Thursday, June 21, 2012

Akatwa kiganja kwa tuhuma za kutembea na mke wa mtu

Best Blogger Tips
MWANAFUNZI wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Nyakamwaga wilayani Geita, Fikiri Mtasimwa, amenusurika kifo baada ya kujeruhiwa kwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake na kukatwa kiganja cha mkono wake wa kushoto na Baba Neema baada ya kumtuhumu kutembea na mke wake.
Akizungumza mjini hapa jana katika wodi aliyolazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita, mwanafunzi huyo ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Gengetano, Kata ya Nyakamwaga, alisema alikutwa na mkasa huo Juni 17, mwaka huu, usiku wakati akinywa uji kijijini hapo.

Alisema mwanamume huyo alimvamia katika kijiwe hicho cha uji na kuanza kumshambulia kwa mapanga sehemu za kichwani, mgongoni na begani, kabla ya kumkata mapanga katika mkono wake wa kushoto na kupelekea kiganja cha mkono wake huo kunyofoka, akimtuhumu kutembea na mkewe, Mama Neema na kumuachia maumivu makali.

“Wakati nakunywa uji kwenye kijiwe hicho mara alitokea huyo jamaa na kumuuliza muuzaji wa uji (Mektirida) kama kuna huduma hiyo, alijibiwa vizuri kwamba uji upo na ndipo baadaye nilimuona anachomoa panga kiunoni mwake na kuanza kunikata kwa kunilenga shingoni.

“Nilikwepa lakini bahati mbaya lilitua kisogoni na kunijeruhi na ndipo nilipoamua kukimbia, lakini sikufika mbali kwani nilidondoka chini, akanifuata na kunikata panga jingine la pili kichwani, sikukata tamaa nilinyanyuka tena na kukimbia huku damu zikiendelea kuvuja, nikadondoka tena kwa mara nyingine akakata jingine la tatu nikajikongoja na kunyanyuka nikakimbia huku nikikinga shingo asinichinje.

“Lakini kwa kuwa jamaa alivyoonekana alikuwa na lengo la kuniuwa hakukata tamaa alizidi kunikimbiza na baada ya kuanguka chini kwa mara nyingine tena alinifuata nilipokuwa nimeangukia na kuanza kukata mkono wangu wa kushoto.

“Alikata panga la kwanza, la pili, la tatu na la nne lilipelekea kiganja kunyofoka na ndipo rafiki yangu mmoja aitwaye Fikiri William, ninayesoma naye kidato cha tatu alipofika kunisaidia na ndipo mwanamume huyo alipoogopa kukamatwa na kuamua kukimbia kusikojulikana,” alisema Mtasimwa.

Alisema kutokana na majeraha hayo alipoteza fahamu na alizinduka akiwa wodini na hakumbuki ni akina nani waliompa msaada wa kumwahisha hospitalini.

Alisema siku moja kabla ya tukio hilo alikutana na mwanamume huyo njiani na kwa kuwa alikuwa akimheshimu kama kaka yake, alimsalimia lakini aligoma kuitikia salamu yake zaidi ya kumpa vitisho.

“Nakumbuka siku moja kabla ya tukio nilikutana naye nilipomsalimia alinijibu wewe kijana unadharau sana wala sihitaji salamu yako, ila kaa ukijua maisha yako ni mafupi sana na utakufa kifo kibaya,” alisema Mtasemwa.

Alisema kutokana na majibu ya mtuhumiwa alipojaribu kuhoji kulikoni ajibiwe hivyo, alidai hakupata ufafanuzi wowote na mwanamume huyo aliondoka akimuacha na maswali mengi kichwani mwake yasiyokuwa na majibu na siku ya tukio ndipo alijua maneno aliyomwambia siku moja kabla hayakuwa ni utani.

Alisema kutokana na hali duni ya kipato cha wazazi wake anajishughulisha pia na upigaji picha, kwa ajili ya kupata mahitaji muhimu ya shule na familia yake na kati ya wateja wake wakubwa mke wa mtuhumiwa naye alikuwa miongoni mwa watu hao na anadhani inaweza kuwa sababu ya kuhisiwa kutokana na kumpiga picha mwanamke huyo.

“Unajua sisi ni masikini wa kipato na ninaishi na mama baada ya kutengana na baba na ninajishughulisha na kupiga picha mtaani baada ya muda wa masomo na mke wa jamaa aliyenifanyiwa unyama huo alikuwa ni mteja wangu, naona ndiyo sababu mwanaume huyo alihisi natembea naye japokuwa sina tabia hiyo na nilikuwa namheshimu kama dada yangu,” alisema Mtasimwa.

Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk. Ndallo Ndallo, alithibitisha kuwapo kwa majeruhi huyo katika hospitali hiyo, aliyelazwa wodi namba nane na kuongeza kuwa hali yake ni mbaya kutokana na majeraha aliyoyapata sehemu mbalimbali za mwili wake na juhudi za kuokoa maisha ya mwanafunzi huyo zinaendelea.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Leonard Paulo, alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo na juhudi za kumsaka mtuhumiwa huyo zinaendelea baada ya kutoroka na kukimbilia kusikojulikana.

Alisema mke wa mtuhumiwa pia alitoroka baada ya kupatiwa taarifa na majirani zake kuwa mumewe huyo amepanga kumchinja baada ya kutoka kumjeruhi kijana huyo.
Chanzo: Mtanzania

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits