Monday, June 18, 2012

Hotuba ya Bajeti ya Kambi ya Upinzani Bungeni

Best Blogger Tips
 I.          UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Kambi ya Upinzani, ninatoa maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusu Bajeti ya Nchi ya mwaka wa fedha 2012/2013 kwa mujibu wa Kanuni za Bunge Kifungu cha 99(7) toleo la Mwaka 2007.

Mheshimiwa Spika, Natoa pongezi za dhati kabisa kwa Ndugu William Augustao Mgimwa, Mbunge wa Jimbo la Kalenga mkoani Iringa kwa kuteuliwa na Rais kuwa Waziri wa Fedha na Uchumi. Vile vile nawapongeza Ndugu Saada Mkuya na Ndugu Janeth Mbene kwa kuteuliwa kwao kuwa Wabunge na baadaye kuwa Manaibu Mawaziri katika Wizara hii nyeti sana.  Ninawapa pole pia maana Wizara ya Fedha sio Wizara lelemama. Kambi ya Upinzani itaendelea kuisimamia Wizara hii kwa ukaribu sana kama ilivyofanya katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. Mtakapofanya vizuri tutawapongeza ili muongeze juhudi, mtakapoharibu tutawawajibisha.

Mheshimiwa Spika, Ni dhahiri kwamba Mwaka wa Fedha uliopita ulikuwa mwaka mgumu sana kwa Watanzania. Ni mwaka ambao gharama za maisha zilipanda kwa kasi kubwa sana na juhudi za Serikali kuwakwamua wananchi na hasa wananchi wanyonge kutoka kwenye lindi la ufukara ziligonga mwamba. Kambi ya Upinzani inawapa pole Watanzania kwani hili ndilo walilochagua. Muhimu ni kuvumilia mpaka uchaguzi ujao na kufanya mabadiliko ya Serikali ili kuweka Serikali itakayoongozwa na CHADEMA na itakayoweza kukabili changamoto za sasa na za baadaye.

Mheshimiwa Spika, naomba tufanye mapitio kidogo ya Bajeti inayomaliza muda wake.

  1. UTEKELEZAJI WA BAJETI ILIYOPITA
Mheshimiwa Spika, kabla ya kutoa bajeti mbadala ya Kambi ya Upinzani ni vema kufanya tathmini ya utekelezaji wa bajeti ya Serikali iliyopita ili kuona ni kwa namna gani Serikali inathamini fedha za walipa kodi, na dhamira yake ya kuleta maendeleo ya kiuchumi katika Taifa. Katika kufanya hivyo, tutapitia baadhi ya maeneo ambayo Kambi ya Upinzani tunaona kuwa hayakutekelezwa katika bajeti iliyopita.

Kupunguza Makali ya Maisha

Mheshimiwa Spika, Katika Bajeti ya mwaka 2011/12 Serikali ilitangaza nia yake ya kupunguza makali ya maisha. Hatua mbali mbali zilichukuliwa ikiwamo kupunguza kodi na tozo kwenye mafuta ya Dizeli na Petroli, kuanza kutekeleza mpango wa dharura wa umeme na kutoa fedha za kununua chakula kwa Wakala wa Chakula. Serikali ilitumia shilingi bilioni 296 na dola za Marekani milioni 183 kwenye Umeme. Vilevile Serikali ilitumia shilingi bilioni 27 kununua Mahindi na kusambaza kwenye masoko.

Mheshimiwa Spika, licha ya hatua hizo zilizochukuliwa Mfumuko wa Bei uliongezeka maradufu kutoka wastani wa asilimia 6.3 mwaka 2010/11 mpaka wastani wa asilimia 17.8 mwaka 2011/12. Serikali imefeli katika lengo lake la kupunguza makali ya maisha kwa wananchi. Sio tu kwamba Serikali imeshindwa kudhibiti upandaji holela wa gharama za maisha bali pia hatua za Serikali zimeongeza kasi ya kupanda kwa makali ya maisha.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni katika Hotuba yake mbadala ya mwaka 2011/12 iliitaka Serikali  kushughulikia msingi wa mfumuko wa Bei hapa nchini ambao ni uzalishaji mdogo wa mazao ya chakula. Tumeelezwa na Waziri Kivuli wa Mipango na Uchumi kwamba Chakula peke yake ni asilimia 48 ya kapu la bidhaa na huduma ambazo mwanachi anatumia. Mfumuko wa Bei ya Chakula kinacholiwa nyumbani na kwenye migahawa ilikuwa asilimia 25 mwezi Aprili 2012 (BoT monthly Economic Review, May 2012). Vile vile mfumuko wa bei wa nishati inayotumika nyumbani na mafuta ya Dizeli na Petroli ulifikia asilimia 25 pia mwezi Mei mwaka 2012. Ni dhahiri kwamba iwapo tutadhibiti mfumuko wa bei ya chakula tutaweza kushusha mfumuko wa bei kurudi kwenye tarakimu moja.

Mheshimiwa Spika, Serikali inapendekeza hatua zilezile ilizofanya mwaka wa fedha unaokwisha kwa kutoa vibali kwa Wafanyabiashara vya kuagiza Mchele na Sukari. Katika hotuba yake Waziri wa Fedha anasema ‘….Serikali ilitoa vibali vya kuagiza sukari bila kutoza ushuru wa forodha kiasi cha tani 200,000 ili kukabiliana na uhaba na kupanda kwa bei ya Sukari…’(uk 9 ibara ya 15). Baada ya hatua hii bei ya Sukari ilipanda kutoka tshs 1700 mpaka tshs 2800 kwenye maeneo mengi nchini. Waziri wa Fedha katika hotuba yake anatoa suluhisho. Ninanukuu. ‘…hatua za haraka ambazo Serikali itachukua ni pamoja na kutoa vibali vya uagizaji wa Sukari na mchele kutoka nje….’! Serikali inachukua hatua zilezile kwa tatizo lile lile ikitegemea matokeo tofauti.
Endelea kusoma hotuba hii......
Chanzo: Matukio - Michuzi

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits