Friday, May 20, 2011

Best Blogger Tips
Sheikh Yahya Hussein afariki dunia

MTABIRI maarufu ndani na nje ya Tanzania, Sheikh Yahya Hussein leo asubuhi amefariki kutokana na tatizo la ugonjwa wa moyo baada ya  kukimbizwa Hospitali ya Ukombozi, Kinondoni, jijini Dar es Salaam leo asubuhi na  ilipotimu saa tatu asubuhi alikataka roho akiwa hospitalini hapo. Kwa mujibu wa mtoto mkubwa wa marehemu aitwaye Hassan, baba yake atazikwa kesho saa saba mchana kwenye makaburi ya Tambaza jijini Dar es Salaam.

Sheikh Yahya ambaye wakati wa uhai wake alipata umaarufu mkubwa kutokana na kutabiri matukio makubwa katika maeneo mbalimbali duniani, alizaliwa wilaya ya Bagamoyo mkoa wa Pwani, mashariki mwa Tanzania mwaka 1932.

Alipata elimu yake ya awali katika shule ya Al Hassanain jijini Dar es Salaam, kabla ya kwenda visiwani Zanzibar ambako aliendelea na masomo katika chuo cha Muslim Academy.

Baada ya kuhitimu alikwenda nchini Misri alikopata elimu ya juu zaidi katika masuala ya dini ya Kiislam katika chuo kikuu cha Al Azhar kilichoko jijini Cairo.

Sheikh Yahya Hussein baadae alirejea nchini Tanzania mwanzoni mwa miaka ya sitini na kuanza shughuli zake za utabiri wa elimu ya nyota akiwa mtabiri wa mwanzo kabisa kueneza shughuli za utabiri wa nyota katika magazeti mbalimbali ya ukanda wa Afrika Mashariki.

Mnajimu huyo, amewahi kuendesha shughuli zake katika nchi za Afrika Mashariki na maeneo mengine duniani.

Pamoja na elimu yake ya unajimu, vile vile Sheikh Yahya Hussein alikuwa kiongozi wa dini ambaye pia alijihusisha na uchambuzi wa masuala ya siasa kupitia utabiri hususan wakati wa uchaguzi, ingawa hakushiriki kikamilifu katika kuwania nyadhifa zozote za kisiasa.

Pia alivuma sana katika kutabiri matokeo ya mechi kubwa za soka katika michuano ya Gossage na hata timu za Simba na Yanga za Tanzania bila kusahau vifo vya watu mashuhuri kama wanasiasa na wasanii pamoja na matukio makubwa duniani.

Marehemu Yahya Hussein ameacha mjane na watoto wapatao ishirini.

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits