Thursday, June 28, 2012

Madaktari 72 watimuliwa kazi Mbeya

Best Blogger Tips
 BODI ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya, imewasimamisha kazi
madaktari 72 kwa kosa la kutoingia kazini kwa siku tano jambo ambalo
ni kinyume cha makubaliano ya mkataba.


Imeelezwa kuwa madaktari hao ambao 54 ni wale wa mafunzo ambao
waliingia mkataba wa miaka miwili na hospitali ya Rufaa na madaktari
18 ni wale walioajiriwa na Wizara ya afya.


Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Bodi Kaimu Mkuu wa
Mkoa wa Mbeya Norman Sigara, alisema kitendo cha madaktari kutoripoti
kazini kwa siku tano ni ukiukwaji wa kanuni za utumisha wa umma toleo
la 2009 kifungu namba F.16-F17 na F. 27.


"Hivyo kupitia kanuni hiyo madaktari hao wamesimamishwa kazi na
kurudishwa kwa mwajiri wao ambaye ni Katibu Mkuu Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii kwa hatua zaidi za kinidhamu,"alisema Sigara.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo wa Bodi, imeelezwa kuwa siku ya tarehe
23/6/2012 wafanyakazi 15 waliokuwa zamu(Intern Doctors 12 na
Registrars3) hawakufika kazini na tarehe 24/6/2012 wafanyakazi
19(Intern doctors 15 na Registrars 4) hawakufika kazini.


Alisema, kuanzia tarehe 25/6/2012 hadi leo imethibitika kuwa Interns
doctor 54 na Registrars 18 hawakufika kazini hadi leo tarehe 28/6/2012
ambapo tarehe 25/6/2012 bodi ya hospitali ilifanya kikao cha dharura
kujadili hali ya utendaji kazi na utoaji huduma hospitalini na kutoa
uamuzi.


Sigara, aliyataja maamuzi hayo kuwa ni Mwenyekiti wa Bodi akutane na
madaktari ambao hawakufika kazini ili awasikilize sababu za kutofika
na kujadili namna ya kumaliza matatizo hayo jambo ambalo madaktari hao
waligoma.


Alisema, baada ya madaktari hao kukaidi ombi hilo, Bodi ya hospitali
ili waandikia barua za kujieleza kwanini wasichukuliwe hatua za
kinidhamu kwa kuvunja mkataba walioingia na hospitali na pia kukiuka
kanuni za kudumu za utumishi wa umma nalo walilikaidi

"Iwapo madaktari ambao hawakuripoti au kueleza sababu za kuridhisha
ifikapo tarehe 28/6/2012. Kwa kuzingatia kanuni za utumishi wa Umma,
madaktari hao watasimamishwa kazi na kurudishwa kwa mwajiri wao ambaye
ni Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,"alisema.


Aidha, alisema kuwa kwa ujumala madaktari hao waligomea barua zote
mbili yaani ya kuitwa kwenye kikao pamoja na ile ya kuwataka kujieleza
hivyo Bodi imechukua hatua za kisheria za kuwafukuza kazi.


Hata hivyo Mwenyekiti huyo wa bodi, alisema kuwa tayari hospitali ya
Rufaa kwa ushirikiano wa Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, madaktari watano
wamepatikana ili kusaidia huduma kwa hospitali hiyo.

Chanzo: Mbeya Yetu

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits