Saturday, June 2, 2012

Mbunge CCM akamatwa kwa rushwa

Best Blogger Tips
 TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) inamshikilia Mbunge wa Jimbo la Bahi (CCM), Omary Badwel kwa tuhuma za kupokea rushwa ya Sh1 milioni kutoka kwa kiongozi wa Serikali.

Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa taasisi hiyo, Alex Mfungo zinaeleza kuwa Badwel alikamatwa na maofisa wa Takukuru jana saa 9:00 alasiri katika Hoteli ya Peacock jijini Dar es Salaam.

Badwel ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) anadaiwa kukamatwa wakati anapokea rushwa kutoka kwa maafisa wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkurunga mkoani Pwani jana.

Mfungo aliliambia Mwananchi Jumapili kuwa wanaendelea kumshikilia huku wakati wanafanya uchunguzi hadi kesho ambapo watamfikisha mahakamani.

“Siwezi kumataja aliyekuwa akitoa rushwa kwa sababu bado tunaendelea na upelelezi, ila mpaka sasa yuko mahabusu na tutamfikisha mahakamani Jumatatu(kesho),” alisema Mfungo.

Alisema kuwa mbali na kumfikisha mahakamani, pia watatoa taarifa zaidi za tukio hilo kesho.

Naye Katibu wa Bunge, Thomas Kashilillah alilithibitishia gazeti hili jana kukamatwa mbunge huyo na kwamba wanasubiri taarifa zaidi kutoka Takukuru kuhusiana na suala hilo.

“Nimepata taarifa ya kukamatwa kwa Badwel, lakini sina taarifa za ndani nasubiri wenzetu wa Takukuru watupe ufafanuzi zaidi,” alisema Kashillilah.

Wakati mbunge huyo akikamatwa jana, Mwenyekiti wa Kamati ya LAAC, Augustine Mrema alikuwa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere akielekea Uingereza.

Bedwel ni mmoja kati ya wabunge wawili waliotajwa na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR Mageuzi) katika Bunge la Bajeti mwaka jana kwamba waliomba rushwa katika halmashauri ambayo hakuitaja.

Akichangia Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano, Kafulila aliwataja bungeni Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi na Mbunge wa Bahi, Omary Badwel wote wa CCM akidai kwamba aliwakuta wakiomba rushwa kwa viongozi wa halmashauri.

Wakati akitaja majina hayo, Kafulila nusra aingie katika mgogoro na aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge, George Simbachawene ambaye alikuwa akimwamuru kukaa chini kutokana na muda wake wa kuchangia kumalizika. Hivi sasa Simbachawene ni Naibu Waziri wa Nishati na Madini.

Wakati Simbachawene akimwamuru akae chin, Kafulila alikuwa akiendelea kuzungumza bila kujali kengele ya pili iliyopigwa kuashiria kwamba muda wake ulikuwa umekwisha.

"Mheshimiwa Mwenyekiti kwa wakati wa sasa ni vigumu kusimamia matumizi kwani mfumo wetu wa uongozi unaruhusu ufisadi, wapo viongozi, mawaziri, wabunge wanaomba rushwa...." alisema Kafulila na kuamsha zogo ambalo liliambatana na sauti zisizo rasmi katika ukumbi wa Bunge zikiuliza ".....wapo humu humu?" Kafulila alijibu "Ndiyo..."

Sauti moja ilisema wataje, hapo ndipo aliposema "....Wapo kina Zambi, Badwel,  niliwakamata na nilichukua hatua, hatuwezi kuendelea namna hii," kisha akaketi.

Baada ya dakika chache tangu alipoketi, Kafulila alionekana akiteta jambo na Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali na Augustine Mrema wa Vunjo na baadaye Mkosamali aliomba mwongozo wa Mwenyekiti wa Bunge, akitaka waliotuhumiwa watajwe ili wafahamike vizuri.

Zambi na Badwel ni wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa pamoja na Kafulila chini ya Mwenyekiti wao, Mrema.

Mwenyekiti wa Bunge, Simbachawene akijibu hoja hiyo alisema atatoa mwongozo wake baadaye, katika muda ambao ataona unafaa. Hata hivyo, hadi sasa hakuna mwongozo ambao umetolewa na bunge kuhusiana na kauli ya Kafulila.

Naibu Spika


Kauli ya Naibu Spika, Job Ndugai alisema taarifa ya tuhuma za rushwa kwa wabunge ziliwahi kutolewa katika kikao cha Kamati ya Uongozi na Mrema, ijapokuwa majina ya watuhumiwa na mlalamikaji hayakutajwa.

Kafulila aliwahi kukaririwa akieleza kuwa tayari taarifa za tuhuma hizo za rushwa zilikuwa zimefikishwa kwa Spika kwa maandishi pamoja na Mrema kwa ajili ya hatua zaidi.

Kadhalika, Mbunge huyo alisema taarifa hizo zilikuwa zimekwishawafikia viongozi wa juu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na kwamba aliwahi kukutana na Spika kuhusu suala hilo ijapokuwa hakukuwa na hatua zozote ambazo zilichukuliwa.

 Wakati hayo yakiendelea Habari zilizopatikana jana kutoka kwa watu walio karibu na Kafulila zimeeleza kuwa huenda leo mbunge huyo akafanya mkutano na waandishi wa habari na kuanika uozo uliopo katika kamati hiyo.
Chanzo: Mwananchi

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits