Saturday, June 25, 2011

Best Blogger Tips
Katiba mpya 2014

Via Tanzania Daima

SERIKALI imetangaza rasmi kuwa Katiba mpya itazinduliwa Aprili 26 mwaka 2014, siku ambayo itakuwa ni maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Kauli hiyo ilitolewa jana mjini Dodoma na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alipokuwa akifungua Semina Elekezi kwa wakuu wa mikoa na wa wilaya kuhusu mchakato wa Katiba Mpya.

Semina hiyo iliyofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya St. Gasper, Pinda alisema mchakato wa uundwaji wa katiba hiyo umeshaanza ambapo wananchi wamepewa fursa ya kutoa maoni yao.

Alisema matarajio ya serikali ni kuwa mpaka ifikapo mwaka 2014 mchakato wa Katiba mpya utakuwa umekamilika na Aprili 26 Katiba mpya itazinduliwa.

“Ni matarajio ya serikali kuwa Katiba mpya itakuwa imekamilika na kuzinduliwa ifikapo Aprili 26, 2014 katika maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar,” alisema.

Pinda alisema kama mambo yote yatakwenda kama yalivyopangwa, Muswada wa Sheria kuhusu Mapitio ya Marekebisho ya Katiba utawasilisha bungeni mwishoni mwa Mkutano wa Nne wa Bunge unaoendelea hivi sasa.

Alisema iwapo muswada huo hautawasilishwa katika mkutano wa nne basi utawasilishwa mwanzoni mwa mkutano wa tano unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Waziri Mkuu, aliwataka wakuu wa mikoa na wa wilaya kutoa ushirikiano kwa Tume ya Kuratibu na Kukusanya Maoni itakayoundwa ili kuwezesha mikutano ya hadhara ya kukusanya maoni kufanyika kama ilivyokusudiwa kwa kuhamasisha wananchi kuhudhuria na kutoa maoni yao.“Suala hili ni kubwa na la kitaifa, ni vyema viongozi wasiingize siasa na wajiepushe kuwashawishi wananchi katika kutoa maoni yao, bali wawaache watoe maoni kwa uhuru au pasipo shinikizo lolote,” alisema.

Waziri Mkuu alisisitiza kuwa hatua ya sasa si ya kutunga Katiba Mpya bali ni kuunda Tume ya Kuratibu na Kukusanya Maoni ya Wananchi kuelekea kutungwa kwa Katiba Mpya.

Mchakato huo wa kuelekea uundwaji wa Katiba Mpya, umekwishaanza na katika hatua ya awali, serikali imeandaa rasimu ya Muswada wa Sheria ya Mapitio ya Marekebisho ya Katiba (The Constitutional Review Act) ya mwaka 2011.

Hata hivyo mchakato huo ulipata upinzani mkali kutoka kwa wadau mbalimbali wakipinga vipengele kadhaa vilivyomo kwenye muswada huo uliopelekwa bungeni kwa hati ya dharura katika Mkutano wa Tatu wa Bunge uliofanyika Aprili mwaka huu.

Miongoni mwa mambo yaliyolalamikiwa na wadau ni kuwa muswada huo uliandikwa kwa lugha ya Kiingereza ambayo ni watu wachache wanaoizungumza na kuielewa.

Wadau walipinga pia vituo vya kutolea maoni kuwa vitatu, ambavyo ni Zanzibar, Dar es Salaam na Zanzibar.

Hata hivyo serikali ililazimika kuuondoa muswada huo katika mkutano wa tatu wa Bunge na kuahidi kuwa utaandikwa kwa lugha ya Kiswahili na kuufanyia marekebisho kulingana na maoni ya wadau.

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits