Tuesday, June 5, 2012

Wabunge wala rushwa CCM watajwa

Best Blogger Tips
 WABUNGE vinara wa rushwa ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) wametajwa na majina yao yako katika ofisi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Tanzania Daima Jumatano limedokezwa.

Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya TAKUKURU kumnasa na kumfikisha mahakamani Mbunge wa Bahi (CCM), Omary Badwel, kwa tuhuma ya kupokea rushwa ya sh milioni moja kutoka kwa kiongozi wa serikali wa halmashauri ya wilaya ya Mkuranga.

Habari ambazo gazeti hili imezipata, zilidai kuwa wabunge waliotajwa ni wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) ambao wanadaiwa kuwamo kwenye mpango wa kutaka kupokea rushwa kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga.

Kamati ya LAAC inayoongozwa na Mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema (TLP), ina wajumbe 15, kati yao wajumbe watatu walipata kutajwa na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR Mageuzi), katika Bunge la Bajeti mwaka jana kwamba waliomba rushwa katika halmashauri ambayo hakuitaja.

Waliotajwa na Kafulila mwaka jana ni pamoja na Godfrey Zambi (Mbozi Mashariki), Zabein Mhita (Kondoa Kusini) na Omar Badwel aliyefikishwa mahakamani juzi kwa tuhuma za kuomba rushwa.

Mkurugenzi wa Upelelezi wa TAKUKURU, Alex Mfungo, alipohojiwa kuthibitisha taarifa hiyo hakukubali wala kukataa kuwapo kwa wabunge wengine ndani ya kamati hiyo wanaotuhumiwa kwa rushwa.

Badwel alikamatwa na maofisa wa TAKUKURU katika Hoteli ya Peacock jijini Dar es Salaam, akidaiwa kupokea rushwa kutoka kwa maafisa wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.

Akichangia Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano, Kafulila aliwataja bungeni Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi na Mbunge wa Bahi, Omary Badwel na Zabein Mhita wote wa CCM akidai kwamba aliwakuta wakiomba rushwa kwa viongozi wa halmashauri.

Wakati akitaja majina hayo, Kafulila nusra aingie katika mgogoro na aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge, George Simbachawene, ambaye alikuwa akimwamuru kukaa chini kutokana na muda wake wa kuchangia kumalizika. Hivi sasa Simbachawene ni Naibu Waziri wa Nishati na Madini.

Kiti cha Spika kiliahidi kutoa mwongozo kuhusu tuhuma hizo, lakini hadi sasa hakuna mwongozo uliotolewa kuhusiana na kauli ya Kafulila.

Bunge limechafuka
Wakati mbunge huyo akifikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuomba rushwa, hatua hiyo imeelezwa na wadadisi wa mambo ya siasa kwamba imezidi kuuchafua muhimili huo wa dola.

Duru za kisiasa zinadai kuwa kashfa ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, ya kukusanya mamilioni ya fedha za kuwapa wabunge ili wapitishe bajeti na hii ya Mbunge wa Kamati ya LAAC kunaswa akiomba rushwa imeanza kupoteza heshima ya Bunge.

Kama hakuna kitakachofanyika kuzuia kasi hii basi jina la Bunge la wala rushwa linaweza kuwa ndilo jina sahihi kwa taasisi hiyo.

Mwenyekiti wa UPDP, Fahmi Dovutwa, amesema wabunge ndio wanaoongoza kwa rushwa na kutolea mfano wa kashfa ya Jairo.

“Ulisikia rushwa ilivyotembea wakati wa uchaguzi wa wabunge wa Afrika Mashariki? Kamati ya LAAC imenaswa lakini naamini kuna kamati nyingi zinafanya mchezo huo. Hii ni aibu kwa Bunge letu,” alisema Dovutwa.
Chanzo: Tanzania Daima

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits