Wednesday, June 27, 2012

Dk. Mwakyembe afanya ziara ya kushitukiza Msamvu

Best Blogger Tips
 WAZIRI wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, amefanya ziara ya kushitukiza katika Kituo cha Mabasi cha Msamvu, Manispaa ya Morogoro na kufanya ukaguzi wa mabasi ya abiria yaendayo mikoani.

Katika ukaguzi huo, mabasi matatu aliyaamrisha yalipe faini ya Sh 250,000 kila moja, kutokana na makosa mbalimbali, likiwamo la kutokuwa na dereva wa akiba.

Ziara hiyo aliifanya mapema wiki hii asubuhi, kwa kushirikiana na maofisa wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) na lengo lake ni kukagua mabasi yanayofanya safari za mikoani na nje ya nchi na kuona kama yanakidhi vigezo katika shughuli ya kusafirisha abiria.

Katika ziara hiyo, Dk. Mwakyembe, alifika katika kituo hicho cha mabasi na kuegesha gari lake mbali kidogo, kisha kuelekea katika mabasi huku akiwa kama abiria na kuingia ndani ya mabasi hayo kisha kuanza kukagua leseni za madereva na vitambulisho vya kampuni za mabasi wanavyotumia madereva.

Ukaguzi mwingine alioufanya ni ratiba za safari pamoja na usalama wa mabasi na baadaye aliamrisha madereva walioonekana kuwa na makosa kulipa faini.

Mabasi yaliyolipishwa faini ni pamoja na Royal Coach linalofanya safari zake kutoka Dar es Salaam kuelekea Bukoba, ambalo dereva wake hakuwa na kitambulisho cha kampuni, basi la Super Najimunisa na Muro Investment yanayofanya safari zake Dar es Salaam kuelekea Mwanza ambayo yalikuwa na kosa la kutokuwa na dereva wa akiba.

Baada ya kubaini makosa hayo, aliwataka madereva ambao walionekana kuwa na makosa kulipa faini ya papo hapo, vinginevyo aliwataka SUMATRA kuwafikisha mahakamani, hata hivyo, madereva hao walikubali kulipa faini hiyo baada ya kuwasiliana na wamiliki wa mabasi wanayofanyia kazi.

Akizungumza na maofisa wa SUMATRA na madereva, alisema makosa kama hayo yanaweza kusababisha ajali za barabara na hivyo kupoteza maisha ya watu, vilema vya kudumu na uharibifu wa mali na ataendelea kufanya ziara za namna hiyo mara kwa mara kwa ajili ya kubaini makosa mengine.

Aidha, aliwataka SUMATRA na kikosi cha usalama barabarani kusimamia sheria za usalama barabarani na kutowaonea aibu madereva watakaoonekana kuwa na makosa, kwa kuwa kufanya hivyo kutasaidia kupunguza ajali ambazo ni tishio hapa nchini.

Kwa upande wake, Mkuu wa Usalama Barabarani mkoani hapa, Leonard Gyindo, alisema Kikosi cha Usalama Barabarani kimejipanga kudhibiti ajali za barabarani kwa kufanya ukaguzi kabla ya gari halijaondoka katika kituo hicho na kwa madereva wenye makosa wamekuwa wakilipishwa faini ya papo hapo na wengine kufikishwa mahakamani.

Hata hivyo, alimpongeza Dk. Mwakyembe kwa jitihada zake katika kusimamia sheria, hasa za usalama barabarani na kuahidi kuwa kikosi hicho kitampa ushirikiano na kutekeleza maagizo yote atakayotoa.
Chanzo: Mtanzania

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits