Saturday, May 7, 2011

Best Blogger Tips
Samunge wazuia helikopta kutua

Via Mwananchi

WAKAZI wa Kijiji cha Samunge jana walizuia helikopta zinazofika hapo kupeleka wagonjwa kupata tiba ya magonjwa sugu kutoka kwa Mchungaji Ambilikile Mwasapila kutua na kuwafukuza wakusanya ushuru wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.

Kitendo hicho ni mwendelezo wa mvutano wa mapato yanayotokana na ushuru unaotozwa kwa helikopta, ndege na magari. Wakazi hao wanapinga halmashauri kukusanya ushuru wa Sh5,000 kwa kila magari na 150,000 kwa helikopta bila ya kupewa mgawo.

Kutokana na hali hiyo, jana Halmashauri ya Ngorongoro ililazimika kuomba msaada wa polisi na askari zaidi ya 20 walipelekwa kuwasimamia maofisa wa halmashauri kukusanya ushuru huo na kulinda uwanja wa ndege. Pia polisi  walimkamata Diwani wa Samunge, Jackson Sandea na kumhoji akidaiwa kuchochea mgogoro huo.

Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya ya Ngorongoro, Dominick Lusasi amekuwa akisisitiza kuwa uamuzi wa kukusanya ushuru huo, ambao awali ulikuwa ukikusanywa na kijiji hicho, unatokana na kikao cha wakuu wa mikoa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi.

Halmashauri ya Ngorongoro ilianza kukusanya ushuru huo tangu April 6, mwaka huu na kila siku wastani wa  magari 800 yanapata huduma Samunge huku helikopta zikitua wastani wa sita.
Wiki iliyopita Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Elias Wawa Lali aliagiza wakusanya ushuru wa kijiji kushirikiana na wale wa halmashauri lakini juzi wakusanya ushuru wa kijiji walisema hawakushirikishwa ipasavyo na fedha zote zinaendelea kupelekwa halmashauri na hakuna anayewalipa.

Kutokana na hali hiyo, wananchi hao juzi jioni waliitisha mkutano wa hadhara kwenye Uwanja wa Nane Nane kijijini hapo na kukubaliana kumwondoa  mkusanya ushuru wa halmashauri, Felix Jackson na kuyaruhusu magari kwenda kupata tiba bila kulipa ushuru kutokana na ofisa huyo kuwanyima kitabu.

Pia walitangaza kuanza kukusanya wenyewe fedha kuanzia jana huku, wakidhibiti uwanja wa helikopta na kukusanya wao wapato.Wakizungumza katika kikao hicho wanakijiji, David Richard na Tito Garaa walisema kitendo cha halmashauri kuchukua mapato yote na kuwaachia uchafu hakikubaliki.

"Mbona Kijiji cha Soitsambu wameanzisha ushuru wa Sh500 kwa magari kutoka Kenya na halmashauri haijakataza? Kwa nini mapato yetu sisi wang'ang'anie?" alisema Garaa.Akizungumzia kukamatwa kwake, Sandea alisema alitakiwa kutoa maelezo kuhusu mgogoro huo… “Sijui kosa langu ila wananiambia twende kuhojiwa."Sandea aliwahi kupeleka hoja kwenye Baraza la Madiwani akiomba Kijiji cha Samunge kipewe ruhusa ya kukusanya mapato ya ushuru.

Wananchi waandamana hadi kwa Babu

Wanakijiji jana waliandamana hadi kwa Mchungaji Mwasapila wakitaka kumweleza kwamba watavuruga utaratibu huo wa kutoa tiba kutokana na tatizo hilo la mapato. Hata hivyo, walishindwa kuzungumza naye kwani alikuwa akiendelea na kazi ya kugawa dawa. Walizungumza na Msaidizi wake, Fredrick Nisajile ambaye aliwaambia kwamba Mchungaji hahusiki na mgogoro huo wa mapato hivyo ni vyema suala hilo likafanyiwa kazi na halmashauri na serikali."Nimewaomba watulie kwani Mchungaji hahusiki mambo ya ushuru wa magari na helikopta yeye anatoa tiba," alisema Nsajile.

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits