yake itaiwezesha Tanzania kupata ujuzi wa teknolojia mbalimbali na biashara ili iwe kitovu cha maendeleo katika Afrika Mashariki kwa kuwa ni mshirika wake wa karibu katika masuala ya kiuchumi.

Dk. Singh anayerejea nchini kwake leo alizindua mradi wa Kituo cha Ubora katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano cha Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) ulioanzishwa kwa ushirikiano wa nchi hizo mbili.

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits